Je, Trump yuko sahihi anaposema Marekani inachezewa rafu kwenye ushuru?

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock
Donald Trump ameamuru kuwekwa ushuru mpya - kwa bidhaa zinazoingia Marekani. Rais huyo alisema nchi nyingine zina ushuru wa juu kwa bidhaa kutoka Marekani na anaamini Marekani "inatendewa isivyo sawa na washirika wake wa kibiashara, wote marafiki na maadui."
Chini ya masharti ya uanachama wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), nchi zinaruhusiwa kutoza ushuru kwa bidhaa zinazotoka nje.
Ushuru huo unaweza kutofautiana kulingana na bidhaa inayoingizwa. Kwa mfano, taifa linaweza kutoza ushuru wa 10% kwa bidhaa ya mchele na ushuru wa 25% kwa magari kutoka nje.
Lakini chini ya sheria za WTO, nchi hazitakiwi kubagua mataifa wakati wa kuweka ushuru kwa bidhaa fulani kutoka nje.
Tanzania kwa mfano, hairuhusiwi kutoza ushuru wa 2% kwa ngano inayotoka Urusi, lakini ushuru wa 50% kwa ngano inayotoka Ukraine. Katika biashara ya kimataifa kila nchi inapaswa kutozwa ushuru sawa na nchi nyingine kwa bidhaa ileile.
Kuna kesi maalumu pale mataifa mawili yanaposaini mkataba wa biashara huria kati yao. Chini ya kesi kama hizi, huwa hawatozi ushuru kwa bidhaa kati yao lakini hutoza ushuru kwa bidhaa zinazotoka nchi nyingine.
Madai ya Trump ni ya kweli?
Nchi nyingi zina viwango tofauti vya ushuru panapohusika bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, na huripoti wastani wa ushuru huo kwa WTO, ambao huonyesha kiwango jumla cha wastani cha ushuru kwa kila nchi.
Marekani ilikuwa na wastani wa ushuru wa 3.3% mwaka 2023. Asilimia hiyo ni chini kidogo kuliko wastani wa ushuru wa 3.8% kwa Uingereza. Pia ni chini ya wastani wa ushuru wa Umoja wa Ulaya wa 5% na wastani wa ushuru wa China wa 7.5%.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wastani wa ushuru wa Marekani ulikuwa chini sana kuliko wastani wa ushuru wa baadhi ya washirika wake wengine wa kibiashara. Kwa mfano, wastani wa ushuru wa India ni 17%, wakati Korea Kusini ni 13.4%.
Wastani wa ushuru wa Marekani ulikuwa chini kuliko wa Mexico (6.8%) na Canada (3.8%), ingawa makubaliano ya biashara kati ya Marekani na nchi hizi yanamaanisha kuwa mauzo ya nje ya Marekani hayatozwi ushuru. Ndivyo ilivyo kwa Korea Kusini, ambayo Marekani ina makubaliano nayo ya biashara huria.
Hivyo kiuhalisia, ni kweli Trump anaposema kwamba baadhi ya nchi zina wastani wa juu wa ushuru kwa bidhaa kutoka nje kuliko wa Marekani.
Na ushuru huo huongeza bei ya bidhaa nyingi za Marekani zinazouzwa katika nchi hizo, jambo ambalo linaweza kweli kuathiri wauzaji wa nje wa bidhaa kutoka Marekani ikilinganishwa na wauzaji bidhaa nje kutoka nchi hizo wanaouza kwenda Marekani.
Hata hivyo, wanauchumi wengi husema gharama za ushuru, hubebwa na watu wa kawaida, kwa sababu bidhaa zinazoagizwa kutoka nje zinakuwa ghali zaidi.
Hilo litamaanisha mataifa yenye viwango vya juu vya ushuru kwa bidhaa kutoka nje kuliko Marekani, hasara itakuwa kwa wanunuaji wao ndani na sio Wamarekani.
Hatari ya kuvunja sheria
Tarehe 10 Februari, Trump alipendekeza kuwa Marekani itaweka ushuru kwa bidhaa kutoka nje sawa na ushuru unaowekwa na kila taifa kwa bidhaa za Marekani.
Aliwaambia waandishi wa habari: "Ikiwa watatutoza ushuru mkubwa, tutawatoza ushuru mkubwa. Ikiwa ni ushuru 25%, nasi tutaweka 25%. Ikiwa ni 10%, na sisi tutaweka 10%."
Hilo likifanyika linaweza kuvunja sheria za WTO, ambazo zinataka taifa kutoza ushuru sawa kwa bidhaa fulani, bila kujali zimetoka wapi.
Iwapo Marekani itaweka ushuru wa 9.4% kwa bidhaa zote zinazotoka Vietnam lakini ikaweka ushuru wa 3.8% kwa bidhaa zote zinazotoka Uingereza (sawa na ushuru wa wastani wa Uingereza kwa bidhaa kutoka nje) huo utakuwa ni ukiukaji wa sheria.
Lakini iwapo Marekani itaweza kuonyesha kuwa nchi inayoilenga tayari yenyewe inakiuka sheria za shirika, kwa namna fulani inaweza kudai kwamba ushuru huo mpya ni wa kulipiza kisasi dhidi ya nchi hiyo na hilo ni halali chini ya sheria za WTO.
Uwezekano mwingine ni kwamba Trump anaweza kujaribu kuweka viwango sawa vya ushuru, kwa bidhaa kutoka jumuiya fulani.
Kwa mfano, Umoja wa Ulaya umeweka ushuru wa 10% kwa magari yote yanayoagizwa kutoka nje ya jumuiya hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoka Marekani.
Lakini Marekani inatoza ushuru wa 2.5% tu kwa magari yanayoagizwa kutoka nje, ikiwa ni pamoja na yale ya kutoka Umoja wa Ulaya.
Marekani inaweza kuamua kutoza ushuru wa 10% kwa magari kutoka Umoja wa Ulaya ili kuweka usawa.
Marekani ina ushuru mkubwa pia
Ikiwa Trump anataka kuweka ushuru sawa kwa bidhaa za mataifa mengine kama mataifa hayo yanavyoweka ushuru kwa bidhaa za Marekani, basi Marekani itahitajika pia kupunguza baadhi ya ushuru, na si kupandisha.
Marekani imeweka ushuru wa juu kwa bidhaa fulani za kilimo kuliko baadhi ya washirika wake wa kibiashara.
Kwa mfano, Marekani kwa sasa imeweka ushuru wa zaidi ya 10% kwa maziwa yanayoingizwa kutoka nje. Lakini New Zealand, mzalishaji mkubwa wa maziwa duniani, ina ushuru wa 0% kwa uingizaji wa maziwa katika nchi yake kutoka nje.
Ushuru wa maziwa wa Marekani umeundwa kuwalinda wazalishaji wa maziwa wa Marekani. Na kupunguza ushuru wa uingizaji wa maziwa kutoka New Zealand, kunaweza kukabiliwa na upinzani wa kisiasa kutoka kwa wanasiasa kutoka majimbo yanayozalisha maziwa kwa wingi kama Wisconsin.
Vile vile, mfumo wa ushuru unaolingana kwa bidhaa, unaweza kuleta changamoto kwa sekta ya magari ya Marekani.
Marekani imeweka ushuru wa 25% kwa malori yanayoagizwa kutoka nje, ikiwa ni pamoja na kutoka Umoja wa Ulaya.
Lakini ushuru wa Umoja wa Ulaya kwa malori yanayoingizwa kutoka nje, ikiwa ni pamoja na malori kutoka Marekani, ni 10% tu.
Kwa hivyo, ikiwa Marekani inataka kuweka ushuru sawa - inamaanisha Marekani inapaswa kupunguza ushuru wake kwa malori yanayoingizwa kutoka Umoja wa Ulaya.
Ingawa Trump aliweka wazi kwamba kuweka ushuru sawa, kwa kweli, sio lengo lake hasa.















