Elon Musk atanufaika vipi na urais wa Donald Trump?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Lily Jamali
- Nafasi, North America technology correspondent
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Kurudi kwa Donald Trump katika Ikulu ya White House kunaweza pia kuwa ushindi kwa mmoja wa wafuasi wake wanaoonekana: Elon Musk.
Mtu tajiri zaidi duniani alisalia na Trump usiku wa uchaguzi huko Florida katika makazi yake ya Mar-a-Lago wakati matokeo yalipokuwa yakitolewa .
"Watu wa Marekani walimpa @realDonaldTrump mamlaka ya wazi ya mabadiliko usiku wa leo," Bw Musk aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X huku ushindi wa Trump ukianza kuonekana.
Na katika hotuba yake ya ushindi katika Palm Beach Convention Center, Trump alitumia dakika kadhaa kumsifu Bw Musk na kusimulia kufanikiwa kurushwa angani kwa roketi iliyotengenezwa na kampuni moja ya Bw Musk, SpaceX.
Bw Musk aliunga mkono chama cha Republican mara tu baada ya jaribio la kumuua Trump huko Butler, Pennsylvania mwezi Julai.
Akiwa mmoja wa waungaji mkono muhimu wa rais mteule, bilionea huyo wa teknolojia alichangia zaidi ya $119m (£92m) kufadhili kundi la kumuunga mkono Trump Super PAC lililomfanyia kampeni Donald Trump.
Pia alitumia wiki za mwisho kabla ya siku ya uchaguzi kuendesha juhudi za kuwahamasisha watu kujitokeza kupiga kura katika majimbo yaliyokuwa muhimu kwa wagombea urais ili kushinda uchaguzi pamoja na zawadi ya kila siku ya $ 1m kwa wapiga kura katika majimbo hayo. Zawadi hiyo ikawa mada ya pingamizi la kisheria, ingawa hakimu baadaye aliamua kwamba wanaweza kuendelea .
Baada ya kuweka jina lake, pesa na jukwaa lake nyuma ya Trump, Bw Musk ana mengi ya kupata kutokana na kuchaguliwa tena kwa Trump.
Rais mteule amesema kuwa katika muhula wa pili, atamualika Bw Musk katika utawala wake ili kuondoa ubadhirifu wa serikali.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Bw Musk ametaja juhudi zinazowezekana kuwa "Idara ya Ufanisi wa Serikali," au DOGE, jina la sarafu ya kidijitali ambayo ameitangaza.
Mfanyabiashara huyo pia anaweza kufaidika na urais wa Trump kupitia umiliki wake wa SpaceX, ambayo tayari inatawala biashara ya kutuma satelaiti za serikali angani.
Akiwa na mshirika wa karibu katika Ikulu ya White House, Bw Musk anaweza kutafuta kujinufaisha zaidi kupitia uhusiano huo na serikali.
Bw Musk amewakosoa wapinzani ikiwa ni pamoja na Boeing kwa muundo wa kandarasi zake za serikali , ambazo anasema zinakatisha tamaa kumaliza miradi kwa bajeti na kwa wakati.
SpaceX pia imehamia katika kujenga satelaiti za kijasusi wakati Pentagon na mashirika ya kijasusi ya Marekani yanaonekana kuwa tayari kuwekeza mabilioni ya dola katika mpango huo.
Tesla inayotengeneza magari ya umeme ya Bw Musk inaweza kuvuna faida kutoka kwa serikali ambayo Trump amesema itatambulika kwa "mzigo mdogo zaidi wa udhibiti."
Mwezi uliopita tu, wakala wa Marekani anayesimamia udhibiti wa usalama barabarani alifichua kuwa anachunguza mifumo ya programu ya Tesla ya kujiendesha kwenye gari.
Bw Musk pia amekashifiwa kwa madai ya kutaka kuwazuia wafanyikazi wa Tesla kujiunga na chama cha kutetea maslahi yao. Wafanyakazi wa United Auto Workers walifungua mashtaka dhidi ya Trump na Musk baada ya wawili hao kuzungumza juu ya Musk akisema angeweza kuwafuta kazi wafanyikazi wanaogoma wakati wa mazungumzo juu ya X.
Trump pia ameahidi kupunguza ushuru kwa mashirika na matajiri.
Hiyo ni ahadi nyingine ambayo Bw Musk huenda anatumai ataitimiza.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Seif Abdalla












