Ni nani anayeimiliki Gaza?

Chanzo cha picha, EPA
- Author, Ethar Shalaby
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Tangu 2007, Hamas imekuwa chombo cha kiutawala katika Ukanda wa Gaza. Ilishinda uchaguzi wa bunge na kuimarisha mamlaka yake huko Gaza baada kumuondoa mpinzani wake, harakati ya Fatah, kutoka katika eneo hilo.
Katika miaka iliyofuata, Hamas na Israel walipambana mara kadhaa. Kila duru ya mapigano ilisababisha hasara kwa pande zote mbili, lakini hasara kubwa zaidi ni kwa Wapalestina wa Gaza.
Kundi hilo - linalotajwa kuwa la kigaidi na Israel, Marekani na serikali nyingine za Magharibi - linadhibiti Ukanda wa Gaza. Ni ukanda wa ardhi yenye urefu wa kilomita 41 na upana wa kilomita 10, uliozungukwa na Israel, Misri na Bahari ya Mediterania.
Oktoba 7, 2023, wapiganaji wa Hamas walianzisha mashambulizi kutoka Gaza, na kuua takribani watu 1,200 nchini Israel na kuchukua zaidi ya mateka 250.
Hilo lilisababisha mashambulizi makubwa ya kijeshi ya Israel huko Gaza, ambayo yamedumu kwa miezi 15. Zaidi ya watu 47,540 wameuawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.
Januari 2025, Israel na Hamas walifikia makubaliano ya kusitisha mapigano - baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo magumu yasiyo ya moja kwa moja. Makubaliano hayo yanalenga kukomesha kabisa mapigano na kuwaachia huru mateka wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza, huku wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israel nao wakiachiwa.
Trump anaweza kuichukua Gaza?

Chanzo cha picha, Reuters
Jumanne iliyopita, Rais wa Marekani Donald Trump alisema Marekani itachukua udhibiti wa Gaza, kuujenga ukanda huo na kuugeuza kuwa "eneo la mapumziko la Mashariki ya Kati."
Maoni yake yalikuja baada ya hapo awali kupendekeza kwamba Wapalestina "wahamishwe" kutoka Gaza na wapelekwe Misri na Jordan.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Viongozi wa dunia, akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, walikosoa mara moja kauli hizo, huku wakieleza kuwa zinaweza kuzua mvutano mpya katika eneo la Mediterania.
Hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa kuhusu jinsi Trump atakavyoweza kuchukua udhibiti wa Gaza. Tangazo hilo lililaaniwa kote duniani, nchi nyingi zikiwemo Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Brazil, Australia, Urusi na China zikikataa mpango huo.
Katika eneo la Ghuba, Saudi Arabia imekataa jaribio lolote la kuwaondoa Wapalestina. Jordan na Misri pia zimeelezea upinzani wao kwa hatua hiyo.
Chini ya sheria za kimataifa, kuwahamisha watu kwa nguvu ni kinyume cha sheria. Trump alipoulizwa iwapo wanajeshi wa Marekani watahusika, alisema "tutafanya kinachohitajika."
Chini ya Katiba, Bunge la Marekani lazima liidhinishe maazimio ya matumizi ya nguvu za kijeshi kutoka mabaraza yote mawili, ambayo kwa yanayoongozwa na chama tawala cha Republican kwa sasa.
Hassan Mneimneh, profesa katika Taasisi ya Mashariki ya Kati huko Washington, anasema, "Trump hapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu Congress kwa sababu ana uungwaji mkono mkubwa kutoka kwao."
Historia ya Ukanda wa Gaza
Kabla ya kuundwa kwa Israel mwaka 1948, Gaza ilikuwa chini ya ukoloni wa Uingereza. Siku moja baada ya kutangazwa uhuru, Israel ilishambuliwa na kuzingirwa na majeshi ya mataifa matano ya Kiarabu.
Mapigano hayo yalipomalizika mwaka 1949, Israel ilidhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya Palestina. Misri ikiukalia Ukanda wa Gaza, Jordan Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, huku Israel ikichukua Jerusalem Magharibi.
Misri ilifukuzwa kutoka Gaza katika vita vya 1967 na ukanda huo ukakaliwa na Israel, ambayo ilijenga makazi ya walowezi na kuwaweka Wapalestina wa Gaza chini ya utawala wa kijeshi.
Mwaka 2005, Israel iliondoa wanajeshi wake na walowezi kutoka Gaza, huku ikishikilia udhibiti wa mpaka wa Gaza, anga na ukanda wa pwani, na kuwa na udhibiti kamili wa shughuli za watu na bidhaa za kuingia na kutoka. Umoja wa Mataifa bado unaichukulia Gaza kuwa eneo linalokaliwa na Israel kwa sababu ya kiwango hicho cha udhibiti.
Hamas ilishinda uchaguzi wa Palestina mwaka 2006 na kuwaondoa wapinzani wake Fatah katika eneo hilo baada ya mapigano makali mwaka uliofuata.
Kujibu hali hiyo, Israel na Misri ziliweka kizuizi, zikidhibiti sehemu kubwa ya kile kilichoruhusiwa kuingia katika eneo hilo.
Katika miaka iliyofuata, Hamas na Israel zimepigana mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na 2008-2009, 2012 na 2014. Mzozo wa mwisho kati ya pande hizo mbili kabla ya huu wa sasa, ulikuwa ni wa mwezi Mei 2021 na ulimalizika kwa kusitishwa mapigano baada ya siku 11.
Kuna gesi na mafuta Gaza?

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu yana mafuta na gesi. Mwaka 2019, ripoti iliyochapishwa na Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD), ilikadiria kiwango cha mafuta na gesi kuwa zaidi ya mapipa bilioni 3.
"Wataalamu wa jiolojia na uchumi wa maliasili wamethibitisha kuwa eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu liko juu ya hifadhi kubwa za mafuta na gesi asilia, katika eneo la Area C la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na pwani ya Mediterania karibu na Ukanda wa Gaza," imesema ripoti hiyo.
Pia liliripoti ugunduzi mpya wa mafuta na gesi asilia katika Bonde la Levant, ambalo liko katika Bahari ya Mediterania, "futi za ujazo trilioni 122 za gesi asilia yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 453 bilioni (kwa bei ya 2017) na mapipa bilioni 1.7 ya mafuta yenye thamani ya takriban dola bilioni 71."
Baadhi ya wataalamu wanaamini mapendekezo ya Trump yanaweza kuhusishwa na uchimbaji wa mafuta na gesi. Lakini wengine wanaamini maslahi ya Trump kwa Gaza ni ya kisiasa zaidi kuliko ya kiuchumi.
Laury Haytayan, mtaalamu wa sera ya nishati katika eneo la Mashariki ya Kati, anasema, ugunduzi wa mafuta na gesi katika maeneo ya pwani ya Gaza ulifanywa katika miaka ya 2000 na kumekuwa na mazungumzo ya uchimbaji. Anasema hii "inaweza kuwa moja ya sababu" ya Trump kupendekeza kuichukua Gaza, lakini huenda sio sababu pekee.
Maher Tabaa, mtaalamu mwingine wa uchumi wa Gaza, anasema: "Trump ana washirika wa Ghuba na nchi nyingine zenye utajiri mkubwa wa gesi na mafuta kuliko Gaza. Mtazamo wake juu ya Gaza ni wa kisiasa zaidi."
Wapalestina wanasemaje?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wapalestina wanaona pendekezo la Trump ni la kuwafukuza moja kwa moja katika ardhi yao.
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amepinga mpango wowote wa kuwatimua Wapalestina kutoka Gaza, akitaja wito wa Trump kuwa ni "ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa."
Mkuu wa ujumbe wa Wapalestina kwenye Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour, anaamini Wapalestina wanapaswa kuruhusiwa kurejea katika yale yaliyokuwa makazi yao, "kwa wale wanaotaka kuwapeleka watu wa Palestina kwenye 'mahali pazuri,' wawaruhusu warejee katika makazi yao ya awali katika eneo ambalo sasa ni Israel."
Katika Ukanda wa Gaza, Mahmoud Almasry, mwenye umri wa miaka 43, anasema hakuna hata mtu mmoja huko Gaza aliyekubaliana na mapendekezo ya Trump, "hata tukibaki na vifusi, hatutaondoka katika nyumba zetu."
Youssef Alhaddad, wakili wa ki-Palestina, anasema Trump anatumia wazo la kujenga upya Gaza kama "shinikizo" la "kuwalazimisha watu wa Gaza kuondoka katika nchi yao," ameliita wazo hilo ni "baya."
Baadhi ya Wapalestina, kama vile Nevin Abdelal, wanapendelea mipango ya kuijenga Gaza upya ifanywe na "Wapalestina," wakisema Wagaza wanaweza kuhamia "maeneo bora zaidi yanayopatikana katika Ukanda huo hadi ujenzi mpya ukamilike, lakini hakuna mtu anayepaswa kuondoka."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












