Mapigano ya Darfur huko Sudan: Kwa nini mhasibu alichukua silaha

Chanzo cha picha, AFP
Mhasibu Mohamed Osman amelazimika kuchukua bunduki aina ya AK-47 kwa mara ya kwanza maishani mwake ili kupifania eneo lake huku mzozo wa Sudan ukizidi, na hivyo kuzidisha mivutano ya kikabila kati ya Waarabu na makundi mengine katika eneo lenye machafuko la Darfur nchini humo.
Bw Osman anaishi El Geneina, ambayo kihistoria ni ishara ya mamlaka ya Waafrika weusi huko Darfur, ambayo imekuwa ikishambuliwa kwa makombora, kuchomwa moto na kuporwa na Wanajeshi wa kikosi maalum (RSF) na wanamgambo washirika wa Kiarabu. Umashuhuri wao umewafanya wapewe jina la utani Janjaweed, neno la Kiarabu linalomaanisha "mashetani wanaopanda farasi".
"Sijawahi kuona kitu kama hicho katika zaidi ya miaka 20 ya vita huko Darfur. Ni mbaya," Bw Osman, 38, alisema. Tumebadilisha jina lake kwa ajili ya usalama wake.
"Wakati wowote kunapotokea shambulio la Janjaweed hapa El Geneina, wa wenzao huja na silaha zao kutoka ng'ambo ya mpaka nchini Chad kwa pikipiki na farasi ili kuwasaidia," aliambia BBC kutoka nyumbani kwake katika kitongoji cha Ardamata kaskazini.
Ofisi ya Bw Osman, iliyokuwa katikati mwa jiji, iliteketezwa.
"Siwezi kwenda huko, hata kama ni kazi," alibainisha ukweli wa mambo.
Mkazi mwingine, Mohammed Ibrahim, alisema jiji hilo limetekwa na RSF na Janjaweed, huku walenga shabaha wakichukua nafasi zao kwenye majengo na watu wenye silaha mitaani.
"Wanapiga tu kila mahali. Ukienda nje utauawa. Huwezi kusogea, hata mita 200 au 300," Bw Ibrahim aliambia BBC. Jina lake pia limebadilishwa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Madaktari waliripoti kuwa takriban watu 280 wameuawa na 160 wamejeruhiwa huko El Geneina katika siku chache zilizopita pekee.
Ghasia za hivi punde zinachukuliwa na wachambuzi kama ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya tarehe 11 Mei yaliyofikiwa kati ya RSF na jeshi la Sudan chini ya uongozi wa Saudi Arabia ili kupunguza mateso ya raia, wakati mazungumzo yenye lengo la kumaliza vita yakiendelea huko Jeddah.
Bw Osman alisema kwamba wakati mapigano yalipofika karibu na Ardamata katika siku za hivi majuzi, yeye na wanaume wengine wengi katika mtaa wake walipata bunduki aina ya AK-47 na kuanza kufanya doria za saa 24 kwa zamu.
Hili lilikuwa jambo ambalo hakuwahi kufikiria kulifanya, kwani maisha yake yalikuwa yanazunguka kufuatilia fedha za wateja wake.
"Hatuna lingine ila kujizatiti na kulinda jiji letu," Bw Osman alisema, akionyesha kwamba hangeweza kuhatarisha familia yake - ikiwa ni pamoja na mama yake, dada zake, wapwa zake - dhidi ya wanamgambo hao wanaoogopwa sana.
Alipoulizwa jinsi alivyopata bunduki yake ya Kalashnikov iliyotengenezwa na Sovieti, alijibu kwa huzuni: "Kitu cha bei nafuu zaidi unaweza kununua hapa ni silaha."
Kinyume chake, chakula kimekuwa haba na bei zimepanda kwa kasi huku RSF na Janjaweed wakichoma masoko.
"Walichoma hata chakula na unga uliokuwa umehifadhiwa sokoni, kana kwamba wanataka manusura wa risasi wafe kwa njaa," alisema Ishaq Hussein, mfanyakazi wa zamani katika shirika lisilo la kiserikali la El Geneina.
BBC haikufaulu katika juhudi ya kufikia RSF kupata maoni.

Chanzo cha picha, Getty Images
El Geneina ni mji mkuu wa jadi wa ufalme wa Massalit. Kulingana na sensa ya mwisho wa mwaka 2010 kuna karibu watu 170,000 huenda ndio maana na Janjaweed waliamua kuifanya kuwa lengo lao.
Kwa muda mrefu wamekuwa wakishutumiwa kwa mauaji ya kikabila dhidi ya makundi yasiyo ya Kiarabu huko Darfur.
"Janjaweed wanaua watu wote wa Kiafrika kuanzia na Massalit," Bw Ibrahim alisema.
Mzozo ulizuka kwa mara ya kwanza huko Darfur mwaka 2003 wakati wengi wao wasio Waarabu walipochukua silaha dhidi ya serikali, wakilalamikia ubaguzi na ukosefu wa maendeleo.
Serikali ililipiza kisasi kwa kuwahamasisha Janjaweed, na baadaye kuwaingiza katika kikosi cha wanajeshi wanaokadiriwa kufikia 80,000 hadi 100,000 ambacho sasa kimemgeukia mtawala wa kijeshi wa Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na jeshi analoliongoza.
RSF ilianzisha mashambulizi katika mji mkuu wa Khartoum tarehe 15 Aprili, huku wanajeshi wakilipiza kisasi kwa mashambulizi ya anga ya kila siku katika jitihada za kurejesha udhibiti wa mji huo.
Lakini huko El Geneina, hakuna jaribio la kupigana dhidi ya RSF na Janjaweed.
"Hakuna jeshi au chombo chochote cha serikali cha kulinda raia," Bw Ali alisema.
Shirika la wakimbizi la Norway (NRC) linakadiria kuwa takriban watu 100,000 wamekimbia makazi yao katika jiji hilo, na kusalia "katika ghasia zisizokoma".
"Kwa sasa hatuna njia ya kutoa msaada wa dharura," NRC iliongeza katika taarifa.
Bw Ibrahim alisema kuwa usambazaji wa maji pia umekatizwa.
“Maji ni tatizo kubwa kwa kila mtu hata kwa punda,” alisema.
Alitoa ombi la kutaka msaada wa kimataifa, akisema jiji hilo limekuwa likishambuliwa kwa siku 23 mfululizo.
"Watu wengi waliojeruhiwa hawana aina yoyote ya matibabu, na ni mamia ya watu," Bw Ibrahim alisema.
Aliongeza kuwa alikuwa peke yake nyumbani, baada ya kupeleka familia yake mahali salama.
"Nina watoto na ni vigumu kwao kusikia milio ya bunduki hizi kila siku. Ndio maana niliwaondoa hapa," alisema, akionyesha kuwa familia huwa zinaondoka katika vikundi kabla ya jua kuchomoza, wakati hatari ya kukabiliwa na RSF. na Janjaweed ni kidogo.
Bw Osman alisema kwamba ikiwa mzozo wa usalama utazidi, yeye pia atakimbilia Chad kuishi katika kambi za muda.
“Iwapo hili halitakoma kwa rehema za Mwenyezi Mungu, nitaichukua familia yangu na kukimbilia Chad kukaa kwenye kibanda kilichojengwa kwa nguo zetu kuliko kuuawa hapa,” alisema.












