Mambo makubwa manne yatakayotawala mazungumzo ya Trump na Putin leo

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amesema "vipengele vingi" vya makubaliano ya amani nchini Ukraine vimekubaliwa na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin. Trump ameyasema hayo kabla ya mazungumzo yao ya simu yanayotarajiwa leo.
Trump alichapisha taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social, akisema atazungumza na Putin siku ya Jumanne asubuhi.
Amesema, ingawa kuna makubaliano, lakini mengi ya makubaliano hayo bado hayajafanyiwa kazi.
"Kila wiki kuna vifo vya askari 2,500, kutoka pande zote mbili, na lazima hilo liishe sasa. Ninatarajia mengi katika simu na Rais Putin," Trump aliandika.
Hapo awali aliwaambia waandishi wa habari "tutaona ikiwa tutaweza kufanya makubaliano ya amani, usitishaji vita na amani, na naamini tutaweza kufanya hivyo".
Katika hotuba yake ya usiku wa kuamkia Jumatatu, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alimshutumu Putin kwa kurefusha vita.
"Pendekezo hili (la kusitisha vita) lingeweza kutekelezwa muda mrefu uliopita," alisema, akiongeza kuwa "kadiri vita vikiendelea, inamaanisha maisha ya binadamu hupotea."
Kumekuwa na usiri kutoka ndani ya utawala wa Trump kuhusu jinsi mazungumzo ya kusitisha mapigano yatakavyo kuwa.
Akizungumza baada ya mkutano wake mjini Jeddah na maafisa wa Ukraine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alitaja mazungumzo hayo na "jinsi mchakato wa mazungumzo utakavyo kuwa" lakini hakutaja " vipengele maalumu."
Mjumbe wa Marekani, Steve Witkoff, ambaye alikutana na Putin siku ya Alhamisi huko Moscow, pia hakuzungumza mengi kuhusu vipengele vya mpango huo.
Wakati huo huo, Uingereza na Ufaransa zimemtaka Putin kuthibitisha kuwa anataka makubaliano ya amani na Ukraine.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amepongeza "ujasiri" wa Zelensy kukubaliana na pendekezo la kusitisha mapigano, na kutoa changamoto kwa Urusi kufanya vivyo hivyo.
"Vifo ni vingi. Vifo vingi vimetokea. Uharibifu wa kutosha. Mapigano lazima yasitishwe," alisema Macron kwenye chapisho kwenye X.

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy, amesema sasa Putin anapaswa kukubali "kusitisha mapigano moja kwa moja na bila masharti," na kuwaambia wabunge kuwa hakuona "kiashiria chochote" kwamba Putin yuko tayari kuhusu makubaliano ya amani.
Alionya kwamba Uingereza na washirika wake wana nguvu za kusaidia kuilazimisha Urusi kufanya mazungumzo "kwa umakini."
Ikulu ya White House ilitoa kauli ya kufurahisha zaidi kuelekea mazungumzo ya Trump na Putin, ambayo yatafanyika kwa simu, ikisema amani nchini Ukraine "iko karibu sasa."
Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu kwamba Trump "amedhamiria" kupata makubaliano ya amani.
Pamoja na yote kuna mambo manne ambayo wengi wanayaona yatatawala mazungumzo ya viongozi hawa wawili, Putin na Trump.
Kusitisha mapigano kwa siku 30
Pendekezo la kusaka amani lilijadiliwa na wajumbe wa Ukraine na Marekani nchini Saudi Arabia wiki iliyopita. Baada ya saa kadhaa za kujifungia ndani ya chumba, walitangaza pendekezo la kusitisha mapigano kwa siku 30, na Ukraine ilisema iko tayari kukubali.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Trump amekuwa akijaribu kupata uungwaji mkono kutoka kwa Putin kwa pendekezo la siku 30 la kusitisha mapigano, lakini pande zote mbili (Urusi na Ukraine) zimeendelea kufanya mashambulio makali ya angani mapema Jumatatu.
Rais wa Ufaransa Macron na Waziri Mkuu mteule wa Canada Mark Carney, waliokutana siku ya Jumanne, walisisitiza mataifa yao yataendeleza uungaji mkono wao "usioyumba" kwa Ukraine na kutaka "ahadi za wazi" kutoka Urusi.
Kinu cha nyuklia
Washington imejadiliana na Ukraine kuhusu udhibiti wa Kinu cha Nyuklia cha Zaporizhzhia kinachokaliwa na Urusi kama sehemu ya makubaliano ya amani, Rais wa Marekani Donald Trump alisema Machi 13.
Kuhusu yale ambayo yatagusiwa katika mazungumzo hayo, Karoline Leavitt amesema: "Kuna mtambo wa kuzalisha umeme ambao uko kwenye mpaka wa Urusi na Ukraine, hilo litazungumzwa katika simu yake na Putin kesho."
Kiwanda kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya, cha Zaporizhzhia katika jiji la Enerhodar, kimekuwa chini ya uvamizi wa Urusi tangu 2022. Wakati kituo hicho kikisalia chini ya udhibiti wa Urusi, kwa sasa hakizalishi umeme.
Ukraine na washirika wake wamesisitiza mara kwa mara Urusi kuondoa wanajeshi wake kwenye kiwanda hicho. Wakati kikidhibitiwa na Urusi, mtambo huo umekuwa ukipoteza umeme mara kwa mara kutokana na gridi ya umeme ya Ukraine kushambuliwa na Urusi.
Ardhi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alipoulizwa siku ya Jumapili ni makubaliano gani yatazingatiwa katika mazungumzo ya kusitisha mapigano, Trump alisema: "Tutazungumza kuhusu ardhi. Tutakuwa na mazungumzo kuhusu mitambo ya kuzalisha umeme."
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alikataa kutoa maoni yake juu ya kile kitakacho jadiliwa na viongozi hao.
Wakati Putin alishawahi kusema anaunga mkono usitishaji vita, pia ameweka orodha ya masharti ya kupatikana kwa amani.
Moja ya maeneo ya mzozo ni eneo la Kursk Magharibi mwa Urusi, ambapo Ukraine ililivamia mwezi Agosti 2024, na kuteka baadhi ya maeneo.
Urusi ilifanya mashambulizi kuvirudisha nyuma vikosi vya Ukraine, na kulirudisha tena chini ya udhibiti wa Urusi katika wiki za hivi karibuni, na Putin anadai eneo hilo limerudi kikamilifu katika udhibiti wake.
Mshauri wa masuala ya kiusalama wa Marekani, Michael Waltz aliulizwa katika mahojiano ya ABC ikiwa Marekani itakubali makubaliano ya amani ambayo Urusi itachukua eneo la Ukraine ililoliteka:
Amesema anaona fursa nzuri ya kumaliza vita baada ya Kyiv kukubali pendekezo la kusitisha mapigano, lakini pia amekuwa akisema mara kwa mara eneo la Ukraine haliwezi kujadiliwa na Urusi lazima isalimishe eneo ililolinyakua.
Urusi iliteka Rasi ya Crimea mwaka 2014 na inadhibiti sehemu kubwa ya maeneo manne ya mashariki mwa Ukraine baada ya kuivamia nchi hiyo mwaka 2022.
Wanajeshi wa Nato

Chanzo cha picha, Getty Images
Pia kuna maswali mengi kuhusu jinsi usitishaji vita utakavyotekelezwa na kufuatiliwa, huku Putin akisema hatakubali wanajeshi wa Nato kwenye eneo hilo.
Urusi itatafuta dhamana katika makubaliano yoyote ya amani kwamba mataifa ya NATO yanaizuia Kyiv kupata uanachama huo na Ukraine itasalia kutoegemea upande wowote, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Alexander Grushko alikiambia chombo cha habari cha Urusi Izvestia katika matamshi yaliyochapishwa Jumatatu.
Putin amesema hatua zake nchini Ukraine zinalenga kulinda usalama wa taifa la Urusi dhidi ya kile anachosema ni nchi za Magharibi zenye uchokozi, hususan upanuzi wa NATO upande mashariki.












