Je, ushuru wa Trump ni nini na ni nchi gani zitaathirika?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Jeremy Howell & Onur Erem
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Rais wa Marekani Donald Trump ameweka ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa zote za chuma na alumini zinazoagizwa kutoka nje, ushuru huo utaanza kutumika tarehe 12 Machi.
Hii itaathiri wasambazaji wakuu wa bidhaa hizo. Pia kuna uwezekano wa bei kuongezeka kwa wazalishaji na watumiaji wa Marekani.
Ushuru ni nini?
Ushuru ni kodi kwa bidhaa kutoka nje. Ushuru huendana na bei ya bidhaa na mara nyingi unatozwa kwa kampuni inayoingiza bidhaa kutoka nje.
Kwa hivyo, ikiwa kampuni inaagiza magari yenye thamani ya dola za kimarekani 50,000 kila moja, kwa ushuru wa 25%, maanake italipa dola 12,500 kwa kila gari.
Waagizaji hupambana na gharama ya ushuru kwa kuongeza bei ya rejareja, na katika mazingira hayo wanunuaji wa rejareja wa Marekani ndio watabeba mzigo wa gharama.
Kwanini Trump anaongeza ushuru?
Donald Trump amesema mara nyingi kwamba ushuru mkubwa hulinda na kuunda kazi za ndani za Marekani na anaiona hii ni njia ya kukuza uchumi wa Marekani na kuongeza mapato ya kodi.
"Chini ya mpango wangu, wafanyakazi wa Marekani hawatakuwa na wasiwasi tena kuhusu kupoteza kazi zao kwa raia wa mataifa ya kigeni," amesema. "Badala yake, mataifa ya kigeni yatakuwa na wasiwasi kuhusu kupoteza kazi zao kwa Wamarekani."
Trump pia amesema ushuru kwa chuma ni muhimu kwa usalama wa taifa la Marekani kwa sababu inawafanya watengeneza chuma wa ndani kuongeza uwezo wao wa uzalishaji. Anataka Marekani iweze kuzalisha silaha za kutosha wakati wa vita bila kutegemea bidhaa kutoka nje.
Trump pia anatumia ushuru kama njia ya kukandamiza mauzo ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na kukuza mauzo ya bidhaa za ndani.
"Hawanunui magari yetu, hawanunui bidhaa zetu za shambani, hawanunui chochote na tunanunua kila kitu kutoka kwao," alisema Trump kuhusu nchi za Umoja wa Ulaya.
Ushuru katika muhula wa kwanza

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwaka 2018, Trump aliweka ushuru wa hadi 50% kwa mashine za kuoshea nguo na paneli za jua kutoka nje. Serikali ya Marekani ilisema wazalishaji wa Marekani katika sekta zote mbili walikuwa wanakabiliwa na ushindani usio wa haki kutoka nje ya nchi.
Katika mwaka huo huo, aliweka ushuru wa asilimia 25 kwa chuma kilichoagizwa kutoka nje na 10% kwa alumini iliyoagizwa kutoka nje, ikiwa ni pamoja na Mexico na Canada, ambao ni walikuwa ni washirika wa Marekani katika Mkataba wa Biashara Huria wa Amerika Kaskazini, au Nafta.
Baadaye aliondoa ushuru huo pale mataifa hayo yalipotia saini Mkataba wa Marekani-Mexico-Canada (USMCA), ambao ulichukua nafasi ya Nafta mwaka 2020 - mkataba wa kibiashara uliokuwa na manufaa zaidi kwa Marekani.
Ushuru wa EU ulianza dhidi ya Ujerumani na Uholanzi, wanaosafirisha chuma kingi kwenda Marekani. Umoja wa Ulaya kama kundi ulilipiza kisasi kwa kuweka ushuru bidhaa za Marekani kama vile dangarizi, pombe kali aina ya bourbon na pikipiki.
Trump pia aliweka ushuru kwa bidhaa za China zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 360, kuanzia nyama hadi ala za muziki. China ililipiza kisasi kwa kuweka ushuru bidhaa zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 110 kutoka Marekani.
Chini ya Rais Joe Biden, ushuru dhidi ya China ulibaki vivo hivyo na ushuru mpya uliwekwa kwa bidhaa kama vile magari ya umeme.
Ushuru ulikuwa na athari gani?

Chanzo cha picha, Reuters
Ushuru wa Trump ulipunguza kiwango cha bidhaa ambazo Marekani ilikuwa inaagiza kutoka katika baadhi ya nchi, lakini ikaongeza kiwango cha bidhaa inachoagiza kutoka nchini zingine.
Kabla ya 2018, bidhaa za China zilijumuisha 22% jumla ya bidhaa ambazo Marekani inaagiza kutoka nje. Mwaka 2024, ilikuwa ni 13.5% tu, kulingana na Ofisi ya Sensa ya Marekani.
Mexico iliipiku China na kuwa msafirishaji nambari moja wa bidhaa kuingia Marekani kufikia 2023. Sasa inasafirisha bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 476 kwenda Marekani, ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 427 zinazoingizwa kutoka China.
Hii kwa kiasi fulani ni kwa sababu makampuni mengi - hasa watengenezaji wa magari - yalihamishia uzalishaji wao na kuupeleka Mexico ili kunufaika na fursa ya mpango wake wa biashara huria na Marekani na gharama ya chini ya kuzalisha huko.
Nchi za Asia mashariki pia zilipata ongezeko la mauzo yao ya kwenda nje hasa Marekani kutokana na ushuru mkubwa wa Trump kwa China.
Kwa sababu bidhaa zao zilikua za bei nafuu kuliko bidhaa za China kwa watumiaji wa Marekani, na makampuni mengi ya China yalihamia nchi hizi ili kuepuka ushuru wa Marekani.
Kulingana na taarifa ya ofisi ya ushauri kwa rais wa Marekani juu ya sera za biashara kimataifa, nchi zilizo katika jumuiya ya biashara ya Asean - kama vile Indonesia, Ufilipino, Thailand na Vietnam - zilisafirisha bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 158 kwenda Marekani mwaka 2016, na zilisafirisha kwenda nje karibu bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 338 kwa 2023.
"Nchi iliyoathiriwa zaidi na ushuru wa 2018 ilikuwa China," anasema Dkt Nicolo Tamberi, mwanauchumi katika Chuo Kikuu cha Sussex nchini Uingereza.
"Nadhani Vietnam ilifaidika pakubwa katika awamu ya kwanza ya ushuru," anasema.
Kwa Marekani, ushuru huo uliongeza pato la chuma na alumini, kulingana na Taasisi ya Peterson ya Uchumi wa Kimataifa, lakini pia uliongeza bei ya chuma. Inasema hilo lilisababisha maelfu ya kazi kupotea katika viwanda vingine.
Taasisi ya Peterson pia inasema hatua za ushuru za Trump zilipandisha bei katika sekta nzima, na kuwaacha watumiaji wa Marekani wakiwa na hali mbaya zaidi.
Ushuru wa sasa utamwathiri nani?
Marekani itatoza ushuru wa 25% kwa uagizaji wa chuma na alumini kutoka kote ulimwenguni. Nchi hiyo inaagiza robo ya chuma inachotumia kutoka nje, na sehemu kubwa zaidi ya alumini.
"Taifa letu linahitaji chuma na alumini kutengenezwa Marekani, sio katika nchi za kigeni," Trump alisema wakati wa kuwasilisha ushuru huo.
Ushuru huo utaathiri wazalishaji wakuu wa chuma kama vile Brazili, Canada, China, Ujerumani, Mexico, Uholanzi, Korea Kusini na Vietnam na wazalishaji wakubwa wa alumini kama vile UAE na Bahrain.
Trump tayari ameweka ushuru wa 10% kwa bidhaa zote kutoka China, juu ya ushuru ambao tayari ulikuwa umeshawekwa. China imejibu kwa kuweka ushuru kwa uagizaji wa makaa ya mawe ya Marekani, mafuta, gesi, mashine za kilimo na magari ya injini kubwa.
Pia imepiga marufuku usafirishaji wa vyuma vingi adimu kwenda Marekani - vinavyohitajika kutengeneza vifaa vya kielektroniki na kijeshi.
Mapema mwezi Februari, Trump alitangaza ushuru wa 25% kwa bidhaa zote kutoka Canada na Mexico (isipokuwa ushuru wa 10% kwa nishati kutoka Canada), kwa sababu ya dawa haramu ya fentanyl na wahamiaji haramu wanaovuka mipaka na kuingia Marekani. Hata hivyo, ameahirisha kutekeleza ushuru huo hadi mwezi Machi.
Canada imetishia kulipiza kisasi kwa ushuru wa 25% kwa bidhaa za Marekani kuanzia bia hadi vifaa vya nyumbani na bidhaa za michezo, na Mexico pia imeahidi hatua za kulipiza kisasi.
Waziri wa viwanda wa Canada, François-Philippe Champagne amesema jibu la Canada kwa ushuru wa chuma na aluminiamu litakuwa "wazi na lililopangwa."
Trump amesema atatoza ushuru kwa bidhaa kutoka nchi za Umoja wa Ulaya "hivi karibuni."
Alikataa hoja kuwa ushuru utaongeza bei ya chuma nchini Marekani na kusema, "mwishowe itakuwa bei nafuu."
Athari kwa Canada na Mexico

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na Profesa Stephen Millard wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii kutoka Uingereza, anasema Canada na Mexico zote zinakabiliwa na ushuru wa chuma na aluminiamu.
Nchi zote mbili zinaitegemea sana Marekani. Mexico inatuma 83% ya bidhaa zake zote kwenda Marekani na Canada inatuma 76% ya bidhaa zake yote.
"Canada inauza kiasi kikubwa cha mafuta na mashine nchini Marekani. Na ushuru wa 25% unaweza kupunguza Pato la Taifa kwa 7.5% katika kipindi cha miaka mitano. Ushuru unaweza kupunguza Pato la Taifa la Mexico kwa 12.5% katika kipindi cha miaka mitano. Hili litakuwa jambo baya," anasema.
Lila Abed kutoka kutoka Mexico, anayefanya kazi katika Taasisi ya fikra tunduizi ya Marekani ya Wilson Center anasema ushuru wa Marekani utakuwa "mbaya" kwa wafanyakazi wa Mexico.
"Takriban ajira milioni tano za Marekani zinategemea biashara za Marekani na Mexico. Na utafiti wa hivi karibuni unasema karibu ajira milioni 14.6 nchini Mexico zinategemea biashara za Marekani," anasema.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












