Je, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu,ICC hufanya nini?

Chanzo cha picha, ICC
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) huko The Hague ni mahakama ya kudumu ya kimataifa ambayo ina uwezo wa kuwashtaki watu binafsi na viongozi kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.
Ilianzishwa mwaka 2002, baada ya zaidi ya muongo mmoja wa jitihada za kujenga chombo ambacho kinaweza kuwawajibisha viongozi wakorofi kwa vitendo vya kikatili.
Viongozi wa dunia walizidi kushinikiza kuundwa kwake baada ya vita vya Yugoslavia na Mauaji ya Kimbari ya Rwanda.
Mkataba wa Roma - ambao ulianzisha mahakama hiyo - umeidhinishwa na nchi 124, lakini Marekani haipo.
Mahakama hii imeundwa kufanya nini?
Hadi mahakama hiyo ilipoanzishwa, mahakama za muda za dharura zilijaribu kuwafikisha mahakamani wale wanaotuhumiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu. ICC ilianzishwa ili kujaza pengo hilo
Ni mahakama ya mwisho, kuingilia kati tu wakati mamlaka ya kitaifa haiwezi au haitaendesha mashtaka.
Je, si tayari hakuna mahakama kadhaa za kimataifa?
Ndio, lakini zinafanya kazi tofauti au hazina pesa za kutosha
Mahakama ya Kimataifa ya Haki (wakati fulani huitwa Mahakama ya Dunia) huamua kuhusu mizozo kati ya serikali lakini haiwezi kuwashtaki watu binafsi.

Chanzo cha picha, Getty
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mahakama ya kimataifa ya wahalifu wa Yugoslavia ya zamani na Rwanda imewahukumu watu binafsi kwa uhalifu dhidi ya binadamu, lakini ikiwa tu walitekeleza uhalifu katika maeneo hayo kwa muda maalum.
Tofauti na mahakama za kimataifa, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ni chombo cha kudumu.
Je, kuna mipaka ya muda kwa kile inachoshughulikia?
Mahakama haina mamlaka ya kuangalia kesi za nyuma - inaweza tu kushughulikia uhalifu uliofanywa baada ya 1 Julai 2002 wakati Mkataba wa Roma ulipoanza kutumika.
Zaidi ya hayo, mahakama ina mamlaka ya kiotomatiki kwa uhalifu unaofanywa katika eneo la nchi ambayo imeidhinisha mkataba; au na raia wa nchi hiyo; au wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaporejelea kesi kwake.
Mahakama inaendesha kesi za aina gani?
Hukumu ya kwanza ya mahakama hiyo, mwezi Machi 2012, ilikuwa dhidi ya Thomas Lubanga, kiongozi wa wanamgambo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alipatikana na hatia ya uhalifu wa kivita unaohusiana na matumizi ya watoto katika vita vya nchi hiyo na alihukumiwa Julai 14 kifungo cha miaka 14.
Mtu mashuhuri zaidi kufikishwa ICC ni Rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo, ambaye alishtakiwa mwaka 2011 kwa mauaji, ubakaji na aina nyinginezo za unyanyasaji wa kingono, mateso na "vitendo vingine vya kikatili".
Kesi nyingine mashuhuri ni pamoja na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu dhidi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ambaye alifunguliwa mashtaka mwaka 2011 kuhusiana na ghasia za kikabila za baada ya uchaguzi mwaka 2007-08, ambapo watu 1,200 walikufa. Mahakama ya ICC ilifuta mashtaka dhidi ya Bw Kenyatta mnamo Desemba 2014.

Chanzo cha picha, AFP
Miongoni mwa wanaosakwa na ICC ni viongozi wa vuguvugu la waasi la Uganda, Lord's Resistance Army (LRA), ambalo linaendesha harakati zake kaskazini mwa Uganda, kaskazini mashariki mwa DR Congo na Sudan Kusini. Kiongozi wake Joseph Kony anashtakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na kuwateka nyara maelfu ya watoto.
Mahakama ina hati ya kukamatwa kwa Rais wa zamani wa Sudan Omar al-Bashir - ya kwanza dhidi ya mkuu wa nchi anayehudumu. Wakati Bw Bashir - ambaye anakabiliwa na makosa matatu ya mauaji ya halaiki, makosa mawili ya uhalifu wa kivita na makosa matano ya uhalifu dhidi ya binadamu - alipohudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika nchini Afrika Kusini mwezi Juni 2015, mahakama ya Afrika Kusini iliamuru azuiwe kuondoka nchini humo wakati ikingoja kuamua iwapo alifaa kukamatwa chini ya waranti ya ICC.
Serikali ya Afrika Kusini ilimruhusu Bw Bashir kuondoka na katika hali hiyo jaji alishutumu kwa hasira serikali kwa kupuuza katiba. Serikali nayo ilitishia kujiondoa ICC.
Mnamo 2023, ICC ilitoa hati ya kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin na Kamishna wake wa Haki za Watoto Maria Lvova-Belova. Wawili hao walishtakiwa kwa kuwahamisha watoto wa Ukraine kinyume cha sheria na kuwapeleka Urusi wakati wa uvamizi wa Bw Putin nchini humo.
Hati hiyo imesababisha matatizo na safari ya kimataifa ya kiongozi huyo wa Urusi. Alilazimika kuepuka mkutano wa kilele wa BRICS nchini Afrika Kusini mnamo 2023, baada ya shinikizo kuongezeka kwa serikali ya Rais Cyril Ramaphosa kumzuilia Bw Putin ikiwa angewasili nchini.
Mnamo 2021, ICC ilianza uchunguzi rasmi juu ya madai ya uhalifu wa kivita katika maeneo ya Palestina. Mamlaka ya Palestina iliwasilisha ushahidi mbele ya mahakama ya kile inachodai kuwa ni uhalifu wa kivita uliofanywa na jeshi la Israel. Ripoti ya Umoja wa Mataifa ilipata ushahidi wa uhalifu wa kivita wa kundi la Hamas la Palestina na jeshi la Israel.
Madai ya uonevu dhidi ya Afrika
Mahakama ya ICC imekosolewa, hasa na Umoja wa Afrika, kwa kuzingatia Afrika. Katika historia ya miaka 22 ya mahakama hiyo imeleta mashtaka dhidi ya watu kutoka Afrika pekee.
ICC inakanusha ubaguzi wowote, ikionyesha ukweli kwamba baadhi ya kesi - kama vile LRA nchini Uganda - ziliwasilishwa na nchi iliyoathirika, na baadhi zilipelekwa na UN.
Fatou Bensouda, mwendesha mashtaka mkuu wa zamani wa ICC raia wa Gambia, amedai kuwa mahakama hiyo inaisaidia Afrika kwa kuwafungulia mashtaka wahalifu.
"ICC inafanya kazi na Afrika, na inafanya kazi kwa ajili ya waathirika wa Afrika, kwa hivyo sidhani kama Umoja wa Afrika unapaswa kupinga hilo," alisema,
Je, mahakama inawezaje kuhakikisha kukamatwa na kuwashtaki watuhumiwa?
Mahakama ya ICC haina polisi wake wa kuwasaka na kuwakamata washukiwa. Badala yake ni lazima itegemee huduma za polisi za kitaifa kukamata watu na kutafuta uhamisho wao hadi The Hague.
Kesi ya Bw Bashir inaonyesha tatizo ambalo hili linaweza kuleta kwa mahakama. Nchi kadhaa zilizotia saini mwafaka wa ICC, zikiwemo Chad na Kenya, na zimekataa kutoa ushirikiano katika kukamatwa kwake.

Chanzo cha picha, AFP
Mahakama ya Afrika Kusini iliamuru azuiwe kuondoka nchini humo,lakini serikali ikabatili amri hiyo.
Umoja wa Afrika umewaagiza wanachama kutotekeleza hati ya ICC ya kukamatwa kwake huku ikifanya uchunguzi wake yenyewe.
Je, mfumo hufanya kazi vipi?
Mwendesha mashtaka anaanzisha uchunguzi iwapo kesi itapelekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa au na nchi iliyoidhinisha.
Anaweza pia kuchukua hatua huru, lakini mashtaka yanapaswa kuidhinishwa na jopo la majaji.
Mwendesha mashtaka na majaji wote huchaguliwa na mataifa wanachama wa mahakama. Luis Moreno Ocampo wa Argentina alikuwa mwendesha mashtaka mkuu wa kwanza wa mahakama hiyo.
Kila taifa lina haki ya kuteua mgombeaji mmoja kwa kuchaguliwa kuwa jaji.
Nani amekubali kushirikiana na mahakama?
Mkataba wa Roma umeidhinishwa na mataifa 124 hadi sasa. Mengine 34 yametia saini na yanaweza kuiridhia siku zijazo.
Ni mataifa matatu tu ya Kiarabu ambayo yameidhinisha mkataba huo hadi sasa - Jordan, Djibouti na Comoro.
Kwa nini Marekani haihusiki?
Wakati wa mazungumzo, Marekani ilisema kwamba wanajeshi wake wanaweza kuwa chini ya mashitaka ya kisiasa au ya kipuuzi.
Ulinzi mbalimbali ulianzishwa, na hatimaye Bill Clinton alitia saini mkataba huo katika mojawapo ya hatua zake za mwisho kama rais lakini haukuwahi kuthibitishwa na bunge la Congress.
Utawala wa Bush ulipinga vikali mahakama hiyo na kuvurugwa kwa uhuru wowote wa Marekani katika haki ya jinai, na Marekani ilitishia kuwaondoa wanajeshi wake kutoka kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Bosnia endapo hawangepewa kinga ya kutoshtakiwa na ICC.

Chanzo cha picha, AFP
Katika uamuzi uliokosolewa sana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura tarehe 12 Julai 2002 juu ya maafikiano ambayo yaliwapa wanajeshi wa Marekani msamaha wa miezi 12 kutoka kwa mashtaka - unaofanywa upya kila mwaka.
Lakini Baraza la Usalama - likichochewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo Kofi Annan - lilikataa kurudisha msamaha huo mwezi Juni 2004, miezi miwili baada ya picha za wanajeshi wa Marekani wakiwadhulumu wafungwa wa Iraq kushtua ulimwengu.
Operesheni ya mahakama hiyo inaonekana kuwa dhaifu bila kuhusika kwa Marekani. Walakini, Washington haijakataza ushirikiano na mahakama katika kesi maalum. Rais Joe Biden ameamuru mashirika ya kijasusi ya Marekani kushiriki ushahidi wa uhalifu wa kivita wa Urusi nchini Ukraine na mahakama.
Je, kuna wapinzani wengine?
Ndiyo, nchi kadhaa muhimu zinaonekana kudhamiria kutosalimu amri kwa ICC. Baadhi hata hawajatia saini mkataba huo, kama vile China, India, Pakistan, Indonesia na Uturuki.

Chanzo cha picha, AFP
Nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na Misri, Iran, Israel na Urusi, zimetia saini lakini bado zina shaka na hazijaidhinisha.
Haiwezekani kwamba uhalifu unaodaiwa dhidi ya binadamu katika mataifa hayo utafunguliwa mashtaka. Baada ya mahakama kutoa hati za kukamatwa kwa makamanda wawili wa Urusi mnamo Machi 2024, katibu wa habari wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Moscow haikutambua vibali hivyo.
Je, ICC inaendana vipi na mfumo wa mahakama wa kila taifa?
Mataifa ambayo yanajiunga na mkataba huo yanaweza kutaka kuhakikisha kuwa wao wenyewe wana uwezo wa kushtaki uhalifu wote unaohusika - vinginevyo mahakama inaweza kuingilia kati.
Baadhi ya serikali tayari zimeanzisha sheria ya kufanya mabadiliko katika mifumo yao ya mahakama.
Nani analipa?
Mataifa ambayo yanashiriki. Hii itakuwa kwa mujibu wa sheria zilezile zinazosimamia michango yao kwa Umoja wa Mataifa -mara nyingi kulingana na utajiri wao wa kitaifa.
Kutokuwepo kwa Marekani hasa hufanya ufadhili wa mahakama kuwa ghali zaidi kwa wengine.
Japan, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ni miongoni mwa wachangiaji wakubwa.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












