Mambo saba makubwa aliyofanya Trump ndani ya mwezi mmoja

Donald Trump

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump
    • Author, Ambia Hirsi
    • Nafasi, Mhariri BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kuanzia kutangaza malengo ya Marekani kuhusu mustakabali wa Gaza na kupunguza kwa kiasi kikubwa shughuli za shirika la misaada la Marekani (USAID) kwa mataifa ya kigeni hadi kuingilia kati mzozo wa gofu na kupiga marufuku wanawake waliobadili jinsia kushiriki mashindano ya michezo ya wanawake, Rais wa Marekani Donald Trump ameendelea kufanya mageuzi kwa kasi ya hali ya juu.

Katika makala haya tunaangazia mambo makubwa saba aliyofanya Trump katika mwezi wake wa kwanza madarakani.

1. Pendekezo la Marekani 'kuichukua' Gaza

Rais Donald Trump amezua mjadala baada ya kupendekeza kuwa wakazi wa Gaza wahamishiwe katika mataifa mengine ili kuwezesha Marekani kuijenga upya Gaza na kuliendeleza eneo hilo kiuchumi.

Pendekezo hilo limepingwa vikali kimataifa lakini Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameonekana kuliunga mkono akisema kuwa wazo la Trump "linafaa kupewa kipaumbele"

Ukanda wa Gaza umezungukwa na Israel, Misri na Bahari ya Mediterania.

Tarehe 7 Oktoba 2023, kundi la Hamas iliishambulia Israel na kuua watu wapatao 1,200 na kuchukua zaidi ya mateka 250.

Hii ilisababisha mashambulizi ya kijeshi ya Israel ambapo zaidi ya watu 47,400 wameuawa, kwa mujibu wa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

2. Kusimamisha shughuli za USAID

Trump ni mkosoaji wa muda mrefu wa Marekani kutumia fedha zake kufadhili mataifa mengine akisema hauwakilishi thamani kwa kodi wanazotoa Wamarekani.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Amekosoa vikali shirika la misaada la Marekani USAID, akiwataja viongozi wake wa juu kama "watu wasiojielewa."

Kufunga USAID kutakuwa na athari kubwa hasa katika mataifa ya Afrika ambayo yalikuwa yanategemea pakubwa misaada yake kuendesha programu zao maalum.

Tafiti za maoni kwa muda mrefu zimeonesha kuwa wapiga kura wa Marekani wanapendelea serikali yao kupunguza matumizi ya misaada ya kigeni.

Kwa mfano, moja ya hatua za kwanza alizochukua Trump alipochaguliwa tena ilikuwa kusaini amri ya kiutendaji inayohusisha kusitisha takribani matumizi yote ya kimataifa kwa muda wa siku 90 ili kupitia upya matumizi hayo.

Notisi ikatolewa ikisitisha shughuli zinazoendelea zisimamishwe mara moja.

Muda mchache baadaye agizo likatolewa kuwa baadhi ya programu za kibinadamu ziendelee, ingawa agizo la awali lilikuwa limevuruga shughuli kadhaa kote ulimwenguni. Soma maelezo zaidi kuhusiana na athari ya kusitishwa kwa kwa huduma za USAID kw akubonyeza hapo chini.

3. Kuiwekea vikwazo ICC

Trump

Rais Donald Trump pia alitia saini agizo lilioiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, akiituhumu kwa "vitendo vinavyokiuka sheria na visivyo na msingi vinavyoilenga Marekani na mshirika wake wa karibu Israel".

Hatua hiyo iliiwekea vikwazo vya kifedha na visa kwa watu binafsi na familia zao wanaosaidia katika uchunguzi wa ICC wa raia au washirika wa Marekani.

Trump alitia saini hatua hiyo wakati Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipokuwa akizuru Washington.

Mahakama ya ICC hata hivyo imeahidi kuendeleza majukumu yake ya kisheria licha ya uamuzi huo wa Trump wa kusaini amri ya kuwawekea vikwazo wafanyakazi wake.

Katika taarifa ICC ilisema "inasimama imara" na wafanyakazi wake na itaendelea kutoa "haki na matumaini", ikiongeza kuwa amri hiyo inalenga kuvuruga kazi yake "huru na isiyo na upendeleo".

Mwaka jana, ICC ilitoa hati ya kukamatwa kwa Benjamin Netanyahu kwa tuhuma za uhalifu wa kivita huko Gaza, ambapo Israel inakana tuhuma hizo. ICC pia ilitoa hati ya kukamatwa kwa kamanda wa Hamas.

Licha ya agizo la Trump dhidi ya ICC Marekani na Israel sio wanachama wa ICC.

4. Kutoza ushuru bidhaa kutoka nje ya nchi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Trump tayari ameweka ushuru wa asilimia10% kwa bidhaa zote kutoka China, juu ya ushuru ambao tayari ulikuwa umeshawekwa. China imejibu kwa kuweka ushuru kwa uagizaji wa makaa ya mawe ya Marekani, mafuta, gesi, mashine za kilimo na magari ya injini kubwa.

Marekani itatoza ushuru wa asilimia 25% kwa uagizaji wa chuma na alumini kutoka kote ulimwenguni. Nchi hiyo inaagiza robo ya chuma inachotumia kutoka nje, na sehemu kubwa zaidi ya alumini.

"Taifa letu linahitaji chuma na alumini kutengenezwa Marekani, sio katika nchi za kigeni," Trump alisema wakati wa kuwasilisha ushuru huo.

Ushuru huo utaathiri wazalishaji wakuu wa chuma kama vile Brazili, Canada, China, Ujerumani, Mexico, Uholanzi, Korea Kusini na Vietnam na wazalishaji wakubwa wa alumini kama vile UAE na Bahrain.

Rais huyu wa Marekani ameeleza kuwa hatishwi na jinsi mataifa mengine yatakavyojibu au kulipa kisasi ushuru alioutangaza akiapa kuendelea kutoza mataifa mengine ushuru kwa bidhaa tofauti.

5. Kuiondoa Marekani katika shirika la Afya Duniani WHO

Katibu mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus,

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Katibu mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus,

Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini amri ya kuanza mchakato wa kuiondoa Marekani katika Shirika la Afya Duniani (WHO).

"Hili ni jambo kubwa," rais Trump alisema mara baada ya kula kiapo cha kurejea tena katika Ikulu ya Marekani.

Ilikuwa ni moja ya amri kadhaa za utendaji alizotia saini siku ya kwanza madarakani.

Hatahivyo uamuzi wake huenda sio tu ukaathiri utandekazi wa shirika hilo la Afya bali hata huduma zake kote duniani.

Pia unaweza kusoma:

6. Kusitisha uraia wa kuzaliwa na kubadilisha jina la Ghuba ya Mexico

Saa chache baada ya kula kiapo cha Urais Trump alitia saini ya kukomesha uraia wa haki ya kuzaliwa kwa watoto waliozaliwa Marekani kwa wazazi wahamiaji ambao wako nchini kinyume cha sheria, pamoja na wale waliozaliwa na wazazi ambao wako nchini kwa muda mfupi.

Trump alisema agizo hilo ni kuirejea hadhi Marekani na kuepuka gharama zinazoletwa na wahamiaji wasio rasmi.

Haikuchukua muda, Trump akaagiza Ghuba ya Mexico ibadilishwe jina kuwa Ghuba ya Marekani kwenye nyaraka rasmi za serikali ya Marekani.

Agizo hilo halikupokelewa vizuri na Rais wa mexico Claudia Sheinbaum akisema Mexico ni huru na haikubaliana na suala hilo.

Kufikia sasa wakosoaji wa kubadilisha jina hilo walivamia shirika la 'Google Maps' mtandaoni kwa kuacha maoni ambayo ilibidi shirika hilo lifunge likitaja ni hatia kwa sheria zao.

Hii ni baada ya Ghuba ya mexico kubadilishwa jina katika ramani.

7.Kuwa mpatanishi kati ya Urusi na Ukraine

Rais Donald Trump baada ya kurejea katika ikulu ya White House kwa muhula mwingine alieleza atahakikisha Marekani haiingili vita vinavyoendelea duniani.

Kama njia moja ya kutekeleza aliyoyaahidi wakati wa Kampeini Trump amemtaka Rais wa Urusi Putin ajitoe kwa upweke aje mezani ya mazungumzo ya maridhiano.

Vita kati ya Urusi na Ukraine vinavyoendelea kwa mwaka wa tatu sasa, Trump amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha amesitisha vita hivyo na amani kurejea.

Baada ya kutangaza amezungumza na Rais Putin kuhusu vita hivyo Rais wa Ukraine volodymyr Zelensky amesema hakubaliana na mkondo huo wa upatanishi na kutaka Ukraine ijumuishwe kwenye mazungumzo.

Akiwa mpatanishi wa vita hivyo, Trump alisema kuwa kuna haja ya Ukraine ipatie Marekani rasilimali ghafi wakiwasaidia kurejesha amani au kuoigana vita na Urusi.

Nani awezaye kuyabadilisha maagizo ya Trump?

Agizo la rais linapaswa kufanya kazi ndani ya mipaka ya sheria, na, kwa nadharia, kila moja iwe "iliyopitiwa na Ofisi ya Mshauri wa Kisheria na kuangaliwa uhalali wake". Hili sio jambo linalofanyika kila wakati.

Ikiwa agizo litachukuliwa kuwa limevuka mipaka ya kile kinachokubalika, linaweza kuchunguzwa kisheria.

Bunge linaweza pia kupitisha sheria ya kubatilisha agizo hilo, lakini rais bado ana kura ya turufu juu ya sheria hiyo, Kituo cha Katiba kilieleza.

Ili kufikia malengo yake, Trump anategemea wingi wa wawakilishi wa Chama cha Republican katika Congress na majaji wa kihafidhina katika Mahakama ya Juu.

Imehaririwa na Yusuph Mazimu