Sudan yalaani vikali hatua za Kenya na kuishtumu kwa kukaribisha kundi la RSF

.

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Aisha Juma
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Serikali ya Sudan imeikosoa vikali Kenya kwa kuwa mwenyeji wa utiaji saini wa mkataba wa kisiasa kati ya wanamgambo wa RSF na washirika wao, mkataba unaolenga kuunda serikali mbadala katika maeneo ya Sudan yanayodhibitiwa na RSF.

Katika taarifa rasmi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilisema kuwa hatua hii ni "uvunjaji wa wajibu wa Kenya chini ya sheria za kimataifa, Mkataba wa Umoja wa Mataifa, misingi ya Umoja wa Afrika na Mkataba wa Kuzuia Uhalifu wa Kimbari."

Sudan inadai kuwa Kenya imekiuka ahadi yake ya kuzuia shughuli za adui dhidi ya Sudan kutoka katika ardhi yake.

"Hatua hii ya serikali ya Kenya si tu inapingana na kanuni za ujirani mwema, bali pia inakwenda kinyume na ahadi zilizotolewa na Kenya katika ngazi ya juu kutoruhusu shughuli za kinyume dhidi ya Sudan kwenye ardhi yake, na pia ni tamko la uadui kwa watu wote wa Sudan," ilisomeka taarifa hiyo.

Serikali ya Sudan ilitupilia mbali madai kuwa shughuli za RSF jijini Nairobi ni "propaganda isiyokuwa na athari halisi" na kuitaka jumuiya ya kimataifa kulaani vitendo vya Kenya.

Wanamgambo wa RSF ambao kimekuwa wakipambana na jeshi la Sudan tangu mwezi Aprili mwaka 2023, wamethibitisha kuwa watashiriki na kutia saini makubaliano ya kuunda serikali mbadala ndani ya Sudan yaliyopangwa kufanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, siku ya Ijumaa.

Makubaliano hayo ambayo yatakuwa kati ya kundi la RSF, makundi ya washirika wake na yenye silaha yanalenga kuunda serikali mbadala ya 'Amani na Umoja' katika maeneo ambayo RSF inadhibiti.

Wanadai kuwa mkataba huo utawezesha utoaji wa huduma za afya, ulinzi, kuwa na uhalali wa kuendesha shughuli zao na mambo mengine kama hayo.

Hata hivyo, washika dau wanaohusika na mchakato wa utekelezaji mkataba huo, hakuna ambaye amesema wazi wazi makubaliano hayo yanahusisha nini lakini kamati husika iliwahi kusema kuwa madhumuni yake ni kurejesha serikali halali ambayo ilipinduliwa na wanamgambo wa harakati za Kiisilamu.

Kulingana nao, itakuwa kama njia ya ujumuishaji wa kila mmoja ili kutengeneza mazingira ya upatikanaji wa uthabiti na amani endelevu.

Lakini hadi kufikia sasa ni jambo ambalo ni la kufuatiliwa kujua nini kilichomo ndani yake.

Soma zaidi:

Serikali ya Sudan inasema nini kuhusu hili?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mkuu wa vikosi vya jeshi vya Sudan Luteni Jenerali Abdelfattah El Burhan ametoa tamko akikanusha taarifa kwamba amekuwa katika mawasiliano na vugu vugu la Forces of Freedom and Change (FFC) na kusisitiza kuwa, "Watu wa Sudan hawatakubali serikali yoyote, Hamdok au mtu mwingine yeyote, ambaye tutalazimishwa".

"Hatujawasiliana na chama chochote isipokuwa wapiganaji [wanaopigana na vikosi vya Rapid Support Forces]," alisema katika hotuba yake kwenye mkutano wa mafunzo ya mtandaoni katika bandari ya Sudan.

Abdalla Hamdok ni waziri mkuu wa zamani wa Sudan ambaye aliondolewa madarakani na aliunga mkono hatua ya RSF kudhibiti baadhi ya maeneo.

Hata hivyo, Jenerali Abdelfattah El Burhan ameondoa uwezekano wa kufanya mazungumzo na RSF au makundi yenye kuwaunga mkono akidai kuwa ndilo kundi lenye kusababisha mauaji kwa raia wasio na hatia nchini Sudan.

Na kufikia hatua hii, ni wazi kwamba Jenerali Abdelfattah El Burhan anapinga makubaliano yoyote yatakayotiwa saini mjini Nairobi kwa ajili ya taifa la Sudan.

Athari ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo ni ipi?

.

Chanzo cha picha, Reuters

Taswira ambayo tayari imejitokeza, kwa kiasi kikubwa huu utakuwa ni muendelezo wa mgogoro. Matumaini ya kupatikana kwa suluhu hata kama yalikuwepo, hili litakuwa ni lenye kukatisha tamaa.

Kundi la RSF limekuwa likishutumiwa kwa utekelezaji wa maovu dhidi ya raia huku wanaohangaika zaidi wakiwa watoto na wanawake.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilionya katika ripoti kwamba "kutokujali" kunakoendelea kunasababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na unyanyasaji nchini Sudan wakati mapigano yanaenea katika maeneo mapya.

"Mashambulio yanayoendelea ya makusudi kwa raia na kuharibiwa kwa mali zao, unyanyasaji wa kijinsia na ukiukwaji mwingine, unasisitiza kushindwa kabisa kwa pande zote kuheshimu sheria na kanuni za kimataifa zenye kuhusisha haki za binadamu," alisema Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu Volker Turk.

Kwa jinsi hali ilivyo, imekuwa vigumu hata kujua idadi kamili ya wanaoendelea kufariki dunia au kujeruhiwa kutokana na vita hivyo huku mapigano ya pande zote mbili yakiendelea kuongezeka kila uchao.

Mashirika mbalimbali yamekuwa yakisema kile kinachoendelea huko ni sawa uhalifu wa kibinadamu.

Pia ikumbukwe kuwa Marekani ilimuwekea vikwazo kiongozi wa kundi la RSF mnamo Januari 8, kwa jukumu lake katika mauaji dhidi ya wasio Waarabu nchini Sudan.

Nchi mbali mbali zimekuwa zikilaani mapigano hayo na kutoa wito wa kusitishwa kwa vita mara moja.

Kenya kuwa mwenyeji wa mkutano huu imepokelewaje?

Hili ni jambo ambali linasababisha utata. Kenya imeruhusu kundi la RSF na washirika wake kukutana mjini Nairobi kufanya mazungumzo ya makubaliano ya kuhalalisha uwepo wao.

Kwa haraka haraka, mtu anaweza akahitimisha kwamba Kenya inaunga mkono kundi la RSF ambalo sio tu limekashifiwa na nchi nyingi lakini hata kufikia hatua ya kuwekewa vikwazo.

Na tayari mkuu wa jeshi la Sudan El Burhan amepinga kile kinachoendelea mjini Nairobi hadharani na kusisitiza kuwa kamwe hayuko tayari kuzungumza na yeyote anayeunga mkono RSF.

Kenya pia imekuwa ikisikika kukemea vita hivyo, lakini hatua iliyochukua ya kumkaribisha yule anayelaumiwa na kukashifiwa kwa utendaji wa yasio kubalika, inaleta picha gonganishi, na kwa kiasi fulani kuna wale ambao wanaweza kuanza kutilia mashaka kujitolea kwao katika kuhakikisha amani endelevu inapatikana.

Lakini pia, Kenya imekuwa mstari wa mbele kutafuta fursa za uwakilishi kimataifa. Mfano, ilikuwa na mgombea kwenye uchaguzi wa mwenyekiti katika Umoja wa Afrika. Suala ibuka likiwa ni iwapo ingefanikiwa katika nafasi kama hiyo, Je ingeshughulikiaje mizozo ya ndani ya bara la Afrika?