"Kazi yetu ni kuua tu"

Onyo: Simulizi hii ina maelezo ya wazi kuhusu vitendo vya mauaji.
Wapiganaji wanacheka wanapopanda nyuma ya lori la kubeba mizigo, wakipita kwa kasi safu ya maiti tisa na kufuata uelekeo wa jua linalozama nchini Sudan.
"Tazama kazi hii yote. Tazama mauaji haya ya halaiki," mmoja anashangilia.
Anatabasamu anapowasha kamera yake na wapiganaji wenzake, sare zao za Kikosi Rappid Support Forces zikiwa zinaonekana: "Wote watakufa hivi."
Wanaume hao wanasherehekea mauaji ya halaiki ambayo maafisa wa mashirika ya kibinadamu wanashuku zaidi ya watu 2,000 katika jiji la El-Fasher la Sudan mwezi uliopita.
Siku ya Jumatatu, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilisema inachunguza ikiwa wanajeshi hao huenda walifanya "uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu".
El-Fasher ilikuwa ngome muhimu kwa wanamgambo wa vya RSF. Ilikuwa ngome ya mwisho huko Darfur kushikiliwa na jeshi la Sudan ambao RSF imeendesha mapigano makali tangu muungano wao tawala ulipoanguka mwaka wa 2023.
Zaidi ya watu 150,000 wanakadiriwa kuuawa na mapigano hayo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na pande zote mbili zinatuhumiwa kufanya vitendo vya uhalifu wa kivita ambavyo vimerudiwa na RSF baada ya kuanguka kwa El-Fasher.
Mji uliotengwa na ulimwengu
Baada ya kuuzingira mji kwa karibu miaka miwili, kuanzia Agosti, RSF ilichukua hatua ya kujimarisha na kuwazuia raia waliosalia.
Picha za setilaiti zinaonyesha wanajeshi walianza kujenga ukingo mkubwa, kizuizi cha mchanga kilichoinuliwa kuzunguka eneo la El-Fasher, wakifunga njia za kuingilia na kuzuia misaada.
Kufikia mwanzoni mwa Oktoba, ukingo ulikuwa umezunguka jiji kabisa huku kizuizi kidogo kikizunguka kijiji jirani.

Wakati kuzingirwa kwa mji huo kulipozidi, watu 78 waliuawa katika shambulio la RSF kwenye msikiti Septemba 19, huku Umoja wa Mataifa ukikadiria zaidi ya watu 53 waliuawa kwa mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani na silaha za makombora kwenye kambi ya wakimbizi waliohama mwezi Oktoba.
Video zilizochapishwa na BBC Verify pia zilionesha kwamba RSF ilitafuta kuweka vikwazo vya chakula na mahitaji muhimu.
Mwezi Oktoba, picha zinaonyesha mwanaume akiwa amefungwa mikono na miguu na kuning'inizwa kichwa chini miguu juu kwenye mti kwa minyororo ya chuma.
Mtu aliyerekodi video hiyo alimtuhumu kwa kujaribu kuingiza nyenzo za usafirishaji ndani ya jiji lililozingirwa.
"Nakuapia kwa Mungu utalipa kwa hili, wewe mbwa," alilia, kabla ya kudai kwamba mtu huyo aombe sala zake za mwisho.
Wakati huo huo, RSF ilisonga mbele ndani ya jiji hilo huku wanajeshi wakiendeleza mapigano makali ya mtaa kwa mtaa.
Picha zinaonesha watu wasio na silaha wakiuawa kwa kupigwa risasi
Kufikia alfajiri Oktoba 26, RSF iliyadhibiti maeneo ya mwisho ya vituo vya jeshi na kuteka kambi kuu jijini humo, makao makuu ya Kitengo cha jeshi huku jeshi likitoroka.
Askari walirekodiwa wakifurahia walipokuwa wakitembelea makao makuu yaliyotelekezwa wakiwa wamebeba kifaa cha kufyatulia mabomu.
Baadaye siku hiyo kamanda wa RSF Abdul Rahim Dagalo kaka wa mkuu wa RSF Mohammad 'Hemedti' Dagalo alionekana akikagua kambi hiyo.
RSF kundi lililotokana na wanamgambo wa Janjaweed waliowaua mamia ya maelfu ya watu huko Darfur kati ya 2003-2005 limekuwa likishutumiwa kwa muda mrefu kwa kufanya ukatili dhidi ya makundi yasiyo ya Kiarabu kote Sudan.
Kulingana na Video zilizochapishwa mtandaoni wapiganaji hao wa kijeshi walikusudia kuanzisha vurugu dhidi ya raia huko el-Fasher.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kabla ya wanamgambo wa RSF kudhibiti mji wa El-Fasher, taarifa chache sana zilikuwa zikipatikana kutoka mjini humo kwa miezi kadhaa. Hata hivyo ndani ya saa chache baada ya jeshi la serikali kusambaratika, video za ukatili uliotekelezwa na RSF zilianza kuonekana mtandaoni, zikivunja ukimya uliokuwa umetanda juu ya jiji hilo.
Moja ya video za kutisha zaidi zilizojitokeza na kuchambuliwa na BBC Verify ilionyesha mauaji yaliyotokea katika jengo la chuo kikuu upande wa magharibi mwa jiji, ambapo makumi ya miili ya watu waliouawa ilionekana imetapakaa sakafuni.
Mzee mmoja aliyekuwa amevalia joho jeupe akiwa amekaa peke yake katikati ya miili hiyo. Aligeuka kutazama mpiganaji aliyekuwa amebeba bunduki akishuka ngazi kuelekea kwake.
Aliinua silaha yake, mwanajeshi huyo alifyatua risasi moja kwa moja, na yule mzee akaanguka chini na kupoteza maisha.
Askari wenzake, walioonekana kutoshtushwa na chochote mara moja waliona mguu wa mtu mwingine ukitetemeka kati ya miili.
"Huyu bado yuko hai kwanini?" mmoja wao alipiga kelele. "Mpige risasi!"
Aidha picha za setilaiti zilizopigwa Oktoba 26 zilithibitisha kwamba kulifanyika mauaji ya wazi barabarani El-Fasher, kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na Yale Humanitarian Research Lab.
Wataalamu wa maabara hiyo walionyesha "makundi makubwa" yaliyoonekana kwenye picha hizo, wakisema kuwa yalikuwa sawa na "ukubwa wa miili ya watu wazima na hayaonekana katika picha za awali."
Ripoti hiyo pia ilitaja "mabadiliko ya rangi" ambayo yanafikiriwa kwamba huenda yalitokana na alama za damu ya binadamu.
Shahidi mmoja aliiambia BBC alisema "wengi wa jamaa zetu walichinjwa,kwa kukusanywa katika eneo moja na wote kuuawa."
Shahidi mwingine alisema anakumbuka alishuhudia mwanamke mmoja akiuawa baada ya RSF "kumpiga risasi kifuani" na kutupa mwili wake kando "baada ya kupora mali zake zote."
Mara kikosi cha RSF kilipovamia El-Fasher, kundi tofauti la wapiganaji lilisalia pembezoni mwa jiji, ambapo walitekeleza mauaji ya kikatili dhidi ya mateka kadhaa ambao hawakuwa na silaha.
Ghasia hizi zilitekelezwa katika eneo lililo karibu kilomita 8 kutoka El-Fasher.
Video zilizothibitishwa zinaonyesha miili kadhaa iliyokuwa na mavazi ya kiraia, baadhi inaonekana kuwa ni wanawake wakiwa wamelala kwenye mtaro unaopita pembezoni mwa kingo iliyojengwa na RSF.
Aidha video nyingine zinaonyesha matukio ya uharibifu,ikiwa ni pamoja na moto ukiwaka na kuteketeza malori yaliyotawanyika katika mazingira hayo.
Nyingine zinaonyesha miili iliyotawanyika katikati ya magari.
BBC Verify iliweza kumtambua Abu Lulu, mtu muhimu katika ghasia hizo kama kamanda wa RSF.
Alionekana akiwaua mateka wasio na silaha katika video mbili, huku shahidi mmoja akiiambia BBC kwamba "aliwaamuru watu wake kuwaua watu kadhaa wasio na hatia, wakiwemo watoto".
Katika sehemu ya kipande cha video kilionesha askari wa RSF akijaribu kuingilia kati wakati Abu Lulu akijiandaa kumuua mtu aliyejeruhiwa, huku mateka huyo akiomba: "Ninakujua. Nilikupigia simu siku chache zilizopita."
Abu Lulu alikataa ombi la mtu huyo kwa kutumia mikono yake, akisema: "Sina huruma. Kazi yetu ni kuua tu." Baada ya kuelekeza bunduki yake karibu, mpiganaji huyo alifyatua risasi nyingi zilizomrarua mtu huyo ambaye hakuwa na silaha.

Video nyingine ilimuonesha akiua kundi la mateka ambao hawakuwa na silaha.
Video hiyo iliyoibuka siku chache baadae ilifichua miili iliyoachwa pale ilipoanguka katika mkao wa kunyongwa na kulala katika uwanja uliojaa vumbi.
Wengi wa waliohusika katika mauaji walikuwa wamevalia nembo za RSF ikiwemo kundi ambalo baadae lilisheherekea mauaji hayo kuwa ya halaiki.

Makamanda wa RSF kudhibiti uharibifu
Siku chache baada ya mauaji hayo, kiongozi wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo alikiri kwamba wanajeshi wake walifanya "ukiukaji" na akasema matukio hayo yatachunguzwa.
Kwa mujibu wa Afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa RSF ilikuwa imetoa taarifa kwamba walikuwa wamewakamata baadhi ya washukiwa miongoni mwa maafisa.
Baadhi ya waliokamatwa ni Abu Lulu baada ya BBC Verify kuchapisha ripoti inayoonyesha akitekeleza mauaji.
Picha zilihaririwa zilizochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa Telegram ya RSF zikimuonesha akiongozwa kwenye seli katika gereza nje kidogo ya mji wa El-Fasher.
Wadadisi wa Yale pia waliishutumu RSF kwa "kufuta ushahidi wa madai ya ukatili mkubwa".
Ripoti ya 4 Novemba ilibainisha kuwa picha za setilaiti zilionesha kuondolewa "kwa vitu vinavyofananishwa na miili kutoka kambi ya kaskazini ya RSF" na kutambua makaburi karibu na hospitali ya watoto huko El-Fasher.
BBC Verify ilichunguza maumbile meupe yaliyoonekana ua wa hospitali mnamo Oktoba 30 yakiwa na kati ya urefu wa mita 1.6 na mita 2.
Hii ni sawa na urefu wa mtu mzima na kuendana na mwili uliovikwa sanda ya mazishi ambayo hutumika zaidi nchini Sudan.
Wakati huohuo RSF na kurasa za mitandao ya kijamii zenye mahusiano ya kundi hilo zilianza kuchapisha taarifa zenye kubadilisha masimulizi hayo.
Taarifa zinazoonesha wapiganaji wake wakitoa misaada kwa raia zilirudiwa kuchapishwa na baadhi ya watumiaji, huku ofisi ya vyombo vya habari ya kijeshi ikichapisha vipande kadhaa vinavyoonesha wafungwa wa kivita wanavyohudumiwa kwa kuzingatia utu.
Licha ya kampeni ya mitandao ya kijamii kutekelezwa na RSF, vitendo vyao katika mji wa El-Fasher vimesababisha hasira duniani kote.
BBC Verify iliwasiliana na RSF, ikiipa fursa ya kujibu madai yaliyomo katika uchunguzi huu. Hata hivyo kundi hilo halikujibu.















