Mgogoro wa Sudan: Kwa nini Misri ipo katika njia panda juu ya mapigano Sudan?

Chanzo cha picha, Reuters
Katika mfululizo wetu wa barua kutoka kwa waandishi wa habari wa Kiafrika, Magdi Abdelhadi wa Misri anaangalia hali tete ya mgogoro wa Sudan kwa nchi yake.
Jirani wa Sudan mwenye nguvu upande wa kaskazini anatazama kile kinachoendelea huko kwa uwoga, lakini Misri inaonekana kuwa katika njia panda , haiwezi kuchukua msimamo wa wazi.
Kwa hakika, inajipata katika hali ya kutatanisha ingawa kuna uwezekano wa kubeba mzigo wa mzozo wa muda mrefu.
Misri iko karibu na moja ya pande mbili katika mapigano - jeshi la Sudan. Wakati huo huo, upande wa pili, Kikosi cha Msadaa wa Dharura au RSF chini ya Mohamed Hamdan "Hemedti" Dagalo, kinaaminika kuungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambao ni wafadhili wakuu wa kifedha wa Misri.
Misri tayari inawakaribisha Wasudani milioni tano, ambao wanakimbia umaskini au mapigano.
Nchi hizo mbili zina makubaliano ya uhuru wa uhamiaji ambayo hutoa uhuru kwa watu wao kuhamia pande zote mbili - kuishi na kufanya kazi.
Katika miaka ya hivi karibuni, imekuwa vigumu kutotambua ongezeko linaloonekana la idadi ya wahamiaji wa Sudan katika mji mkuu wa Misri.
Unakutana nao kila mahali mjini Cairo - kama wafanyakazi katika maduka makubwa au maduka madogo ya mboga, kama watumishi wa nyumbani au wafanyakazi katika mikahawa.
Ongezeko hilo ni la kushangaza sana hivi kwamba katika mwaka mmoja tu, vituo viwili vya mabasi ya dharura vilichipuka katikati mwa Cairo.
Wamisri wanayataja haya kwa mzaha kama "uwanja wa ndege wa Sudan".
Kijana mmoja wa Sudan ananiambia inachukua siku tatu kufika Khartoum katika safari ya gharama ya pauni 800 za Misri ($26; £21).
Kuna wastani wa safari 25 za kila siku za basi kati ya Khartoum na Cairo, zinazofikia takriban safari 37,000 kila mwezi.
Idadi hii inaweza kuongezeka kwa urahisi ikiwa mapigano hayataisha hivi karibuni.

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini hiyo sio sababu pekee ya amani na utulivu nchini Sudan ni muhimu kwa Misri.
Utawala dhaifu huko Khartoum, au kuibuka kwa uongozi mbadala wa kisiasa ambao hasimu kwa Cairo, kunaweza kuwa na madhara makubwa zaidi kaskazini.
Misri kwa muda mrefu imekuwa ikiiona Sudan kama mshirika muhimu katika mzozo wake wa muda mrefu na Ethiopia kuhusu Bwawa la Renaissance lenye utata .
Misri imeelezea mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa maji ya Mto Blue Nile kaskazini mwa Ethiopia kama tishio lililopo kwa sababu ya uwezo wake wa kudhibiti mtiririko wa mto huo ambao ni muhimu kwa maisha nchini humo.
Licha ya umuhimu mkubwa wa Sudan kwa masilahi ya kimkakati ya Misri, serikali ya Rais Abdul Fattah al-Sisi inaonekana kuwa imejitahidi kutoka na jibu la kuaminika kwa machafuko huko Khartoum.
Ni baada ya kubainika kuwa baadhi ya wanajeshi wake wamekamatwa na Kikosi cha RSF ndipo jeshi hilo lilipotoa taarifa fupi.
Siku mbili baadaye Rais Sisi alisema kuwa Misri haitaunga mkono upande wowote katika mzozo huo na akajitolea kuwa mpatanishi.
Lakini wachache waliamini ukweli kuhusu msimamo huu wa kutoegemea upande wowote.
Imekuwa dhahiri kwa muda kwamba Misri ilikuwa ikishirikiana kwa karibu na jeshi la Sudan - wanajeshi waliokuwa wamekamatwa walikuwa nchini humo kama sehemu ya mazoezi ya pamoja.
Tangu wakati huo wamesharudishwa nyumbani .
Lakini unaweza kuelewa ni kwa nini ni vigumu kwa Misri kutangaza hadharani inaegemea wapi.
Hii kwakiasi fulani inatokana na utata wa mazingira ya kisiasa nchini Sudan na kufanana kabisa kwa matukio ya hivi majuzi katika nchi hizo mbili.
Misri na Sudan zote zimekuwa na mapinduzi yao.
Hosni Mubarak nchini Misri mwaka 2011, na Rais Omar al-Bashir nchini Sudan mwaka 2019. Katika visa vyote viwili jeshi lilichukua jukumu kubwa katika kumuondoa mkuu wa nchi.
Nchini Misri, wanajeshi wamezuia mpito kuelekea demokrasia. Ndio maana kuna hofu inayokubalika miongoni mwa baadhi ya raia wa Sudan kwamba jeshi la Misri lingehimiza jeshi la Sudan kufanya vivyo hivyo.
Hadharani, jeshi la Sudan linaendelea kusema kwamba wanajeshi wake hawatazuia kipindi cha mpito, lakini vuguvugu la maandamano lililoongoza mapinduzi mwaka 2019, Vikosi vya Uhuru na Mabadiliko, haziwaamini na wanaogopa kuingilia Misri.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hatua inazoweza kuchukua Misri zimepunguzwa zaidi na ukweli kwamba nchi hiyo iko katika mgogoro wa kiuchumi ambao haujawahi kutokea.
Sarafu yake imepoteza karibu nusu ya thamani yake dhidi ya dola ya Marekani katika mwaka uliopita.
Pia kuna kasi kubwa ya mfumuko wa bei na umaskini unaoongezeka huku kukiwa na hofu kwamba Misri inaweza kushindwa kulipa deni lake kubwa la nje baadaye mwaka huu.
Mmoja wa wafadhili wakuu wa Rais Sisi katika Ghuba, UAE, inajulikana kuunga mkono RSF.
Kwa hivyo ni vigumu kidogo kwa Bw Sisi kuonekana akichukua upande tofauti wa mzozo huo.
Kwa utawala wa Misri kila hatua ni hatari kwa maslahi yake.
Baada ya kuunga mkono upande mmoja katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Libya - Jenerali Khalifa Haftar, ambaye alishindwa kutawala - Cairo lazima iwe imejifunza kutokana na kosa hilo.
Hatimaye ingawa nchi inataka kuona "utulivu, usalama na uendelevu kwa Wasudan ambao wanatumikia maslahi ya taifa letu", Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Misri Nabil Fahmy aliiambia BBC.
Lakini utulivu mara nyingi umetumika kama kisingizio kwa tawala za kimabavu kama zile zinazotawala nchini Misri kukandamiza upinzani.
Hili ndilo jambo ambalo tabaka la kisiasa la Sudan linahofia wakati jirani yao wa kaskazini anapozungumza kuhusu "maslahi yake ya kitaifa".












