Waisraeli waliojitolea kupigana Gaza sasa hawataki kurudi vitani

gg

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Fergal Keane
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Kila mmoja katika kikosi hii anajua mtu mmoja aliyeuawa katika vita kati ya Israel na Gaza.

Yuval Green mwenye umri wa miaka 26 alijua wanajeshi wenzake watatu waliouawa.

Ni mwanajeshi wa akiba,daktari katika kikosi cha kijeshi cha Israel ,ambapo alisikia mara ya kwanza shambulizi la Hamas tarehe 7 mwezi Oktoba.

''Israel ni nchi ndogo , kila mmoja anamjua mwingine., 'anasema.

Siku hiyo wapiganaji wa Hamas waliwaua watu 1200 na kuteka watu 251 na kuwapeleka hadi Gaza.

Mateka 97 walibaki katika ukanda wa Gaza na nusu yao wanaaminika bado wako hai.

Yuval alitikia wito wa nchi yake kwa kujiunga na vita mara moja.

Alikumbuka machungu ya kuingia kwenye makaazi ya jamii za Wayahudi yaliyoharibiwa karibu na mpaka wa Gaza.

"Ungeona… maiti barabarani, magari yaliyojaa risasi."

Wakati huo, kulikuwa na maswali kuhusu kujitolea kwa huduma. Nchi ilikuwa inashambuliwa. Mateka walihitaji kuokolewa.

Kisha, vita vilianza Gaza. Aliona mambo ambayo hayawezi kufutwa akilini mwake, kama usiku alipoona paka wakila miili ya binadamu barabarani.

"Ni kama kiyama. Uangalie kulia, uangalie kushoto, kila mahali ni majengo yaliyoharibiwa, yaliyochomwa, yaliyoathiriwa na makombora, kila kitu. Hii ndiyo Gaza sasa."

Mwaka mmoja baadaye, Yuval ambaye alijitolea kwa huduma ya kivita tarehe 7 Oktoba sasa anakataa kupigana.

Yuval Green ni mmoja wa wanajeshi wa akiba ambaye amekataa kurudi Gaza kupigana

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Yuval Green ni mmoja wa wanajeshi wa akiba ambaye amekataa kurudi Gaza kupigana

Yuval ni mmoja wa waandaaji wa barua ya umma iliyosainiwa na zaidi ya wanajeshi wa akiba Israel (IDF)165, na askari wa kudumu wachache, wanaokataa kutumikia au wanatishia kukataa kupigana isipokuwa mateka waachiliwe huru.

Hii itahitaji makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas.

Katika nchi ambayo bado inakumbwa na mgogoro wa kivita katika historia yake, wale wanaokataa kutumikia kwa sababu za dhamiri ni wachache katika jeshi lenye zaidi ya wanajeshi 465,000.

Kuna sababu nyingine kwa baadhi ya wanajeshi wa akiba wa IDF: Uchovu.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Israeli, kumekuwa na upungufu mkubwa wa wanajeshi wa akiba wanaojitokeza kutumikia, na baadhi ya vyanzo kama vile gazeti la The Times of Israel vikikadiria kupungua kwa asilimia 25.

Sababu nyingi za kujitokeza zinahusiana na mtazamo wa kutokuwa na sababu ya kupigana,hasa baada ya kuona uharibifu mkubwa na vifo vya watu wengi.

Mabadiliko katika Mtazamo wa Waisraeli

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ingawa hakuna msaada mkubwa wa umma kwa wale wanaokataa kutumikia kwa sababu za dhamiri, kuna ushahidi kwamba baadhi ya maombi muhimu ya wale waliotia saini barua yanashirikishwa na idadi inayoongezeka ya Waisraeli.

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Taasisi ya Demokrasia ya Israel (IDI) ulionyesha kwamba asilimia 45 ya Wayahudi wa Israeli wanataka vita kumalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka, wakati asilimia 43 wanataka Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) liendelee kupigana hadi Hamas ishindwe.

Hata hivyo, mshikamano wa kitaifa uliokuwepo baada ya mashambulizi ya Oktoba 7 umeanza kupungua, huku migawanyiko ya kisiasa ikiongezeka.

Wakosoaji wanasema kwamba vita inavunjwa kwa kushinikizwa na vyama vya siasa vya mrengo wa kulia, kauli ambayo inapata umaarufu miongoni mwa Waisraeli wa mrengo wa kushoto ambao wanataka suluhu ya amani.

Hii inaashiria mabadiliko ya kisiasa, hasa kati ya wapinzani wa serikali ya Netanyahu na wafuasi wa siasa kali za kulia.

Kwa mujibu wa baadhi y aripoti wanajeshi wa akiba wengi wao wanasusia kazi ya kushika doria Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kwa mujibu wa baadhi y aripoti wanajeshi wa akiba wengi wao wanasusia kazi ya kushika doria Gaza

Netanyahu, ambaye pamoja na Gallant wanakabiliwa na hati ya kukamatwa kutoka kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa tuhuma za uhalifu wa kivita, amekanusha mara kwa mara na kusisitiza dhamira yake ya kuwaachilia mateka.

Chembe cha kukataliwa

Chembe chembe za Yuval kukataa kutumikia zilianza mara baada ya vita kuanza.

Wakati huo,Naibu Rais wa Knesset, Nissim Vaturi, alitoa wito wa kuharibu ukanda wa Gaza kabisa.

Rabii maarufu,Eliyahu Mali, akizungumzia wapalestina wa Gaza,alisema: ''ikiwa hautawaua, watakuua wewe.''

Alisisitiza kwamba wanajeshi wanapaswa kutii maagizo ya jeshi na kwamba sheria za serikali haziruhusu kuuawa kwa raia.

Lugha hii, ambayo ilikuwa zaidi ya mifano hii miwili, ilimstua Yuval.

"Watu walikuwa wakizungumza kuhusu kuua watu wote wa Gaza, kana kwamba ni wazo la kawaida… Na katika hali hii, wanajeshi waliingia Gaza miezi michache tu baada ya marafiki zao kuuawa, wakiendelea kusikia kuhusu vifo vya wanajeshi kila siku. Na wanajeshi walikuwa wakifanya mambo mengi."

Kulikuwa na picha kwenye mitandao ya kijamii za wanajeshi wakitesa wafungwa, kuharibu mali na kudhihaki Wapalestina, ikiwa ni pamoja na mifano mingi ya wanajeshi wakijivunia picha na vitu vya watu, kama vile mavazi ya wanawake na nguo za ndani.

"Kwa wakati huo nilijaribu kupinga hali hii kadri niwezavyo," anasema Yuval. "Kulikuwa na hali ya kudhalilisha na kulipiza kisasi."

Maelfu ya Palestina walilazimika kukimbia makazi yao

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maelfu ya Palestina walilazimika kukimbia makazi yao

Mabadiliko ya kibinafsi ya Yuval Green yalitokea alipoletewa amri ya kuunguza nyumba Gaza bila sababu za kijeshi.

Alijuliza kuhusu agizo hilo, na alipopewa majibu yasiyoridhisha, alikataa kutekeleza.

Huo ulikuwa mwisho wa utumishi wake Gaza, na tangu wakati huo amekuwa akikosowa hatua za kijeshi zinazochukuliwa. Anaamini kuwa kuna uchaguzi muhimu kati ya kuendelea na vurugu na kutafuta suluhu mbadala ya mgogoro.

Jibu la IDF ni kuwa utendakazi wao kwa kuzingatia umuhimu wa kijeshi na kwa mujibu wa sheria za kimataifa" na kubainisha kuwa Hamas "inapachika mali zake za kijeshi kinyume cha sheria katika maeneo ya kiraia."

Watatu kati ya askari wa akiba waliokataa kuhudumu walizungumza na BBC. Wawili walikubali kutaja majina yao, huku mmoja akiomba kuhifadhiwa jina kwa sababu aliogopa madhara.

Wote wanasisitiza kwamba wanaipenda nchi yao, lakini uzoefu wa vita na kushindwa kufikia makubaliano ya kuwaachilia mateka uliwaongoza kwenye maamuzi ya kimaadili.

"watu walizungumza kwa utulivu kuhusu unyanyasaji na mauaji"

Mwanajeshi mmoja ambaye hakutaka jina lake litambulishwe, alikuwa katika uwanja wa ndege wa Tel Aviv Ben Gurion ambapo taarifa kuhusu shambulizi la Hamas ilianza kusambaa.Anakumbuka alipata mshtuko wa moyo.

"Nilikumbuka safari yangu ya kwenda nyumbani...redio inalia huku watu wakinipigia wakiwa na uoga ''baba ametekwa nyara nisaidie,'' hakuna anayenisaidia,sauti kutoka upande wa pili ilisikika.

Ilikuwa ni jinamizi ambalo siwezi kulisaua kamwe.

Lakini mtazamo wake ulibadilika kadri vita vilivoendea. ''Nadhani nilihisi kuwa kampeini hii haikuwa ya kulinda raia wa Israeli.''

RambiRambi katika eneo la tamasha ya Nova

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, RambiRambi katika eneo la tamasha ya Nova

Anasema alijua unyanyasaji ulivyokuwa mkubwa baada ya kuona na kusikia wenzake wakijivunia kupiga Wapalestina wasio na ulinzi, na kuzungumzia mauaji kwa utulivu kama jambo la kawaida.

Aliona wafungwa wakifungwa machoni na kupuuziliwa chakula kidogo, jambo lililomshangaza.

Alikata kauli ya kutorejea baada ya kumaliza huduma yake ya kwanza ya ulinzi.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa unyanyasaji na ukatili wa kingono uliotekelezwa na wanajeshi wa Israel ulikiuka sheria na ulichochewa na kutokuwa na hofu ya kuadhibiwa wala kuumia.

"Ni mazingira yanayokuza ukatili''

Michael Ofer-Ziv,mwenye umri wa miaka 29, alifahamu watu wawili ambao waliuawa katika mashambulizi ya tarehe 7 mwezi Oktoba , ikiwemo Shani Louk, ambao mwili wake uliburutwa hadharani mtaani Gaza.

Alianza akiamini kuwa hatua ya kijeshi ilikuwa muhimu, lakini alijikuta akiwa na wasiwasi juu ya uendeshaji wa vita.

Michael anakumbuka mazungumzo aliyosikia kati ya wanajeshi ambapo walionyesha kutojali kuhusu madhara kwa Wapalestina, huku baadhi yao wakielezea kuwa watoto wa Wapalestina walionusurika kutoka kwa vita za awali waligeuka kuwa magaidi.

Aliguswa na picha hiyo na hali ya kimazingira kwenye vita.

Michael Ofer-Ziv alikuwa afisa wa oparesheni akiangalia na kuelekeza hatua hiyo kama inavyotangazwa na kamera zisizo na rubani.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Michael Ofer-Ziv alikuwa afisa wa oparesheni akiangalia na kuelekeza hatua hiyo kama inavyotangazwa na kamera zisizo na rubani.

Anaeleza kuwa mawazo haya makali yalikuwepo kati ya wachache wa wanajeshi, lakini wengi wao walikuwa "wasiokuwa na shauku" kuhusu madhara yasiyokusudiwa au maisha ya Wapalestina.

Michael pia aliguswa na kauli zinazosema kuwa makazi ya Wayahudi yanapaswa kujengwa Gaza baada ya vita, jambo linalopigiwa debe na mawaziri wa mrengo wa kulia na baadhi ya wanachama wa chama cha Likud cha Netanyahu.

Takwimu zinaonyesha kuwa kuna ongezeko la maafisa na askari wa IDF wanaotoka katika familia za kidini za Kiyahudi, wanaounga mkono siasa za kitaifa za mrengo wa kulia na kupinga serikali ya Palestina.

Kwa Michael, tukio kuu lililotia doa lilitokea Desemba 2023, wakati IDF iliwapiga risasi mateka watatu wa Kiyahudi katika Gaza.

Alikumbuka kufikiria kuwa hiyo ilikuwa ni ishara ya ufisadi wa kimaadili.

IDF ilisema kwamba kukataa kwa wanajeshi wa akiba huchukuliwa kwa kesi binafsi, na waziri mkuu Netanyahu anasisitiza kuwa jeshi la Israel ni "jeshi lenye maadili bora zaidi duniani."

Kwa Waisraeli wengi, IDF ni dhamana ya usalama wao; ilisaidia kuanzisha Israel mwaka 1948 na ni ishara ya taifa. Kila raia wa Israeli mwenye umri wa miaka 18 anapaswa kutumikia jeshi.

Wale wanaokataa kutumikia wamepokea upinzani kutoka kwa wanasiasa, kama vile Miri Regev, ambaye alisema, "Wale wanaokataa kutumikia wanapaswa kukamatwa na kushtakiwa."

Hata hivyo, serikali haijachukua hatua kali kwa sababu, kulingana na Yuval Green, "jeshi limejua kuwa linavuta tu umakini kwa vitendo vyetu, kwa hiyo wanajaribu kutufanya tuondoke kimya.

Mustakabali wa maadili katika jimbo la kiyahudi

Askari niliokutana nao walielezea hisia mseto za hasira, kutokuwa na matumaini, maumivu na "kimya" kutoka kwa wenzao waliokataa kutumikia.

"Napinga vikali wale wanaokataa kutumikia," anasema Meja Sam Lipsky, askari mstaafu mwenye umri wa miaka 31, ambaye alishiriki vita Gaza lakini sasa anahudumu nje ya ukanda wa Gaza. Anakosoa kundi la wahifadhi huduma kwa kusema wanatumia suala hili kuwa jukwaa la siasa na kupinga serikali ya sasa.

"Hahitaji kuwa mfuasi wa Netanyahu ili kutilia shaka watu wanaotumia jeshi, taasisi tunayopaswa kuunga mkono, kama chombo cha kufikia malengo ya kisiasa," asema Lipsky.

Lipsky anakiri mateso ya raia wa Gaza, lakini pia hawezi kupuuza na amekiri kuwepo kwa picha za wanawake na watoto waliouawa na kujeruhiwa.

Sam Lipsky, ambaye alipigana Gaza katika vita vnavyoendelea, kwasasa anahudumu nje ya ukanda.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sam Lipsky, ambaye alipigana Gaza katika vita vnavyoendelea, kwasasa anahudumu nje ya ukanda.

Wakati nilipokutana na Meja Lipsky, alikuwa akikusudia kurudi kazini, akiwa na uhakika wa wajibu wake. Alisema hakuna amani hadi Hamas itakaposhindwa.

Katika mazungumzo na wanajeshi wa akiba waliokataa kutumikia, walionesha uthubutu wa kusimamia misimamo yao.

Michael Ofer-Ziv anafikiria kuhamia nje ya Israel kwa sababu anahisi ni vigumu kuishi na maadili yake nchini, hasa kutokana na hali ya kisiasa inayozidi kuwa ngumu. Anasema, "Inavyoonekana si rahisi kudumisha maadili yangu na kuishi hapa, na hiyo ni ya kutisha."

Yuval Green anajiandaa kuwa daktari na ana matumaini ya kuwa na makubaliano kati ya wapatanishi wa Israeli na Wapalestina.

Anasema, "Hapa kuna pande mbili tu katika mgogoro huu; moja inaunga mkono vurugu, nyingine inaunga mkono kutafuta suluhu bora."

Hata hivyo, wengi wa Waisraeli hawawezi kukubaliana na mtazamo huu, lakini hiyo hawezi kuzuia jitihada zao.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid