Mali: Je, jukumu la Ukraine katika shambulio dhidi ya Corps Africa ni mwiba wa kujidunga?

Mwanamume akisimama mbele ya kumbukumbu ya muda ya Wagner huko Moscow, iliyojengwa kwa mara ya kwanza mwaka jana, wakati wa hafla ya kumbukumbu iliyofanyika kuwakumbuka wapiganaji wa Wagner waliouawa hivi karibuni nchini Mali na waasi wa Tuareg kaskazini - 4 Agosti 2024

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Heshima zimetolewa mjini Moscow kwa wapiganaji wa Wagner waliofariki kaskazini mwa Mali mwezi uliopita
    • Author, Paul Melly
    • Nafasi, Mchambuzi Afrika
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Wakati waziri wa mambo ya nje wa Ukraine anapokamilisha ziara yake ya hivi punde barani Afrika, nchi yake inakabiliwa na tisho la mzozo kidiplomasia kwa kuwasaidia waasi wanaotaka kujitenga kaskazini mwa Mali kuwashambulia vikali mamluki wa Urusi Corps Africa zamani wakijulikana kama Wagner mwishoni mwa mwezi uliopita.

Shambulio la kuvizia huko Tinzaouten mnamo tarehe 27 Julai liliripotiwa kuwaua wapiganaji 84 wa Africa corps na wanajeshi 47 wa Mali.

Shabulio hilo lilikuwa pigo kubwa dhidi ya kikosi hicho cha mamluki kilichokuwa kinaongozwa na marehemu Yevgeny Prigozhin, lakini sasa kinadhibitiwa na muundo rasmi wa amri ya ulinzi ya Urusi.

Siku mbili tu baadaye Andriy Yusov, msemaji wa idara ya ujasusi ya kijeshi ya Kyiv (GUR), alisema kuwa waasi wa kabila la Tuareg nchini Mali "wamepokea taarifa muhimu, na sio tu taarifa, ambazo ziliwezesha operesheni ya kijeshi yenye mafanikio dhidi ya wahalifu wa kivita wa Urusi".

Ripoti zilizofuata zilidokeza kwamba vikosi maalum vya Ukraine viliwafunza waasi hao kutumia ndege zisizo na rubani.

Kwa baadhi ya Waafrika, hiki kilikuwa kisa kingine cha mataifa ya nje kutumia bara hili kama uwanja wa umwagaji damu kwa wapinzani wao wenyewe.

Kama ilivyotabiriwa, utawala wa kijeshi nchini Mali, na serikali ya washirika katika nchi jirani ya Niger, zilijibu hatua hiyo kwa kusitisha uhusiano wa kidiplomasia na Kyiv.

Lakini jambo la msingi zaidi lilikuwa ni tamko la kambi ya kikanda, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas). Licha ya mvutano kati yake na tawala za kijeshi nchini Mali, Niger na Burkina Faso, ilikemea hatua ya Ukraine.

Ilitangaza kwamba "hataikubalina na uingiliaji wowote wa mataifa ya nje katika kanda hiyo kwani hatua hiyo ni tishio kwa amani na usalama katika Afrika Magharibi na kulaani vikali jaribio lolote linalolenga kuliingiza eneo hilo katika makabiliano ya sasa ya kijiografia".

Msimamo huo mkali huenda umetokana na mapendekezo kwamba baadhi ya wanamgambo wa kijihadi walijiunga na waasi wa Tuareg katika kuendeleza mashambulizi ya Tinzaouaten.

Wizara ya mambo ya nje ya Senegal iliwasilisha malalamiko yake kwa balozi wa Ukraine mjini Dakar baada ya kuchapisha video ya Facebook kuhusu maoni ya bwana Yusov.

Wafuasi wa utawala wa kijeshi nchini Mali wakipeperusha bendera za Urusi wakati wa maandamano ya kuiunga mkono Urusi huko Bamako, Mali - Mei 2022

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Tangu mapinduzi ya 2020 nchini Mali, utawala wa kijeshi umewafukuza wanajeshi wa Ufaransa na Umoja wa Mataifa na kuchukua msimamo wa kuunga mkono Urusi.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba wiki iliyopita alizuru mataifa ya Malawi, Zambia na Mauritius. Lakini baada ya matamshi makali yaliyotolewa na Ecowas na Senegal sasa huenda akalazimika kushughulikia mzozo wa kidiplomasia ulioibuka kati ya nchi yake na Afrika Magharibi.

Kile ambacho serikali kadha za Afrika hasa katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara - hata zile ambazo kimya kimya hazina imani na Moscow - labda zitakiona kama ujio wa kijeshi wa Kyiv usio na manufaa kinaweza kuondoa nia njema iliyokuzwa kwa bidii katika miaka miwili iliyopita kupitia diplomasia ya amani ya Ukraine.

Mamluki wa Wagner - ambao sasa wamepewa jina rasmi la Corps Africa baada ya kuwekwa chini ya udhibiti wa serikali ya Urusi - walikuwa ameongeza wafanyikazi wake mara mbili hadi 2,000 nchini Mali katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Kwa hivyo taarifa za mashambulizi ya Tinzaouaten zilikuja kama mshtuko, hasa ikizingatiwa kwamba jeshi la Mali na vikosi vya Wagner viliuteka mji wa Kidal, "makao makuu" ya waasi wa Tuareg, Novemba iliyopita.

Tukio la Tinzaouaten limeashiria kurejea tena kwa mashambulizi ya kijihadi - na hivi karibuni wakiuungwa mkono na mshirika mpya.

Vidokezo vya Kyiv vya kuhusika moja kwa moja vinathibitisha ni kwa kiasi gani nchi hiyo iko tayari kwenda ili kufikia malengo yake katika mapambano dhidi ya Rais wa Urusi Vladimir Putin zaidi ya uwanja wa vita wa nyumbani.

Hii sio mara ya kwanza kwa Ukraine kuingilia moja kwa moja operesheni za kijeshi za Corps Africa (Wagner) barani Afrika.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba mwezi Agosti na Septemba mwaka jana vikosi maalum vya Ukraine vilifanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani nchini Sudan kwa ajili ya kuunga mkono utawala wa kijeshi unaoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja, amekuwa ikizozania mamlaka na washirika wake wa zamani wa Rapid Support Forces (RSF) wanaongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, maarufu "Hemedti", ambaye amesaidiwa na Wagner.

Baadhi ya wachanganuzi wa kijeshi wa Ukraine, kama vile Evgeniy Dikiy, kamanda wa zamani wa kikosi cha Aidar cha Ukraine, wanaonyesha uingiliaji kati wa kijeshi wa nchi yao barani Afrika ulioripotiwa sana kama suala la kulipiza kisasi baada ya majeshi ya Urusi kuvamia Februari 2022.

Bw Dikiy amedai kuwa Kyiv haina sera za Afrika lakini inaazimia kulipiza kisasi hatua ya Urusi hususan kundi la Wagner.

Lakini utawala wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky huenda usione mambo kwa njia rahisi kama hiyo.

Kwani inajua kuwa mapambano dhidi ya Moscow hayafanyiki tu kwenye uwanja wa vita. Diplomasia na biashara ni mambo muhimu pia.

Na mara tu baada ya uvamizi wa 2022, Kyiv ililazimika kutilia maanani suala hilo, hasa kuhusu Afrika.

Katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 2 Machi mwaka huo, ni nchi 28 pekee kati ya 54 za Afrika zilizopiga kura kulaani uvamizi huo.

Ingawa ni washirika wachache wa karibu wa Moscow waliopiga kura kuunga mkono hatua ya Urusi, serikali kadhaa za Kiafrika, ikiwa ni pamoja na baadhi kwa ujumla zilizochukuliwa kuwa zinaunga mkono mataifa Magharibi, zilijizuia au hazikupiga kura.

Na baadaye, wakati Rais Putin alipojiondoa katika makubaliano ya kuruhusu mauzo ya nje ya nafaka ya Ukraine na Urusi - nyingi zikielekezwa Afrika - kusafirishwa usalama kupitia Bahari Nyeusi, serikali kadhaa za Kusini mwa Jangwa la Sahara ziliamua kuchukua msimamo wa kutoegemea upande wowote badala ya kulaumu Moscow.

Ingawa suala hilo limefifia, kwa sababu Ukraine imepata uhuru wake wa kusafirisha nafaka baada ya kushambulia meli za Urusi katika Bahari Nyeusi, usimamizi wa wizara ya mambo ya nje mjini Kyiv imeshawishika juu ya umuhimu wa kujenga upya mitandao yao ya kisiasa na kiuchumi kote Afrika.

Bw Kuleba tayari amefanya ziara nne katika mataifa ya Afrika. Ingawa juhudi zake za kutafuta uungwaji mkono katika mkakati wa kubuni upya ushirikiano kusini mwa Jangwa la Sahara umeendelea vyema - matumaini ya kupokelewa na Rais Cyril Ramaphosa wakati wa ziara ya Afrika Kusini mwishoni mwa mwaka jana yaligonga mwamba - lakiniamepiga hatua muhimu.

Ukrainian Foreign Minister Dmytro Kuleba (L) shakes hands with Zambia's President Hakainde Hichilema

Chanzo cha picha, @MFA_Ukraine

Maelezo ya picha, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba wiki iliyopita

Zambia, kwa mfano, ilihudhuria Mkutano wa Amani wa Ukraine nchini Uswizi mwezi Juni na, tofauti na washiriki wengine, ilitia saini taarifa ya mwisho (ambayo masharti yake yaliiridhisha Kyiv).

Na wiki iliyopita Bw Kuleba alitembelea mji mkuu wa Zambia, Lusaka, ambako alipokelewa na Rais Hakainde Hichilema.

Katika juhudia ya kuzileta karibu nchi za Kiafrika, Ukraine sasa inaelekeza macho yake katika uwanja wa kidiplomasia uliopotea katika miongo mitatu ya kwanza baada ya uhuru wake wakati ilipojishughulisha zaidi na mambo yake ya ndani.

Wakati Urusi ilirithi uwepo wa kidiplomasia duniani kote zama za Umoja wa Kisovieti , mataifa mapya huru kama vile Ukraine yalilazimika kujenga mitandao yao tangu mwanzo.

Kwa kuwa ilikuwa rasilimali chache, zaidi ya miaka 30 Kyiv iliweza kufungua balozi nane pekee katika bara zima la Afrika - nchini Algeria, Angola, Misri, Ethiopia, Kenya, Nigeria, Senegal na Afrika Kusini.

Lakini baada ya kuvamiwa na Urusi 2022 Kyiv sasa imeamua kutafuta washirika wapya kwa kupanua wigo wake, ikilenga kujenga balozi 20 za katika mataifa ya Afrika, na Balozi ndogo 10 za ziada tayari zimetangazwa.

Mnamo Aprili Ukraine ilimtuma mjumbe maalum wa Mashariki ya Kati na Afrika, Maksym Soubkh, mjini Abidjan kufungua ubalozi nchini Ivory Coast.

Na Kyiv inapendekeza zaidi ya ushirikiano wa kidiplomasia.

Nchi nane za Kusini mwa Jangwa la Sahara tayari zimenufaika na mpango wake wa msaada wa chakula wa "Nafaka kutoka Ukraine".

Pia inapanga kutoa msaada wa maendeleo, kuimarisha biashara ya pande mbili na kutoa nafasi zaidi za vyuo vikuu kwa wanafunzi wa Kiafrika.

Matukio ya kutatanisha ya kijeshi yanayolenga mamluki wa Urusi huenda yakahatarisha nia njema ya kidiplomasia na mapato ya kiuchumi ambayo Ukraine inatarajia kupata kutoka kwa mkakati wake wa msingi mpana wa kusini mwa Jangwa la Sahara.

Paul Melly ni mwanachuo katika Mpango wa Afrika katika Chatham House huko London.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Seif Abdalla