Watekaji waliniuliza kama nahofia kuvushwa upande wa pili wa mpaka- Maria Sarungi

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Na Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Mwanaharakati wa Tanzania Maria Sarungi amehusisha tukio la kutekwa kwake nchini Kenya na ukosoaji wake wa serikali ya Tanzania.
Akizungumza na vyambo vya habari jijini Nairobi siku moja baada ya kuachiwa alisema watekaji hao walimuuliza ikiwa anahofia kuvushwa upande wa pili wa mpaka.
''Naamini kuwa Mtanzania alihusika. Sioni kwa nini Serikali ya Kenya iwe na nia kuniteka na kujaribu kuchukua simu zangu.''alisema.
Maria Sarungi ni mkosoaji mkubwa wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, na ameishutumu serikali yake kwa kurudisha "udhalimu" nchini humo.
Wakati akiwa mikononi mwa watekaji hao anasema kuwa alihisi waliokuwa nyuma ya gari walikuwa Wakenya, kwa sababu yeye hakuzungumza Kiswahili hata kidogo.
''Nilizungumza Kiingereza kote. Lakini mtu aliyekuwa mbele alizungumza Kiswahili mara kwa mara ili kujaribu kupata ufikiaji wa simu yangu.''
Hata hivyo aliongeza kuwa hana uhakika kama utekaji huo ulikuwa ushirikiano rasmi kati ya nchi hizo mbili za Afrika Mashariki.
Watekaji hao anasema walisimama mara tano tofauti na mmoja wao alikuwa aikitoka kwenye gari kushauriana na mtu kwa simu.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwanaharakati huyo alidai kwa Mwaka 2025 kutakuwa na vitisho zaidi dhidi ya wakosoaji wa serikali kama yeye ndani na nje ya Tanzania.
''Nilihisi kana kwamba walinipeleka kwenye barabara kuu kutokana na matuta yaliyokuwa kwenye barabara hiyo,'' alisema Sarungi
Hatimaye walimuachia kwenye barabara mbovu, mahali palipokuwa na giza sana na kumwambia atembee bila kuangalia nyuma na kwamba asiseme na mtu yeyote.
Bi Sarungi aidha alisema hakuja Kenya kutafuta hifadhi nchini huma. ''Nilikuja kuanzisha biashara nchini Kenya. Nilikuwa katika harakati za kuanzisha biashara nilipopata taarifa kuwa wanataka kuniweka kizuizini, ndiyo maana nililazimika kuondoka Tanzania wakati wa utawala wa hayati Rais John Magufuli''
Amesema ataendelea kushinikiza utawala wa sheria na kuomba visa vya utekaji kukomweshwa kwani anatetea demokrasia ya kweli.
Serikali ya Kenya imesisitiza kuwa hali ya usalama nchini humo ni shwari licha ya wimbi la utekaji wa watu linaloshuhudiwa katika taifa hilo katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni. Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura amesema sio visa vyote vya watu wasiojulikana waliko ni vya utekaji nyara.
Akihojiwa na BBC kuhusu idadi ya watu waliotekwa nyara, msemaji huyo wa serikali ametaka watu kujikita katika takwimu zinazotolewa na maafisa wa usalama na sio mashirika ya kutetea haki za binadamu akihoji zinazotolewa na polisi ndizo zilizohakikiwa lakini amewaomba raia walio na taarifa kuhusu waliotekwa waziwasilishe kwa polisi.
Kumekuwa na wasiwasi kuwa Tanzania inaweza kurejea katika utawala dhalimu wa hayati Rais John Magufuli, licha ya mrithi wake Samia Suluhu Hassan kuondoa zuio la mikutano ya upinzani na kuahidi kurejesha siasa za ushindani.
Mwaka jana, makumi ya wapinzani walikamatwa na wengine kuuawa kikatili. Kiongozi mmoja mkuu wa upinzani alifariki baada ya kumwagiwa tindikali.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilielezea kuongezeka kwa visa vya kukamatatwa kwa wanaharakati wa upinzani kama "ishara mbaya" kabla ya uchaguzi wa rais wa 2025, ambao utafanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Change Tanzania, vuguvugu lililoanzishwa na Bi Sarungi, lilisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa X kwamba linamini kuwa Maria alichukuliwa na na maafisa wa usalama wa Tanzania "wanaofanya kazi nje ya mipaka ya Tanzania ili kunyawamazisha wakosoaji wa serikali."Iliongeza kuwa "ujasiri wake katika kutetea haki umemfanya kulengwa".
Mamlaka ya Tanzania mpaka sasa haijatoa tamko lolote.
Katika miezi ya hivi majuzi, Sarungi alielezaa wasiwasi wake kuhusu usalama wake, akiripoti tukio ambapo wanaume wawili wasiojulikana walionekana wakimtafuta nyumbani kwake alipokuwa hayupo.

Chanzo cha picha, EPA
Kenya ina historia ya kuwezesha serikali za kigeni kuwateka raia wao na kuwasafirisha kwa nguvu, hivyo kukiuka sheria za kimataifa.
Mwaka jana, kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, alitekwa jijini Nairobi, na watu waliodaiwa kuwa maafisa wa usalama wa Uganda, na kuvushwa mpaka na hatimaye kushtakiwa katika mahakama ya kijeshi.
Serikali ya Uganda ilisema Kenya iliwasaidia katika operesheni hiyo - lakini serikali ya Kenya ilikanusha taarifa hizo.
Roland Ebole wa Amnesty International nchini Kenya, aliambia BBC "huenda ikawa ni tukio lingine" lile lililomkuta Bw Besigye.
Kenya imekumbwa na wimbi la watu kutoweka, kufuatia maandamano ya mwaka jana yaliyoongozwa na vijana kupinga msururu wa nyongeza ya kodi.
Imehaririwa na Munira Hussein. Maelezo ya ziada na Peter Mwangangi













