Urusi inataka nini Afrika?

Chanzo cha picha, Reuters
Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov nchini Misri, Jamhuri ya Kongo, Uganda na Ethiopia "ilikusudiwa kuonyesha kwamba Moscow bado ina marafiki katika ulimwengu ‘, kulingana na wataalam.
Kampeni hiyo ya kidiplomasia hata hivyo iligubikwa na tishio lililokuwa likijitokeza la uhaba wa chakula kwa mamilioni ya watu katika bara la Afrika, sababu mojawapo ikiwa ni kuziba kwa Urusi bandari za Ukraine na usafirishaji wa chakula nje ya nchi.
Katika miji mikuu ya Afrika, Lavrov alilaumu vikwazo vya Magharibi kwa mzozo wa chakula unaoendelea, na baadhi ya viongozi waliungana naye.
Lakini mapokezi mazuri aliyoyapata haimaanishi kuwa bara linachagua Urusi badala ya Magharibi; Mataifa ya Afrika hayawezi kumudu kupoteza washirika, wataalam wanasema
Lawama kuhusu nafaka
Kulikuwa na matarajio kwamba Lavrov angetoa suluhu kwa uhaba wa mafuta na nafaka unaoathiri mataifa ya Afrika, anasema Patience Atuhaire, mwandishi wa BBC Afrika nchini Uganda.
"Lakini Bw Lavrov alisema kuwa hana suluhu zozote za haraka, kwa sababu Urusi haihusiki na mzozo huu wa kimataifa."
Badala yake, aliishutumu Marekani na washirika wake kwa kusababisha uhaba huo kwa kuiwekea vikwazo Urusi na kuhifadhi akiba ya chakula.
"Wakati wa mgogoro wa corona, nchi za Magharibi zilifyonza bidhaa na mtiririko wa chakula, na hivyo kuzidisha hali katika nchi zinazoendelea zinazotegemea uagizaji wa chakula kutoka nje," aliandika Lavrov katika op-ed iliyochapishwa katika magazeti nchini Misri, Jamhuri ya Kongo, Uganda. na Ethiopia, mataifa manne aliyotembelea.

Chanzo cha picha, Reuters
Zaidi ya watu milioni 50 katika Afrika Mashariki watakabiliwa na uhaba wa chakula mwaka huu, kulingana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani.
Lakini Waafrika wengi hawailaumu Urusi hata kidogo, anasema Patience Atuhaire wa BBC Africa: "Nafikiri watu wengi wa kawaida nchini Uganda kwa mfano hawatahusisha moja kwa moja mzozo wa chakula duniani na vita vinavyoendelea."
Rais wa Uganda Yoweri Museveni aliunga mkono msimamo wa Lavrov, akisema kuwa kuzipiga marufuku meli za Urusi kuingia katika bandari za kimataifa kunazidisha mzozo.
"Katika vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Urusi, hawataji kwamba wameidhinisha ngano au mbolea […] kwa hivyo mbolea itaendaje?" Rais Museveni alihoji.
Uhusiano wa kihistoria
Mataifa ya Afrika hadi sasa yamekataa kujiunga na vikwazo vya Magharibi dhidi ya Urusi, na mengi yamechukua msimamo wa kutoegemea upande wowote katika vita vya Ukraine, huku mkuu wa Umoja wa Afrika na Rais wa Senegal Macky Sall akitaka vikwazo viondolewe.
Wakati nchi nyingi za Ulaya mashariki zinaiona Ukraine kama mwathirika wa ghasia zile zile za kikoloni walizofanyiwa na Muungano wa Kisovieti wakati wa Vita Baridi, barani Afrika, Moscow ina sifa tofauti.
Kotekote katika bara zima, kuna kumbukumbu za uungaji mkono wa Soviet kwa harakati za kupinga ukoloni, na wasomi wa Kiafrika wanajumuisha idadi kubwa ya wahitimu wa vyuo vikuu vya Soviet.
"Wakati wowote masuala yanapoibuka na baadhi ya watu wanataka tuchukue misimamo dhidi ya Urusi, tunasema, 'Lakini ninyi watu, watu hawa wamekuwa nasi kwa miaka 100 iliyopita, tunawezaje kuwapinga moja kwa moja?" Rais Museveni alisema katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Lavrov.

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia pia aliashiria historia ya madola ya Magharibi ya ubeberu barani humo huku akieleza kuunga mkono Afrika.
"Nchi yetu, ambayo haijajitia doa na uhalifu wa umwagaji damu wa ukoloni, daima imekuwa ikiwaunga mkono Waafrika kwa dhati katika mapambano yao ya ukombozi kutoka kwa ukandamizaji wa wakoloni," Lavrov aliandika katika makala ya kutoa maoni.
Lakini wasomi wanaoikosoa Urusi na Umoja wa Kisovieti wanaeleza kuwa kutoka Siberia hadi Caucasus hadi Ukraine, ukoloni wa ndani na nje wa Urusi umegubikwa na ghasia, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kikabila, njaa na kufukuzwa kwa lazima.
Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo ya Afrika, ujumbe wa Lavrov ulikaribishwa, kwani huko ni Magharibi ambayo inalaumiwa kwa maafa ya bara, na sio tu yale ya zamani.
Wengi katika bara hilo wanashutumu nchi za Magharibi kwa unafiki na wanataja vita nchini Libya, pamoja na hifadhi ya hivi karibuni ya chanjo za Covid-19, anasema David McNair, mkurugenzi mtendaji wa ONE Campaign, Shirika la NGO la kimataifa ambalo linapambana na umaskini uliokithiri na magonjwa yanayozuilika.
Pia wanalinganisha ukatili ambao wahamiaji wa Kiafrika wamepokea barani Ulaya, ambayo baadhi wanadai kuwa ya kibaguzi, pamoja na kukaribishwa vizuri kwa wakimbizi wa Ukraine, McNair, ambaye pia ni mwanazuoni asiye mkaazi wa Mpango wa Afrika katika Wakfu wa Carnegie kwa Amani ya Kimataifa, anaongeza
Uwekezaji wa Urusi barani Afrika
Wakati Urusi na China zinawekeza katika miundombinu, ulinzi, nishati ya nyuklia na kilimo, miradi ya Magharibi barani Afrika inaelekea kuanguka zaidi katika nyanja ya kijamii ya huduma za afya na elimu, anasema Atuhaire.
Urusi na Uchina pia zinadai kuwa uwekezaji wao haujaunganishwa na masharti ya kisiasa, wakati "Magharibi yanaonekana kuwa na maoni juu ya siasa na demokrasia ya nchi zinazounga mkono".
Lakini uwepo wa Urusi labda ni muhimu zaidi katika uwanja wa usalama. Moscow ilitoa 44% ya uagizaji wa silaha zote za Kiafrika kutoka 2017-2021, kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm.
Baadhi ya serikali za Kiafrika ziliomba usaidizi wa Urusi katika kupambana na makundi ya wanamgambo kama Islamic State au Al-Qaeda, na katika miaka michache iliyopita, mamia ya mamluki wa Urusi wanadaiwa kupigana barani Afrika, mara nyingi kusaidia serikali zilizo na rekodi mbaya za haki za binadamu.
Licha ya Kremlin kukanusha, waandishi wa habari za uchunguzi wameripoti kuwepo kwa wakandarasi hao wa kijeshi maarufu 'Wagner' nchini Libya, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali, Msumbiji na Sudan.
"Wagner ni kundi la mamluki la Urusi linalofanya kazi kwa amri ya Kremlin," Jenerali Stephen J. Townsend, kamanda anayeondoka wa Kamandi ya Marekani ya Afrika, alisema Jumanne. "Kitu pekee ninachoona Wagner Ikifanya ni kuwainua madikteta na kunyonya maliasili katika bara," jenerali huyo alisema.

Chanzo cha picha, EPA
Mikataba ya biashara au njia ya kuboresha uhusiano mwema?
Jiografia ya ziara ya Lavrov inaweza kueleweka kutoka kwa mtazamo wa kiuchumi, anasema Zawadi Mudibo, mhariri wa biashara wa BBC Afrika.
Misri ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Moscow katika bara hilo. Ushirikiano baina ya nchi mbili ni pamoja na mtambo wa nyuklia unaoendelea kujengwa, na kuna mipango ya eneo la viwanda la Urusi karibu na mfereji wa Suez.
Kati ya nchi tatu za Kiafrika ambazo Lavrov alitembelea, Uganda inaweza kuwa soko muhimu zaidi, anasema Mudibo, kwani inafungua ufikiaji wa jumuiya nzima ya Afrika Mashariki, yenye zaidi ya watu milioni 180. Kenya, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi katika eneo hilo, ni mwanachama.
Katika safari yake, Lavrov amejadili miradi mbali mbali na viongozi wenzake wa Afrika na wakuu wa nchi, kutoka kwa upatikanaji wa maliasili na uboreshaji wa mafuta hadi miundombinu, usalama wa mtandao na nishati. Nchini Uganda, Rais Museveni pia alitaja hamu ya nchi yake kurusha satelaiti.
Lakini nyuma ya matamshi kabambe kulikuwa na umuhimu mdogo sana, na hakuna mikataba iliyotiwa saini, anasema Mudibo.
"Sidhani kama Urusi ina nia ya kufanya kile inachoahidi. Haijaweka ahadi zozote. Inahusu zaidi uhusiano mwema na kuonyesha nchi za Magharibi kwamba bado wana marafiki."
Ikiwa ndivyo, safari ya Lavrov inaweza kuchukuliwa kuwa ya mafanikio kwa Moscow. Viongozi wa Afrika waliomkaribisha walisisitiza nia yao ya kufanya biashara na Urusi na kuendeleza ushirikiano zaidi.
"Nchi za Kiafrika haziwezi kumudu kupoteza msaada wowote wa kiuchumi, kiufundi au uhusiano wa kidiplomasia na nchi yoyote, ndiyo maana wamekaa kwenye uzio," anasema Atuhaire.
Wasiwasi wa Magharibi
Kuna ishara kwamba kampeni ya diplomasia ya Urusi inasababisha wasiwasi katika nchi za Magharibi. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitembelea Cameroon na Benin wiki hii, na Balozi Mike Hammer, Mjumbe Maalum wa Marekani katika Pembe ya Afrika, anasafiri kwenda Misri, Ethiopia na UAE.
Wiki iliyopita, Msimamizi wa USAID Samantha Power alitembelea Afrika Mashariki, na kuahidi msaada wa $ 1.2bn wa Amerika kuzuia njaa katika eneo hilo.
"Katika miongo kadhaa iliyopita, Urusi na China zimekuwa zikiichukulia Afrika kama mshirika wa kimkakati, na nchi za Magharibi hazijafanya hivyo," anasema McNair "Magharibi sasa yanaamka kwa hilo."
Lakini vita vya Ukraine vinaweza kuzuia nchi za Magharibi kuzingatia zaidi Afrika, anasema McNair.
Gharama ya msaada kwa Ukraine, kuwahifadhi wakimbizi wa Kiukreni na ujenzi mpya wa baada ya vita inaweza kupunguza pesa ambazo zingetolewa kwa Afrika, na Magharibi inaweza kupoteza ushawishi zaidi katika bara.















