Uchaguzi wa Marekani 2024: Ahadi saba za Trump atakazozitekeleza kama rais

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, James FitzGerald
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Donald Trump anarejea Ikulu ya White House, baada ya kuahidi atachukua hatua kuhusu masuala ya uhamiaji, uchumi na vita nchini Ukraine. Na katika Bunge la Congress, Chama chake cha Republican kinadhibiti Seneti.
Katika hotuba yake ya ushindi, Trump aliapa "atatawala kwa kauli mbiu: Ahadi zilizotolewa, zitatekelezwa. Tutatimiza ahadi zetu."
Lakini katika baadhi ya mambo, ametoa maelezo machache kuhusu jinsi anavyoweza kufikia malengo yake.
Kuwafukuza wahamiaji wasio na vibali
Wakati akifanya kampeni, Trump aliahidi uhamisho mkubwa wa wahamiaji wasio na vibali katika historia ya Marekani.
Pia aliahidi kukamilisha ujenzi wa ukuta kwenye mpaka na Mexico ambao ulianza wakati wa muhula wake wa kwanza.
Wataalamu wameiambia BBC, kufukuzwa wahamiaji kwa kiwango kilichoahidiwa na Trump kutakabiliwa na changamoto kubwa za kisheria na utaratibu - na kunaweza kupunguza ukuaji wa uchumi.
Uchumi, kodi na ushuru
Kupitia kura ya maoni inaonyesha uchumi ulikuwa suala muhimu kwa wapiga kura. Trump ameahidi "kumaliza mfumuko wa bei" - ambao umepanda hadi viwango vya juu chini ya Rais Joe Biden kabla ya kupungua tena. Lakini uwezo wa rais kupungua bei moja kwa moja ni mdogo.
Amependekeza ushuru mpya wa 10% kwa bidhaa nyingi za kigeni, ili kupunguza nakisi ya biashara. Uagizaji bidhaa kutoka China unaweza kubeba ushuru wa ziada wa 60%, amesema. Baadhi ya wachumi wameonya kuwa hatua kama hizo zinaweza kuongeza bei kwa watu wa kawaida.
Kanuni za mabadiliko ya tabia nchi
Wakati wa urais wake, Trump aliondoa mamia ya kanuni za ulinzi wa mazingira na kuifanya Marekani kuwa taifa la kwanza kujiondoa katika makubaliano ya tabia nchi ya Paris.
Ameapa kupunguza tena kanuni hizo, kama njia ya kuisaidia tasnia ya magari. Amekuwa akiyashambulia magari ya umeme, na ameahidi kupindua malengo ya usafiri safi ya Biden.
Ameahidi kuongeza uzalishaji wa nishati ya mafuta - akiapa "kuchimba mafuta zaidi" – lakini anapendelea vyanzo vya nishati mbadala kama vile nishati ya upepo.
Anataka kufungua maeneo kama vile Arctic kwa uchimbaji wa mafuta, ambayo anasema yatapunguza gharama za nishati.
Kumaliza vita vya Ukraine
Trump amekosoa mabilioni ya dola zilizotumiwa na Marekani kusaidia Ukraine katika vita vyake na Urusi - na ameahidi kumaliza mzozo huo "ndani ya saa 24" kupitia makubaliano.
Trump anataka Marekani ijitenge na migogoro ya kigeni kwa ujumla. Kuhusu vita vya Gaza- Trump amejiweka kama mfuasi mkubwa wa Israel, lakini amemtaka mshirika huyo wa Marekani kusitisha operesheni yake.
Pia ameahidi kukomesha ghasia za Lebanon, lakini hakutoa maelezo namna atakavyo fanya hivyo.
Hakuna marufuku ya utoaji mimba
Kinyume na matakwa ya baadhi ya wafuasi wake, Trump alisema wakati wa mjadala wa urais na Kamala Harris, hatatia saini sheria ya marufuku ya kitaifa ya utoaji mimba.
Mwaka 2022, haki ya kikatiba ya nchi nzima ya kutoa mimba ilibatilishwa na Mahakama ya Juu, ambayo ilikuwa na majaji wengi wa kihafidhina walioteuliwa na Trump.
Haki za uzazi zikawa mada kuu katika kampeni za Harris, na majimbo kadhaa yameidhinisha hatua za kulinda au kupanua haki za uavyaji mimba siku ya kupiga kura.
Trump mwenyewe amekuwa akisema mara kwa mara, majimbo yanapaswa kuwa huru kujiamulia sheria zao kuhusu uavyaji mimba.
Msamaha wa Januari 6
Trump amesema "atawaachilia huru" baadhi ya wale waliopatikana na hatia ya makosa wakati wa ghasia huko Washington DC, 6 Januari 2021, wafuasi wake walipovamia jengo la Capitol katika juhudi za kuzuia ushindi wa 2020 wa Joe Biden.
Vifo kadhaa vilitokea kutokana na ghasia hizo, ambazo Trump alishutumiwa kuzichochea.
Amefanya kazi ili kupunguza ukali wa ghasia hizo na kuwataja mamia ya wafuasi wake waliopatikana na hatia kama wafungwa wa kisiasa.
Anaendelea kusema wengi wao "wamefungwa kimakosa," ingawa amekiri kwamba "wachache wao, huenda walivuka mstari."
Kumfuta kazi Jack Smith
Trump ameapa kumfukuza kazi "ndani ya sekunde mbili" baada ya kuchukua ofisi mwendesha mashtaka anayeongoza uchunguzi wa uhalifu dhidi yake.
Wakili Maalum Jack Smith amemfungulia mashtaka Trump kwa madai ya kuupindua matokeo ya uchaguzi wa 2020, na kwa madai ya ubadhirifu wa nyaraka za siri.
Trump anakanusha makosa yoyote, na aliweza kuzuia kesi zote mbili kusikilizwa kabla ya uchaguzi. Anasema Smith anamuwinda kisiasa.
Trump atarejea Ikulu ya White House kama rais wa kwanza kuwahi kuwa na hatia ya uhalifu, baada ya kupatikana na hatia mjini New York ya kughushi rekodi za biashara.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












