Sudan: Jinsi vikosi hasimu vya jeshi Sudan vinavyotoa madai ya ushindi yanayopingana

Chanzo cha picha, Getty Images
Haijabainika ni nani anayeongoza nchini Sudan.
Masimulizi ya kutatanisha yameibuka kufuatia mapigano mabaya ambayo yalizuka mapema Aprili 15 kati ya jeshi (SAF) na Kikosi chenye nguvu cha Msaada wa dharula (RSF) na ambayo yakiendelea.
Takriban watu 83 wameuawa, kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, wakati ghasia zikienea kutoka mji mkuu Khartoum hadi miji mingine.
Kutokana na kukosekana kwa vyombo vya habari vya serikali - ambavyo vilisimamisha ghafla matangazo ya moja kwa moja baada ya makabiliano katika makao makuu yake huko Omdurman - SAF na RSF zimetumia zaidi mitandao ya kijamii kutoa taarifa zinazokinzana.
Taarifa hizi ni pamoja na kudai udhibiti wa maeneo ya kimkakati kama vile kambi za jeshi, viwanja vya ndege na Ikulu ya rais.
Mapigano hayo yamechangiwa na mzozo wa madaraka kati ya mkuu wa jeshi na rais wa nchi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na naibu wake ambaye pia anaongoza RSF, Jenerali Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemeti.
Tangu kuteka nyara uasi maarufu wa raia walioandamana kumwondoa madarakani Rais wa muda mrefu Omar al-Bashir mnamo 2019, jeshi limeonekana kujilimbikizia madaraka.

Nani wa kulaumiwa kwa mapigano?
Vikosi hivyo viwili vimetupiana lawama na shutuma juu ya nani aliyenzisha ghasia.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Siku chache kabla ya mapigano kuanza, jeshi kubwa la RSF liliripotiwa kuonekana huko Khartoum na mji wa kimkakati wa kaskazini wa Merowe (pia Meroe na Marawi).
SAF iliita hatua hiyo ya RSF "haramu" na "hatari".
Tarehe 15 Aprili, RSF ilitoa taarifa kwenye ukurasa wake wa Facebook ikidai kwamba "idadi kubwa ya vikosi vya jeshi la Sudan viliingia katika kambi zetu za kijeshi" huko Khartoum na kuzizingira.
Hata hivyo Jeshi, lilidai kuwa RSF ilijaribu kuteka makao makuu ya jeshi la nchi katika mji mkuu.
Katika taarifa za baadaye, jeshi lilianza kuitaja RSF kama "waasi", "wanamgambo" au "wanamgambo wa waasi", na kuwadharau zaidi wanamgambo ambao ushirikiano wao katika jeshi ni kitovu cha mzozo mkubwa wa kisiasa.
RSF iliundwa mwaka 2013 hasa kutoka kwa wapiganaji wa wanamgambo mashuhuri wa Janjaweed ambao walikomesha kikatili uasi wa waasi katika eneo la magharibi la Darfur.
Jeshi lilichapisha video kadhaa kwenye ukurasa wake wa Facebook tarehe 16 Aprili zikidai kuwaonyesha wanajeshi wakivamia vituo vya RSF katika maeneo mbalimbali ya nchi, likisema "saa ya ushindi imekaribia."

Maeneo gani yameathiriwa na mashambulizi?

SAF na RSF zina kambi zilizoenea nchini kote, na kuunda vituo pinzani vya kamandi ambavyo mara kwa mara vimedhoofisha mipango ya kuunganisha majeshi ya Sudan.
Kwa mujibu wa tovuti ya binafsi ya Sawt al-Hamish tarehe 15 Aprili, RSF ilidai kuwa imemkamata kamanda mkuu wa jeshi na makao makuu katika majimbo ya Darfur. Pia ilidai udhibiti wa anga ya nchi.
Jeshi lilikanusha hili, likisema Jeshi la Anga la Sudan "litafanya uchunguzi kamili wa maeneo ambayo waasi wa Msaada wa dharula [Vikosi] wapo".
Jeshi la wanamgambo kisha lilishutumu nchi ya kigeni ambayo haikutajwa jina kwa kulipua maeneo yake katika jimbo la Bahari Nyekundu na "kuonya juu ya kitakachotokea", kwa mujibu wa Al Jazeera.
Jeshi na RSF kila moja liliripoti makabiliano makali ya kutaka udhibiti wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum pamoja na vituo vya anga vya Merowe na Al-Obeid.
Sky News Arabia yenye makao yake UAE iliripoti tarehe 15 Aprili kwamba vikosi vya Misri vilivyokuwa Sudan kwa mazoezi ya pamoja na SAF " vilijisalimisha" kwa wanamgambo huko Merowe.
"Video [A] ilionyesha idadi ya wanaume waliovalia mavazi ya kijeshi wakiwa wamejiinamia chini na kuzungumza na wanachama wa RSF kwa lahaja ya Kiarabu ya Kimisri. [Hemeti] aliiambia Sky News Arabia kwamba wanajeshi wa Misri walikuwa salama na kwamba RSF imetoa msaada wa chakula na maji na walikuwa tayari kuwawezesha kurudi kwao," idhaa hiyo ilisema.
Kwa nini kuna uhaba wa taarifa kutoka vyombo vya habari vya Sudan?

Chanzo cha picha, Sudan TV
Televisheni na redio za serikali hazikutoa matangazo ya moja kwa moja ya matukio ya tarehe 15 Aprili lakini badala yake zilitangaza nyimbo za kizalendo na amani, pamoja na jumbe zinazohimiza umoja.
Lakini Saa 10:56 (GMT) tarehe 15 Aprili, taarifa ya moja kwa moja ilitatizwa na milio ya risasi.
Ufuatiliaji wa BBC ulibaini kuwa runinga iliendelea kupeperusha nyimbo hadi karibu 12:00 (GMT) mnamo Aprili 16 ilipoanza kuonyesha matangazo mengine.
SAF na RSF kila moja ilidai kudhibiti shirika la utangazaji kufuatia makabiliano makali katika majengo yake.
Mnamo tarehe 16 Aprili, jeshi lilichapisha video ya wanajeshi wake wakisherehekea kwa kufyatua risasi hewani mbele ya jengo ambalo lilisema ni makao makuu ya Televisheni na redio ya Sudan.
Nini kimesemwa kwenye vyombo vya habari vya pan-Arab?
Viongozi wa kijeshi wa Sudan wametoa maoni yao kuhusu vyombo vya habari vya Kiarabu, ambavyo vimekuwa na taarifa nyingi kuhusu matukio nchini mengi humo, huku wakionya juu ya hatari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Katika mahojiano ya simu na kituo kinachofadhiliwa na Saudia cha Al-Hadath TV tarehe 15 Aprili, Hemeti alimtaka Burhan ajisalimishe au akamatwe na RSF.
"Hatuna mawasiliano yoyote na Burhan. Anapaswa kujisalimisha tu. Ikiwa hatajisalimisha, tutamkamata," kamanda wa RSF alisema.
Pia alidai kuwa Burhan alikuwa amezingirwa na kwamba wanajeshi wa RSF walikuwa wamemzunguka.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Al Jazeera, Burhan alisema jeshi linadhibiti maeneo ya kimkakati, yakiwemo makao yake makuu na Ikulu ya rais.
Jeshi pia lilidai kwamba makamanda wa RSF walikuwa "wakijificha" baada ya kuhisi kushindwa, tovuti binafsi ya Baj News iliripoti tarehe 15 Aprili.
"Wanamgambo waasi wa Hemeti walikuwa wakieneza uongo na taarifa zisizo na maana kuhusu udhibiti wake wa Kamanda Mkuu [wa jeshi], Kambi kubwa za Kijeshi na Ikulu ya Rais huku askari na maafisa wake wakianguka katika mitaa ya Khartoum bila kupata matibabu wala dawa," ikilinukuu jeshi likisema katika taarifa yake.
Umoja wa Afrika unaongoza ujumbe wa viongozi kutoka nchi jirani kujaribu kutafuta suluhu na kusitishwa kwa vita kati ya majenerali wa Sudan.
Mgawanyiko zaidi katika vikosi vya jeshi la nchi hiyo unaweza kupanua mzozo na kuharibu zaidi eneo hilo.














