Kwanini Israel inaendelea kujenga makazi katika Ukingo wa Magharibi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Takriban Wayahudi nusu milioni wanaishi katika makazi zaidi ya 130 katika Ukingo wa Magharibi, isipokuwa Jerusalem Mashariki.
Inakadiriwa pia kuwa Wapalestina milioni tatu wanaishi katika maeneo hayo. Jamii za Palestina na Kiyahudi zinaishi katika maeno tofauti.
Makazi haya yenye utata yamechukuliwa kuwa haramu na Umoja wa Mataifa kwa miongo kadhaa; msimamo ambao Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilisisitiza mwezi Julai. Lakini ni kwanini Israel inaendelea kujenga makazi haya?
Ni maeneo gani ya makazi ya Israeli?
Makazi haya ni jamii ambazo Israel ilianzisha katika ardhi ilizoziteka katika vita vya siku sita vya mwaka 1967. Maeneo hayo ni pamoja na ukingo wa magharibi wa mto Jordan , Jerusalem Mashariki na milima ya Golan.
Kabla ya hapo, Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki zilikaliwa na Jordan kufuatia vita vya Waarabu na Waisraeli mwaka 1948-1949.
Israel pia ilikuwa imeanzisha makazi katika maeneo ya Ukanda wa Gaza ambayo iliyachukua kutoka Misri katika vita vya mwaka 1967, lakini iliyaharibu makazi hayo mwaka 2005, wakati ilipoondoka eneo hilo.
Israel pia ilijenga makazi katika rasi ya Sinai, ambayo iliiteka kutoka Misri mwaka 1967, lakini iliyavunja mwaka 1982 kama sehemu ya makubaliano ya amani na Cairo.
Makazi haya yametawanyika katika eneo lote la ardhi ya Palestina na yanalindwa na majeshi ya Israeli.
Hii inawafanya Wapalestina wa kawaida wasiweze kuishi katika makazi haya isipokuwa biashara za Israeli ziwaajiri kufanya kazi katika makazi hayo. Matokeo yake, miji ya Palestina imetengana, na hivyo kufanya uhusiano wa usafiri na maendeleo ya miundombinu kuwa magumu katika ardhi ya Palestina.

Chanzo cha picha, Getty Images
Makazi ya Ukingo wa Magharibi ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa, lakini sheria ya Israel inayachukulia kuwa halali.
Maeneo ya nje ya ukingo wa magharibi yanachukuliwa kuwa haramu chini ya sheria ya Israeli kwa sababu yalijengwa bila ruhusa kutoka kwa serikali ya Israeli.
Nani anayedhibiti Ukingo wa Magharibi?
Mwaka 1993 na 1995, Israel ilitia saini mkataba wa Oslo na Wapalestina, ambao ulipelekea kuundwa kwa serikali ya mpito katika Ukingo wa Magharibi na Gaza, inayojulikana kama Mamlaka ya Palestina.
Huku Mamlaka ya Palestina inatawala miji mikubwa ya Palestina, Israel inashikilia udhibiti wa karibu wa asilimia 60 ya Ukingo wa Magharibi (inayojulikana kama Area C), inayosimamia utekelezaji wa sheria, mipango, na ujenzi. Ni wajibu

Chanzo cha picha, Getty Images
Makazi yana ukubwa gani?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ukubwa wa makazi ni tofauti. Wengine wana wakazi mia chache tu, huku mengine maelfu ya Waisraeli wakiishi kwenye makazi mengine.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, kati ya Novemba 1, 2022 na Oktoba 31, 2023, karibu vitengo 24,300 vya makazi vilijengwa au kupitishwa kwa ujenzi ndani ya makazi ya Israeli katika Eneo C katika Ukingo wa Magharibi. Hii ni idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa tangu kuanza kwa ufuatiliaji wa ujenzi mwaka 2017. Idadi hii inajumuisha takriban nyumba 9,670 za makazi katika Jerusalem Mashariki.
Picha za satelaiti pia zinaonyesha jinsi makazi yalivyopanuka kadri muda unavyosonga. Kwa mfano, mwaka 2004, mji wa Givat Ziv ulikuwa na wakazi wapatao 10,000. Kwa sasa idadi ya watu wake imefikia 17,000.
Makazi yamepanuliwa hadi magharibi na nyumba mpya, sinagogi na kituo cha ununuzi vimeongezwa katika makazi hayo.
Modi'in Ailit ni mji mkubwa wenye wakazi 73,800. Katika miaka 15 iliyopita, idadi ya watu wa mji huu imeongezeka mara tatu. Taarifa hii ilikusanywa na kikundi cha "Now Peace" ambacho kinapinga ujenzi wa makazi.
Kwa nini Wayahudi wanataka kuishi katika Ukingo wa Magharibi?
Baadhi ya watu huamua kuhamia kwenye makazi hayo kwa sababu ruzuku ya serikali ya Israeli hufanya gharama za makazi kuwa nafuu na wanaweza kuwa na maisha bora.
Wengine huhamia katika maeneo haya kuishi katika jumuiya za kidini sana, wakiamini kwamba Mungu amewapa ruhusa ya kuishi huko kulingana na tafsiri yao ya Biblia ya Kiebrania. Theluthi moja ya jamii za walowezi ni wafuasi wa dini ya ultra-orthodox.
Jamii hizi mara nyingi huundwa na familia kubwa ambazo kwa ujumla ni maskini, kwa hivyo ubora wa maisha ni jambo muhimu.
Lakini baadhi ya jamii zina imani za kiitikadi kuhusu; Kwamba wana haki ya kuishi huko kwa sababu wanaamini kwamba maeneo haya ni ardhi ya mababu ya Wayahudi.

Chanzo cha picha, Getty images
Makazi katika Ukingo wa Magharibi yako chini ya utawala wa raia wa Israel na wana barabara zao wenyewe na njia za usafiri. Lakini Wapalestina katika eneo hili wako chini ya utawala wa kijeshi wa Israel na kwa hivyo lazima wapitie vituo vya ukaguzi vya kijeshi vya Israeli.
Wapiganaji wengi walowezi wamejihami kwa silaha na wametekeleza mashambulizi ya kikatili dhidi ya raia wa Palestina. Mwezi Agosti, wakati ghasia za walowezi dhidi ya Wapalestina zilipoongezeka, Marekani iliwekea vikwazo kikundi cha walowezi cha Israel cha Hashomer Yosh, na kampuni ya ulinzi wa raia ya Isaac Levy Philant.
Marekani imeishutumu vikundi hivyo kwa kuanzisha vituo vya ukaguzi na doria mapema mwaka huu ili "kuwatafuta na kuwashambulia Wapalestina katika ardhi yao na kuwafurusha kwa nguvu." Marekani pia imesema kuwa kundi la Hashomer Yosh liliweka uzio katika kijiji cha Palestina cha Kharba Zenuta na kuwazuia wakaazi wake waliohamishwa kurejea majumbani mwao.
"Vurugu kubwa za walowezi katika Ukingo wa Magharibi zinasababisha mateso makubwa ya kibinadamu, na kuathiri usalama wa Israeli, na kudhoofisha matarajio ya amani na utulivu katika eneo hilo," Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema katika taarifa.
"Ni muhimu kwamba serikali ya Israeli iwajibike kila mtu na taasisi inayohusika na vurugu dhidi ya raia katika Ukingo wa Magharibi."

Chanzo cha picha, Getty images
Je, ni msaada gani wa kisiasa ambao makazi hayo yanao?
Baada ya vita vya Waarabu na Waisraeli vya mwaka 1967, mwanasiasa wa Israel Yigal Alon aliandaa mpango wa sera unaolenga kuimarisha usalama wa Israel huku akipunguza ongezeko la idadi ya Waarabu walio wachache.
Mpango wa Alon, ambao ulijulikana kwa jina Alon, ulitokana na imani kwamba uhuru wa Israeli kwa sehemu kubwa ya maeneo yake yaliyokaliwa ulikuwa muhimu kwa ulinzi wa Israeli.
Tangu vita vya mwaka 1967, serikali zote za Israeli zimeendelea kupanua idadi ya walowezi katika maeneo yaliyokaliwa.
Serikali ya sasa ya Israel imehimiza sana ujenzi wa makazi. Serikali hii, serikali ya mrengo wa kulia na ya kizalendo ya Israel hadi sasa, imetangaza wazi nia yake ya kuongeza mara mbili idadi ya walowezi hadi milioni moja, na ina wanaharakati wa muda mrefu wa makazi katika nafasi muhimu za baraza la mawaziri.
Kituo cha televisheni cha Israel cha Channel 12 kiliripoti mwezi Aprili kwamba waziri wa fedha wa Israel Betsalel Smotrich amekuwa akihimiza kuanza kwa mchakato wa kuhalalisha vituo 68 haramu katika Ukingo wa Magharibi.
Baadhi ya vituo hivi [ambavyo vilijengwa bila ruhusa] baadaye vilitambuliwa na serikali.
Sheria ya kimataifa inasema nini?
Nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya zinasema kuwa makazi ya walowezi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi yanakiuka sheria za kimataifa.
Maazimio ya Umoja wa Mataifa yalipiga marufuku makazi hayo katika miaka ya 1979 na 2016, na Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilisema katika maoni ya kihistoria mwezi Julai kwamba uvamizi wa Israel wa ardhi ya Palestina unakiuka sheria za kimataifa.
Mahakama hiyo imesema kuwa Israel inapaswa kusitisha shughuli za ujenzi wa makaazi katika maeneo yaliyokaliwa ya Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki na kukomesha uvamizi wa "kinyume cha sheria" wa maeneo hayo na Ukanda wa Gaza haraka iwezekanavyo.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alijibu kwa kusema kuwa mahakama hiyo ilifanya uamuzi kwa misingi ya uongo.

Chanzo cha picha, Getty images
Maoni ya ushauri wa mahakama hayafungamani kisheria, lakini bado yana uzito mkubwa wa kisiasa.
Serikali nyingi pia zinaamini kuwa makazi ya walowezi wa Israel yanakiuka Mkataba wa Nne wa Geneva uliopitishwa mwaka 1949.
Israel imekanusha kuwa makazi yake ni haramu. Mwaka 2012, serikali ya Israel ilichapisha ripoti ya Tume ya Levy, ambayo ilikataa matumizi ya Mkataba wa Nne wa Geneva kwa Ukingo wa Magharibi. Ripoti hiyo ilidai kuwa Ukingo wa Magharibi haujawahi kuwa sehemu halali ya taifa lolote la kiarabu.
Ripoti hiyo inasema kuwa haki ya kisheria ya Wayahudi kukaa huko, kama inavyotambuliwa na Muungano wa Mataifa wa Udhamini kwa Palestina - League of Nations Trusteeship for Palestine mnamo 1922, imehifadhiwa chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












