Taifa ambalo watoto wengi wanatoroka vita duniani

.

Chanzo cha picha, Joyce Liu / BBC

Maelezo ya picha, Watoto
Muda wa kusoma: Dakika 5

Mahmoud ni kijana machachari ambaye hutabasamu zaidi ingawa alipoteza meno yake ya mbele katika mchezo hatari wa kitoto.

Yeye ni yatima wa Sudan aliyetelekezwa mara mbili, na aliyekimbia makazi yao mara mbili katika vita nchini mwake – ni miongoni mwa karibu watoto milioni tano wa Sudan ambao wamepoteza karibu kila kitu huku wakisukumwa kutoka sehemu moja hadi nyingine katika hali ambayo sasa ni mbaya zaidi ya kibinadamu duniani.

Hakuna mahali pengine popote duniani kunakoshuhudiwa idadi kubwa ya watoto wanaokimbia, au hata kuishi na njaa kali kama hiyo.

Njaa tayari imetangazwa katika eneo moja -huku wengine wengi wakishi katika uhitaji mkubwa wa chakula bila kujua mlo wao ujao utatoka wapi.

"Ni shida isiyoonekana," anasisitiza mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa wa kibinadamu Tom Fletcher.

"Wasudan milioni ishirini na tano, zaidi ya nusu ya nchi, wanahitaji msaada sasa," anaongeza.

Katika wakati wa machafuko mengi sana ambayo hayajawahi kushuhudiwa kabla, ambapo vita vikali katika maeneo kama Gaza na Ukraine vinatawala misaada na tahadhari ya ulimwengu, Bw Fletcher aliichagua Sudan kwa misheni yake ya kwanza ya kuangazia masaibu yake.

"Mgogoro huu hauonekani kwa Umoja wa Mataifa, kwa wahudumu wetu wa kibinadamu walio mstari wa mbele kuhatarisha na kupoteza maisha yao ili kuwasaidia watu wa Sudan," aliiambia BBC, tulipokuwa tukisafiri naye katika safari yake ya wiki moja.

Wengi wa watu wa timu yake wanaofanya kazi huko pia ni Wasudan ambao wamepoteza makazi yao, maisha waliyoishi awali, kufuatia mapambano haya ya kikatili ya kuwania madaraka kati ya jeshi na Wanajeshi wa RSF.

Ziara ya kwanza ya Bw Fletcher ilimpeleka katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Mahmoud’s Maygoma huko Kassala mashariki mwa Sudan, ambayo sasa ni nyumbani kwa karibu watoto 100 katika shule iliyobomoka ya ghorofa tatu.

.

Chanzo cha picha, Joyce Liu / BBC

Maelezo ya picha, Mahmoud, ambaye sasa ana umri wa miaka 13, amekimbia makazi yao mara mbili tangu mzozo ulipozuka nchini Sudan mwaka jana

Waliishi na walezi wao katika mji mkuu, Khartoum, hadi jeshi na RSF waliposhambuliana mwezi Aprili 2023, wakikiingiza mtegoni kituo cha watoto yatima na nchi yao kwenye wimbi la vurugu za kutisha, uporaji wa kimfumo na unyanyasaji wa kushangaza.

Mapigano yalipoenea hadi kwenye makazi mapya ya mayatima huko Wad Madani, katikati mwa Sudan, wale walionusurika walikimbilia Kassala.

Nilipomuuliza Mahmoud mwenye umri wa miaka 13 kuhusu matamanio yake ghafla aliangua kilio akibubujikwa na machozi.

"Nataka kuwa gavana wa jimbo ili niwe na mamlaka na kujenga upya nyumba zilizoharibiwa," alijibu.

Kwa Wasudan milioni 11 waliofukuzwa kutoka eneo moja hadi jingine, kurejea kile kilichosalia kama makazi yao na kuweza kuyajenga upya maisha yao kunaweza kuwa zawadi bora kuliko zote.

Kwa sasa, hata kupata mlo wa siku ni mapambano kwelikweli.

Na kwa mashirika ya misaada, pamoja na UN, kuwafikishia ni changamoto kubwa.

.

Chanzo cha picha, Joyce Liu / BBC

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya siku nne za mikutano ya ngazi ya juu ya Bw Fletcher huko Port Sudan, mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alitangaza kwenye mtandao wa kijamii X kwamba ametoa ruhusa kwa Umoja wa Mataifa kuanzisha vituo zaidi vya usambazaji na kutumia viwanja vya ndege vingine vitatu vya kikanda kuingizia msaada.

Baadhi ya ruhusa zilikuwa zimetolewa hapo awali lakini zingine ziliashiria hatua ya kusonga mbele.

Tangazo hilo jipya pia lilikuja wakati Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) likipata kibali kufikia jamii zilizo katika maeneo yanayodhibitiwa na RSF, ikiwa ni pamoja na kambi ya Zamzam huko Darfur inayohifadhi takriban watu nusu milioni ambapo njaa ilithibitishwa kuwakumba hivi karibuni.

"Tumekuwa tukisukumana kwa miezi kadhaa kufika katika jamii hizi," anasema Alex Marianelli, ambaye anaongoza oparesheni za WFP huko Port Sudan.

Nyuma yetu katika ghala la WFP, vibarua wa Sudan wanaimba huku wakipakia malori na masanduku ya chakula kuelekea maeneo yenye hali mabaya zaidi.

Bwana Marianelli anaonyesha kuwa hajawahi kufanya kazi katika mazingira magumu na hatari kama haya.

Ndani ya jumuiya ya misaada, baadhi wanaukosoa Umoja wa Mataifa, wakisema kuwa mikono yake imefungwa kwa kumtambua Jenerali Burhan kama mtawala mkuu wa Sudan.

"Jenerali Burhan na mamlaka yake wanadhibiti vituo hivyo vya ukaguzi na mfumo wa vibali na ufikiaji," Bw Fletcher anasema

"Ikiwa tunataka kwenda katika maeneo hayo tunahitaji kukabiliana nao."

Anatumai RSF pinzani pia itaweka watu mbele.

"Nitaenda popote, kuzungumza na mtu yeyote, ili kupata usaidizi huu, na kuokoa maisha," Bw Fletcher anaongeza.

Katika vita visivyo na huruma vya Sudan, pande zote zinazopigana zimeshutumiwa kutumia njaa kama silaha ya vita.

Vile vile unyanyasaji wa kingono, ambao Umoja wa Mataifa unauelezea kama "janga" nchini Sudan.

Ziara hiyo ya Umoja wa Mataifa ilienda sambamba na "siku 16 za harakati" zilizoadhimishwa duniani kote kama kampeni ya kukomesha unyanyasaji wa kijinsia.

Huko Port Sudan, tukio la kambi ya waliokimbia makazi yao, la kwanza wakati vita vilipopamba moto, lilikuwa la kuhuzunisha sana.

"Lazima tufanye vyema zaidi, lazima tufanye vizuri zaidi," aliapa Bw Fletcher, ambaye alitupilia mbali hotuba yake aliyoitayarisha alipozungumza huku wanawake na watoto wa Sudan, wakipiga makofi na kelele.

.

Chanzo cha picha, Joyce Liu / BBC

Maelezo ya picha, Mama Nour anasimamia kituo cha salama kwa wanawake wasio na waume na mayatima walionyanyaswa, na amekimbia pamoja na wale walio chini ya uangalizi wake.

Niliuliza baadhi ya wanawake waliokuwa wakisikiliza walichofanya kuhusu ziara yake.

"Kwa kweli tunahitaji msaada lakini kazi kubwa inapaswa kuwa kutoka kwa Wasudan wenyewe," anaeleza Romissa, ambaye anafanya kazi katika kikundi cha misaada na anasimulia safari yake ya kuhuzunisha kutoka Khartoum mara vita ilipoanza.

"Huu ni wakati wa watu wa Sudan kusimama pamoja."

Wasudan wamekuwa wakijaribu kufanya mengi kwa kidogo.

Katika makazi rahisi ya vyumba viwili, nyumba salama iitwayo Shamaa, au "Mshumaa", huleta mwanga kwa maisha ya wanawake wasio na waume walionyanyaswa na watoto mayatima.

Mwanzilishi wake, Nour Hussein al-Sewaty, anayejulikana kama Mama Nour, pia alianza maisha katika kituo cha watoto yatima cha Maygoma.

Pia ilimbidi kutoroka Khartoum ili kuwalinda wale waliokuwa chini ya uangalizi wake. Mwanamke mmoja ambaye sasa anajihifadhi naye alibakwa kabla ya vita, kisha kutekwa nyara na kubakwa tena.

Hata Mama Nour sasa yuko katika hali mbaya.

"Tumechoka sana. Tunahitaji msaada," anaeleza.

"Tunataka kuvuta hewa safi. Tunataka kuhisi bado kuna watu duniani wanaotujali sisi watu wa Sudan."

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Seif Abdalla