Mzozo wa Sudan: Mgogoro wa Sudan unaweza kuisha kwa njia hizi tatu

Helikopta

Chanzo cha picha, AFP

Licha ya kusitishwa kwa mapigano kwa muda na kudorora kwa mapigano nchini Sudan, ni wachache wanaoamini kuwa huu ndio mwisho wa mzozo huo na kuna maswali kuhusu jinsi mambo yanavyoweza kutokea katika wiki na miezi michache ijayo.

BBC imekuwa ikizungumza na baadhi ya wachambuzi wa Sudan kuangalia matukio yanayoweza kutokea.

1) Ushindi wa haraka wa jeshi

Hili linaonekana kutowezekana kwani pande zote mbili zina nguvu zinazozipendelea katika awamu tofauti za migogoro.

Ni utawala wa kijeshi ambao umegawanyika vipande viwili - huku wapinzani wote wakidai ushindi wa mapema.

• Jeshi linaongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, rais wa junta

• Kikosi cha Wanajeshi wa (RSF) kinaongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama Hemedti, makamu wa rais wa baraza tawala la jeshi.

Inaonekana, kutokana na ushahidi kutoka kwa wale wanaoondoka katika mji mkuu, Khartoum, kwamba RSF ina uwezo wa ziada dhidi ya jeshi katika jiji hilo.

Ni jeshi linalotembea, la msituni ambalo linaweza kukabiliana haraka zaidi kuliko wapinzani wao wa kawaida. Uwezo huu umewapendelea katika vita vya katikati mwa jiji la Khartoum.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini jeshi linadhaniwa kuwa na uwezo wa kufikia silaha nzito zaidi , iwe mizinga au nguvu ya angani.

Huku wanadiplomasia na wageni wakiondoka mjini, inahofiwa kuwa huenda hivi karibuni silaha hizo zikaelekezewa jiji la Khartoum.

"Katika sehemu kubwa za jiji RSF imewajaza wapiganaji wake katika maeneo ya makazi," anasema Alan Boswell kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Migogoro (ICG).

"Kimsingi wanalithubutu jeshi kuharibu mji wake wenyewe. Mtu anaweza kudhani [jeshi halitaki] kuiangamiza Khartoum, lakini kwao haya ni mapambano yaliyopo."

Pande zote mbili pia zinaweza kuomba msaada kutoka kwa waungaji mkono kutoka nje, ambayo inaweza kusaidia kurefusha mapigano, kulingana na mchambuzi huru wa Sudan Jonas Horner.

Jeshi linadhaniwa kuungwa mkono kikamilifu na nchi yenye nguvu ya Misri - ingawa rasmi jirani huyo wa kaskazini amesalia kutoegemea upande wowote.

RSF, wakati huo huo, inaungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kundi la mamluki la Wagner la Urusi na wanamgambo wengine wa kikanda .

2) Mgogoro wa muda mrefu

th

Kuna njia nyingi mzozo huu unaweza kuibuka, hakuna hata moja nzuri kwa watu wa Sudan.

"Kwa hakika ina vipengele vyote vya kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu," anafikiri mwandishi wa BBC Mohanad Hashim, ambaye mwenyewe ni Msudani.

"Kumekuwa na jitihada nyingi kutoka kwa wale watiifu kwa utawala wa zamani wa Omar al-Bashir na Chama chake cha National Congress Party, ambao wana itikadi ya Kiislamu."

Bashir aliondolewa madarakani na jeshi mwaka 2019 baada ya maandamano makubwa ya mitaani. Wakati wa utawala wake wa miaka 30, wanamgambo wengi wa kikabila waliokuwa na silaha za kutosha waliibuka.

"Bashir alifanya kazi kwa bidii sana kuunda migawanyiko hii kati ya makabila haya tofauti, ambayo yalianzisha wanamgambo," anasema Bw Horner.

"Pengo la usalama lililoanzishwa [kwa kuondolewa kwake] kumemaanisha kuwa pameibuka tena makundi ya wanamgambo kwa sababu wamelazimika kusimamia usalama wao wenyewe."

Iwapo wanamgambo watachukua upande wowote, mzozo huu unaweza kubadilika na kuwa kitu hatari zaidi ambacho kinaweza "kupanua mzozo huu na kufanya iwe vigumu kuuzuia," Bw Horner anaamini.

Kipengele cha kikabila kimewatia wasi wasi waangalizi wengi. Pia ni jambo ambalo majenerali wote wawili wametafuta kugeuza kwa faida yao.

"Kabla ya vita kuanza, tuliona Hemedti na Jenerali Burhan wakichochea migawanyiko ya kikabila, wakihutubia ngome zao," anasema Hashim.

Ramani

Tunaweza kuona hali ambapo RSF, ikiwa imesajili wapiganaji katika maeneo yaliyotengwa nchini, inajaribu kujionyesha kama kundi la kuunganisha maeneo ya vijijini," anasema Ahmed Soliman wa kitengo washauri wabobezi cha Chatham House.

Hii inaweza kugawanya nchi na RSF kuhamia "kwenye ngome yake ya Darfur kujaribu na kujihami tena na kuwapata wapiganaji zaidi’

3) Mkataba wa amani

Wanadiplomasia wanajaribu kuwafanya majenerali hao wawili wakubaliane kuongeza muda wa usitishaji mapigano lakini inapokuja suala la kuanza mazungumzo ya amani, hakuna anayefikiria kuwa huenda yakaanza hivi karibuni.

Pia kuna swali la nini kinaweza kukubalika kwa Wasudan wa kawaida.

Hashim alikuwa Khartoum wakati wa mapinduzi ya 2019 na amewatazama majenerali hao mara kwa mara wakishindwa kukabidhi madaraka kwa raia, na kufikia kilele katika mapinduzi ya 2021.

"Wamekuwa na mwaka mmoja na nusu baada ya mapinduzi ambapo walishindwa kuendesha nchi. Je, watu hawa wawili wanaweza kufikia makubaliano gani ambayo yanaweza kuwa mazuri kwa Wasudani?" anauliza.

Kila mtu anaonekana kukubaliana kwamba mpango utatoka tu kwa shinikizo la nje.

"Wazo kwamba tutaweza kumaliza uhasama bila nguvu kubwa, shinikizo la kisiasa, shinikizo la kiuchumi kutumiwa na washirika wa kikanda, kama vile Misri, UAE, Saudi Arabia, ni vigumu kufikiria," anasema Bw Boswell.

Mgogoro wa muda mrefu unaweza kuathiri miundombinu mingi huko Khartoum

Chanzo cha picha, AFP

Shida ni kwamba kuna masilahi mengi yanayoshindana, mengi yao yanahusiana moja kwa moja.

Bw Horner anaamini kwamba "mamlaka za kikanda zina upendeleo fulani kwa mwanajeshi au mtu mwenye nguvu kuchukua usukani wa nchi. Hizi ni habari mbaya kwa mashirika ya kiraia."

Hata hivyo, kuna hofu kwamba ikiwa mazungumzo ya amani hayataanza hivi karibuni - kama inavyopendekezwa katika nchi jirani ya Sudan Kusini - mzozo huo unaweza kutapakaa na kufanya kuwa vigumu kupata suluhu.

"Bado kuna dirisha la mazungumzo ya amani. Changamoto ni kwamba hakuna nia ya kuacha uhasama kutoka pande zote mbili. Na kwa bahati mbaya mtazamo wa muda mfupi wa kidiplomasia unabaki katika kujihusisha na kile ambacho majenerali wawili wanataka, kwa gharama ya matarajio ya demokrasia ya kiraia," anasema Bw Soliman wa Chatham House.

Tatizo ni kwamba wanachotaka wanaume wote wawili kinakinzana moja kwa moja sio tu na wengine, lakini muhimu zaidi na matakwa ya watu wa Sudan.

Hivi ni vita kuhusu mamlaka, udhibiti na utajiri, ambao kila upande unapigania kwa udi na uvumba.

Kuna gharama kubwa ya kulipwa kwa tamaa ya watu hawa wawili, na ni watu wa Sudan ambao watailipia gharama hiyo.