AI: Teknolojia ya kuiga sauti yaibuka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan

Chanzo cha picha, reuters
Kampeni inayotumia akili mnemba yaani akili bandia kumuiga Omar al-Bashir, kiongozi wa zamani wa Sudan, imepokea maoni ya mamia kwa maelfu kwenye mtandao wa TikTok, na kuongeza mkanganyiko mtandaoni kwa nchi iliyosambaratishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Akaunti isiyojulikana imekuwa ikichapisha kile inachosema ni "rekodi zilizovuja" za rais huyo wa zamani tangu mwishoni mwa Agosti. Kumechapishwa klipu nyingi - lakini sauti ni ya uwongo.
Bashir, ambaye ameshutumiwa kwa kupanga uhalifu wa kivita na kupinduliwa na jeshi mwaka 2019, hajaonekana hadharani kwa mwaka mmoja na anaaminika kuwa mgonjwa sana. Anakanusha tuhuma za uhalifu wa kivita.
Siri inayozunguka aliko inaongeza hali ya sintofahamu kwa nchi iliyo katika mzozo baada ya mapigano kuzuka mwezi Aprili kati ya wanajeshi, wanaoongoza kwa sasa na kundi pinzani la Rapid Support Forces.

Chanzo cha picha, reuters
Kampeni kama hizi ni muhimu kwani zinaonyesha jinsi zana mpya zinavyoweza kusambaza maudhui ghushi haraka na kwa urahisi kupitia mitandao ya kijamii, wataalam wanasema.
"Ni demokrasia ya upatikanaji wa teknolojia ya kisasa ya upotoshaji wa sauti na video ambayo inanipa wasiwasi zaidi," amesema Hany Farid, ambaye anatafiti uchunguzi wa kidijitali katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley, Marekani.
"Waigizaji wa kisasa wameweza kupotosha ukweli kwa miongo kadhaa, lakini sasa mtu wa kawaida mwenye ujuzi kidogo wa kiufundi au hata ambaye hana kabisa anaweza kutengeneza maudhui bandia haraka na kwa urahisi."
Rekodi hizo zimewekwa kwenye chaneli inayoitwa ‘Voice of Sudan’. Ujumbe huo unaonekana kuwa mchanganyiko wa klipu za zamani za mikutano ya waandishi wa habari wakati wa majaribio ya mapinduzi, ripoti za habari na "rekodi zilizovuja" zinahusisha sauti hizo na Bashir.
Sauti mara nyingi huiga kuwa ujumbe huo umechukuliwa kutoka kwa mkutano au mazungumzo ya simu, na yanasikika kama unavyoweza kutarajia kutoka kwa laini mbaya ya simu.
Ili kuangalia uhalisi wa ujumbe huo, tulishauriana kwanza na timu ya wataalam wa Sudan kutoka BBC Monitoring, Ibrahim Haithar na alituambia hazikuwa za hivi karibuni:
"Sauti inasikika kama Bashir lakini amekuwa mgonjwa sana kwa miaka michache iliyopita na kuna mashaka kuwa angeweza kuzungumza na kusikika vizuri namna hii."
Hii haimaanishi kuwa sio yeye.

Chanzo cha picha, bbc
Pia tuliangalia uwezekano wa maelezo mengine, lakini hii ni sauti ya zamani inayoibuka upya na hakuna uwezekano kuwa ni kazi ya anayeweka video hizo.
Ushahidi wa uhakika zaidi ulitoka kwa mtumiaji kwenye mtandao wa X, zamani ukijulikana kama Twitter.
Walitambua rekodi za kwanza kabisa za Bashir zilizochapishwa mnamo Agosti 2023. Inaonekana inaangazia kiongozi akimkosoa kamanda wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah Burhan.
Rekodi ya Bashir ililingana na tangazo la Facebook Live lililorushwa siku mbili mapema na mchambuzi maarufu wa kisiasa wa Sudan, anayejulikana kama Al Insirafi. Inaaminika kuwa anaishi Marekani lakini hajawahi kuonyesha uso wake kwenye kamera.
Jozi hizi hazisikiki sawa lakini maneno ni sawa, na unapocheza klipu zote mbili pamoja zinalingana kabisa.
Kulinganisha mawimbi ya sauti kunaonyesha mifumo sawa katika usemi na ukimya, anabainisha Bw Farid.
Ushahidi: Sauti ya Omar al Bashir iliigwa

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ushahidi unapendekeza kwamba programu ya kubadilisha sauti imetumika kuiga kuzungumza kwa Bashir. Programu ni zana yenye nguvu ambayo hukuruhusu kupakia kipande cha sauti, ambacho kinaweza kubadilishwa kuwa sauti tofauti.
Baada ya kuchunguza zaidi, muundo uliibuka. Tulipata takriban rekodi nne zaidi za Bashir ambazo zilichukuliwa kutoka kwa matangazo ya moja kwa moja ya mwanablogu huyo huyo. Hakuna ushahidi kwamba anahusika.
Akaunti ya TikTok ni ya kisiasa na inahitaji ujuzi wa kina wa kile kinachoendelea nchini Sudan, lakini ni nani anayenufaika na kampeni hii ni mjadala unaoendelea kwa sasa. Simulizi moja thabiti ni ukosoaji wa mkuu wa jeshi, Jenerali Burhan.
Msukumo unaweza kuwa kuwahadaa wananchi waamini kwamba Bashir amejitokeza na kujiunga katika vita. Au pia inaweza kuwa inajaribu kuhalalisha mtazamo fulani wa kisiasa kwa kutumia sauti ya kiongozi wa zamani. Lakini lengo linaweza kuwa nini, haijulikani.
Voice of Sudan imekanusha kupotosha umma na kusema kuwa hawafungamani na makundi yoyote. Tuliwasiliana na akaunti hiyo, na tukapokea jibu la maandishi likisema: "Nataka kutoa ujumbe wangu na kuelezea kile ambacho nchi yangu inapitia kwa mtindo wangu."
Jitihada za ukubwa huu za kumuiga Bashir zinaweza kuonekana kama "muhimu kwa eneo" na zina uwezo wa kuwadanganya wananchi, anasema Henry Ajder, ambaye mfululizo wa kipindi chake kwenye BBC Radio 4 ulichunguza mapinduzi ya jumla (video, picha, maandishi au sauti ambayo imetolewa kikamilifu au kwa kiasi kwa kutumia algoriti za akili mnemba) katika vyombo vya habari.
Wataalamu wa AI kwa muda mrefu wamekuwa na wasiwasi kwamba video na sauti ghushi zitasababisha wimbi la upotoshaji na uwezekano wa kuzua machafuko na kuvuruga za uchaguzi.
"Kinachotisha ni kwamba rekodi hizi pia zinaweza kutengeneza mazingira ambapo wengi hawaamini hata rekodi za kweli," anasema Mohamed Suliman, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Northeastern Civic AI Lab.
Unawezaje kugundua habari zisizo za kweli za sauti?
Kama tulivyoona kwenye mfano huu, watu wanapaswa kuhoji ikiwa rekodi inakubalika kabla ya kushirikisha wengine.
Kuangalia ikiwa ilitolewa na chanzo kinachoaminika ni muhimu, lakini ni vigumu kuthibitisha sauti, hasa maudhui yanaposambazwa kwenye programu za kutuma ujumbe. Ni changamoto zaidi wakati wa machafuko ya kijamii, kama yanayoshuhudiwa hivi sasa nchini Sudan.
Teknolojia ya kuunda algoriti zilizofunzwa kutambua sauti ya sintetiki bado iko katika hatua za awali za maendeleo, ilhali teknolojia ya kuiga sauti tayari ni ya juu kabisa.
Baada ya BBC kuwasiliana na TikTok, akaunti hiyo ilipigwa marufuku.















