Familia zazungumzia uokoaji wa 'muujiza' wa mateka wa Hamas

"Walilazimishwa kuzungumza kwa kunong'ona," anasema Michael Kozlov, ambaye mtoto wake wa kiume alikuwa mmoja wa mateka wanne waliookolewa na vikosi maalumu vya Israel kutoka katika himaya ya Hamas katikati mwa Gaza siku ya Jumamosi.
Kwa wazazi wa Waisraeli wa Urusi, Andrey, moja ya kile jeshi liliita "almasi" wakati wa operesheni yake, haikuwa "muujiza".
Wakizungumza na BBC, Eugenia na Michael Kozlov walitoa maelezo ya hisia jinsi walivyosikia habari kwamba mtoto wao alikuwa huru na maelezo ya masaibu yake kwa muda wa miezi minane.
Picha za kamera zilizotolewa na jeshi la Israel zinaonesha Andrey, 27, na mateka mwingine, wakiwa wameinua mikono yao kwa woga walipokuwa wamejificha ya baada ya waokoaji kuingia ndani ya chumba walimokuwa wamezuiliwa.
Ajabu, baada ya miezi kadhaa mama yake, Eugenia Kozlova anasema watekaji hawakuwa wazi kama mpango huo ulikuwa "kuwaua au kuwaachia".

Chanzo cha picha, Reuters
Wanaume hao walikuwa wameambiwa kwamba Waisraeli walikuwa wamesahau kuhusu wale waliokuwa mateka, kwamba walionekana kuwa tatizo na mamlaka ya Israel na wangeweza kulengwa kuwaondoa, ikiwa uwepo wao utagunduliwa.
Michael Kozlov anasema mwanaye na mateka wengine waliambiwa wapunguze sauti zao kwa sababu, kulingana na walinzi wao, "ndege maalum ya upelelezi, ndege isiyo na rubani, ilikuwa ikisikiliza na inaweza kusikia walichokuwa wakisema kwa Kiebrania".
"Hii ilisababisha kiwewe kikubwa sana cha kisaikolojia ambacho kilimlazimu kwa kiasi fulani kuamini maneno yao," Bw Kozlov anaongeza.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Alipotea hadi akagundua kuwa alikuwa akiokolewa."
Andrey, pamoja na wengine watatu waliokolewa kutoka kambi ya Nuseirat ya Gaza, Noa Argamani, Almog Meir Jan na Shlomi Ziv, walikuwa wametekwa nyara kutoka kwenye tamasha la muziki la Nova asubuhi ya 7 Oktoba.
Alikuwa akifanya kazi huko kama mlinzi baada ya kuhamia Israel kutoka Urusi miezi 18 tu iliyopita.
Eugenia Kozlova, ambaye hasa anaishi St Petersburg, amekuwa akija Israel mara kwa mara ili kujiunga na mikutano ya familia ya mateka na kukutana na wanasiasa na wawakilishi wa jeshi, na alitarajiwa kurejea Tel Aviv wakati maafisa wa Israel walipompigia simu na kumpa habari kuhusu mtoto wake.
"Nilifikiri ni habari mbaya na nikaanza kupiga kelele: 'Hapana!' Nilitupa simu yangu na ikaanguka mahali fulani chini ya meza," anakumbuka.
"Niliweza kuwasikia wakipiga kelele kutoka chini ya meza: 'Tuna habari njema!'
"Niliingia chini ya meza. 'Unasema nini?'
"Habari njema sana: Andrey aliachiliwa. Kiingereza changu si kizuri. Niliwaomba warudie tena."

Chanzo cha picha, Israel Police
Wote wawili walikuwa na wasiwasi kuhusu jinsi Andrey angetokea walipomwona kwa mara ya kwanza kwenye simu ya video lakini walifarijika kujua kwamba alionekana vyema.
"Alicheka, alitania. Saa tatu tu baada ya kuwa Gaza aliweza kufanya mzaha," mama yake anasema.
"Alikuwa gerezani, alikuwa mfungwa, kisha baada ya saa chache sana, alijikuta amerejea katika eneo la Israel," anaongeza.
Wana Kozlov hawaendi katika maelezo ya kile mtoto wao amesema kuhusu hali ya uokoaji wake. Baada ya mateka watatu wa kiume kuokolewa, jeshi la Israel linasema kulikuwa na ufyatulianaji wa risasi na walinzi wa Hamas.
Baadaye, lori lililokuwa likitumiwa kuwahamisha mateka na maafisa wa kikosi maalumu waliojeruhiwa vibaya liliharibika na kuzingirwa na watu wenye silaha, kulingana na maafisa wa Israel.
Mashambulizi makali ya mabomu yaliyofanywa na jeshi la anga la Israel yalikusudiwa kuwapa waokoaji muda na kujifunika ili kutoroka.
Maafisa wa afya wa Gaza wanasema kuwa tukio hilo lilikuwa moja ya matukio mabaya zaidi tangu vita hivyo kuanza na kwamba zaidi ya Wapalestina 270 waliuawa.
Jeshi la Israel linasema kuwa chini ya 100 waliuawa. Inaeleza kuwa Hamas inawajibika kwa vifo vya raia kwani ilikuwa ikiwaficha mateka katika sehemu yenye watu wengi.

Chanzo cha picha, Reuters
"Kwa muda wa miezi miwili alikuwa amefungwa mikono na miguu," mama yake anasema, sauti yake ikitetemeka. Kwa vile Andrey alichukia kula "kama mnyama", alijaribu kujipindapinda ili kutoa mikono yake iliyokuwa nyuma ya mgongo wake.
Watekaji "waliwadhalilisha na kuwapiga", Michael Kozlov anaendelea, lakini mbaya zaidi ilikuwa dhihaka ya kikatili.
"Walikuwa daima chini ya shinikizo la kisaikolojia. 'Mama yako tayari ameenda likizo Ugiriki. Tunafahamu. Tuliona. Mke wako anachumbiana na mtu mwingine," Eugenia anasimulia.
Katika Israel kote kumekuwa na mwitikio wa furaha kwa operesheni hiyo ya uokoaji.
"Watu wanaegemea magari yao na kupiga kelele na kumsalimia Andrey. Sasa tunatazama habari, na ninashangaa kwamba kuachiliwa kwa mateka wanne imekuwa sherehe kwa Israel yote," anasema Eugenia.
Israel bado inayumbayumba kutokana na mashambulizi yanayoongozwa na Hamas ambayo yaliwauwa takriban watu 1,200 miezi minane iliyopita.
Kati ya mateka zaidi ya 240 ambao walikamatwa na kupelekwa Gaza, zaidi ya 100 waliachiliwa katika usitishaji mapigano wa wiki moja mnamo Novemba.
Israel inasema sasa kuna mateka 116 ambao walitekwa nyara siku hiyo ambao wamesalia Gaza, ikiwa ni pamoja na karibu theluthi moja ambao imehitimisha kuwa hawako hai tena.
Kabla ya uokoaji wa Jumamosi ni mateka watatu tu wa Israel waliokuwa wameshikiliwa huko Gaza waliachiliwa huru kutokana na shambulio la ardhini la jeshi, na mafanikio ya operesheni ya hivi karibuni yaliipa taifa hilo nguvu.
Kwa Eugenia, ambaye amejua jamaa nyingi za mateka, kuna ukumbusho wa mara kwa mara wa jinsi alivyo na bahati. Karibu na Tel Aviv na karibu na nyumba ya Andrey katikati mwa Israel, kuna mabango mengi yaliyobandikwa ya wale ambao bado hawajapatikana.
"Inasikitisha sana kutazama picha hizi," anasema. "Wako kila mahali. Na sasa ninatazama nyuso zao, na ninaonekana kuwa na hisia ya hatia, kwa sababu tunaelewa vizuri sana, tunaambiana mara kadhaa kwa siku, kwamba huu ni muujiza!"
Licha ya yote ambayo mtoto wao aliteseka, wana Kozlov wana mwelekeo wa kuamini walinzi ambao walimwambia kwamba alishikiliwa katika hali bora kuliko mateka wengine wengi wa Israel, waliwekwa kwenye vichuguu chini ya ardhi na kunyimwa mwanga.
"Tunafikiria mara kwa mara juu ya watu hao ambao bado wako. Lazima tuwaokoe," Michael anasema kwa msisitizo.
Ingawa hawajakata tamaa ya kuwafanyia kampeni mateka, familia hiyo sasa inatumia nguvu zao nyingi kumsaidia Andrey kuzoea maisha ya nyumbani baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Baada ya siku 245 akiwa utumwani, bado anapata matukio yote ambayo yametokea ,ikiwa ni pamoja na maandamano makubwa ya kudai serikali ya Israel kuwarudisha mateka nyumbani.
"Anashangazwa na mambo mengi halafu habari ambazo hakujua wakati mwingine zinamzuia kulala," mama yake anasema.
"Kisha anasoma makala, na anasema: "Je, hii ni kweli? Je, hii ni kweli? Ilifanyika?"
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












