Je, sera za Marekani zinaathiri vipi safari za kimataifa?

Trump ametishia mara kwa mara kutwaa Canada

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Trump ametishia mara kwa mara kutwaa Canada
Muda wa kusoma: Dakika 6

Kadiri mvuto wa utalii kuelekea Marekani unavyoendelea kupungua kutokana na ongezeko la hatari za kisiasa na kiusalama, wasafiri wengi wameanza kujiuliza ikiwa ni salama kutembelea maeneo ambayo hivi karibuni yametajwa au kutishiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Kwa hakika, mwaka huu ulitarajiwa kuwa wa kihistoria kwa sekta ya utalii nchini Marekani.

Mwaka 2026, taifa hilo lingeadhimisha miaka 100 ya barabara maarufu ya Route 66, miaka 250 ya uhuru wake, na wakati huohuo kuwa mwenyeji mwenza wa Kombe la Dunia la FIFA.

Katika mazingira ya kawaida, matukio haya yangetosheleza kuifanya Marekani kuwa kivutio kikubwa cha watalii, na kuwaletea matumaini makubwa wawekezaji wa hoteli na mashirika ya ndege.

Hata hivyo, miezi 12 iliyopita imekuwa tofauti kabisa na matarajio hayo.

Tangu Donald Trump alipoingia madarakani kwa mara ya pili Januari 2025, utawala wake umechukua hatua kali zilizotikisa uhusiano wa kimataifa.

Miongoni mwa hatua hizo ni kutoza ushuru washirika wa muda mrefu, kutoa kauli za mara kwa mara za kuitwaa Canada, kuwazuia watalii wa kigeni mipakani, kuendesha oparesheni za uhamisho wa wahamiaji kwa wingi, pamoja na mipango ya kukagua akaunti za mitandao ya kijamii za wageni kabla ya kuwaruhusu kuingia nchini humo.

Hatua hizi zimesababisha nchi kadhaa kutoa tahadhari dhidi ya kusafiri kwenda Marekani, huku baadhi ya makundi yakitoa wito wa kususia kabisa safari kuelekea huko.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa wengine, Marekani imeanza kuonekana kama "taifa lisilo rafiki".

Ripoti ya Baraza la Dunia la Usafiri na Utalii (WTTC) ilitabiri kuwa Marekani ingeweza kupoteza takribani dola bilioni 12.5 za matumizi ya watalii wa kimataifa mwaka 2025.

Kati ya nchi 184 zilizofanyiwa utafiti kwa kushirikiana na Oxford Economics, Marekani ilikuwa taifa pekee lililotarajiwa kushuhudia kushuka kwa matumizi ya watalii wa kigeni.

Akichambua hali hiyo, Sarah Cubitt aliandika kwenye tovuti ya Skift kwamba safari iliyokuwa ndoto kwa wengi sasa "imegeuka kuwa kitendo cha kisiasa, hatari kubwa, na mzigo wa kifedha".

Utafiti huo pia ulibaini kuwa asilimia 46 ya wasafiri walioshiriki walisema hamu yao ya kutembelea Marekani ilipungua kutokana na uongozi wa Trump.

Hayo yalikuwa mwaka uliopita. Hata hivyo, mwanzo wa mwaka 2026 ulileta mshtuko mpya kwa jumuiya ya kimataifa.

Serikali ya Marekani ilifanya mashambulizi ya anga mjini Caracas, ikatangaza kumkamata Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, na kudai kuwa sasa ingesimamia nchi hiyo. Sambamba na hilo, ilifufua mazungumzo ya kununua Greenland na kutoa vitisho kwa mataifa kadhaa, yakiwemo Cuba, Iran, Colombia na Mexico.

Matokeo yake, athari za sera hizi hazijaishia tu kwa wasafiri wanaotafakari kuitembelea Marekani, bali pia zimeanza kuathiri mtazamo wa wasafiri kuhusu nchi nyingine zilizoingia kwenye mvutano huo wa kisiasa na Marekani.

Heather Storgard, mkazi wa Denmark, alikuwa amepanga safari ya kwenda Greenland Februari kutembelea marafiki zake. Hata hivyo, kauli kali za Trump kuhusu kununua au kuiteka kisiwa hicho chenye rasilimali nyingi kwa nguvu za kijeshi zilimfanya aanze kusita.

"Bado ninafikiria kwenda, lakini nafanya hivyo kwa tahadhari kubwa," alisema Stourgard.

Hali kama hiyo inamkabili pia Jackie Arruda, mtaalamu wa masoko ya sekta ya ukarimu anayeishi Brazil.

Alikuwa amepanga kumtembelea rafiki yake Greenland mwezi Mei, lakini sasa anaendelea kufuatilia hali kwa karibu.

Migomo ya hivi majuzi ya Marekani katika mji mkuu wa Venezuela, Caracas, imeibua wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wasafiri kuhusu kuzuru Greenland.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mashambulizi ya hivi majuzi ya Marekani katika mji mkuu wa Venezuela, Caracas, yameibua wasiwasi miongoni mwa wasafiri waliokuwa na azma ya kuzuru Greenland.

Jackie Arruda anasema: Matukio ya Venezuela yameonyesha kuwa vitisho vya kisiasa vinaweza kubadilika na kuwa hatua halisi kwa kasi. Ikiwa lolote litatokea katika miezi ijayo, nitaghairi safari hii, lakini nina wasiwasi sana kuhusu usalama wa rafiki yangu, watu wa Greenland kama taifa, mustakabali wao, na athari na matokeo ya uvamizi huu duniani kote.''

Jesus Noguera, mmiliki wa kampuni ya utalii ya Cuba Caro Tours mjini Havana, anasema matamshi ya Trump yaliyoitaja Cuba kuwa "iko ukingoni mwa kuporomoka" yamesababisha hofu ya haraka miongoni mwa watalii wanaotarajiwa kuitembelea nchi hiyo. Safari kadhaa zimeahirishwa, na kampuni yake imepokea barua pepe nyingi za wasafiri waliokuwa na wasiwasi mkubwa. Kwa mtazamo wake, ''sekta ya utalii haiwezi kustawi katika mazingira ya sintofahamu, misukosuko na hofu inayoendelea kuongezeka''.

Kwa mujibu wa Laura Rendell Dunn, msemaji wa kampuni ya Journey Latin America, inayojishughulisha na kuandaa safari za kitalii katika Amerika ya Kusini, hatua za Marekani nchini Venezuela bado hazijaathiri uwekaji nafasi wa kampuni hiyo kwa safari za kwenda Colombia, baada ya Trump kumuonya Rais wa Colombia Gustavo Petro, akimwambia "kuwa mwangalifu".

Vivyo hivyo, safari za kwenda Mexico zimeendelea kama kawaida licha ya kauli za Trump kuhusu kutuma wanajeshi wa Marekani kupambana na magenge ya dawa za kulevya.

Baadhi ya mashirika yaliripoti kuwa kukamatwa kwa Maduro kumeathiri utalii wa ndani wa Cuba.

Chanzo cha picha, Alamy

Maelezo ya picha, Baadhi ya mashirika yaliripoti kuwa kukamatwa kwa Maduro kumeathiri utalii wa ndani wa Cuba.

Kwa upande wa waendeshaji wa safari wa Uingereza, maamuzi hufanywa kwa misingi ya tahadhari rasmi.

Sean Tipton wa Chama cha Mawakala wa Usafiri wa Uingereza anasema mara tu serikali inapotoa onyo la kusafiri, kampuni za utalii haziwezi kupeleka wateja katika maeneo hayo, kwani kufanya hivyo kunakiuka wajibu wao wa ulinzi na kunaweza kufuta uhalali wa bima ya safari.

Wasafiri binafsi wanaweza kuendelea kusafiri kwa hiari yao, lakini wanahimizwa kufuatilia taarifa za Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza (FCDO), ambayo husasishwa mara kwa mara.

Kwa sasa, FCDO inashauri kuepuka safari kwenda Venezuela na Iran, na kusafiri kwa tahadhari kubwa katika baadhi ya maeneo ya Colombia na Mexico, huku Greenland bado haijawekwa chini ya onyo rasmi.

Wakati huo huo, msamiati wa maonyo ya safari ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa baadhi ya nchi unatofautiana, ikipendekeza "kuchukua tahadhari za kawaida" na "kutosafiri" sehemu fulani za Mexico, "kuongezeka kwa tahadhari" katika Cuba na Greenland, "kuzingatia upya safari" kwenda Colombia, na "kutosafiri" kwenda Iran.

Hivi karibuni utawala wa Trump ulitishia kuingilia kati maandamano ya Iran.

Chanzo cha picha, Alamy

Maelezo ya picha, Hivi karibuni utawala wa Trump ulitishia kuingilia kati maandamano ya Iran.

Wakati huo huo, mashirika ya utalii katika maeneo yaliyolengwa yanafikiria namna ya kutumia au kudhibiti uangalizi mkubwa wa vyombo vya habari.

Inga Rus Antonisdottir, mtaalamu wa utalii katika maeneo ya Aktiki, anaona kuwa taharuki hii inaweza kuwa fursa endapo itasimamiwa kwa busara, hasa kwa maeneo changa ya utalii kama Greenland, ambayo yanaweza kutumia uangalizi huo kujitangaza kimataifa kupitia utamaduni, historia na mazingira yake ya kipekee.

"Je, aina hii ya umakini wa vyombo vya habari ni jambo baya au zuri?" aliuliza.

Aliongeza, akisema: "Yote inategemea jinsi sekta ya utalii inavyoshughulikia maslahi haya."

Badala yake, Eshraqi anabainisha kwamba mitazamo hasi ya Wamarekani iliyokita mizizi juu ya nchi hiyo, pamoja na mabadiliko ya kisiasa, yamesababisha makampuni ya usafiri na watu binafsi kuepuka masoko na kutembelea nchi.

Wasafiri wengi wanahisi kuwa hatari za kusafiri hadi Marekani hivi sasa ni kubwa kuliko manufaa.

Chanzo cha picha, Alamy

Maelezo ya picha, Wasafiri wengi wanahisi kuwa hatari za kusafiri hadi Marekani hivi sasa ni kubwa kuliko manufaa.

Nchini Iran, Mehdi Eshraghi wa kampuni ya Surferan anasisitiza kuwa kupungua kwa watalii wa Magharibi si matokeo ya kauli za hivi karibuni pekee, bali ni zao la mitazamo hasi ya muda mrefu iliyoimarishwa tangu Marekani ijiondoe kwenye makubaliano ya nyuklia mwaka 2018.

Katika ulimwengu wa utalii, taswira ni kila kitu.

Na chini ya miaka miwili tangu Marekani itangazwe kuwa kivutio bora zaidi cha utalii duniani, wasafiri wengi sasa wanaanza kuona kuwa hatari zinazohusishwa na safari hazilingani na faida zake.

Ingawa bado ni mapema kusema iwapo hali hiyo itaenea kwa mataifa mengine yaliyotajwa, kinachoonekana wazi ni kwamba mazingira ya kisiasa yanaweza kubadilisha mwelekeo wa utalii wa kimataifa kwa kasi isiyotabirika.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid