'Tunaishi kwa uoga' - utekaji wawatia hofu wakimbizi na waomba hifadhi Kenya

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Wycliffe Muia
- Nafasi, BBC News, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kenya kwa muda mrefu imekuwa ikichukuliwa kuwa kimbilio salama kwa wakimbizi, lakini taswira hiyo imeanza kubadilika pole pole na kuwa mahali pa kulipiza kisasi watu wanaotafuta ulinzi dhidi mateso kutoka utawala nchini mwao, mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema.
Wasiwasi wao unakuja baada ya watu waliojifunika nyuso zao kuwateka nyara wakimbizi wanne wa Uturuki wakiwa wamewaelekezea bunduki katika mji mkuu, Nairobi, mwezi uliopita - ikiwa ni kisa cha hivi punde zaidi katika msururu wa visa kama hivyo katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Mamlaka ya Kenya ilisema watu wanne waliyotambuliwa na shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, walirudishwa makwao kwa ombi la serikali ya Uturuki , ambayo inataka kuwafungulia mashtaka ya uhaini.
Wakosoaji wanaishtumu Kenya kwa kupuuza kanuni inayozuia kuwarejesha kwa nguvu watu wanaokabiliwa na hatari ya kuteswa.
Hili limetia doa sifa ya Kenya, huku gazeti la Daily Nation nchini humo likiripoti wakuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na shirika la ujasusi la Uingereza MI6 - William Burns na Richard Moore mtawalia - walizua hilo la kuwarejesha wakimbizi makwao kwa lazima wakati walipokutana na Rais William Ruto wakati wa ziara yao jijini Nairobi mwishoni mwa mwezi uliopita.
Kamishna wa wakimbizi wa Kenya John Burugu alikataa kutoa maoni yake kuhusu kufukuzwa kwa raia wa kigeni, lakini afisa mkuu wa wizara ya mambo ya nje Korir Sing'oei aliangazia mtanziko ambao serikali ilikabiliana nao aliposema kuwa ilihitaji kuchukuwa hatua "muhimu kwa maslahi ya taifa na manufaa makubwa".
"Kuwapa hifadhi waasi wanaotuhumiwa kufanya shughuli zinazohatarisha nchi rafiki kulisababisha mtanziko wa kidiplomasia na kibinadamu kwa Kenya," aliongeza.
Mwishowe, hali halisi ya kisiasa ilitawala, huku Kenya ikiwa haijajiandaa kuhatarisha uhusiano wake wa karibu na Uturuki, uliofanya nchi hizo mbili kutia saini makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi mnamo Julai.
Ikilinganishwa na majirani zake, Kenya imejivunia amani na utulivu kwa miaka mingi, na kuifanya kuwa kivutio kikuu kwa wakimbizi na wanaotafuta hifadhi, kutoka nchi mbalimbali zilizokumbwa na migogoro au utawala wa kimabavu katika eneo hilo kama vile Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Eritrea, Rwanda na Sudan Kusini.
Kenya ni nyumbani kwa zaidi ya wakimbizi 800,000, kulingana na Burugu.
Lakini makundi ya kutetea haki za binadamu yanahofia kwamba nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni haijakuwa salama kwa watu wanaokimbia mateso katika nchi zao.

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Polisi nchini Kenya pia wamelaumiwa maraka dhaa kwa kushirikiana na mashirika ya usalama ya kigeni kuwakamata watu wanaoonekana kuwa tishio kwa tawala zilizopo madarakani .
Mfano wa hivi punde ni wakati Kenya iliposhtumiwa kwa kutoa mazingira rafiki - kama lilivyonukuu gazeti la Observer la Uganda - katika makala yake "utekaji nyara usiokuwa na haya wa kuvuka mpaka" wa wafuasi 36 wa upinzani nchini Uganda mnamo mwezi Julai.
Kundi hilo lilikuwa limesafiri hadi mji wa Kisumu magharibi mwa Kenya kwa mafunzo, kulingana na mawakili wao lakini walirejeshwa nyumbani Uganda bila kanuni za kisheria kufuatwa.
Polisi wa Uganda waliwatuhumu washukiwa kwa kujihusisha na vitu ambavyo vilitiliwa shaka na maafisa wa polisi wa Kenya".
Lakini kundi hili lilikanusha madai hayo kupitia mawakili wao.
"Kwa kuruhusu maafisa wa usalama wa Uganda kuvuka mpaka na kuingia Kenya na hatimaye kuwateka nyara watu hao Kenya ilizembea katika jukumu lake la kuwahakikishia usalama watu watu walio kwenye himaya yao bila kujali misimamo yao ya kisiasa ," the Observer ilisema katika tahariri yake.
Mnamo mwezi Mei, mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu Mnyarwanda Yusuf Ahmed Gasana alitekwa nyara kutoka nyumbani kwake na watu wasiojulikana na hajawahi kuonekana kutoka wakati huo.
Vyanzo vya habari viliiambia familia ya Gasana kwamba alikuwa akishikiliwa katika kituo cha siri cha kuwazuilia watu nchini Rwanda akiwa na watu wengine kadha ambao bado hawajafunguliwa mashtaka.
Visa vingine ni pamoja na:
- Kutekwa nyara kwa mkimbizi wa Sudan Kusini Mabior Awikjok Bak, jijini Nairobi mwezi Februari na wanaume walioripotiwa kuvalia sare za polisi wa Kenya. Mkosoaji huyo wa serikali kwa sasa yuko kizuizini nchini mwake.
- Mwanahabari wa Pakistan Arshad Sharif, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi viungani mwa jini la Nairobi na maafisa wa polisi mwezi Oktoba 2022, miezi miwili baada ya kukimbilia Kenya kwa kuhofia usalama wake nchini. Polisi walisema aliuawa kimakosa.
- Nnamdi Kanu, kiongozi anayepigania kujitenga kwa jimbo la Biafra nchini Nigeria, ambaye alikamatwa mwaka 2021 katika uwanja wa ndege wa Kenya na Majasusi wa Nigeria. Kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya ugaidi na uchochezi. Serikali zote zimekanusha kuhusika na kukamatwa kwake.
Wale wanaotafuta hifadhi nchini Kenya wanaishi kwa uoga.
"Siku hizi situmii tena mitandao ya kijamii kwa sababu ya tishio kutoka pande zote," mkimbizi wa Rwanda na mkosoaji wa serikali ya Rwanda, ambaye amekuwa akiishi nchini humo kwa zaidi ya miaka 10, aliimbia BBC.
Mtu huyo aliye ana umri wa miaka 40- anaamini kuwa mamlaka nchini Kenya inawaelekeza maafisa wa Rwanda kumfuatilia.
"Kurejea nyumbani sio chaguo kwangu na kwa familia yangu lakini tunaishi kwa hofu," alisema.
"Ninaishi kwa hofu kwasababu nafikiwa na watu ambao natoroka kwao na kuna uwezekano wanaweza kunidhuru," mkimbizi huyo aliongoza.
Kwasababu ya tishio linaloongezeka, zaidi ya wakimbizi 3,000 na waomba hifadhi kwa sasa wanaishi chini ya ulinzi wa mashirika yasio ya kiserekali, unasema Muungano wa Wakimbizi wa Kenya (RCK).
Hofu ya kukamatwa au kurejeshwa nyumbani ni miongoni mwa sababu zilizowafanya kutafuta usaidizi wa RCK, mtafiti mkuu wa shirika hilo, Shadrack Kuyoh, aliimbia BBC.
Alisema kurejeshwa nyumbani kwa wakimbizi bila ridhaa ni kukiuka Sheria ya Wakimbizi ya Kenya, ambayo inalenga kuhakikisha kuwa "hawarejeshwi katika maeneo ambayo wanawezakudhuriwa".
Hatima ya raia wa Uturuki waliorudishwa nchini mwao haijulikani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanne hao wanaaminika kuwa sehemu ya vuguvugu la Gulen, lililopewa jina la Sheikh wa Kiislamu kutoka Uturuki Fethullah Gulen, ambalo linaendesha shule za kibinafsi nchini Kenya na maeneo mengine duniani.
Kufukuzwa kwao kulikuja mara baada ya Gulen, ambaye Uturuki ilimshutumu kwa kupanga mapinduzi yaliyotibuka mwaka 2016, kufariki, na kupendekeza kuwa Uturuki ilitumia kifo chake kuwakandamiza wafuasi wake.
Mwenyekiti wa Baraza la Madhehebu ya Kidini nchini Kenya, Askofu Willybard Kitogho Lagho, aliwataja wanne hao kama "watu wanaopenda amani" ambao walihusika katika kazi ya kibinadamu.
"Utekaji nyara wao unaashiria wasiwasi unaoongezeka kuhusu usalama wa wakimbizi wote na wanaotafuta hifadhi nchini Kenya," alisema.
Mchambuzi wa sera za kigeni wa Kenya Edgar Githua alisema serikali ilipaswa kuwakabidhi kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi ili kujikinga na ukosoaji.
"Kenya imechafua hadhi yake ya kimataifa. Hii itaangaziwa kwa miaka mingi. Hatuwezi kutengua tulichofanya," alisema.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah












