Serikali kadhaa za Afrika zimezidisha ukiukaji wa Haki za Binadamu - Ripoti ya HRW

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Anita Nkonge and Maureen Nyukuri
- Nafasi, BBC News
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Serikali kadhaa katika Pembe ya Afrika na Mashariki mwa Afrika zinadaiwa kupuuza haki za binadamu za kimsingi na kutumia vurugu kukandamiza wakosoaji wao, imesema ripoti ya shirika la Human Rights Watch (HRW) iliyochapishwa wiki hii.
Ripoti hiyo ya haki za binadamu ya mwaka 2024, iliyotolewa Alhamisi wiki hii, imeorodhesha nchi kama Sudan na Kenya kati ya nchi nyingine za Afrika zinazokumbwa na changamoto kubwa za haki za binadamu.
Ripoti hii inaangalia hali ya haki za binadamu katika zaidi ya mataifa 100, ikiwa ni pamoja na nchi 25 barani Afrika.
Mkuu wa HRW kwa Afrika, Mausi Segun, alisema kuwa mwaka 2024 ulishuhudia kupungua kwa uadilifu wa "taasisi za kidemokrasia na misingi ya haki za binadamu za kimataifa na sheria za kimataifa za kibinadamu."

Chanzo cha picha, Getty Images
'Nguvu ya upinzani maarufu'
Hali ya haki za binadamu nchini Kenya imedidimia mwaka huu, hasa baada ya maandamano ya wanarika wa Gen Z kupinga serikali yaliyofanyika mwezi Juni 2024.
Maandamano haya yalilenga kuikosoa serikali kwa ongezeko la ushuru, utawala mbaya, na ufisadi unaozidi kuongezeka.
Ripoti ya HRW inaeleza kwamba "mamlaka zilishindwa kushughulikia sababu za kijamii na kiuchumi za maandamano na badala yake, walitumia mbinu za mateso, vitisho, na kukamata viongozi wa maandamano, wanaharakati, na vikundi vya kijamii vilivyoshukiwa kusaidia maandamano."
Tangu mwezi Juni, watu wasiopungua 60 wameuawa, na 82 wamepotea kulingana na Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya.
HRW pia inasema kuwa "miili ya watu wenye dalili za mateso inaendelea kupatikana katika mito, misitu, mashimo yaliyotelekezwa, na makafani."
Zaidi ya hayo, vikundi vya haki za kiraia vinaendelea kukutana na vitisho kutoka kwa serikali kwa kudaiwa kufadhili maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika kila mara.
Mgogoro Sudan waongezeka huku Umoja wa Afrika ukihangaika kulinda raia
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ripoti ya HRW imeweka kipaumbele vita vikali kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada (RSF), ambavyo vimekuwa vikigombana tangu Aprili 2023.
Vita hivi vimesababisha janga kubwa la kibinadamu, na imesababisha umaskini, njaa, na maafa makubwa.
HRW inasema kuwa pande zote mbili zinazogombana, hasa RSF, zinatenda "uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu," na ukiukwaji mwingine wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Uhalifu unaotekelezwa na RSF na washirika wake ni pamoja na mauaji ya kiholela, unyanyasaji wa kijinsia, na matumizi ya silaha nzito za milipuko katika maeneo yenye watu wengi.
Kwa upande mwingine, SAF na vikosi vyake vya washirika vimevizia maeneo ya raia, vikiharibu miundombinu ya kiraia, kutenda unyanyasaji wa kijinsia, mauaji yasiyo halali, mateso ya wafungwa, na kuharibu miili ya watu waliouawa.
Hali hii ya vurugu inasababisha Sudan kuwa na idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao duniani, ambapo zaidi ya milioni 10.8 walikimbia majumbani mwao kufikia mwezi Septemba 2024.
Vizuizi vya vita vimeenea pia katika majimbo ya katikati na mashariki, hivyo kuhatarisha maisha ya wakimbizi wengine.
Baadhi ya raia wa Sudan wanaokimbia vita wamepata hifadhi katika mataifa jirani kama vile Chad, Misri na Uhabeshi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Nyuma ya pazia nchini Eritrea
Serikali ya Eritrea inaendelea kukandamiza haki za binadamu za raia wake, ikiwa ni pamoja na ukandamizaji wa uhuru wa dini.
Ripoti ya HRW inasema kuwa hakujafanyika uchaguzi nchini Eritrea tangu ilipopata uhuru mwaka 1993, na rais asiyechaguliwa, Isaias Afwerki, bado anashikilia madaraka.
Hakuna chama kingine cha kisiasa kinachoruhusiwa, na vitendo vya kukamatwa kiholela, kutoweka kwa watu na unyanyasaji wa wanahabari, watumishi wa serikali, na wakosoaji wa serikali ni jambo la kawaida.
Ripoti inataja pia suala la kushurutishwa kwa wananchi wengi pamoja na watoto kujiunga na huduma ya kijeshi na kitaifa isiyo na ukomo, jambo ambalo limepelekea wengi kutoroka nchi hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mikakati ya ujumbe wa amani Somalia
Serikali ya Somalia inaendelea na operesheni zake za kijeshi dhidi ya kundi la kigaidi la Al-Shabab, na ripoti ya HRW inabainisha kwamba mashambulizi ya kikatili yamesababisha vifo vya mamia ya raia na kuwalazimu maelfu ya wengine kukimbia makwao.
Vikundi vya Al-Shabab, majeshi ya usalama na wanamgambo wanadaiwa kuendelea kutenda unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana, na pia kueneza unyanyasaji mkubwa kwa watoto.
Pamoja na baadhi ya mikakati ya kuboresha hali ya kibinadamu, ripoti inasema kuwa watu milioni 4.4 nchini Somalia wanahitaji msaada wa dharura wa chakula kufikia mwisho wa mwaka 2024.
Katika kusuluhisha mgogoro uliopo Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wanajiandaa kuhamasisha operesheni ya kulinda amani nchini Somalia kuwa inayoongozwa na Umoja wa Afrika, kwa lengo la kudhoofisha Al-Shabab na kulinda raia, lakini maswali bado yanajitokeza kuhusu ufadhili wa mpango huu na msaada wa vifaa.HRW imetilia shaka ufadhili huo .
Joto la kisiasa lapanda Burundi
Wanahabari ,watetezi wa haki za biandamu na viongozi wa upinzani wameendelea kutishiwa na kukamatwa nchini Burundi.
Ripoti ya HRW imeweka wazi kuwa wanachama wa kundi la vijana la chama kinachotawala,'the Imbonerakure' wamekuwa wakiendelea kuhusika kwa mauaji ya kiholela ,mateso na mashambulizi ya ghafla kwa waathiriwa kote nchini.
Muamko wa mapinduzi
Uchambuzi wa HRW pia unagusia mataifa kadhaa ya Afrika Magharibi ambayo sasa yanatawaliwa na jeshi, kama vile Burkina Faso, Mali na Niger. Inasema tawala hizi zimeendelea kukandamiza upinzani na uhuru wa kujieleza, na kuongeza kuwa juhudi nyingi za hivi karibuni za kukabiliana na ufisadi zimerudi nyuma.
HRW pia iliangazia ghasia zinazoshuhudiwa nchini Msumbiji baada ya uchaguzi ambapo mamia ya watu wameuawa.















