Ni nani anamiliki Ghuba ya Mexico na kweli Trump anaweza kuibadilisha jina?

Rais Mteule wa Marekani Donald Trump

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Mteule wa Marekani Donald Trump
    • Author, Drafting
    • Nafasi, BBC News World
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Hotuba za rais mteule wa Marekani, zimejaa tamko la kisiasa na mustakabali wa Marekani baada ya kuapishwa kwake.

Jumanne, Trump alielezea wazo lake la kubadili jina la Ghuba ya Mexico kuwa Ghuba ya Amerika.

"Tutatangaza mabadiliko haya hivi karibuni… kwa sababu sisi ndiyo tunaojikita kwa wingi katika kazi huko na ni yetu… tutabadilisha jina la Ghuba ya Mexico kuwa Ghuba ya Amerika," alisema Trump katika mkutano wa waandishi wa habari katika makazi yake ya Mar-a-Lago, Florida.

"Ghuba ya Amerika, jina zuri sana. Na linastahili…" aliongeza, na bila kutoa maelezo zaidi kuhusu pendekezo lake, aliendelea kusema kuhusu Mexico ambayo, alisema, "lazima iache kuruhusu mamilioni ya watu kuingia kwenye nchi yetu."

Rais mteule baadaye alisisitiza tishio lake la kuweka "ushuru wa forodha wa juu zaidi" kwa Mexico na Kanada.

Trump hakusema ni vipi au lini anapanga kutekeleza mabadiliko ya jina la Ghuba ya Mexico, lakini muda mfupi baada ya kauli zake, mbunge wa Republican, Marjorie Taylor Greene, alitangaza kuwa atawasilisha muswada kwa haraka kubadilisha jina la Ghuba ya Mexico.

"Rais Trump anaanza muhula wake wa pili kwa mwanzo mzuri," aliandika Taylor Greene kwenye X.

"Nitawasilisha sheria mara moja kubadilisha rasmi jina la Ghuba ya Mexico kuwa jina lake halali, Ghuba ya Amerika!"

Lakini je, inawezekana kutekeleza mabadiliko kama haya kwenye mhimili wa kimataifa?

Pia unaweza kusoma:

Ni nani anamiliki Ghuba ya Mexico?

Ghuba ya Mexico iko kati ya pwani ya mashariki mwa Mexico, kusini mashariki mwa Marekani, na magharibi mwa Cuba.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ghuba ya Mexico iko kati ya pwani ya mashariki mwa Mexico, kusini mashariki mwa Marekani, na magharibi mwa Cuba.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ghuba ya Mexico, inayofunika zaidi ya kilomita za mraba milioni 1.6, ni mabonde ya bahari yaliyo kati ya Bahari ya Atlantiki na Bahari ya Kariba, kati ya fukwe za mashariki za Mexico, kusini mashariki mwa Marekani, na magharibi mwa Cuba.

Nchi tano za Mexico zina fukwe kwenye Ghuba: Tamaulipas, Veracruz, Tabasco, Campeche na Yucatán.

Nchi za Marekani za Florida, Alabama, Mississippi, Louisiana na Texas, pamoja na mikoa ya Cuba ya Pinar del Río na Artemisa, pia zina fukwe kwenye Ghuba.

Ghuba ni mojawapo ya maeneo makubwa zaidi ya uzalishaji mafuta baharini duniani, ikiwa na asilimia 14 ya uzalishaji jumla wa mafuta ghafi wa Marekani na asilimia 5 ya uzalishaji wa gesi asilia kavu.

Kwa Mexico, Ghuba pia ni muhimu, kwani ni mahali ambapo mafuta mengi ya nchi hiyo yanachimbwa, moja ya vichocheo vikuu vya uchumi wake.

Kuna makubaliano ya mipaka ya majini ya kimataifa yaliyowekwa na mashirika kama vile Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sheria ya bahari kati ya Marekani na Mexico, Marekani na Cuba, na Mexico na Cuba.

Mipaka ya Ghuba ya Mexico kati ya Marekani, Mexico na Cuba pia imewekwa na mamlaka ya kimataifa juu ya mipaka ya bahari, Shirika la Kimataifa la Hidrografia (IHO).

Kwanini inaitwa Ghuba ya Mexico?

Sehemu hii ya maji ilipata jina la Ghuba ya Mexico kwa mara ya kwanza kwenye ramani za Ulaya za karne ya 16.

Kama Susan Parker anavyosema katika gazeti la St. Augustine Record, gazeti la Florida, "Baptiste Boazio, mchora ramani na mchoraji wa safari za (mchunguzi wa Uingereza) Francis Drake katika Kariba kati ya miaka ya 1580, alitumia 'Ghuba ya Mexico' kwenye ramani yake iitwayo 'Muhtasari wa Njia Nzima ya Safari ya Sir Francis Drake hadi West Indies.'"

"Ramani ya De Bry ya 1591 pia inatumia jina la Ghuba ya Mexico," anasema.

Ramani nyingine kutoka mwaka 1630 ilitaja mwili huu wa maji kama "Ghuba ya Hispania mpya," jina ambalo chini ya Enzi ya Makoloni ya Hispania liliwajumuisha maeneo ambayo sasa ni Florida, sehemu za kusini mashariki mwa Marekani, Mexico, na sehemu kubwa ya Amerika ya Kati.

Lakini Ghuba ya Mexico ni jina ambalo liliendelea kutumika zaidi ya miaka 400.

Ghuba ya Mexico ni mojawapo ya mikoa muhimu zaidi ya uzalishaji wa mafuta katika nchi za pwani.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ghuba ya Mexico ni mojawapo ya mikoa muhimu zaidi ya uzalishaji wa mafuta katika nchi za pwani.

Je, inawezekana kubadilisha jina la Ghuba?

Kwa awamu ya awali, Trump angehitaji idhini kutoka Mexico na Cuba ili kubadili jina la Ghuba ya Mexico.

Hata hivyo, huko Mexico, Rais Claudia Sheinbaum alijibu pendekezo la Trump Jumatano kwa kusema: "Kwa nini tusiiite Amerika ya Mexico (Marekani)? Inasikika vizuri."

Na Waziri wa Uchumi, Marcelo Ebrard, alisema kuwa eneo hilo "litaendelea kuitwa Ghuba ya Mexico."

"Hatuwezi kujibu matamko yote kila siku," alisema Ebrard.

"Ikiwa tutaona mbele kwa miaka 30, Ghuba ya Mexico bado itaitwa Ghuba ya Mexico. Lakini hatutajitosa katika mjadala huo. Tunachofanya ni kulinda uhusiano wa nchi zetu mbili."

Trump pia atahitaji tathmini na idhini kutoka kwa mashirika mengi ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Shirika la Kimataifa la Hidrografia, Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu sheria ya bahari na Kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa juu ya Majina ya Kijiografia (UNGEGN).

Zaidi ya hayo, kwa kuwa Ghuba ya Mexico ni makazi ya aina mbalimbali za mimea na wanyama wa baharini na mazingira ya pwani, jina jipya litahitaji mabadiliko ya kisheria kwenye ramani za baharini, ramani rasmi, na sheria za kitaifa ambazo kila nchi husika itabidi zitambulishe.

Je, Trump anaweza kubadilisha jina la Ghuba?

Hata kama Mexico na Cuba zitapinga kubadilisha jina la Ghuba, Donald Trump huenda akaweza kutimiza ombi lake, hata kama nchi zingine hazitakubaliana na jina la Ghuba ya Amerika.

Huko Marekani, kuna mifumo ya kubadili majina ya maeneo yanayotambuliwa na serikali kuu.

Mojawapo ya mifumo hiyo ni Bodi ya Majina ya Kijiografia ya Marekani (BGN).

Hii ni taasisi yenye lengo la kuanzisha na kudumisha matumizi ya majina ya kijiografia kwa usawa katika serikali kuu.

Bodi hii haibuni majina mapya ya maeneo, lakini inakubali au kukataa majina mapya yanayopendekezwa na mashirika ya serikali kuu, serikali za majimbo au za mitaa, na umma.

Ikiwa pendekezo lake litatekelezwa, Trump hatakuwa rais wa kwanza wa Marekani kuomba kubadilishwa kwa jina la kijiografia.

Mwaka 2015, BGN ilikubali ombi la Rais Barack Obama la kubadili jina la Mlima McKinley, kilele cha juu zaidi cha Amerika Kaskazini, kuwa Mlima Denali, jina la Kiatabascan linalotumika na vizazi vya Waasiliya wa Alaska lenye maana ya "mkubwa zaidi."

Mlima huu ulipatiwa jina la William McKinley, mwanasiasa wa Ohio aliyechaguliwa rais wa Marekani mwaka 1896 na kuuawa miezi sita baada ya kuingia madarakani kwa muhula wake wa pili.

McKinley hakuwahi kufika Alaska, na Obama alisema lengo lake la kubadili jina la mlima lilikuwa kuboresha uhusiano na Wamarekani asili.

Kwa njia hii, Trump amekariri mara kadhaa kuwa anataka kurudisha jina la Denali kuwa Mlima McKinley.

Na ikiwa BGN itakubali ombi la Trump kubadili jina la Ghuba ya Mexico, haitakuwa mara ya kwanza kwa Wamarekani na Wamexico kutofautiana kuhusu jina la sehemu hiyo ya maji ilioko ndani ya mipaka yao.

Mto unaopita kwenye mpaka kati ya jimbo la Texas la Marekani na majimbo ya Mexico ya Chihuahua, Coahuila, Nuevo León na Tamaulipas unaitwa Rio Grande na Wamarekani. Wamexico wanauita Rio Bravo.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid