Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?

Maandamao ya raia wa Ukraine

Chanzo cha picha, AFP

Umoja wa Ulaya, Marekani, Uingereza na washirika wamekubali kuzitenga benki kadhaa za Urusi kutoka kwa Swift, mfumo wa malipo wa kimataifa unaotumiwa na maelfu ya taasisi za kifedha.

Hatua hiyo inalenga kugusa mtandao wa benki nchini humo na upatikanaji wake wa fedha kupitia Swift, ambayo ni muhimu kwa shughuli za fedha duniani kote.

Swift ni nini?

Swift ni nguzo muhimu sana kama 'mshipa' wa kifedha wa kimataifa ambao unaruhusu uhamishaji laini na wa haraka wa pesa kuvuka mipaka. Inamaanisha ,Society for Worldwide Interbank Financial Telecommunication kwa kirefu .

Swift iliundwa mwaka wa 1973 na ina makao yake Ubelgiji, inaunganisha benki na taasisi 11,000 katika zaidi ya nchi 200.

Lakini Swift sio benki yako ya jadi ya hali ya juu. Ni aina ya mfumo wa ujumbe wa papo hapo ambao huwafahamisha watumiaji wakati malipo yametumwa na kufika.

Inatuma zaidi ya ujumbe milioni 40 kwa siku, huku matrilioni ya dola yakibadilishana mikono kati ya makampuni na serikali.

Zaidi ya 1% ya ujumbe huo unadhaniwa kuhusisha malipo ya Urusi

Nani anayemiliki na kudhibiti Swift?

Swift iliundwa na benki za Marekani na Ulaya, ambazo hazikutaka taasisi moja kuendeleza mfumo wao wenyewe na kuwa na ukiritimba.

Mtandao huo sasa unamilikiwa kwa pamoja na zaidi ya benki 2,000 na taasisi za fedha.

Swift inasimamiwa na Benki ya Kitaifa ya Ubelgiji

Chanzo cha picha, Reuters

Inasimamiwa na Benki ya Kitaifa ya Ubelgiji, kwa ushirikiano na benki kuu duniani kote - ikiwa ni pamoja na Hifadhi ya serikali kuu Marekani na Benki ya Uingereza.

Swift husaidia kufanya biashara salama ya kimataifa iwezekane kwa wanachama wake, na haitakiwi kuchukua upande katika mizozo.

Walakini, Iran ilipigwa marufuku kutoka Swift mnamo 2012, kama sehemu ya vikwazo juu ya mpango wake wa nyuklia. Ilipoteza karibu nusu ya mapato yake ya mauzo ya mafuta na 30% ya biashara ya nje.

Swift inasema haina ushawishi juu ya vikwazo na uamuzi wowote wa kuviweka unategemea serikali.

Je, kupiga marufuku Urusi kutoka Swift kutaiathirije?

Katika hatua hii, haijulikani ni benki gani za Urusi zitaondolewa kutoka Swift. Hii inatarajiwa kuwa wazi katika siku zijazo.

Taarifa ya EU, Marekani, Uingereza na nyinginezo zilisema hatua hiyo "itahakikisha kwamba benki hizi haziunganishwa na mfumo wa fedha wa kimataifa na kudhuru uwezo wao wa kufanya kazi duniani kote".

Lengo ni kwa makampuni ya Urusi kupoteza upatikanaji wa shughuli za kawaida zilizo laini na za papo hapo zinazotolewa na Swift. Malipo ya nishati yake ya thamani na bidhaa za kilimo yatatatizwa sana.

Benki zitakuwa na uwezekano wa kushughulika moja kwa moja na nyingine, na kuongeza ucheleweshaji na gharama za ziada, na hatimaye kukata mapato kwa serikali ya Urusi.

Urusi ilitishiwa kufukuzwa kwa Swift kabla - mnamo 2014 ilipoiteka Crimea. Urusi ilisema hatua hiyo itakuwa sawa na kutangaza vita.

Washirika wa Magharibi hawakuendelea na hatua hiyo lakini tishio hilo liliifanya Urusi kukuza mfumo wake wa uhamishaji wa kuvuka mpaka.

Ili kutayarisha adhabu hiyo, serikali ya Urusi iliunda Mfumo wa Kitaifa wa Kadi ya Malipo, unaojulikana kama Mir, ili kushughulikia malipo ya kadi. Walakini, ni nchi chache za kigeni zinazoitumia hivi sasa.

Kwa nini nchi za Magharibi zimegawanyika kuhusu Swift?

Baadhi ya mataifa - kama vile Ujerumani, Ufaransa na Italia - yalikuwa yamesita kuchukua hatua dhidi ya matumizi ya Urusi ya Swift.

Urusi ndiyo mtoa huduma mkuu wa Umoja wa Ulaya wa mafuta na gesi asilia, na kutafuta bidhaa mbadala haitakuwa rahisi. Huku bei ya nishati ikiwa tayari inapanda, usumbufu zaidi ni jambo ambalo serikali nyingi zinataka kuepuka.

Kampuni zinazodaiwa pesa na Urusi zingelazimika kutafuta njia mbadala za kulipwa. Hatari ya machafuko ya benki ya kimataifa ni kubwa mno, wanasema baadhi ya watu.

Alexei Kudrin, waziri wa zamani wa fedha wa Urusi, alipendekeza kutengwa na Swift kunaweza kudhoofisha uchumi wa Urusi kwa 5%.

Lakini kuna mashaka juu ya athari ya kudumu kwa uchumi wa Urusi. Benki za Urusi zinaweza kuelekeza malipo kupitia nchi ambazo hazijaweka vikwazo, kama vile Uchina, ambayo ina mfumo wake wa malipo.