Jinsi kujiuzulu kwa kamanda wa RSF kulivyopelekea mauaji ya kimbari Sudan

Chanzo cha picha, Social media
Uchambuzi wa BBC Verify ulivyoangazia video za wapiganaji wakijivunia mauaji na kisha wakicheka waathiriwa, imebaini kwamba waliotekeleza mauaji hayo ni wanachama wa Kikosi cha kukabiliana na dharura (RSF) cha Sudan.
BBC imethibitisha kwamba watu 80 waliuawa kwenye shambulio la Oktoba katika mji wa al-Seriha, jimboni Gezira, huku Umoja wa Mataifa ukiripoti idadi ya vifo inaweza kufikia 124.
Mauaji haya yalitokana na kutoroka kwa kamanda mkuu wa RSF.
Mauaji haya yanadhihirika kuwa ni kulipiza kisasi baada ya kamanda mkuu wa RSF, Abu Keikal, kutoroka na kujiunga na jeshi la Sudan.
Hii ilitokea mnamo Oktoba 20, na kusababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi katika vijiji vya Gezira hadi mwezi Novemba 4.
Mashahidi walieleza jinsi watu walivyotekwa na kuuawa kwa risasi wakijaribu kutoroka.
Akitoa taarifa kwa BBC, msemaji wa kikosi cha RSF alikanusha kuwa kikosi chao hakikutekeleza mauaji hayo akiongezea kuwa majukumu ya kikosi cha kukabiliana na dharura ni kulinda raia na kudumisha amani na usalama na sio kuwadhuru.
Mzozo ambao umechukua miezi ishirini wakipigania mamlaka kati ya jeshi la Sudan na marafiki wa RSF umeshutumiwa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa kusababisha maafa wakilaumu pande zote mbili.
Tahadhari: Taarifa hii ina simulizi za mauaji na picha za wafu,ambapo baadhi ya wasomaji itakuwa ni vigumu kwao na kusikitisha.
Jinsi uasi ulivyosababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi
Mwezi Oktoba tarehe 20, jeshi la Sudan lilitangaza kuwa Abu Keikal, kamanda mkuu wa RSF katika jimbo la Gezira ameasi kundi hilo na kujiunga na jeshi akiwa na baadhi ya wanajeshi.
Uamuzi wa Keila kurejea katika jeshi la Sudan alikokuwa akihudumu kabla ya vita hivyo kuchacha kumeleta ufanisi mkubwa huku wanajeshi wa RSF wakihimizwa kujisalimisha katika mpango wa kuwapa msamaha.
Dakika chache baada ya Keikal kujiondoa kwa RSF mashambulizi 69 ya kulipiza kisasi yalielekezwa katika miji na vitongoji katika jimbo la Gezira kati ya tarehe 20 mwezi Oktoba hadi tarehe 4 mwezi Novemba, haya ni kulingana na data iliyonakiliwa na shirika la kutathmini vita (ACLED).
BBC Verify imefanya uchunguzi wa mashambulizi haya kwa kina, wakitumia mashahidi wa vita hivyo, picha za setilaiti, video na picha ili kubaini nini haswa kilitokea.
Jinsi uhalifu wa vita ulivyotokea al-Seriha
Mohammad Ismail alieleza kuwa alipokuwa akifanya maombi asubuhi ya mwezi Oktoba 25, alisikia wapiganaji wakivamia al-Seriha.
Watu wengi walikufa kwa kupigwa risasi wakiwa wanajaribu kutoroka, huku wengine wakipigwa risasi kwa umbali mfupi kwenye mashamba.
Ismail alisema aliona wanajeshi wa zamani wa RSF waKishiriki kwenye shambulio hilo.
Aliiambia BBC kuwa alipoona vita vimechacha alikimbilia nyumbani ili kuokoa familia yake.
Wapiganaji walikuwa wamekwea hadi katika mnara wa msikiti na kupiga risasi chochote kilichokuwa kina uhai.
Alielezea kuwa wengi waliouawa ni jamaa zake wa karibu.
Kutambua walio na hatia
BBC Verify ilinasa video ambazo wapiganaji hao walijirekodi wenyewe, wakijipiga kifua namna walivyovuruga eneo hilo na ukatili waliofanya wakimkejeli Keikal,aliyekuwa kamanda wao wa awali wa RSF, kuvamia watu kutoka eneo lake.
Katika moja ya video ilionyesha kuwa walikuwa na nembo ambazo zilikuwa na alama ya bendera ya Sudan iliyo na rangi nyeusi - ikiwa na ishara kuwa ni ya wanajeshi wa RSF.
Picha za satelaiti zilithibitisha kuwa video hiyo ilifanyika al-Seriha.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ismail anaiambia BBC kuwa alipokuja mjini alitambua baadhi ya wapiganaji walikuwa ni wa kikosi cha RSF kwani aliwatambua kuwa walikuwa wamejisajili kujiungana na kikosi hicho.
BBC Verify ilijaribu kutumia picha hizo na kuzieka katika mashine ya kutambua sura za binadamu lakini hawakufanikiwa kuwatambua kikamilifu.
Kikosi hicho kilikamilisha mashambulizi yake na kuthibitisha kwamba ilikuwa ni kulipiza kisasi baada ya Keikal kuasi kikosi hicho na kuondoka.
Katika pilka pilka za kufanya uchunguzi mazingira ya mashambulizi hayo wakichambua picha walizoziona mitandaoni ilibaini kuwa majengo yalionyesha fika kuwa ni al-Seriha.
Katika video nyingine wapiganaji walisikika wakitumia neno la kiarabu la ''ashawis'' ikiwa na maana ni mashujaa, neno ambalo RSF hupendelea kuitumia.
Na BBC Verify ilipowajibisha RSF kwa shambulizi hilo, walipinga kuwa walionekana katika video hizo ni wapiganaji wa kikosi chao.
''Ni rahisi kupata sare ya RSF na kuivaa ..kisha utekeleze mashambulizi ili kikosi kionekana kinafanya uhalifu'', msemaji wa kikosi hicho alisema hivi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la kutetea haki za binadamu kuhusianana na mashambulizi ya al-Sehira na majimbo mengine tangu Keikal ajiondoe RSF mwezi Oktoba, imebaini RSF imekuwa ikitekeleza ukatili huo.
Umoja wa mataifa pia uliwashutumu vikali RSF kwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya raia.
Idadi ya raia waliouawa
BBC imepata video nne tofauti za baada ya shambulio la al-Seriha.
Miili hiyo iliyopigwa picha inaonyesha imepangwa kwenye ua wa msikiti, iliyofunikwa na sanda na blanketi. Matoleo ya awali zaidi ya video hizi yalionekana mtandaoni tarehe 26 Oktoba.
BBC Verify imethibitisha kuwa picha iliyo hapa chini ilipigwa katika ua wa msikiti kwa kulinganisha vipengele muhimu, ikiwa ni pamoja na lango la chuma na sahani ya satelaiti nyuma, na picha ya msikiti kutoka kwenye ramani ya Google.

Chanzo cha picha, Social media
Baada ya mauaji, BBC iliona picha za maiti 82 zilizopangwa kwenye vitanda na sakafuni.
Umoja wa mataifa unasema takriban watu 124 waliuawa katika shambulizi la kulipiza kisasi katika eneo la al-Seiha. Hata hivyo shirika la kiraia katika eneo hilo limesema idadi hiyo ya waliouawa huenda ikawa ni ya juu zaidi ya 140.
Ismail alieleza kuwa kaburi la pamoja lilichimbwa, na picha za satelaiti zilionyesha mabaki ya ardhi yaliyochimbwa hivi karibuni.
Mkurugenzi mtendaji wa maabara ya utafiti ya kibinadamu ya Yale Nathaniel Raymond, alithibitisha kuwa picha ilionasa kupitia setilaiti inadhihirisha ni kweli kulikuwa na uchimbaji wa makaburi katika eneo hilo mwezi Oktoba tarehe 30.
"Picha hizi zinaashiria kuwa kuonekana kwa kilima cha makaburi ni ishara kuwa ilikuwa ni hivi karibuni kwani ingekuwa ni siku kadhaa kilima hicho hakineonekana ingekuwa ni tambarare,''anasema Nathaniel.
Ingawa BBC Verify haiwezi kubaini ni watu wangapi walizikwa katika kaburi hilo lakini upana wa kilima cha kaburi la pamoja unaonyesha kuwa miili mingi ilizikwa katiika kaburi hilo.
Walionusurika walichukuliwa kwa fidia
Baada ya mashambulizi hayo kukamilika, walionusurika walichukuliwa na kuzuiliwa .
BBC Verify ina video ambazo zinaonyesha mateka waliozuiliwa.
Katika picha moja inaonyesha takriban mateka 60 wamekaa huku wengine wamesimama kando ya ukuta wakiangaliwa kwa ukaribu na wapiganaji waliojihami.

Chanzo cha picha, Social media
Baadhi ya mateka walionekana ni wakongwe na wengine mavazi yao yamelowa damu.
Video zilionyesha mateka wakiwa wamelazimishwa kutoa sauti za wanyama huku wapiganaji wakicheka.
BBC Verify imethibitisha video hiyo kuwa ilichukuliwa magharibi kaskazini mwa mji huo ukishabihiana na picha za setilaiti.
Mateka walijipata pabaya wengine wakielekezwa kuchuchumaa na kudhalilishwa.
Elmubir Mahmoud, katibu mkuu wa bunge la Gezira aliambia BBC kuwa wapiganaji waliteka mateka 150 na kwenda nao. Anasema kuwa mateka 11 wameuawa ikiwemo msichana wa miaka 3. Hata hivyo madai haya hayajathibitishwa.
Kulingana na ushahidi wa mkaazi Mohammad Ismail ulionyesha kuwa manusura walilazimishwa kulipa fidia ili waachiliwe huru. Wapiganaji walitaka dola 100 hadi dola 1000 ili waachilie huru manusura.
Kupitia taarifa iliyowasilisha na balozi wa Marekani wa UN, Linda Thomas-Greenfield ilitoa wito kwa mataifa kutowapatia majeshi hayo bunduki kwani hilo linachangia vita kuendelea.
''Raia wa Sudan wamepitia dhiki,''anasema.''Wana haki yakuishi, usalama na ustaarabu.''
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Asha Juma












