Vita vya Sudan: 'Unaweza kula usiku wa leo, lakini usile kesho'

Madina Yahya
    • Author, Khadidiatou Cissé
    • Nafasi, BBC News

"Unaweza kula usiku wa leo, lakini usile kesho," anasema mwanamke wa Sudan, Madina Yahya.

Madina anazungumzia kuhusu maisha ya El Fasher, jiji kubwa huko Darfur, Kaskazini mwa Sudan.

Hadi hivi karibuni, jiji hilo lilikuwa ni kimbilio salama. Kiasi kwamba Madina na familia yake walikimbilia huko kutoka kijijini kwao kwa sababu walikuwa na uhakika watapata chakula na usalama.

Lakini sasa, huku jiji hilo likizingirwa na waasi wa Rapid Support Forces (RSF), Madina na maelfu ya raia wengine wanapambana ili kunusurika.

Pia unaweza kusoma

Wakati vita kati ya wanamgambo wa RSF na Wanajeshi wa Sudan (SAF) vikiendelea, El Fasher ndio eneo la mwisho la mjini kuwa chini ya udhibiti wa serikali.

Jiji hilo lina wakazi takribani milioni 1.5, ambao ni pamoja na wakimbizi wa ndani 800,000 waliokimbilia hapa kwa sababu ya mzozo unaoendelea.

El Fasher una umuhimu mkubwa, ni makao makuu ya kihistoria ya vikosi vya jeshi na kitovu cha biashara na nchi jirani za Chad na Libya.

Kulingana na wizara ya Afya ya Sudan, takribani majeruhi 250 wameripotiwa, wakiwemo, tangu mapigano yalipoanza huko El Fasher.

Siku ya Jumapili, shirika la misaada la matibabu la MSF lilisema watoto wawili waliuawa na wengine kujeruhiwa baada ya bomu kuanguka karibu na hospitali ya watoto. Bado haijabainika nani alihusika na shambulio hilo.

Huku RSF ikiimarisha udhibiti wake, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameelezea hofu yao juu ya "hatari kubwa na ya haraka" kwa raia waliokwama ndani ya jiji bila njia salama ya kutoka.

Mzozo wa mwaka mzima

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tangu Aprili 2023, Sudan imekumbwa na mzozo wa kikatili kati ya RSF, inayoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan "Hemedti" Dagalo, na vikosi vya jeshi la nchi, vinavyoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

Hapo awali majenerali hao walikuwa washirika katika mapinduzi ya mwaka 2019 yaliyomuondoa madarakani aliyekuwa rais Omar al-Bashir. Lakini kutoelewana juu ya mageuzi kuhusu vikosi vya usalama na uwekaji wa serikali mpya ya mpito kulisababisha mzozo mbaya wa madaraka.

Ghasia zilianza katika mji mkuu wa Sudan Khartoum, zilienea haraka hadi Darfur, Kordofan Kaskazini, na jimbo la Gezira.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, takribani watu 15,000 wameuawa tangu kuanza kwa mzozo huo. Lakini, mjumbe maalumu wa Marekani kwa Sudan, Tom Perriello, amesema idadi ya waliofariki inaweza kufikia 150,000.

Upatikanaji wa chakula, malazi, maji salama ya kunywa na huduma za afya umesalia kuwa mgumu na kutajwa kuwa mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani.

"Nimepoteza watu wengi"

Shamu Abker
Maelezo ya picha, Shamu Abker alikimbia kijiji chake kwa sababu ya makombora

"Tunakabiliwa na uhaba wa chakula," anasema Shamu Abker, ambaye asili yake ni eneo la Tawila magharibi mwa El Fasher.

"Ulaji wa chakula kwa kawaida hupungua hadi mlo mmoja kwa siku, ambacho ni kifungua kinywa," anasema.

Makombora yalimlazimisha kutoroka kijijini kwao na wanawe. Wakiwa wanasafiri kwenye barabara mbovu kukwepa vizuizi jeshi, mtoto mmoja wa Shamu alifariki kwa ajali ya gari. Shamu mwenyewe alipoteza uwezo wa kuona kwa kukosa huduma ya matibabu.

"Nilipoteza watu wengi kutokana na vita siwezi kuwaorodhesha wote," anasema.

“Nyumbani kwangu hakuna usalama. Sasa ninakaa chini ya mti na chini ya hema hili, nikitamani nyumba yangu."

Madina Yahya, aliyewasili El Fasher na familia yake miezi sita iliyopita, anapitia hali kama hiyo ya kukata tamaa.

"Watoto wetu ni waathiriwa wa vita. Tumechoshwa na hali hii,” anasema.

Katika kambi ya watu waliokikimbia makazi yao, aliona uwepo wa uhusiano mbaya kati ya wale wanaohitaji msaada na wale wanaoutoa. Anasema kila watu wapya wakiwasili - mzigo huonekana umeongezeka kwenye rasilimali ambazo tayari ni haba.

"Wanaendelea kutuita wapya au wakongwe kama vile sisi ni mapipa," anasema kuhusu jinsi watu wanavyoitwa.

"Hawana uwezo wa kusaidia yeyote kati yetu. Sote tumekimbia, lakini wanaendelea kutofautisha kati ya wa zamani na wapya, "anasema.

Madina pia ameelezea hofu yake kuhusu mahitaji maalumu ya binti zake.

"Tuna wasichana wadogo, ni vijana na ni watoto. Kuna wasichana wadogo wanaobalehe na wanahitaji vitu ambavyo hatuna uwezo wa kuwapatia, hivyo inawapa watu fursa ya kuwatendea vibaya,” anasema.

Mbali na mashambulizi ya mabomu, mapigano, mauaji ya kiholela, uporaji na uchomaji moto ambao umetokea wakati wa vita hivi, Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya haki za binadamu yameeleza juu ya unyanyasaji wa kijinsia ulioenea dhidi ya wanawake na wasichana.

"Vikosi vya RSF na wanamgambo washirika wanahusika kwa kiasi kikubwa na ubakaji na uhalifu mwingine wa kivita," Human Rights Watch ilisema katika ripoti iliyotolewa Agosti mwaka jana.

'Hakuna amani'

Raia katika eneo la Darfur wanasema wanaishi kwa hofu huku kukiwa na maeneo machache sana ya kukimbilia na upatikanaji mdogo wa misaada.

Shirika la kimataifa la misaada la Oxfam linasema, watu waliokimbia makazi yao wako katika hatari ya kuwa mateka katikati ya vita vya vikosi hivyo viwili.

"Wananchi wanaoishi mji huu wanatoka katika jumuiya zote za Darfur. Kutakuwa na waathirika kutoka kila jamii ya Darfur, Waarabu na Waafrika, kama pande zinazozozana zitapigania udhibiti wa El Fasher,” anasema Toby Harward, mtaalamu wa haki za binadamu.

Wakati vita vya El Fasher vikiendelea, hakuna matumaini ya usitishaji mapigano.

"Hakutakuwa na mazungumzo, hakuna amani, na hakuna kusitisha mapigano isipokuwa baada ya kuushinda uasi huu," alisema kamanda mkuu wa jeshi, Al-Burhanon, Mei 7.

Internally displaced women wait in a queue to collect aid from a group at a camp in Gadaref on May 12, 2024.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Ni vigumu kwa raia kupata misaada huko Darfu

Licha ya mipango ya Saudi Arabia, Jumuiya ya Maendeleo ya Kikanda (IGAD), Umoja wa Afrika na Marekani, juhudi za kujadili makubaliano ya amani hadi sasa hazijafaulu.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), zaidi ya theluthi moja ya wakazi wa Sudan wanakabiliwa na janga la njaa na watu milioni 8.7 wamekimbia makazi yao.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah kuhaririwa na Yusuf Jumah