'Tutaishi na kufa katika nchi yetu': Kauli ya Wagaza baada ya Trump kupendekeza kuichukua

"Maadamu watoto wetu wangali hai, hatutaondoka Gaza, na hatutaiacha."
Kwa Jamalat Wadi, na kwa Wapalestina walio wengi zaidi huko Gaza, pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu uwezekano wa kukaliwa kwa mabavu kwa Ukanda huo na kuhamishwa kwa wakazi wake kutoka katika ardhi ya mababu zao halifai kabisa.
"Ninasubiri kujenga upya nyumba yetu ili tuweze kuishi tena, na hatujali kuhusu Trump au mtu mwingine yeyote," Gazan aliiambia BBC.
Katika Ukanda wa Gaza, ni wachache wanaotaka kusikia kuhusu suala la kuondoka katika nyumba zao, ingawa sehemu kubwa ni milima ya vifusi baada ya miezi 15 ya vita na kushuhudia karibu vifo 47,000 vya Wapalestina.
"Tutaishi na kufa katika ardhi yetu," mwanamke mmoja wa Kipalestina aliambia idhaa ya Kiarabu ya BBC.
"Tumevumilia mwaka mmoja na nusu wa mauaji na uharibifu. Baada ya haya yote, tunawezaje kukubaliana na uamuzi huu?" aliongeza.
"Hii ni ardhi yetu na hatuwezi kuishi popote pengine isipokuwa Gaza. Gaza ni nchi yetu, tulikulia hapa," alisema Mahmoud Bahjat, ambaye, aliposikia maoni ya rais wa Marekani, aliomba kwa Mungu kwamba "nchi za Kiarabu zikatae jambo kama hilo, kwa sababu tuliishi na kukulia hapa."

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Washington akiwa na waziri mkuu wa Israel, Trump alipendekeza siku ya Jumanne kwamba Marekani inapaswa kudhibiti Ukanda wa Gaza na kuugeuza kuwa "Riviera ya Mashariki ya Kati," na kwamba Wapalestina wapewe makazi mapya Misri na Jordan.
Maneno yake yametikisa eneo zima, ambapo wamepata upinzani mkali na kwa kauli moja.
Pia inakuja wakati Israel na Hamas wanatarajiwa kurejea kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya awamu ya pili ya usitishaji mapigano ambao umesimamisha, kwa sasa, vita huko Gaza.
"Uhalifu wa kimataifa"
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas "amekataa vikali" pendekezo la Trump la "kuchukua" Ukanda wa Gaza na kuwaondoa Wapalestina "nje ya nchi yao," kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi yake.
"Haki halali za Wapalestina haziwezi kujadiliwa," Abbas alisema, akiongeza kwamba Gaza "ni eneo muhimu la Palestina" na kwamba matamshi ya Trump yalikuwa "ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa."
Hamas, ambayo imedhoofishwa sana lakini bado inadhibiti Ukanda huo, ilisema matamshi ya Trump ni "ya kipuuzi."
Sami Abu Zuhri, msemaji wa wanamgambo wa Kiislamu ambao mashambulizi yao ya kikatili kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, 2023 yalizua vita ambayo usitishaji wake bado ni dhaifu, alionya kwamba "mawazo ya aina hii yanaweza kuteketeza eneo hilo."
Misri na Jordan pia zimeweka wazi kwamba hazitakubali kuhamishwa kwa Wapalestina katika ardhi yao, baada ya kusema hivyo kufuatia taarifa kama hizo, ingawa hazina maelezo zaidi, za Trump kuhusu Gaza mwezi uliopita.
Katika taarifa ya pamoja ya nchi na mashirika kadhaa ya Mashariki ya Kati, wameonya kwamba hatua hiyo inaweza "kuhatarisha utulivu wa eneo hilo, hatari ya kuongeza migogoro na kudhoofisha matarajio ya amani na kuishi pamoja miongoni mwa watu wake."
Washirika wengine wawili wakuu wa kikanda pia wameukataa mpango huo. Uturuki iliutaja mpango huo kuwa "usiokubalika" na Saudi Arabia ikasisitiza msimamo wake "madhubuti na usioyumba" kwamba haitaanzisha uhusiano na Israeli bila kuunda taifa la Palestina, kinyume na uvumi uliotoka Ikulu ya White House.

Chanzo cha picha, Reuters
Uhamisho wa mara kwa mara wa wakazi wa Ukanda wa Gaza kuelekea kusini, ulioshinikizwa na wanajeshi wa Israel wakati wa vita, ulisababisha wengi kuogopa kwamba Israel ilikuwa inataka kuwafukuza Wapalestina kuelekea Sinai nchini Misri.
Mawaziri wenye itikadi kali zaidi katika serikali ya Benjamin Netanyahu wamerejelea mara kwa mara kusisitiza, ingawa Israel imekuwa ikikanusha.
Maneno ya Trump sasa yanaenda mbali zaidi.
"Ni kinyume cha sheria, ni kinyume cha maadili na kutowajibika kabisa," alisema Francesca Albanese, ripota maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ardhi ya Palestina inayokaliwa kimabavu, akielezea pendekezo la rais wa Marekani kama "uchochezi wa watu kulazimika kuyahama makazi yao, ambayo ni uhalifu wa kimataifa."
Umoja wa Mataifa umekuwa thabiti sana katika jibu lake kwa Trump, ikikumbuka kwamba "kuondoa au uhamisho wa watu kwa kulazimishwa bila msingi wa kisheria ni marufuku" na kwamba sheria ya kimataifa iko wazi sana juu ya suala hili, alisema Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Türk, kwa mujibu wa EFE.
Uchambuzi wa Tamer Qarmout, Profesa wa Sera ya Umma katika Taasisi ya mafunzo Doha
Kwa Tamer Qarmout, "eneo lazima lijiandae kwa hali mbaya zaidi, lakini pia kwa mtindo wa mazungumzo wa Trump, ambao ni maarufu kwa kujielekeza zaidi kutimiza malengo yake," anachambua BBC Mundo.
Vitisho vya hivi karibuni kwa Mexico, Panama, Canada na Denmark juu ya eneo la Greenland vinaonyesha, kwa mujibu wa mtaalam huyo, Inaweza kuwa mkakati wa majadiliano,tishio linaandaliwa,lengo Fulani linafikiwa na baadae mpango kusitishwa,hatua ambayo anaiita mbinu za Trump.
Lakini tishio hilo linatokana na nguvu kubwa yenye maslahi katika eneo hilo, hivyo "ni wakati kwa nchi za Kiarabu, badala ya kuchukua hatua kwa upande mmoja na kueneza kauli za kushoto na kulia, kuchukua hatua kwa pamoja na kuweka mezani ushawishi wao wote, maslahi yao ya kisiasa, kiuchumi au kijeshi ambayo wamekuwa nayo na Marekani."
"Lazima waonyeshe meno wakati huu, kuweka wazi kuwa huu ni mstari mwekundu ambao hakuna mtu anayeweza kuvuka," anasema Qarmout.
Kwa maoni yake, baada ya miezi 15 ya vita, Israel iko "katika mkwamo wa kimkakati, kwa sababu licha ya kuweza kugeuza Gaza kuwa kifusi, Hamas bado iko na Wapalestina bado wako, hivyo Israel imenaswa katika hali mbaya."
Kwa maneno yake, Trump anainua kiwango na kuziweka nchi za Kiarabu katika njia panda kwa mujibu wa Qarmout.
"Ama washughulikie hatua ya kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza, au wajitolee kwa aina fulani ya makubaliano ambayo yanaipa Israel hadhi, mkakati wa kujiondoa kwenye vita hivi na kuitenga Gaza na Israel."
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa kikanda, Trump anataka kuzishirikisha nchi za Kiarabu katika utawala wa Gaza baada ya vita "ili waweze kukamilisha kazi, ambapo Gaza haitakuwa tatizo tena kwa Israel na Israel iweze kuelekeza nguvu kwenye Ukingo wa Magharibi."
Waarabu, ambao hadi sasa wamekataa kuchukua udhibiti wa Gaza kwa sababu wanaamini kwamba ingetenga suala la suluhisho la Palestina la serikali mbili kwa kugawanya zaidi eneo hilo, "sasa wako kati ya mwamba na mahali pagumu na wanapaswa kupima uamuzi wao," anasema profesa kutoka Taasisi ya Doha.
Swali sasa, kwa mujibu wa Qarmout, ni iwapo Trump anataka kutenga eneo "ambalo limejifungamanisha zaidi au kidogo na Marekani kimkakati na kiuchumi, na ambapo baadhi ya nchi zimerekebisha uhusiano wao na Israel."
"Je, Marekani iko tayari kutupa kila kitu, miungano hii yote, ushawishi wote ilio nao katika eneo hili, ili kuhatarisha hali hii? Sidhani Wamarekani wanataka kufanya hivi sasa, na Waisraeli wenyewe wanaelewa kuwa hali hii inatishia kuanzisha vita na Jordan na Misri."
"Lakini lazima tumchukulie kwa uzito kwa sababu Trump ni mtu mwenye hamaki, ni rahisi kufanya maamuzi yenye madhara.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Ambia Hirsi












