China na Marekani: Nani kuibuka mbabe katika vita yao inayofukuta?

Chanzo cha picha, Getty Images
China imeionya Marekani wiki hii kwamba iko tayari kupigana vita ya "aina yoyote" baada ya kujibu vikwazo vya kibiashara vilivyotangazwa na Donald Trump
Nchi mbili zenye uchumi mkubwa zaidi duniani zimekaribia kuingia kwenye vita. Vita ya kibiashara baada ya Trump kuweka vikwazo zaidi vya kibiashara kwa bidhaa zote za China. China ilijibu haraka kwa kuweka vikwazo (ushuru) wa asilimia 10-15 kwa bidhaa za kilimo za Marekani.
Ubalozi wa China mjini Washington, katika chapisho lake kwenye mtandao wa X, ulisema: "Ikiwa vita ndivyo Marekani inavyotaka, iwe ni vita vya ushuru, vita vya biashara au aina nyingine yoyote ya vita, tuko tayari kupigana hadi mwisho. Swali hapa katika vita hii nani atashinda?
Chanzo cha vita vya mafahari wawili
Kwa sababu ya ukubwa wa mataifa haya, vita vyao vyovyote vinaitwa vita vya mafahari wawili. Na vita hivi vimekuwepo kwa muda kidogo lakini kwa hivi karibuni, mvutano huu ulianza na sera za "America First" za Rais wa Marekani, Donald Trump, katika awamu yake ya kwanza ya utawala, ambaye aliamini kuwa China ilikuwa ikiitumia Marekani vibaya kibiashara. Alianzisha vikwazo vya ushuru kwa bidhaa za China, na China ikajibu kwa vikwazo vyake.
Hata baada ya Trump kuondoka madarakani, mvutano uliendelea, akaja kuurithi Rais Marekani, Joe Biden, ambaye aliendeleza baadhi ya sera za mtangulizi wake na kuongeza vikwazo vipya.
Lakini baada ya kurejea rasmi mamlakani mwaka huu, Trump akakazia zaidi vikwazo dhidi ya bidhaa za China na hapo ukaibuka mvutano mkubwa wiki na kauli nzito kutoka kwa mamlaka za China.
"tuko tayari kwa vita ya aina yoyote'. Hii ilikuwa kauli nzito kuwahi kutolewa na China tangu trump aingie madarakani.
Kiongozi wa China, Li Keqiang alisema pia Jumatano kwamba nchi yake itaongeza bajeti yake ya ulinzi kwa asilimia 7.2 mwaka huu na kuonya kwamba "dunia inapitia mabadiliko makubwa na ya kasi kuliko ilivyokuwa karne iliyopita.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
kauli za kuongeza bajeti ya ulinzi na vikwazo vya kibiashara baina ya China na Marekani, wengi wamekuwa na maswali. Kwamba vita vya kibiashara vilivyoanza, vitavuka mipaka na kufikia vta vya kisilaha?
Usisahau pia kwamba kuna hili lingine la habari ya China Kusini ambayo imekuwa kitovu cha mvutano, huku madai ya China yakizidisha mvutano kati ya Taiwan, Ufilipino na hata Marekani, taifa rafiki ambalo linaunga mkono nchi zote mbili.
Katika mvutano ya mwaka jana wanajeshi wa pwani ya China waliripotiwa kupanda meli ya Ufilipino na kuwashambulia wanajeshi kwa mapanga na visu.
Marekani, kwa upande mwingine, ikaja kuanzisha mashirikiano kadhaa ya kijeshi na nchi kama vile Ufilipino na Japan, na kuhaidi kulinda haki za washirika wake katika Bahari ya Kusini ya China.
Na hii ikasababisha kuzorota zaidi kwa uhusiano kati ya Marekani na China. kwa hivyo uhusiano wa Marekani na China punatikiswa na masuala matatu: uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, mvutano kati ya China na Taiwan, na vita vya kibiashara.
Wakati huo balozi wa Marekani nchini China, Robert Nicholas Burns alikiri kwamba masuala haya yanasalia kuwa chanzo cha "mgawanyiko" kati ya nchi hizo mbili. Kwa upande mwingine, anasema ni muhimu kufanya jitihada za "kuwaleta watu pamoja" katika maeneo ambayo inawezekana.
"China imekubali kuongeza mawasiliano ya kijeshi na Marekani. Hili ni muhimu sana kwetu. Mawasiliano ni muhimu, ni jambo lisiloepukika kabisa kwani ajali na kutoelewana kutasababisha migogoro."
Vita ya nguvu za kiuchumi na athari zake
Marekani ina uchumi mkubwa zaidi duniani, na nguvu kubwa ya kiteknolojia na kifedha. China yenyewe ni nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani, na inakua kwa kasi. Ni kitovu cha uzalishaji wa bidhaa nyingi za dunia.
Vita ya kibiashara inaweza kuathiri vibaya uchumi wa nchi zote mbili, na pia uchumi wa dunia kwa ujumla. Nchi hizi zinashindana sana katika maeneo haya.
Ushindani wa kiteknolojia:
Nchi zote mbili zinashindana katika teknolojia muhimu kama vile akili mnembo (AI), 5G, na kompyuta za quantum. Nani atakayeongoza baina yao katika teknolojia hizi atakuwa na faida kubwa.
Ushirikiano wa kimataifa:
Nchi zote mbili zinajaribu kujenga ushirikiano na nchi nyingine ili kupata uungwaji mkono. Ushirikiano huu unaweza kuwa na athari kubwa katika matokeo ya vita.
Athari kwa watumiaji:
Vita ya kibiashara inaweza kusababisha kupanda kwa bei ya bidhaa kwa watumiaji katika nchi zote mbili. Hii inaweza kusababisha hasira ya umma na shinikizo kwa serikali. Lakini vita vyao vinaweza kuathiri hata mataifa mengine, ikiwemo ya Afrika yanayotegemea sana bidhaa za China na baadhi Marekani, pamoja na huduma zingine na misaada kutoka nchi hizo.
Achilia mbali, vita ya kibiashara ikuweza kuathiri utulivu wa kisiasa ndani ya nchi zote mbili.
Kuibuka kwa vita vya kijeshi? na je nani kushinda?
Ingawa hakuna anayetaka kuwepo kwa vita halisi kama ilivyo kwa Ukraine na Urusi, lakini kuna hatari kwamba mvutano unaweza kuongezeka na kusababisha mapigano ya kijeshi.
Kauli kama hizi za ubalozi wa china nchini Marekani, zinatishia hilo kutokea.
"Kama Marekani inataka vita, iwe vya kikodi, kibiashara au vita vya aina yoyote ile, tuko tayaritutapigana mpaka mwisho.
Ikiwa itatokea hivyo, swali la kujiuliza nani ataibuka mshindi?
Ni vigumu kutabiri nani atashinda vita hii. Ushindi hautapimwa tu kwa ukuaji wa uchumi, bali pia kwa mambo mengine kama vile ushawishi wa kisiasa na kiteknolojia.
Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba vita ya kibiashara haina mshindi wa kweli. Nchi zote mbili zitapata hasara, na pia uchumi wa dunia kwa ujumla.
Hivyo mvutano kati ya China na Marekani ni changamoto kubwa kwa dunia. Ni muhimu kwa nchi zote mbili kutafuta njia za kutatua tofauti zao kwa amani na kuepuka vita ambayo itakuwa na madhara makubwa kwa wote.













