Sudan: Mapigano kati ya jeshi na RSF yasababisha vifo vya watu 56

.

Mgogoro wa kuwania mamlaka kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo wenye sifa mbaya umetikisa nchi hiyo, huku zaidi ya raia 50 wakiripotiwa kupoteza maisha.

Wakazi walikwepa milio ya risasi katika mji mkuu, Khartoum, wakati vikosi hasimu vikipigania ikulu ya rais, TV ya serikali na makao makuu ya jeshi.

Watu 25 wakiwemo raia 17 wamefariki katika mji huo, shirika la madaktari lilisema.

Mapigano hayo yalizuka baada ya mvutano kuhusu pendekezo la mpito kwa utawala wa kiraia.

Jeshi na wapinzani wake, Rapid Support Forces (RSF), walidai udhibiti wa uwanja wa ndege na maeneo mengine muhimu huko Khartoum, ambapo mapigano yaliendelea usiku kucha.

Sauti za silaha nzito za kivita zilisikika huko Omdurman, inayopakana na Khartoum, na eneo Jirani la Bahrilililopo karibu mapema siku ya Jumapili. Watu walioshuhudia pia waliripoti milio ya risasi katika mji wa Bahari Nyekundu wa Port Sudan.

Jeshi lilisema ndege za jeshi zilikuwa zikigonga vituo vya RSF, na jeshi la anga la nchi hiyo liliwaambia watu kusalia majumbani mwao Jumamosi usiku wakati likifanya uchunguzi kamili wa angani wa shughuli za kijeshi.

Wakazi wa Khartoum waliiambia BBC kuhusu hofu yao , huku raia mmoja akielezea milio ya risasi iliyofyatuliwa katika nyumba iliyo jirani.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Takriban raia 56 wameuawa katika miji na mikoa kote nchini, kamati ya madaktari ya Sudan ilisema, ikiongeza kuwa makumi ya wanajeshi walikufa, baadhi yao wakiwa wametibiwa hospitalini.

Kwa jumla, angalau watu 595 walikuwa wamejeruhiwa, ilisema.

Wafanyakazi watatu wa Shirika la Chakula Duniani (WFP), shirika la Umoja wa Mataifa linalopeleka msaada wa chakula kwa jamii zilizo hatarini, waliuawa baada ya RSF na wanajeshi kufyatuliana risasi katika kambi ya kijeshi huko Kabkabiya, magharibi mwa nchi.

Majenerali wamekuwa wakiongoza Sudan tangu mapinduzi ya Oktoba 2021.

Mapigano hayo ni kati ya vitengo vya jeshi vinavyomtii kiongozi mkuu, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na RSF, inayoongozwa na naibu kiongozi wa Sudan, Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti.

Hemedti alisema wanajeshi wake wataendelea na mapigano hadi kambi zote za jeshi zitakapokamatwa.

Likijibu jeshi la serikali lilkifutilia mbali mazungumzo yoyote na RSF "hadi watakapokiangamiza kikosi hicho ".

'Hofu kubwa na uwoga'

Huko Khartoum, watu walirekodiwa wakikimbia na kujificha huku moshi mweusi ukiongezeka juu ya jiji hilo.

Mwandishi wa habari wa Reuters alisema kulikuwa na magari ya kivita mitaani, huku video ikionyesha ndege ya raia ikichomeka moto katika uwanja wa ndege wa Khartoum. Shirika la ndege la Saudia limesema kuwa moja ya ndege zake za Airbus ilishambuliwa

Mashirika mengi ya ndege yamesitisha safari za ndege kuelekea Khartoum na nchi jirani ya Chad imefunga mpaka wake na Sudan.

"Hatuna umeme wowote," daktari wa Uingereza-Sudan, ambaye anawatembelea jamaa zake mjini Khartoum, aliambia BBC. "Kuna joto. Hatuna uwezo wa kufungua madirisha, kelele ni nyingi."

Shahidi mwingine akiongea na BBC kupitia dada yake anayeishi Kenya alisema: "Ufyatuaji risasi bado unaendelea na watu wanasalia ndani - kuna hofu na uwoga."

Wakazi hawakutarajia mapigano hayo, alisema, na wengi walijipata wamekwama wakitaka kusafiri , huku madaraja, barabara na shule nyingi zikiwa zimefungwa.

Duaa Tariq alikuwa akizungumza na BBC wakati ndege ya kijeshi ilipopita juu ya nyumba yake. "Wanapiga risasi za moto kwenye paa la nyumba jirani na sasa hivi tunajificha," alisema

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Moshi unafuka katika kila eneo Sudan

Uingereza, Marekani, EU, Uchina na Urusi zote zimetoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano hayo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezungumza na Jenerali Burhan na Jenerali Dagalo, akiwataka kukomesha ghasia hizo.

Balozi wa Marekani John Godfrey alisema "aliamshwa na sauti za kutatanisha za milio ya risasi na mapigano", na kwamba "anajikinga na timu ya ubalozi, kama Wasudan kote Khartoum na kwingineko wanavyofanya".

RSF siku ya Jumamosi ilidai udhibiti wa angalau viwanja vitatu vya ndege, makazi ya mkuu wa jeshi na ikulu ya rais, lakini Jenerali Burhan alikanusha hayo katika mahojiano na al-Jazeera.

Pia kuna ripoti za mapigano katika kituo cha televisheni cha serikali, ambacho walioshuhudia wanasema sasa kinadhibitiwa na RSF.

Mwanajeshi mkuu wa Sudan anasema mapinduzi yalikuwa makosa

Hapo awali, RSF ilisema kwamba moja ya kambi zake kusini mwa Khartoum imeshambuliwa. Na Jumamosi jioni, Reuters iliripoti kwamba jeshi lilianzisha mashambulizi ya angani kwenye kambi ya RSF kaskazini-magharibi mwa jiji hilo, likiwataja watu walioshuhudia.

Jeshi limesema kuwa wapiganaji wa RSF wamekuwa wakishambulia kambi za jeshi na kujaribu kuteka makao makuu ya jeshi.

"Mapigano yanaendelea na jeshi linatekeleza wajibu wake wa kulinda nchi," shirika la habari la AFP lilimnukuu msemaji wa jeshi Brig Jenerali Nabil Abdallah akisema.

Shirika la habari la Reuters pia limewataja walioshuhudia wakisema kuwa kulikuwa na milio ya risasi katika mji wa kaskazini wa Merowe.

RSF ilitoa video ambayo ilisema ilionyesha wanajeshi wa Misri ambao "wamejisalimisha" kwao huko Merowe. Jeshi la Misri limesema wanajeshi wake walikuwa nchini Sudan kufanya mazoezi na wenzao wa Sudan na kwamba wanashirikiana na mamlaka ya Sudan ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wake.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo anaongoza Vikosi vya RSF

Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo anaongoza Vikosi vya RSF

Majenerali wanaendesha Sudan kupitia Baraza Kuu. Jenerali Burhan ndiye rais wake, huku Hemedti akiwa makamu wake wa rais.

Pendekezo la serikali ya kiraia imeanzisha ratiba ya kuunganisha kikosi cha RSF katika jeshi. RSF lilitaka kuchelewesha kwa miaka 10, lakini jeshi lilisema inapaswa kutekelezwa katika miaka miwili.

Hemedti alikuwa mhusika mkuu katika mzozo wa Darfur ulioanza mwaka 2003 na kusababisha vifo vya mamia kwa maelfu.

Mataifa yenye nguvu ya Magharibi na viongozi wa kieneo walikuwa wamezitaka pande hizo mbili kupunguza mvutano na kurejea kwenye mazungumzo yenye lengo la kurejesha utawala wa kiraia.

Kulikuwa na ishara siku ya Ijumaa kwamba hali hiyo ingetatuliwa.

Mapinduzi ya 2021 yalimaliza kipindi cha zaidi ya miaka miwili ambapo viongozi wa kijeshi na raia walikuwa wakigawana madaraka. Makubaliano hayo yalikuja baada ya Rais wa muda mrefu wa kimabavu wa Sudan Omar al-Bashir kupinduliwa.

Kumekuwa na maandamano ya mara kwa mara ya kuunga mkono demokrasia mjini Khartoum tangu mapinduzi.