Je, Misri inajiandaa kufuta mkataba wa amani na Israel?

dxc

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Vifaru vya Misri ndani ya Sinai kwenye mpaka wa Misri na Ukanda wa Gaza mwaka jana 2024
    • Author, Abdel Moneim Halawa
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Misri imeanza kukusanya vikosi vyake vya kisiasa na kidiplomasia ili kuzuia mipango ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kuwaondoa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, na wachambuzi wa masuala ya kiusalama katika idhaa mbalimbali za Misri wameeleza kuwa jeshi la nchi hiyo "limeanza kuimarisha vikosi vyake" huko Sinai.

Siku ya Jumanne, Waziri wa Ulinzi wa Misri, Luteni Jenerali Abdel Meguid Saqr alitoa wito kwa jeshi "kujiweka katika kiwango cha juu cha utayari wa mapigano, ili vikosi vya jeshi vibaki na uwezo wa kutekeleza majukumu watakayo pewa chini ya hali yoyote," kulingana na taarifa ya msemaji wa jeshi la Misri Brigedia Jenerali Gharib Abdel Hafez.

Siku ya Jumatatu Rais wa Marekani Donald Trump alitishia kusitisha misaada ambayo nchi yake inatoa kwa Jordan na Misri ikiwa hazitowapokea Wapalestina, baada ya nchi zote mbili kukataa mapendekezo ya Trump ya kuwaondoa wakaazi wa Gaza na kuigeuza Gaza kuwa "eneo la mapumziko la Mashariki ya Kati."

Trump hakuishia kwenye kauli hizi, pia alifichua mpango mpya wa "kuinunua Gaza na kuimiliki kikamilifu," na alisema katika mahojiano na Fox News, siku ya Jumatatu, "Wapalestina hawatakuwa na haki ya kurudi Gaza, kwa sababu watapata makazi bora zaidi."

Pia unaweza kusoma

Msimamo wa Misri

D

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sisi alikutana na Trump wakati wa muhula wake wa kwanza katika Ikulu ya White House 2019

Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi alisema siku ya Jumanne, ni muhimu kuujenga upya Ukanda wa Gaza "bila kuwafukuza wakaazi wake," kulingana na taarifa kutoka kwa rais, ambayo pia ilitaja mazungumzo ya simu kati ya rais wa Misri na Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen.

Taarifa hiyo inasema, Sisi alisisitiza kwa Waziri Mkuu wa Denmark "umuhimu wa kuanza operesheni za ujenzi mpya katika Ukanda wa Gaza, kwa lengo la kuwafanya watu waweze kuishi, bila ya kuwafukuza wakaazi wake, na kwa njia ambayo itahakikisha uhifadhi wa haki zao na uwezo wa kuishi katika ardhi hiyo".

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdel Aati pia alimweleza mwenzake wa Marekani Marco Rubio mjini Washington siku ya Jumatatu kwamba nchi za Kiarabu zinaunga mkono Wapalestina katika kukataa kwao mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kuwaondoa watu wa Gaza na kuchukua udhibiti wa Ukanda huo, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuter.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilisema katika taarifa yake Jumanne, Waziri Abdel Aati alisisitiza wakati wa ziara yake mjini Washington umuhimu wa "ushirikiano wa Misri na Marekani ili kufikia amani kati ya Wapalestina na Waisraeli, kwa mujibu wa maazimio ya kimataifa na kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina kwa kuzingatia suluhisho la mataifa mawili."

Bahaa El Din Mahmoud, mtafiti katika Kituo cha Al-Ahram cha Mafunzo ya Kisiasa na mikakati, ameiambia BBC, Trump "hataweza kutekeleza mipango yake yoyote huko Gaza au Mashariki bila ya kuungwa mkono na Misri, na shinikizo lake kwa Misri juu ya misaada, iwe ya kijeshi au ya kiuchumi, halitafanya kazi."

Anasema, "sehemu kubwa ya misaada hii kutoka Marekani ni kutuma wataalamu na wakufunzi wa Marekani. Msaada huu ni mdogo sana, na sio msingi wa uchumi wa Misri, na hautaleta tatizo; hasa ikiwa nchi nyingine za Kiarabu zitaingilia kati ili kuifidia Misri."

Mkataba wa amani uko hatarini?

R

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mkataba wa amani wa Misri na Israel wa 1979 uliipatia Misri msaada wa Marekani lakini ulipunguza idadi ya wanajeshi huko Sinai.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Gazeti la Israel la Maariv liliripoti, maafisa wa Misri walimweleza Mkurugenzi wa Idara ya Ujasusi ya Marekani, William Burns, kwamba Cairo "itafuta makubaliano ya amani na Israel" ikiwa Marekani itaendelea kushinikiza watu wa Gaza waondoke, au kusitisha misaada yake kwa Misri.

Bahaa El Din Mahmoud anasema, makubaliano ya amani ni mtaji wa kisiasa mikononi mwa Misri katika kujadiliana na Trump kuhusu mustakabali wa Gaza na suala la Palestina kwa ujumla.

Mahmoud anasema, Waisraeli "hakika hawataki kusitisha mkataba wa amani na Misri, hasa kwa kuzingatia wasiwasi wa kurejea kwa vita huko Gaza."

Anasema kuna wasiwasi nchini Israel "ulionekana wazi katika maandamano ya Jumanne huko Tel Aviv ya kukataa kusitishwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano au kusitishwa kwa makubaliano ya kubadilishana mateka kati ya Israel na Hamas."

Ripoti za Israel zilizungumzia juu ya athari za mgogoro wa sasa kwenye makubaliano ya amani kati ya Israel na Misri, na gazeti la Times of Israel liliripoti kuwa maafisa wa Misri waliweka wazi kwa utawala wa Trump kwamba makubaliano ya amani na Israel "yako hatarini."

Afisa wa Misri alinukuliwa akisema, ujumbe huu "ulifika Pentagon, Wizara ya Mambo ya Nje, na wajumbe wa Congress wa Marekani." Afisa wa pili wa Misri amenukuliwa akisema ujumbe huo pia uliifikia Israel na washirika wake barani Ulaya zikiwemo Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.

Hani al-Gamal, mkuu wa Kitengo cha Mafunzo ya Ulaya na Mikakati katika kituo cha Arab Center, ameiambia BBC News Arabic: "Misri tayari imeanza kujiandaa kufuta mkataba huo, au kusitisha makubaliano ya amani na Israeli, na kwa sasa kuna jeshi zima huko Sinai."

"Hatua za Misri zilianza kwa kuongeza idadi ya wanajeshi huko Sinai, na kupeleka silaha nzito, jambo ambalo liliwatia wasiwasi sana Waisraeli," anasema.

Anasema, "mipango ya Marekani na Israel haitaishia kwenye mipaka ya Gaza."

Mtafiti wa Israel, Yaakov Beilan, kutoa Kituo cha Begin-Sadat cha Chuo Kikuu cha Israel cha Bar-Ilan, anashangaa kwa nini "Misri inaendelea kuongeza vikosi vyake vya kijeshi huko Sinai."

Uchambuzi uliochapishwa kwenye tovuti ya Jewish News Syndicate, anasema, Israel "ilikubali Misri itume vikosi huko Sinai ili kupambana na ugaidi, lakini leo kuna vikosi vikubwa vya kijeshi vilivyo tayari kwa vita."

Ameongeza kuwa Misri "imeanzisha viwanja vya ndege vitatu, kimoja kikiwa kimetengwa kwa ajili ya ndege za kivita, pamoja na kuhifadhi akiba kubwa ya mafuta."

Pia amefichua kuwa Misri imejenga "mahandaki makubwa huko Sinai, kwa ajili ya kuhifadhi zana za kijeshi, na vivuko na mahandaki yanayowezesha vikosi vingi vya jeshi kufika Sinai ndani ya saa chache," alisema.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi