Mgogoro wa Sudan: Majenerali wanaopigania hatima ya Sudan

Chanzo cha picha, Getty Images
Msururu wa milipuko, anga inayotawaliwa na moshi mweusi, hali ya kila siku ya hofu na kutokuwa na uhakika huku risasi, roketi na uvumi ukizagaa.
Maisha katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, na katika maeneo mengine mengi ya nchi, yamechukua mkondo wa ghafla na wa kustaajabisha na kuwa mbaya zaidi.
Kati kayo ya zogo hili ni majenerali wawili: Abdel Fattah al-Burhan, kiongozi wa Kikosi cha Wanajeshi wa Sudan (SAF), na Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti, mkuu wa Kikosi cha Dharura (RSF).
Wawili hao walifanya kazi pamoja, na kufanya mapinduzi pamoja - sasa vita vyao vya kuwania uongozi vinasambaratisha Sudan.
Uhusiano kati ya wawili hao ni wa tangu jadi.
Wote wawili walitekeleza majukumu muhimu katika mapambano dhidi ya waasi wa Darfuri, katika vita vya wenyewe kwa wenyewe katika eneo la magharibi mwa Sudan vilivyoanza mwaka 2003.
Jenerali Burhan aliinuka kudhibiti jeshi la Sudan huko Darfur.
Hemedti alikuwa kamanda wa mojawapo ya wanamgambo wengi wa Kiarabu, ambao kwa pamoja walijulikana kama Janjaweed, ambao serikali iliwatumia kuwaangamiza kikatili makundi mengi ya waasi wa Darfuri wasiokuwa Waarabu.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Majak D'Agoot alikuwa naibu mkurugenzi wa Huduma za Kitaifa za Ujasusi na Usalama wakati huo - kabla ya kuwa naibu waziri wa ulinzi nchini Sudan Kusini ilipojitenga mwaka 2011.
Alikutana na Jenerali Burhan na Hemedti huko Darfur, na akasema walifanya kazi vizuri pamoja. Lakini aliiambia BBC kwamba aliona dalili ndogo kwamba mmoja kati yao atainuka hadi kilele cha serikali
Hemedti alikuwa tu kiongozi wa wanamgambo "akitekeleza jukumu la kukabiliana na waasi, kusaidia jeshi", wakati Jenerali Burhan alikuwa mwanajeshi kitaaluma , ingawa "kwa matarajio yote ya kikosi cha maafisa wa Sudan, chochote kiliwezekana".
Jeshi limekuwa likiendesha Sudan kwa sehemu kubwa ya historia yake ya baada ya uhuru.
Mbinu za serikali huko Darfur, ambazo ziliwahi kuelezewa na mtaalam wa Sudan Alex de Waal kama "kukabiliana na waasi kwa bei nafuu", ilitumia wanajeshi wa kawaida, wanamgambo wa kikabila na nguvu za anga kupambana na waasi - bila kujali kuhusu mauaji ya raia.
Darfur imetajwa kuwa mauaji ya kwanza ya halaiki katika Karne ya 21, huku Janjaweed wakishutumiwa kwa mauaji ya kikabila na kutumia ubakaji mkubwa kama silaha ya vita.
Hatimaye Hemedti akawa kamanda wa kile kinachoweza kuelezewa kama kilichotokana na Janjaweed, RSF yake.

Chanzo cha picha, Getty Images
Nguvu ya Hemedti iliongezeka sana mara tu alipoanza kusambaza wanajeshi kupigania muungano unaoongozwa na Saudia huko Yemen.
Mtawala wa wakati huo wa kijeshi wa Sudan, Omar al-Bashir, alikuja kumtegemea Hemedti na RSF kama mkandarasi dhidi ya vikosi vya kawaida vya kijeshi, kwa matumaini kwamba itakuwa vigumu sana kwa kundi lolote lenye silaha kumuondoa madarakani.
Mwishowe - baada ya miezi kadhaa ya maandamano - majenerali walikusanyika pamoja ili kumpindua Bashir, mnamo Aprili 2019.
Baadaye mwaka huo, walitia saini makubaliano na waandamanaji kuunda serikali inayoongozwa na raia inayosimamiwa na Baraza Kuu, chombo cha pamoja cha kiraia na kijeshi, na Jenerali Burhan akiwa mkuu wake, na Hemedti kama naibu wake.
Ilichukua miaka miwili - hadi Oktoba 2021 - wakati jeshi liliposhambulia, na kuchukua madaraka na Jenerali Burhan tena mkuu wa serikali na Hemedti tena naibu wake.
Siddig Tower Kafi alikuwa mwanachama wa kiraia wa Baraza Kuu, na hivyo mara kwa mara alikutana na majenerali wawili.
Alisema haoni dalili zozote za kutoelewana hadi baada ya mapinduzi ya 2021.
Kisha "Jenerali Burhan alianza kurejesha Waislamu wenye misimamo mikali na watawala wa zamani kwenye nyadhifa zao za zamani", aliiambia BBC.
"Ilionekana wazi kuwa mpango wa Jenerali Burhan ulikuwa kurejesha utawala wa zamani wa Omar al-Bashir madarakani."
Bw Siddig anasema kwamba hapo ndipo Hemedti alipoanza kuwa na mashaka, kwani alihisi wapambe wa Bashir hawakuwahi kumwamini kabisa.
Siasa za Sudan siku zote zimekuwa zikitawaliwa na watu ambao kwa kiasi kikubwa wanatoka katika makabila yanayozunguka Khartoum na Mto Nile.
Hemedti anatoka Darfur, na watawala wa Sudan mara nyingi huzungumza juu yake na askari wake kwa maneno ya dharau, kama "wasiofaa kutawala serikali.
Katika kipindi cha miaka miwili au mitatu iliyopita, amejaribu kujiweka kama mtu wa kitaifa, na hata kama mwakilishi wa maeneo ya pembezoni yaliyotengwa - akijaribu kuunda ushirikiano na makundi ya waasi huko Darfur na Kordofan Kusini ambayo hapo awali alikuwa amepewa jukumu la kuyaangamiza.
Pia amezungumza mara kwa mara juu ya hitaji la demokrasia licha ya vikosi vyake kuzima kikatili maandamano ya raia hapo awali.
Mvutano kati ya jeshi na RSF ulikua kama tarehe ya mwisho ya kuunda serikali ya kiraia inakaribia, ililenga suala la jinsi RSF inapaswa kuunganishwa tena katika vikosi vya kawaida vya kijeshi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Na ndipo mapigano yakaanza, yakihusisha RSF dhidi ya SAF, Hemedti dhidi ya Jenerali Burhan, kwa ajili ya udhibiti wa taifa la Sudan.
Kwa namna moja, angalau, Hemedti amefuata nyayo za mkuu huyo wa jeshi , ambaye sasa anapigana dhidi yake - katika miaka michache iliyopita, amejenga himaya kubwa ya biashara, ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika migodi ya dhahabu na sekta nyingine nyingi.
Jenerali Burhan na Hemedti wote wamekabiliwa na wito kutoka kwa viongozi wa kiraia na wahasiriwa wa mzozo wa Darfur na mahali pengine kushtakiwa kwa madai ya unyanyasaji.
Uhasama ni mkubwa sana, na kuna sababu nyingi kwa hawa waliokuwa washirika-waliogeuka-maadui-wakali kutorudi nyuma.















