Watano wafariki helikopta ikianguka mlima Kilimanjaro

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 2

Helikopta ya kampuni ya uokoaji Kilimediair Aviation imepata ajali katika Mlima Kilimanjaro nchini Tanzania na kusababisha vifo vya watu wote watano waliokuwemo kwenye helkopta hiyo, wakiwemo raia wa kigeni wawili na rubani.

Ajali hiyo imetokea Jumatano ya Desemba 24 saa 11:30 jioni, katika eneo lililopo kati ya kilele cha Kibo na Barafu Camp, moja ya njia zinazotumiwa sana na watalii wapandaji wa mlima huo mrefu barani Afrika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, akieleza kuwa helikopta hiyo iliyokuwa imebeba watu hao watano ilikuwa katika zoezi la kuwachukua wagonjwa waliokuwa mlimani.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, waliopoteza maisha ni Plos David na Plosova Anna raia wa Jamuhuri ya Czech walipandishwa mlimani kutalii na kampuni ya Mikaya Tours, Jimmy Daniel (daktari), Innocent Mbaga ambaye alikuwa muongoza watalii na rubani Costantine Mazonde raia wa Zimbabwe.

Kwa mujibu wa mtandao wa Mwananchi, Maigwa amesema kuwa taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.

Eneo la Kibo Hut na Barafu Camp linapatikana katika urefu wa kati ya mita 4,670 hadi mita 4,700 kutoka usawa wa bahari, ikimaanisha kuwa ajali hiyo imetokea katika mazingira magumu ya kijiografia, zaidi ya mita 4,600 juu ya usawa wa bahari.

Ajali ya helikopta iliyotokea Mlima Kilimanjaro inaongeza orodha ya matukio yanayojitokeza mara kwa mara katika operesheni za anga kwenye maeneo ya milimani yenye miinuko mikubwa, ambako hali ya hewa na mazingira ya kijiografia hubadilika kwa kasi.

Mwezi uliopita kwenye mlima mrefu zaidi duniani wa Everest, helikopta moja ilianguka wakati wa kutua, eneo la Lobuche, karibu na Everest Base Camp nchini Nepal, katikati ya dhoruba kali ya theluji. Tukio hilo la Oktoba 29 lilitokea wakati helikopta kadhaa zilikuwa zikihamisha watalii wa kigeni kutoka eneo la Khumbu kufuatia mvua kubwa na theluji iliyosababisha hatari kwa wapandaji milima.

Matukio kama hayo pia yameripotiwa katika maeneo mengine ya milima mikubwa duniani, ikiwemo Himalaya, Alps barani Ulaya na Andes Amerika Kusini, hasa wakati wa shughuli za uokoaji au usafirishaji wa dharura wa wapandaji na watalii.

Changamoto zinazokabili safari za helikopta katika mazingira hayo ni pamoja na upepo mkali, mabadiliko ya ghafla ya hali ya hewa, pamoja na hewa nyembamba katika miinuko ya juu, hali inayoongeza ugumu wa shughuli za rubani na hatari za kiufundi.

Licha ya hatari hizo, helikopta bado hutumika kama njia muhimu ya uokoaji na usafiri wa dharura katika milima mikubwa, hasa pale ambako njia za ardhini hazipitiki au zinahitaji muda mrefu kufikika.