Je, nini kilichojadiliwa katika mkutano wa Marekani-Ukraine Saudi Arabia?

.

Chanzo cha picha, EPA

Muda wa kusoma: Dakika 6

Ukraine ilikubali pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano kwa siku 30, lakini kwa masharti kwamba wakati huo huo, Urusi itakubali na kutimiza yanayotarajiwa kutoka upande wake.

Ikijibu, Marekani iliahidi kuanza tena kuipatia vifaa vya kijeshi na ubadilishanaji wa taarifa za kijasusi.

Katika Makala hii tunachanganua matokeo ya mazungumzo kati ya wawakilishi wa nchi hizo mbili nchini Saudi Arabia.

.

Chanzo cha picha, AFP

Kufuatia mazungumzo ya Jeddah, Marekani na Ukraine zilitoa taarifa ya pamoja ikisema kwamba Ukraine iko tayari "kukubali pendekezo la Marekani la kuanzisha mara moja usitishaji vita wa muda wa siku 30, ambao unaweza kuongezwa kwa makubaliano ya pande zote," mradi tu Urusi ikubali kutimiza makubaliano yatakayofikiwa.

Kwa upande wake, Marekani iliahidi kuujulisha uongozi wa Urusi kwamba ushirikiano wa upande zote ndio "msingi wa kupatikana kwa amani."

Taarifa hiyo pia ilibainisha kuwa Marekani "inaanza mara moja ushirikiano wa taarifa za kijasusi na kurejesha usaidizi wa usalama kwa Ukraine."

Kufuatia mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema kwamba sasa "kilichobakia ni Urusi kufanya maamuzi." Ikiwa Urusi "itakataa" pendekezo la kusitisha mapigano, basi "kwa bahati mbaya tutajua kile ambacho ni kikwazo kwa upatikanaji wa amani," Rubio alisisitiza.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pia alibainisha kwamba sasa Marekani "lazima ishawishi Urusi kukubali pendekezo hilo."

Akizungumzia kuhusu wakati ambapo matokeo ya mazungumzo ya Jeddah yatakabidhiwa Urusi, Rubio alisema kuwa upande wa Marekani inatarajia kufanya hivyo "haraka iwezekanavyo."

Muda mfupi baadaye, Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa mkutano kati ya wawakilishi wa Marekani na Urusi utafanyika baadaye Jumanne au Jumatano.

Rais wa Marekani pia alisema ana mpango wa kuzungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin, na kuongeza kuwa kuna uwezekano yakafanyika mapema wiki hii.

Trump pia alisema atamkaribisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwenye Ikulu ya White House tena.

Taarifa ya pamoja ya nchi hizo mbili pia ilisema Marekani na Ukraine walikubaliana kuhitimisha "makubaliano ya kina juu ya maendeleo ya rasilimali muhimu ya madini ya Ukraine" haraka iwezekanavyo.

Aidha, wakati wa mkutano huo, wajumbe walijadili umuhimu wa shughuli za misaada ya kibinadamu kama sehemu ya mchakato wa amani na usitishaji mapigano - ikiwa ni pamoja na kubadilishana wafungwa wa vita, kuachiliwa kwa raia waliowekwa kizuizini na kurudishwa kwa watoto wa Ukraine waliochukuliwa kwa nguvu.

Ukraine pia ilisisitiza umuhimu wa ushiriki wa Ulaya katika mchakato wa mazungumzo, ilisema taarifa hiyo.

Matokeo ya mazungumzo ya Jeddah kwa Ukraine yanachambuliwa na mwandishi wa BBC nchini Ukraine Svyatoslav Khomenko:

Taarifa fupi kufuatia mazungumzo ya Jeddah inafungua mazungumzo ya pande mbalimbali kuhusu mzozo wa Ukraine.

Kwanza, ni wazi kwamba upande wa Ukraine, baada ya kuonyesha upinzani kwa kipindi kifupi, ulikubaliana na mpango wa suluhu ambao timu ya Donald Trump imekuwa ikishinikiza wakati huu wote.

Madai ya awali ya Ukraine – kwanza kabisa, kwamba ipewe hakikisho la usalama kabla ya kutia saini usitishaji vita wowote - yamesahauliwa.

Pendekezo la kutangaza kusitisha mapigano baharini na angani, lakini sio ardhini, ambalo pia Volodymyr Zelensky alisisitiza siku chache zilizopita.

Sasa Kyiv inasema inakubali kusitisha mapigano mara moja na bila masharti, na huu utakuwa uthibitisho ambao Donald Trump anatafuta machoni pake kwamba Ukraine inataka amani.

Ukweli ni kwamba, hii ilikuwa mantiki ya rais wa Marekani. Hakuna anayejua nini kitatokea katika siku zijazo. Usitishaji wa siku thelathini unaweza kufuatiwa na usitishaji vita mwingine wa siku thelathini, na mwingine na mwingine.

Wanaojadiliana wanaweza kuzungumza wakitafuta suluhu kwa yaliyoonekana kuwa vikwazo hadi wafikie muafaka.

Ajenda kuu kwa Trump ni kwamba mashambulizi yakome na watu wasiuliwe tena. Na ukweli kwamba Urusi imevunja makubaliano ya usitishaji mapigano mara kadhaa katika kipindi cha makubaliano ya Minsk haionekani kutiliwa maanani sana na Trump: tuachane na yaliyopita na kugange yajayo.

Zaidi ya hayo, Vladimir Putin binafsi alimwambia kwamba anataka kwa dhati kumaliza vita, na rais wa Marekani anamwamini mwenzake wa Urusi bila masharti.

Je, Volodymyr Zelensky alibadilisha mawazo yake kuhusu Urusi kusitisha mapigano kwa muda ili apate wasaa wa kujipanga upya kijeshi na kuhami jeshi lake kivingine?

Pengine jibu ni hapana au ndio, lakini, hakukuwa na njia nyingine isipokuwa kukubaliana na mpango wa Trump katika hali hii - wakati ni wazi kuwa Ulaya haiko tayari kuchukua nafasi ya Marekani katika suala la kusaidia Ukraine.

Swali kwa sasa ni jinsi gani Ukraine itatumia fursa hii ya kusitisha mapigano.

Pili, sasa mazungumzo ya amani yanategemea muitikio wa Urusi. Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, mjumbe wa Rais wa Marekani Steve Witkoff atasafiri wiki hii Kwenda Urusi. Hii itakuwa sawa na kuingia katika kipindi kisichoweza kutabirika.

Vladimir Putin, inaonekana, hajawahi kutoa sababu yoyote kwa dunia kufikiria kwamba atakubali kukomesha vita hadi "malengo yake yote ya operesheni maalum yatimie," haijalishi hilo litakuwa na maaana gani.

Hivyo basi, ni vigumu kutabiri majibu ya rais wa Urusi kwa pendekezo lililotolewa huko Jeddah.

Putin kukubali huenda kukamaanisha mkutano katika siku za usoni ili kurasimisha usitishaji vita huu wa siku 30 na kuanza mchakato mpana wa mazungumzo unaolenga "kuanzisha amani endelevu ambayo itahakikisha usalama wa muda mrefu wa Ukraine."

Lakini kitakachotokea ikiwa atakataa au kukwepa kutoa jibu la moja kwa moja ni swali la wazi. Tunaweza kujua ikiwa Donald Trump ana uwezo wa kutoa shinikizo kwa Vladimir Putin hata kidogo, na shinikizo hili litakuwaje?

Tatu, tuangazie matokeo yanayoonekana wazi juu ya mazungumzo ya Jeddah kwa ajili ya Ukraine, inaelezwa kwa maneno "Marekani kuondoa mara moja kikwazo cha usitishaji ushirikiano wa taarifa za kijasusi na kurejesha usaidizi wa usalama kwa Ukraine."

Vyanzo vya wanajeshi wa Ukraine viliwaambia waandishi wa habari kwamba kukataa kwa Marekani kutoa msaada huu moja kwa moja kumeathiri utayari wa wanajeshi wa Ukraine katika eneo vita, na habari hii kutoka Jeddah hakika itatia moyo wengi nchini Ukraine.

.

Chanzo cha picha, Ukrainian Presidency / Handout/Anadolu via Getty Images

Mazungumzo yalikwendaje?

Mazungumzo kati ya Marekani na Ukraine huko Jeddah yalichukua zaidi ya saa nane.

Upande wa Ukraine, mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje Andriy Sybiha, Waziri wa Ulinzi Rustem Umerov, na Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Ukraine Andriy Yermak. Naibu Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Ukraine Pavlo Palis pia alikuwepo.

Upande wa Marekani uliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Donald Trump Mike Waltz. Wote wawili tayari walishiriki mazungumzo na Urusi huko Riyadh. Mjumbe Maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati Steve Witkoff pia alitarajiwa kuwepo kwenye mazungumzo hayo mjini Jeddah, lakini hakuonekana kwenye picha zilizochapishwa.

Baada ya masaa matatu ya kwanza ya mazungumzo, mwandishi wa CNN alimuona Rubio na Waltz kwenye ukumbi wa Hoteli ya Ritz-Carlton ambapo mkutano ulikuwa unafanyika. Alipoulizwa jinsi mazungumzo yalivyokuwa yakiendelea, Waltz aliwaambia waandishi wa habari kwa ufupi: "Wanasonga mbele."

Wakati huo huo, afisa mkuu wa Ukraine aliiambia AFP kwa sharti la kutotajwa jina kwamba mazungumzo na Marekani huko Jeddah "yanaendelea vizuri, masuala mengi yameangaziwa." Daria Zarivnaya, mshauri wa mawasiliano kwa mkuu wa Ofisi ya Rais Andriy Yermak, alielezea mkutano huo kwa njia ile ile kwenye akaunti yake katika mtandao wa Telegraph .

Wakati wa mkutano huo, Yermak mwenyewe alichapisha ujumbe uliojumuisha emoji ya kupeana mikono na picha za wajumbe hao wawili.

Baada ya mkutano huo, katibu wa habari wa rais wa Marekani Caroline Leavitt alitaja habari kutoka Jeddah kuwa "chanya" na mkutano "wenye tija."