Urusi yaikana Marekani kuhusu mazungumzo ya Saudi Arabia
Urusi inasema hakuna mazungumzo yoyote yatakayofanyika baina yake na Marekani yatakayofanyika Saudi Arabia kuhusu kuondoa mizozo
Muhtasari
- Watu wawili wathibitishwa kuwa na virusi vya Mpox Tanzania
- Joto kali yasababisha shule kufungwa nchini Sudan Kusini
- Mgomo wasitisha safari zaidi ya 100 za ndege Ujerumani
- Canada yasema 'itashinda' Marekani katika vita vya kibiashara
- Waethiopia waliokwama katika vituo vya utapeli Myanmar warejeshwa
- Zelensky kutua Saudi Arabia katika jitihada za kumaliza mzozo wake na Urusi
- Urusi yaikana Marekani
- Iran yakanusha kuishambulia Syria
- Mchango wa Rais Ruto kwa kanisa wazua ghasia Kenya
- Trump aanza kudhibiti mamlaka ya Elon Musk
- Marekani yasema Ukraine 'iko tayari kusonga mbele' na mpango wa usitishaji mapigano
- Trump asema uchumi wa Marekani uko katika 'mpito' wakati vita vya kibiashara vikiongezeka
- Wadukuzi wa Korea Kaskazini waiba sarafu za kidigitali za mamilioni ya dola za ByBit
- Papa Francis aonyesha 'kuendelea vizuri ' na matibabu, asifu 'huruma' ya wahudumu wa matibabu
Moja kwa moja
Na Lizzy Masinga, Dinah Gahamanyi & Mariam Mjahid
Watu wawili wathibitishwa kuwa na virusi vya Mpox Tanzania

Chanzo cha picha, Reuters
Wizara ya afya ya jamhuri ya Tanzania imethibitsha watu wawili wamegunduliwa na Ugonjwa wa homa ya nyani unaojulikana kama Mpox.
Mmoja wa waathiriwa ni dereva wa lori aliyekuwa ametoka nchi jirani kuelekea Dar es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya sampuli zilichukuliwa na kupelekwa maabara ya kitaifa kwa uchunguzi wa kina na kupata watu wawili wanaathirika na virusi vinavyosababishwa na homa ya nyani.
Wizara ya afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi na vituo vyote vya huduma ya afya nchini humo imetangaza kuendelea na ufuatiliaji, uchunguzi na utambuzi kubaini kama kuna waathiriwa wengine wa virusi hivyo ili wapate matibabu hitajika.
Haya yakijiri Wizara ya Afya imewahakikishia watanzania kuwa serikali imejipanga kudhibiti ugonjwa huu kwa kutoa elimu kwa umma na pia inanuia kuanza upimaji katika mipaka ya nchi hiyo.
Vile vile serikali ya Tanzania imetaka raia wake wajikinge kwani magonjwa yanayaosababishwa na virusi hayana tiba.
Virusi hivyo vinaenea kwa kasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na hivi majuzi nchini Uganda huku wataalamu wakisema ni aina hatari zaidi ya virus
Ugonjwa wa Mpox husababishwa na virusi vya monkeypox, virusi kutoka familia ya virusi vya smallpox.
Awali maambukizi yalianza kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu, hasa katika nchi zilizo karibu na misitu ya mvua ya kitropiki.
Katika maeneo haya, kuna maelfu ya maambukizi na vifo kutokana na ugonjwa huo kila mwaka - na watoto chini ya umri wa miaka 15 wameathirika zaidi.
Huenezwa kwa mgusano wa moja kwa moja na watu walioambukizwa.
Dalili ni pamoja na homa, maumivu ya kichwa, uvimbe, maumivu ya mgongo na misuli kuuma.
Mara baada ya kupata homa, upele unaweza kutokea, mara nyingi huanza kwenye uso kisha kuenea kwenye sehemu nyingine za mwili, viganja vya mikono na nyayo za miguu.
Upele ambao unaweza kuwasha au kuuma, hubadilika hatua tofauti kabla kutengeneza kipele ambacho hupasuka baadaye.
Vidonda vinaweza kusababisha makovu. Maambukizi kwa kawaida huisha yenyewe na hudumu kati ya siku 14 na 21.
Kesi mbaya zinaweza kusababisha vidonda kushambulia mwili mzima, na haswa mdomo, macho na sehemu za siri.
Shirika la Afya Ulimwenguni linashauri ikiwa umeambukizwa Mpox, unapaswa kujitenga kwa kipindi chote cha maambukizi hadi upele utakapo pasuka.
Pia kufunika vidonda na kuvaa barakoa kunaweza kusaidia kuzuia kuenea.
Pia unaweza kusoma:
Joto kali yasababisha shule kufungwa nchini Sudan Kusini

Chanzo cha picha, Paula Bronstein
Maelezo ya picha, Watoto wamefukuzwa shule katika mji mkuu, Juba (picha ya faili) Masomo ya msingi nchini Sudan Kusini yamesitishwa kutokana na ongezeko la joto zinazofikia nyuzi 42.
Kutokana na hali hii ya hewa mamlaka nchini humo zilitangaza kufungwa kwa shule kwa wiki mbili baada ya baadhi ya wanafunzi kuzimia.
‘’Watoto 12 walishindwa kuhimili joto na kukimbiziwa hospitalini kwa matibabu ya dharura’’ anasema Waziri wa Mawasiliano Michael Makuei.
Wanafunzi wengi bado hawajaweza kurejea madarasani.
Wafanyakazi wa serikali pia wameonywa kutofanya kazi nyakati za mchana, huku nchi hiyo ikiendelea kutaabika kutokana na ongezeko la joto kali.
‘’Tangu mwezi Disemba, hatujashuhudia mvua.Watu wameanza kuingiwa na wasiwasi . Tunapata vipindi vya joto jingi kuanzia macweo hadi mawio’’ anasema Abraham Mabior msimamizi wa shule moja huko Sudan Kusini.
Kuongezeka kwa joto sio mara ya kwanza kushuhudiwa nchini humo mwaka jana taifa hilo changa pia lilishuhudiwa hali hiyo ikishurutisha serikali kuchukua hatua ya kusitisha masomo ya msingi.
Ingawa hali hii ya hewa inashuhudiwa shule nyingi zimejengwa na mabati na huzidisha athari ya joto hii ni kwa mujibu wa wasimamizi wa shule za umma.
Wasiwasi umeibuliwa wanafunzi kukosa kushiriki masomo kwa kipindi kirefu huenda wakapata uja uzito kwani wataalam wa masomo wanaamini mazingira ya masomo huhifadhi wanafunzi.
Naye Patrick Sokiri ambaye ni daktari wa masuala ya mwili ametoa wito kwa serikali ifanye mageuzi ya kalenda ya masomo kwani imekuwa hali ya kujirudia joto jingi kushuhudiwa mwezi Machi.
‘’Kwa sababu za kisaikolojia watoto wanaathirikwa zaidi wakikabiliwa na joto jingi mwilini. Ni joto sana haswa nyakati kati ya Februari na Machi. Kwa hivyo nadhani inaweza kuhitaji marekebisho ya kalenda na mambo mengine.’’
Japokuwa taifa la Sudan Kusini linajivunia kuwa na mafuta ni kati ya nchi maskini zaidi duniani.
Joto jingi imekuwa changamoto kubwa huku ikiendelea kukabiliwa na makali ya ukame ba vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Wazee, watoto wachanga na watoto wadogo wako hatarini zaidi kwa sababu miili yao haiwezi kudhibiti joto kwa ufanisi.
Kwa mfano, shirika la The Lullaby Trust nchini Uingereza linapendekeza kuwa joto la chumba cha mtoto mchanga liwe kati ya 16-20°C (60-68°F) ili kuzuia hatari ya kifo cha ghafla cha watoto wachanga (SIDS).
Kwa upande mwingine, wazee wanahitaji nyumba zao ziwe na joto zaidi kwa sababu kasi yao ya metaboli inapungua wanapozidi kuzeeka.
Hii inamaanisha kuwa miili yao haitengenezi joto la kutosha.
Pia, magonjwa kama kisukari yanaweza kuathiri mtiririko wa damu, hivyo kufanya iwe vigumu kwa mwili kupata joto.
Tafiti zinaonyesha kuwa hata nyumba zilizo na joto la 18°C (65°F) zinaweza kusababisha baridi kali kwa wazee, na kuongeza hatari ya hypothermia.
Soma pia:
Mgomo wasitisha safari zaidi ya 100 za ndege Ujerumani

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamia ya safari za ndege zimekatishwa nchini Ujerumani kutokana na mgomo wa wafanyakazi kutokana na maslahi madogo. Hatua hiyo imesababisha usumbufu kwa karibu abiria 500,000.
Mgomo huo ulianza bila kutarajiwa siku ya Jumapili kwenye Uwanja wa Ndege wa Hamburg, kabla ya keener hadi kwenye maeneo mengine ya nchi nzima. Abiria katika miji ya Frankfurt, Munich, Berlin na vituo vingine vikuu wametakiwa kutosafiri kwenda kwenye viwanja vya ndege, huku shughuli zikitatizika kwa kiasi kikubwa.
Chama cha wafanyakazi Verdi, ambacho kinawakilisha wafanyakazi wa sekta ya umma na uchukuzi, kiko kwenye mzozo unaoendelea kuhusu mishahara na mazingira ya kazi.
Vyombo vya habari vya Ujerumani vinaripoti maelfu ya safari za ndege zinaweza kughairiwa siku nzima, na kutatiza safari kwa zaidi ya abiria nusu milioni.
Uwanja wa Ndege wa Munich ulionya kuhusu kupungua zaidi kwa "ratiba ya safari za ndege". Hii ni pamoja na safari za ndege za Eurowings, Austrian Airlines na Swiss Air. Katja Bromm, msemaji wa Uwanja wa Ndege wa Hamburg, ambapo safari zote 143 zilizopangwa kuondoka Jumatatu tayari zimehairishwa.
Soma pia:
Canada yasema 'itaishinda' Marekani katika vita vya kibiashara

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Waziri mkuu mpya wa Canada Mark Carney akitoa hotuba ya ushindi Saa chache baada ya Mark Carney kushinda na kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Liberal nchini Canada, amepinga vitisho vya Donald Trump kuifanya Canada kuwa "jimbo la 51", akisema Canada kamwe haitakuwa sehemu ya Marekani kwa njia yoyote.
Akitarajiwa kuapishwa kuwa waziri mkuu wa 24, na ambaye amebobea katika masuala ya uchumi wa ulimwengu amepinga vikali ushuru uliotozwa na Marekani, akiwaambia wafuasi wake kuwa, “katika biashara, kama ilivyo katika mpira wa Magongo, Canada itashinda.
Akiongea katika hotuba ya ushindi baada ya kumrithi Justin Trudeau aliyejiuzulu mapema mwaka huu Carney amegusia ushuru mpya wa Donald Trump kwa bidhaa zinazotoka Canada kuelekea Marekani, na kuapa kutomruhusu kufanikiwa. Alisema pia kuwa Canada itatekeleza mikakati yake ya kulipiza kisasi.
''Serikali ya Canada imelipiza kisasi kwa njia ifaayo na tunalipiza kisasi na ushuru wetu ambao utakuwa na athari kubwa kwa Marekani na athari ndogo kwa Canada. Serikali yangu itatekeleza ushuru wetu hadi Marekani watuonyeshe heshima. Hadi watakapo ungana nasi kutengeneza misimamo ya kuaminika na kutegemewa katika biashara huru.''
Carney pia amehakikishia Wacanada kuwa chama cha Liberal kitaendelea kusimamia uwajibikaji wa fedha, haki ya jamii na uongozi wa kimataifa.
''wakati huu, tutahakikisha mapato kutoka kwenye ushuru wetu yatatumika kuwalinda wafanyakazi wetu."
Haya yanajiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza atatoza ushuru wa asilimia 25% kwa bidhaa za chuma na alumini zinazoingia Marekani kutoka Canada.
Pia unaweza kusoma:
Waethiopia waliokwama katika vituo vya utapeli Myanmar warejeshwa

Chanzo cha picha, Thai News Pix
Maelezo ya picha, Matapeli wa mtandaoni hutafuta wafanyakazi wanaojua lugha za wale wanaolengwa kufanyiwa utapeli, udanganyifu au wizi wa mtandaoni, mara nyingi ni lugha ya Kiingereza na Kichina. Makumi ya raia wa Ethiopia ambao walikuwa wamezuiliwa na magenge ya utapeli na kuhangaishwa nchini Myanmar wamerejeshwa nchini kwao.
Mwezi jana, zaidi ya watu 250 kutoka mataifa 20, ikiwemo Tanzania na Kenya ambao walikuwa wakifanya kazi katika vituo vya utapeli na wizi wa mtandaoni katika Jimbo la Kayin, nchini humo wameachiliwa na moja ya makundi ya kijeshi huko Myanmar, na kupelekwa Thailand.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Ethiopia imetangaza inashirikiana na ubalozi wake ulioko India, raia wake 32 kati ya 133 wamerejeshwa nyumbani haya ni kwa mujibu wa gazeti moja nchini humo.
Serikali ya Ethiopia pia imetoa wito kwa umma kuepuka hadaa zinazotolewa na magenge ya utapeli, ili kuepuka uhamiaji haramu kwenda katika nchi ambazo mikataba ya ajira haina dhamana.
Wafanyabiashara na wamiliki wa vituo ama ofisi hizo hutafuta wafanyakazi wanaojua lugha za wale wanaolengwa kufanyiwa utapeli, udanganyifu au wizi wa mtandaoni, mara nyingi ni lugha ya Kiingereza na Kichina.
Wamekuwa wakiingizwa katika shughuli za uhalifu mtandaoni, kuanzia ulaghai wa mapenzi unaojulikana kama "pig butchering" na wizi wa fedha kwa njia ya mtandao, hadi utakatishaji wa fedha na kamari haramu.
Baadhi yao waliridhia kufanya kazi hii, lakini wengine walilazimishwa kufanya kazi hiyo, na kuachiliwa kwao kunategemea familia zao kulipa fidia kubwa.
Baadhi ya wale waliofanikiwa kutoroka wamesema walikuwa wakiteswa.
Wiki moja iliyopita, Serikali ya Kenya ilitangaza kuwa inajadiliana na serikali ya Thailand ili kufungua tena mpaka wa Thailand na Mnyamar ili kuwahamisha Wakenya 64 waliookolewa kutoka katika mitandao ya magendo ya binadamu nchini Myanmar.
Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora ilifichua kwamba kundi hilo limekwama mpakani na ni miongoni mwa raia wa kigeni zaidi ya 7,000 walioachiliwa na makundi yenye silaha lakini hawakuweza kuvuka kufika Thailand tangu Februari 12, lakini kundi la kwanza la watu 260 wakiwemo Wakenya 23 waliruhusiwa kupita.
"Serikali ya Kenya inashauriana na Serikali ya Thailand ili kivuko cha mpaka kifunguliwe tena kwa misingi ya kibinadamu ili kuruhusu raia waliookolewa kuingia katika eneo la Thailand na kurejeshwa Kenya," imesema taarifa ya wizara hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la KBC, Wizara hiyo ilisema Balozi wa Kenya nchini Thailand amekuwa akiwasiliana kila siku na raia hao huku maafisa wakitafuta njia mbadala za kuwarudisha nyumbani.
Wakati huohuo, hali katika kambi za kijeshi za muda katika Jimbo la Karen nchini Myanmar ambako waathiriwa wamehifadhiwa ni mbaya kutokana na upatikanaji mdogo wa matibabu, maji safi, umeme na vyoo.
Soma pia:
Zelensky kutua Saudi Arabia katika jitihada za kumaliza mzozo wake na Urusi

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock
Rais Volodymyr Zelensky amesafiri Saudi Arabia kukutana na mwana mfalme Mohammed bin Salman akitarajia kufanya majadiliano kati yake na ujumbe wa Marekani kusitisha vita na Urusi.
Marekani ambayo kwa wakati mmoja ilikuwa na ukaribu na Ukraine imebadilisha sera zake za kivita kwa kufanya mazungumzo moja kwa moja na Moscow huku wakisitisha usaidizi wa kijeshi na ujasusi kwa Kyiv.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio na mshauri wa kitaifa wa usalama Mike Waltz wanatarajiwa pia kufika Saudia kwa mazungumzo ambayo yanatarajiwa kufanyika hapo kesho siku ya Jumanne.
Ujumbe huo wa Marekani unaazimia kubuni sera na mpango mkakati utakaoleta amani na kuanzisha awamu ya kwanza ya kusitisha mapigano kati ya Ukraine na Urusi .
Rais wa Marekani Donald Trump ameendelea kushinikiza Rais wa Ukraine kukubali matakwa yake ili mapigano yasitishwe- bila ya kumhakikishia kuwa Marekani itadumisha usalama.
Siku kumi zilizopita Trump na Zelensky walirushiana maneno katika ikulu ya White house huku Trump akidai Rais wa Ukraine hayuko tayari kusitisha mapigano.
Soma pia:
Urusi yaikana Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi imekana kuwepo kwa mazungumzo baina yake na Marekani huko Saud Aarabia. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov anasema Urusi na Marekani ziko katika “hatua za awali za kurejesha uhusiano wetu”.
Akizungumza na wanahabari amesema: “itakuwa ni safari ndefu na ngumu, lakini angalau Marais wawili wameonyesha utashi wao wa kisiasa kueleka katika muelekeo huu.”
Ameongeza kuwa Maraisi wa Marekani Urusi, wamezungumza mara moja tangu Donald Trump aingie madarakani kaika amwamu ya pili.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, mazungmzo yalikuwa “yakujenga kiasi yanatosha kutatua matatizo”.
Iran yakanusha kuishambulia Syria

Chanzo cha picha, Reuters
Wizara ya ulinzi ya Syria imetengaza rasmi kusitisha operesheni za kijeshi katika Ukanda wa nchi hiyo wakithibitisha kupitia kanali Hassan Abdul Ghani, kuwa taasisi za umma zimerejea na shughuli za kawaida.
Kulingana na serikali mpya vikosi vya usalama vitaendelea kushika doria na kudumisha amani na kuhakikishia usalama wa wakaazi.
Wizara hiyo pia imethibitisha kuwa imebuni mikakati ya kukabiliana na watu wanaounga mkono utawala wa Assad ulioanguka na kuhakikisha hawatakuwa tishio siku za usoni.
Awali, wizara ya ulinzi imetangaza vikosi vyake vimetibua shambulizi lilikuwa litekelezwe katika eneo la Ashrafieh iliyoko Aleppo, ambayo ingesababisha hasara kubwa.
Rais mteule wa Syria Ahmad al-Sharaa amedokeza atawajibisha yeyote atakayepatikana na ''hatia ya mauaji ya raia '' kufuatia mapigano kati ya wanajeshi wa Syria na vikosi vya Rais Bashar- al- Assad ambapo watu elfu moja waliuawa.
Umoja wa Mataifa, na Marekani wameshutumu vikali mauaji hayo ya raia wakitaka mamlaka ya Syria kukomesha uhalifu huo wa kivita.
Rais huyo wa Syria pia ametangaza kubuni jopokazi huru ichunguze mauaji hayo yaliyofanyika magharibi mwa nchi hiyo akidokeza itahusisha watu saba.
Wakati huo huo,Iran imekanusha shutuma kwamba ilihusika katika vurugu katika eneo la pwani ya magharibi mwa Syria, baada ya ripoti za vyombo vya habari kudokeza uwezekano wa Tehran katika mapigano makali zaidi tangu kuondolewa madarakani kwa mshirika wake,aliyekuwa Rais Bashar al-Assad.
"Tuhuma hii ni ya kipuuzi na haikubaliki kabisa, na tunaamini kuwa kunyooshea vidole Iran na marafiki wa Iran ni makosa...na kwa asilimia 100 ni kupotosha," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Esmail Baghaei alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari wa kila wiki.
Huku kukiwa na uvamizi zaidi wa Israel nchini Syria, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Katz alitangaza kuwa wakaazi wa eneo la kusini mwa Syria la Druze wataruhusiwa kuingia kwenye milima ya Golan inayokaliwa na Israel kwa ajili ya kuajiriwa "kuanzia wiki ijayo", shirika la utangazaji la Israel la Kan liliripoti jana.
Pia unaweza kusoma:
Mchango wa Rais Ruto kwa kanisa wazua ghasia Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images
Polisi nchini Kenya wamefyatua gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakijaribu kuvamia kanisa ambalo lilipokea mchango mkubwa kutoka kwa Rais William Ruto.
Zawadi ya shilingi milioni 20 (karibu dola 155,000 au pauni 120,000) kwa Jesus Winner Ministry huko Roysambu, Nairobi, imelaaniwa na baadhi ya vijana wa Kenya wanaokutana na changamoto kubwa ya gharama ya juu ya maisha.
Ruto alitetea mchango wake na aliahidi kutoa zawadi kama hiyo kwa kanisa jingine huko Eldoret.
Mwaka jana, viongozi wa makanisa ya Kikatoliki na Anglikana nchini Kenya walikataa zawadi, wakisema kuwa ni muhimu kulinda makanisa dhidi ya kutumika kwa madhumuni ya kisiasa.
Watu kadhaa wamekamatwa katika ghasia hizo, ambapo waandamanaji walijaribu kuingia kanisani, kuwasha moto na kutumia mawe kuzuia barabara zinazozunguka eneo hilo.
Hata hivyo, ibada ya kanisa iliendelea kama kawaida huku kukiwa na ulinzi mkali , kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.
Trump aanza kudhibiti mamlaka ya Elon Musk

Chanzo cha picha, Getty
Rais wa Marekani Donald Trump alifanya mkutano na Baraza lake la Mawaziri na kusema kwamba usemi wa mwisho juu ya sera ya wafanyakazi utatolewa na wakuu wa mashirika ya shirikisho, sio mkuu wa DOGE Elon Musk.
Vyombo vya habari vya Reuters, Politico na CNN vimeripoti ripoti hii, wakinukuu vyanzo vya kuaminika vya serikali.
Mkutano wa Trump na viongozi wa mashirika ya shirikisho ulichukua dakika 90 na haukuwajumuisha waandishi wa habari. Hata hivyo, vyombo vya habari vinaeneza habari vikiwanukuu viongozi walioshiriki mkutano huo..
Rais Trump amesema anaunga mkono kikamilifu juhudi za Elon Musk za kupunguza idadi ya wafanyakazi na matumizi katika serikali ya shirikisho. Lakini Trump alisema kuwa Idara ya ufanisi wa Serikali, inayoongozwa na Musk, inapaswa kuwa na jukumu la ushauri tu, Reuters imeripoti.
Elon Musk amesema hadharani kwamba anakubaliana na agizo la Trump. Kulingana na Politico, idara inayoongozwa na Musk ilikiri kuwa "ilifanya makosa kadhaa."
Unaweza pia kusoma:
Marekani yasema Ukraine 'iko tayari kusonga mbele' na mpango wa usitishaji mapigano

Chanzo cha picha, EPA
Utawala wa Trump unadhani kuwa uongozi wa Ukraine "uko tayari kuendelea" na pendekezo la Marekani la kuanzisha mchakato wa kusitisha mapigano na Urusi, kulingana na afisa mmoja mwandamizi wa Idara ya Nchi za Nje za Marekani.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Marco Rubio, na Mshauri wa Usalama wa Taifa, Mike Waltz, wanatarajiwa kufika Saudi Arabia kwa mazungumzo na wenzao wa Ukraine siku ya Jumanne.
Rais Donald Trump ameongeza shinikizo kwa rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kumkubalia ombi lake la kusitisha mapigano haraka na Moscow - lakini bila ahadi ya mara moja ya dhamana ya usalama kutoka Marekani.
Siku kumi zilizopita, wawili hao waligombana hadharani kwenye Ikulu ya White House, ambapo Trump alidai kuwa Zelensky hakuwa tayari kumaliza mapigano.
Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alianzisha uvamizi wa kijeshi nchini Ukraine mnamo Februari 2022, na Moscow kwa sasa inadhibiti takribani 20% ya ardhi ya Ukraine.
Unaweza kusoma;
Trump asema uchumi wa Marekani uko katika 'mpito' wakati vita vya kibiashara vikiongezeka

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amekataa kusema kama uchumi wa Marekani unakabiliwa na hali ya kuporomoka au kupanda kwa gharama za bidhaa kutokana na mabadiliko ya msimamo wa utawala wake kuhusu vitisho vya ushuru dhidi ya baadhi ya washirika wake wakubwa wa kibiashara.
Alipoulizwa kama anatarajia hali ya kuporomoka kwa uchumi mwaka huu, Trump alisema kwamba kuna "kipindi cha mabadiliko" kinachotokea.
Waziri wa Biashara Howard Lutnick, hata hivyo, alisisitiza kwamba hakutakuwa na kuporomoka kwa uchumi mkubwa zaidi duniani, ingawa alikiri kwamba bei ya baadhi ya bidhaa inaweza kuongezeka.
Haya yanajiri baada ya wiki yenye mabadiliko makubwa kwa masoko ya fedha ya Marekani wakati wawekezaji wakikumbana na hali ya siutafahamu kutokana na mabadiliko ya msimamo wa utawala wake kuhusu baadhi ya sehemu muhimu za sera zake za biashara.
Unaweza kusoma;
Wadukuzi wa Korea Kaskazini waiba sarafu za kidigitali za mamilioni ya dola za ByBit

Chanzo cha picha, Getty Images
Wadukuzi wanaoshukiwa kuwa wanatumikia utawala wa Korea Kaskazini wamefanikiwa kutengeneza kiasi cha takribani $300m (£232m) kutoka kwenye wizi wao mkubwa wa $1.5bn za fedha za kidigitali.
Wahalifu hawa, wanaojulikana kama Kikundi cha Lazarus, walivamia na kuiba kiasi kikubwa cha fedha za kidijitali kwenye ubadilishaji wa crypto wa ByBit wiki mbili zilizopita.
Tangu wakati huo, imekuwa kama mchezo wa paka na panya kufuatilia na kuzuia wahalifu hawa wasifanikiwe kubadilisha fedha hizo kuwa pesa za kawaida.
Wataalamu wanasema kwamba timu hii maarufu ya wahalifu inafanya kazi karibu saa 24 kwa siku na inaweza kuwa inatuma fedha hizo kwa ajili ya maendeleo ya kijeshi ya utawala wa Korea Kaskazini.
"Wanajaribu kuchanganya njia ya fedha na ni watu wenye ujuzi mkubwa katika wanachokifanya," anasema Dr. Tom Robinson, mwanzilishi mwenza wa uchunguzi wa crypto kutoka kampuni ya Elliptic.
Kati ya wahalifu wote wanaohusika na fedha za crypto, Korea Kaskazini ndio bora zaidi katika kusafisha fedha za crypto, anasema Dr. Robinson.
"Nadhani wana chumba kizima cha watu wanaofanya kazi hii kwa kutumia zana za kiatomatiki na uzoefu wa miaka mingi. Tunaweza pia kuona kutoka kwenye shughuli zao kwamba huchukua mapumziko kwa saa moja kwa siku, labda wakifanya kazi kwa zamu ili kufanikisha crypto ibadilishwe kuwa pesa."
Marekani na washirika wake wanawaashiria Wakorena Kaskazini kwa kutekeleza mfululizo wa uvamizi katika miaka ya hivi karibuni ili kufadhili maendeleo ya kijeshi na ya nyuklia ya utawala wao.
Mnamo tarehe 21 Februari, wahalifu walivamia mmoja wa wasambazaji wa ByBit ili kubadilisha kwa siri anwani ya mkoba wa dijitali ambapo sarafu 401,000 za Ethereum zilikuwa zinatumwa.
ByBit ilidhani ilikuwa inapeleka fedha hizo kwenye mkoba wake wa digitali, lakini badala yake ilitumwa yote kwa wahalifu.
Unaweza kusoma;
Papa Francis aonesha 'maendeleo mazuri ', asifu 'huruma' ya wahudumu wa matibabu

Chanzo cha picha, Getty Images
Papa Francis, ambaye amekuwa akiugua homa ya mapafu kwa zaidi ya wiki tatu, aliwasifu wahudumu wa afya wanaomhudumia kwa uangalizi wao "wa huruma".
Kwa Jumapili ya nne mfululizo, papa wa Argentina hakuwepo kutoa baraka zake za kila wiki, lakini Vatican ilishiriki maandishi yaliyotayarishwa na papa.
"Nikiwa hapa, ninafikiria watu wengi ambao wako karibu na wagonjwa," Papa alisema, akimaanisha wafanyakazi wa matibabu, akiwaelezea kama watu wenye "kuleta mwanga kidogo katika usiku wa maumivu."
Vatican ilisema Jumamosi kwamba papa ameonesha "mwitikio mzuri" katika siku za hivi karibuni katika matibabu yake yanayoendelea katika Hospitali ya Gemelli ya Roma.
Francis aliandika kwamba anahisi "kutunzwa kwa busara na huruma, hasa kutoka kwa madaktari na wafanyakazi wa afya, ambao ninawashukuru kutoka moyoni mwangu."
"Nafikiria watu wengi walio karibu na wagonjwa kwa njia mbalimbali, ambao ni ishara ya kuwapo kwa Bwana," aliongeza.
"Tunahitaji huu - muujiza wa wema - ambao wale walio katika dhiki wanauhitaji, na ambao huleta mwanga mdogo katika usiku wa maumivu," aliongeza.
Unaweza pia kusoma:
Hujambo na karibu kwa matangazo haya ya mubashara ya Jumuatatu tarere 10.03.2025, tukikuletea habari za kikanda na kimataifa.
