Je, Ukraine inahusika katika vita vya Sudan kama Urusi inavyohusika?

er

Chanzo cha picha, getty images

Maelezo ya picha, Tangu Aprili 2023, vita vya kuwania madaraka vimekuwa vikiendelea nchini Sudan kati ya Al-Burhan na Hemedti

Septemba 2023, mkutano ambao haukutarajiwa ulifanyika - Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alishuka katika Uwanja wa Ndege wa Shannon wa Ireland alipokuwa akirejea kutoka kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, ambako alikutana na kamanda wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al- Burhan.

Viongozi hao wawili walijadili masuala ya usalama wa kimataifa na vitisho kutoka kwa makundi yenye silaha yanayofadhiliwa na Urusi.

Ripoti za baadaye zilionyesha vikosi maalumu vya Ukraine vilichukua jukumu kubwa katika kufanikisha mkutano huo.

Sudan iko katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, kati ya Meja Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kamanda wa jeshi na rais wa nchi hiyo, kwa upande mmoja, na makamu wake wa zamani na kamanda wa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF), Meja Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, kwa upande mwingine.

Pia unaweza kusoma
fdvc

Chanzo cha picha, getty images

Maelezo ya picha, Mkutano kati ya Zelensky na Al-Burhan ulifichua kuhusika Ukraine nchini Sudan

Maelfu ya watu wamefariki katika mzozo huo, mamilioni wamelazimika kuacha nyumba zao au kukimbilia nchi zingine, na uchumi wa nchi umepata athari kubwa.

Ripoti zilizoibuka hivi karibuni, zinaeleza kwa nini Ukraine inaunga mkono serikali ya Sudan katika mapigano haya.

Kulingana na gazeti la Wall Street Journal, wanajeshi wa Ukraine walimsaidia Al-Burhan kukimbia mji mkuu, Khartoum, Agosti 2023 wakati Vikosi vya Rapid Support Forces vilipozingira makao yake makuu.

Gazeti hilo liliripoti, takribani wanachama mia moja wa kikosi maalumu cha Ukraine, wakiongozwa na afisa wa ujasusi anayejulikana kama "Timur," walifika Sudan baada ya mazungumzo ya simu kati ya Al-Burhan na Zelensky.

Wall Street Journal linaripoti, kikosi cha Ukraine sio tu kilitoa msaada kwa Burhan, lakini pia kilitoa ushauri uliosaidia kuanzishwa mashambulizi ya usiku dhidi ya Vikosi vya Rapid Support Forces.

Ujasusi wa Ukraine haukuthibitisha kwa BBC wala kukanusha ripoti za kuhusika kwa Kiev nchini Sudan, lakini ilibainisha hufanya shughuli zake katika maeneo tofauti, kulinda maslahi ya Ukraine."

Ukraine inafanya nini Sudan?

refd

Chanzo cha picha, getty images

Maelezo ya picha, Vikosi vya Ukraine vinaelezwa kuweko nchini Sudan kupambana na Urusi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwezi Februari, video iliibuka ikionyesha wanajeshi wa Ukraine nchini Sudan wakikagua gari la kijeshi lililolipuliwa kwa bomu likiwa na mwili wa mpiganaji kutoka Urusi ndani.

Gari hilo lilikuwa na alama ya kundi la mamluki la Urusi, Wagner. Katika video hiyo, wanajeshi wa Ukraine walionekana wakiwahoji wanajeshi wa Wagner waliokamatwa.

“Mupo hapa kwa lengo gani?” aliuliza ofisa wa Ukraine.

Askari alijibu: “Kuipindua serikali.”

Haijabainika mara moja ni lini na wapi video hiyo ilichukuliwa nchini Sudan, na BBC haikuweza kuithibitisha.

Kundi la Urusi la Wagner lilikuwepo nchini Sudan muda mrefu kabla ya kuzuka kwa mapigano kati ya jeshi la Sudan na Rapid Support Forces. Video ya kwanza ya mamluki wa Wagner nchini Sudan iliibuka 2017.

Ilisemekana wakati huo mamluki wa Urusi walihusika katika kuwafunza wanajeshi wa Sudan na kulikuwa na madai walivisaidia vikosi vya usalama vya eneo hilo kuzima maandamano.

Baada ya mauaji ya mwanzilishi wa Wagner Yevgeny Prigozhin Agosti 2023, vitengo vya Wagner vinavyofanya kazi barani Afrika, pamoja na Sudan, vilikuwa chini ya udhibiti wa Urusi.

Kwa sasa inaonekana mamluki wa Wagner wanaosaidia Rapid Support Forces, ndio walengwa wakuu wa Ukraine nchini Sudan, kulingana na mchambuzi wa BBC Monitoring, Beverley Ochieng.

Ochieng anaongeza, "ripoti ambazo zimeibuka kuhusu vikosi vya Ukraine (nchini Sudan), vinaonekana kuwalenga zaidi Wagner kuliko kutoa msaada kwa jeshi la Sudan katika kupambana na Rapid Support Forces."

efd

Chanzo cha picha, getty images

Maelezo ya picha, Wagner wanaaminika kuwaunga mkono RSF

Mkuu wa ujasusi wa kijeshi wa Ukraine, Kirilo Budanov, alidokeza baadhi ya mamluki walioko Sudan huenda walishiriki katika vita vya Ukraine.

Aliongeza, "wahalifu wote wa kivita wa Urusi ambao walipigana au watapigana dhidi ya Ukraine wataadhibiwa popote duniani."

Ukraine pia inajaribu kuhujumu mapato ya mamluki wa Urusi nchini Sudan, kulingana na Murad Batal Shishani, kutoka kituo cha utafiti chenye makao yake makuu London cha Notes on Political Violence.

Shishani anasema, "Hemedti amekuwa mshirika mkubwa wa Urusi barani Afrika, kupitia Kundi la Wagner. Anadhibiti dhahabu ambayo ni chanzo kikuu cha mapato ya Wagner.’’

Mwaka 2022, ripoti ya CNN ilidai kuhusika kwa Wagner katika uchimbaji wa dhahabu na biashara nchini Sudan, na Warusi walituma ndege 16 zilizojaa dhahabu kutoka Sudan hadi Syria.

Ikiwa uhusiano wa Ukraine na Sudan utaimarika - huenda kukazuia mipango ya Urusi ya kuanzisha kambi ya kijeshi huko Port Sudan kwenye Bahari ya Shamu.

'Adui wa adui yangu ni rafiki yangu'

fdc

Chanzo cha picha, getty images

Maelezo ya picha, Hemedti anaaminika kuwa mmoja wa watu tajiri zaidi nchini Sudan

Baadhi ya wachambuzi wanaelezea kile kinachotokea Sudan sasa ni vita vya mawakala - mzozo unaohusisha nchi tatu, kila moja ikifuata maslahi yake.

"Hemedti anaungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu na Urusi, na Burhan anapata msaada wa kifedha kutoka Saudi Arabia na msaada wa kijeshi kutoka vikosi vya Ukraine," anasema Glenn Howard, rais wa zamani wa taasisi ya utafiti ya Jamestown Foundation .

Ukraine pia inajaribu kujenga taswira kuwa ni nchi yenye uwezo wa kutishia maslahi ya Urusi popote pale, kulingana na Nicholas A. Heras, mtafiti katika Taasisi ya New Lines yenye makao yake mjini Washington.

fde

Chanzo cha picha, getty images

Maelezo ya picha, Volodymyr Zelensky wa Ukraine akiwa Mohammed bin Salman Al Saud wa Saudi Arabia

Heras anasema, ''ushirikiano kati ya Zelensky na Burhan unatokana na ile kanuni ya; adui wa adui yangu ni rafiki yangu.''

Aliongeza, "hilo ni kwa maslahi ya Ukraine kama njia ya kuthibitisha kwa jumuiya ya kimataifa kwamba Zelensky atakabiliana na Putin wakati wowote na mahali popote, sio tu Ulaya."

Hata hivyo, uwezo wa Ukraine nchini Sudan hadi sasa ni mdogo kutokana na vita vinavyoendelea vya Urusi. Kyiv inaweza kupeleka vikosi kidogo tu nchini Sudan.

Kinyume chake, uwepo wa Urusi nchini Sudan ni mkubwa zaidi.

"Urusi ina uwezo mkubwa zaidi wa kufanya uchunguzi nchini Sudan kupitia kundi la Wagner, pamoja na vikosi vya wapiganaji vinavyosaidiwa na mifumo ya mizinga na makombora ya ardhini, na hutoa vifaa kwa vikosi vya Rapid Support Forces," anasema Heras.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah