'Ninatamani kurudi shule': BBC yazindua kipindi kwa ajili ya watoto katika maeneo ya vita

Tareq, mwenye umri wa miaka 10, kutoka Gaza, na Safaa, mwenye umri wa miaka14, kutoka Sudan wanaishi umbali wa kilomita 2,000. Hawajawahi kukutana, lakini wanaelezea ukweli mchungu kuhusu vita vilivyo haribu elimu yao.
"Nilipoona shule yangu ikiwa magofu, huzuni kubwa ilinitawala. Natamani irudi kama ilivyokuwa zamani," Tareq anaiambia BBC akiwa Gaza.
"Pamoja na yote, sijaacha kujifunza, nasoma nyumbani, nahakikisha sipotezi muda, ili nikirudi shuleni, niwe niko tayari," anaongeza.
Safaa ana ndoto ya kuwa daktari wa upasuaji wa moyo. "Bado nina matumaini," anasema, lakini ana kumbukumbu za kutisha za vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan.
"Miili ilitawanyika kila mahali, jambo ambalo lilinigusa sana na kunifanya nitake kuwa muokoaji wa maisha badala ya kuwa mpotezaji wa maisha."
Watoto milioni 30

Tareq na Safaa ni miongoni mwa watoto milioni 30 ambao, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto Unicef, hawako shuleni katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini. Inakadiria kuwa zaidi ya nusu - milioni 16.5 - wako Sudan pekee.
Kutokana na hali hiyo BBC World Service imezindua kipindi kwa lugha ya Kiarabu kupitia kipindi cha elimu kilichoshinda tuzo cha Dars - or Lesson.
Katika mwaka uliopita huko Gaza, "zaidi ya watoto 600,000 – ambao wana umri wa kwenda shule - hawakupata elimu," anasema msemaji wa Unicef, Saleem Oweis.
"Tunaona jinsi migogoro na ukosefu wa usalama inavyoleta madhara makubwa kwa elimu na watoto kujifunza," anaongeza.
Nchini Sudan, karibu miaka miwili baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka kati ya jeshi na wanamgambo wa Rapid Support Forces, mamilioni ya watoto wanaishi katika kambi za wakimbizi ambapo elimu inapatikana kwa tabu sana.
Katika mahojiano na BBC, waziri wa elimu wa Sudan, Ahmed Khalifa, ameelezea ukubwa wa tatizo.
"Hakuna jimbo lililosalimika," anasema. "Sudan ina takribani shule za umma 15,000. Kati ya 60% na 70% ya shule hizi zimeharibiwa kabisa na kupoteza kila kitu, miundombinu na vitabu.
"Hata katika majimbo salama, shule zimepata uharibifu kutokana na mashambulizi ya wanamgambo."

Kipindi cha Dars kilizinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2023 kwa ajili ya watoto nchini Afghanistan, wakiwemo wasichana waliozuiliwa kwenda shule za sekondari, huku Umoja wa Mataifa ukikielezea kama "njia ya kujifunza" kwa watoto wasioweza kuhudhuria shule.
Dars Arabic, iliyozinduliwa kwa ajili ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 11 na 16, ina masomo ya kila wiki kuhusu fani mbalimbali ikiwemo hisabati, teknolojia, hali ya hewa na afya ya akili.
Pia kinaangazia maisha ya watoto, kama vile Tareq na Safaa, ambao licha ya vita na vikwazo vingine, bado wameazimia kujifunza.
Kipindi cha kwanza kilionyeshwa Jumapili tarehe 9 Februari, kwenye BBC News Arabic TV. Vipindi vipya huonyeshwa kila wiki Jumapili saa 05:30 GMT (07:30 EET), na marudio saa 10:05 GMT (12:05 EET) na wiki nzima.
Kipindi hiki pia kinapatikana kwenye majukwaa ya kidijitali, ikijumuisha BBC News Arabic YouTube, pamoja na redio washirika huko Gaza na Syria.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












