Maagizo ya rais ni nini?

Chanzo cha picha, EPA
Maagizo ya rais ni chombo muhimu kwa yeyote anayeongoza Marekani na kutaka kuacha kumbukumbu kwenye sera ya serikali - na inaonekana kuwa Donald Trump hana cha kupoteza muda katika hili kwenye urejeo wake katika Ikulu ya White House.
Anatarajiwa kutia saini zaidi ya maagizo 200 siku ya Jumatatu. Hii itajumuisha maagizo ambayo ni ya kisheria, na mengineo ya rais kama vile amri, ambayo kwa kawaida sivyo.
Trump ameahidi kuweka maagizo ambayo yataimarisha mipango ya kijasusi yenye kuhusisha akili mnemba kuunda Idara ya Ufanisi wa Serikali, kutoa rekodi zinazopatikana kuhusiana na mauaji ya John F Kennedy yaliyotokea mnamo 1963, kuelekeza jeshi kuunda mfumo wa kujilinda wa Iron Dome kukabiliana na makombora na kuondoa utofauti, sera za usawa na ujumuishaji jeshini.
Katika muhula wake wa awali, alitia saini maagizo ya rais 220, baadhi yalipingwa mahakamani.
Agizo la rais ni nini?
Ni amri iliyoandikwa na kutolewa na rais kwa serikali na haihitaji idhini ya bunge.
Maagizo yanaanzia mabadiliko makubwa ya sera, kama vile idhini ya Trump ya ujenzi wa mabomba mawili ya mafuta yaliyoshindaniwa sana mnamo mwaka wa 2017, hadi ya kawaida kama vile maagizo ya Barack Obama kuhusu kufungwa kwa nusu siku kwa idara za serikali Siku ya mkesha wa Krismasi mwaka 2015.
Mamlaka ya rais kutoa maagizo yanayotokana na Ibara ya II ya katiba ya Marekani, ambayo inasema: "Mamlaka ya juu yatakabidhiwa kwa rais wa Marekani."
Kwanini marais wanatoa maagizo?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati mwingine maagizo hufanywa wakati wa vita au kuzuia tatizo la ndani ya nchi.
Mnamo Februari mwaka 1942, Rais Franklin D Roosevelt alitia saini agizo lililosababisha kujengwa kwa vituo vya kizuizini kwa Wamarekani wa Kijapani wapatao 120,000.
Mnamo 1952 Rais Harry Truman alitoa agizo ambalo liliweka tasnia ya chuma chini ya udhibiti wa serikali ili kujaribu kuzuia shambulizi.
Katika siku yake ya kwanza ofisini tarehe 20 Januari, 2021, Biden alitia saini agizo la kuanza mchakato wa kujiunga tena na makubaliano ya hali ya hewa ya 2015 ya Paris, ambayo mtangulizi wake Trump alijiondoa rasmi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wa Biden, Antony Blinken, alisema ilikuwa "kutusaidia sote kuzuia janga la joto la sayari".
Nani awezaye kuyabadilisha?
Agizo la rais linapaswa kufanya kazi ndani ya mipaka ya sheria, na, kwa nadharia, kila moja iwe "iliyopitiwa na Ofisi ya Mshauri wa Kisheria na kuangaliwa uhalali wake". Hili sio jambo linalofanyika kila wakati.
Ikiwa agizo litachukuliwa kuwa limevuka mipaka ya kile kinachokubalika, linaweza kuchunguzwa kisheria.
Bunge linaweza pia kupitisha sheria ya kubatilisha agizo hilo, lakini rais bado ana kura ya turufu juu ya sheria hiyo, Kituo cha Katiba kilieleza.
Kwanini yanahusishwa sana kisiasa?
Maagizo ya rais yana utata kwa sababu yanakwepa idhini kutoka kwa Bunge, na kumruhusu rais kuchukua hatua kivyake.
Warepublican walifanikiwa kumshtaki Obama kuhusu sehemu ya mabadiliko yake ya huduma ya afya ya 2010, wakisema kwamba alikuwa amevuka mamlaka yake ya kikatiba alipochelewesha kwa upande mmoja tarehe ya mwisho ya bima.
Marufuku ya Trump ya kusafiri kwa baadhi ya nchi zenye Waislamu wengi ilikuwa na utata mkubwa, na Biden aliimaliza alipoingia Ikulu ya White House.
Rais pia anaweza kutoa agizo wakati wabunge watachukua hatua polepole sana au wakati rais anahisi anahitaji kufafanua maelezo ya sheria mpya.
Maagizo ya rais hutolewa mara ngapi?
Franklin D Roosevelt alitoa maagizo mengi zaidi - 3,721 wakati wa miaka 12 ya uongozi wake huku Woodrow Wilson na Calvin Coolidge walitia saini 1,803 na 1,203 mtawalia.
Trump alitia saini maagizo 220 katika muhula wake wa kwanza.
Kwa kulinganisha, Joe Biden alitoa maagizo 160 na Barack Obama na George W Bush, ambao wote walitumikia mihula miwili mfululizo, walitoa 277 na 291 mtawalia.
Je, rais mpya anaweza kutengua maagizo ya mtangulizi wake?
Katika siku za hivi karibuni, marais wamezidi kutumia maagizo yao kutengua yaliyopitishwa na watangulizi wao.
Mnamo mwaka 2017, Trump alianza na agizo kuu lililolenga bima ya afya maarufu kama Obamacare.
Biden alibatilisha tamko la dharura la utawala wa Trump ambalo lilisaidia kufadhili ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa Mexico na pia kumaliza marufuku ya kusafiri kwa baadhi ya nchi zenye Waislamu wengi.
Pia alirejesha Marekani kwenye makubaliano ya hali ya hewa ya Paris.
Huku Trump akirejea kwa muhula wa pili, ameapa kutia saini msururu wa maagizo ndani ya muda mfupi baada ya kuapishwa, yanayohusu masuala kuanzia uhamiaji na kufukuzwa nchi hiyo hadi mazingira na haki za watu waliobadili jinsia.
Imetafsiriwa na Asha Juma








