Wagner: Mamluki wa Urusi wamekuwa wakifanya nini Sudan?

Chanzo cha picha, TELEGRAM
Kikosi cha mamluki cha Wagner cha Urusi kinashutumiwa kuwa na uhusiano tofauti wa kibiashara na kijeshi na Sudan, lakini kundi hilo linakanusha kuhusika kwa vyovyote vile katika mzozo wa sasa nchini humo.
Yevgeny Prighozin - ambaye ana uhusiano wa karibu na Rais Vladimir Putin - amesema kwamba "hakuna hata mpiganaji wa Wagner PMC [kampuni ya kijeshi ya binafsi] ambaye amekuwepo nchini Sudan" kwa zaidi ya miaka miwili.
Hatujapata ushahidi kuwa mamluki wa Urusi kwa sasa wako nchini. Lakini kuna ushahidi wa shughuli za awali za Wagner nchini Sudan, na shughuli za Bw Prighozin nchini humo zikilengwa na vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya.
Mikataba ya uchimbaji dhahabu
Mnamo mwaka wa 2017, Rais wa wakati huo wa Sudan Omar al-Bashir alitia saini msururu wa mikataba na serikali ya Urusi alipokuwa ziarani Moscow.
Haya yalijumuisha makubaliano ya Urusi kuanzisha kituo cha jeshi la majini katika Bandari ya Sudan kwenye Bahari Nyekundu, pamoja na "mikataba ya makubaliano ya uchimbaji madini ya dhahabu kati ya kampuni ya Urusi ya M Invest na Wizara ya Madini ya Sudan".
Hazina ya Marekani inadai kuwa M Invest na kundi tanzu, Meroe Gold, ni wahusika wa shughuli za Kundi la Wagner nchini Sudan, nchi ya tatu kwa uzalishaji wa dhahabu barani Afrika.
"Yevgeniy Prigozhin na mtandao wake wananyonya maliasili ya Sudan kwa manufaa binafsi na kueneza ushawishi mbaya kote ulimwenguni," Waziri wa Hazina wa wakati huo Steven Mnuchin alisema mnamo 2020.
Wote M Invest na Meroe wamekumbwa haswa na vikwazo vya Marekani.
Kulingana na uchunguzi wa CNN, dhahabu imesafirishwa nchi kavu hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako Wagner inajulikana kufanya kazi - mauzo ya nje ambayo hayajarekodiwa katika data rasmi ya biashara ya Sudan.
Kiasi kikubwa cha dhahabu pia kimetoroshwa kupitia mtandao wa viwanja vya ndege vya kijeshi, kulingana na ripoti ya mwaka jana katika Daily Telegraph.
Ni nini kingine ambacho Wagner wamekuwa wakifanya huko Sudan?
Tangu 2017, vyanzo vya Urusi na kimataifa vimechapisha picha zinazoonekana kupata mamluki wa Urusi ndani ya Sudan.
Haya yanasemekana kuwaonesha wakifanya kazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Sudan au kudaiwa kusaidia vikosi vya usalama kukabiliana na maandamano. BBC haijathibitisha picha hizi kwa kujitegemea.
Mnamo mwaka wa 2021, kituo cha Telegram kilichounganishwa na Wagner kilichapisha picha zinazoonesha kamanda mkuu wa Wagner ambaye hakutajwa jina akiwatunuku wanajeshi wa Sudan katika hafla iliyofanyika miaka miwili mapema.

Chanzo cha picha, TELEGRAM
Na mnamo Julai 2022, kituo hiki kilisambaza video inayodaiwa kuwaonesha mamluki wa Wagner wakifanya mazoezi ya kutua kwa miamvuli kwa vikosi vya Sudan.
Chanzo hichohicho kilihusishwa na wasifu wa Instagram wa mamluki wa Urusi ambaye jina lake halikujulikana, akijiita "mfanyakazi huru" na kushiriki hadithi za ushujaa wake nchini Sudan katika machapisho ya kuanzia Agosti na Oktoba 2021.
Katika filamu ya 2020 ya propaganda ya Wagner, Sudan iliangaziwa kama moja ya nchi ambapo mamluki wanafanya kazi.
Wagner imekuwa na ushawishi kiasi gani?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hazina ya Marekani inasema Kundi la Wagner limefanya "operesheni za kijeshi, msaada wa kuhifadhi tawala za kimabavu, na unyonyaji wa maliasili".
"Hapo awali, mwaka wa 2018, walikuwa na wanaume wapatao 100 wanaofundisha kikamilifu vikosi vya kijeshi vya Sudan, na uhusiano umeongezeka kutoka hapo," anasema Dk Joana de Deus Pereira wa Taasisi ya Huduma ya Royal United yenye makao yake makuu nchini Uingereza.
Ripoti za vyombo vya habari vya Sudan zinasema kwamba idadi hiyo iliongezeka na kufikia takriban 500, na wengi wao waliwekwa kusini-magharibi karibu na Um Dafuq, karibu na mpaka wa Sudan na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).
Gazeti la Sudan Tribune liliripoti kuwa wakati Rais Bashir alipokabiliwa na maandamano ya watu wengi mwaka 2019, "wapiganaji wa Urusi" walitumwa kuchunguza maandamano dhidi ya serikali pamoja na idara za kijasusi na usalama za Sudan, ingawa hilo lilikataliwa na mamlaka ya Sudan.
Kundi la Wagner lilibuni kampeni zake za vyombo vya habari ili kumsaidia Rais Bashir kusalia madarakani, anasema Dk Samuel Ramani, mwandishi wa kitabu kuhusu shughuli za Urusi barani Afrika.
"Waandamanaji walishutumiwa kuunga mkono Israeli na kupinga Uislamu," anasema.

Chanzo cha picha, AFP
Hii ilisababisha msuguano na vikosi vya usalama vya rais mwenyewe, na kwa hivyo Wagner Ikabadilisha uungwaji mkono wake kwa mtu aliyemwondoa - Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.
"Wakati Wizara ya Mambo ya Nje huko Moscow ikipinga mapinduzi hayo, Prigozhin na Kundi la Wagner walikaribisha unyakuzi wa al-Burhan," anasema Dk Ramani.
Kwa mujibu wa Dk Ramani, ilikuwa mwaka wa 2021 na 2022 ambapo Kundi la Wagner liliongeza uhusiano wake na Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF), ambacho kwa sasa kinapambana na jeshi la kawaida la Sudan, linaloongozwa na Jenerali Burhan.
Bw Prigozhin alikuwa na nia ya kutafuta dhahabu zaidi kupitia migodi iliyopatikana hivi karibuni na kiongozi wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana sana kama Hemedti.
Mwaka jana, Hemedti alitembelea Moscow, akisema anatumai kuimarisha uhusiano kati ya Sudan na Urusi.
Hata hivyo, Taasisi ya Kholood Khair Think-tank , kuhusu masuala ya Sudan, inaamini Kundi la Wagner halichagui upande katika mzozo wa sasa.
"Wagner imekuwa na uhusiano na makampuni ya General al-Burhan na makampuni ya Bw Hemedti kwa viwango tofauti na kwa njia tofauti," anasema.
Uwepo wa Wagner kwingineko barani Afrika
Wapiganaji wa Wagner wameripotiwa kuwepo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kwa miaka kadhaa, wakilinda migodi ya almasi ya nchi hiyo, pamoja na Libya na Mali.
Uchunguzi wa BBC mwaka 2021 ulipata ushahidi wa kuhusika kwao katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya kutoka kwa kifaa cha kidijitali kilichoachwa na mpiganaji wa Wagner na kutokana na kuzungumza na wanajeshi na raia wa Libya.
Nchini Mali, serikali imeigeukia Wagner kusaidia kupambana na wanamgambo wa Kiislamu, ingawa haijawahi kukiri rasmi uwepo wa kundi hilo.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limewashutumu mamluki wa Urusi kwa unyanyasaji mkubwa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mali, yakiwemo mateso na mauaji.












