Kuanzia Harare, Luanda, hadi Brussels: Kwanini wiki hii ni muhimu kwa mzozo wa DRC?

g

Chanzo cha picha, X/Présidence RDC, Paul Kagame/Flickr

Maelezo ya picha,
Muda wa kusoma: Dakika 6

Wiki hii yatashuhudiwa matukio muhimu kuhusu vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo mazungumzo ya amani yanatarajiwa kufanyika Harare na Luanda huku mjini Brussels ukitarajiwa kufanyika mkutano ambao unasemekana huenda ukapitisha azimio la vikwazo.

Mgogoro wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa muda mrefu umekuwa ukisumbua nchi za kikanda, hasa kwa vile nchi hii ya pili kwa ukubwa barani Afrika na ya 11 kwa ukubwa duniani ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika ya Kati.

Juhudi za mashirika ya kikanda sasa ni mojawapo ya mambo yanayotoa matumaini ya kumalizika kwa vita hivi, kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali.

Wakati mpatanishi wa mgogoro wa Congo, Rais wa Angola João Lourenço, Jumamosi aliomba kwamba kuanzia usiku wa manane wa siku hiyo - siku moja kabla ya jana, Jumapili, pande zinazozozana zianze usitishaji mapigano kabla ya mazungumzo kuanza, Jumapili kulikuwa na ripoti za mapigano katika sehemu za Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

EAC na SADC hadi Harare

Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Afrika Mashariki -EAC na nchi wanachama wa SADC umepangwa kufanyika Jumatatu hii mjini Harare, Zimbabwe, kujadili suala la DRC.

Mkutano huu ambao ulipangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa Februari uliahirishwa na sasa unachunguza mapendekezo yaliyotolewa na viongozi wa kijeshi kutoka nchi hizo mbili kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kutatua mzozo huo.

Wakuu wa kijeshi wa nchi kutoka makundi haya walikutana mjini Harare siku ya Jumapili - mkutano wao wa pili baada ya ule uliofanyika Nairobi, Kenya, mwishoni mwa mwezi uliopita - mkutano wao wa Jumapili "ulilenga kuhakiki" maazimio ya mikutano ya mawaziri wa EAC na SADC ambayo itafanyika Harare Jumatatu, kulingana na sekretarieti ya SADC.

Duru za habari zinasema kuwa wakuu wa kijeshi wa nchi hizo mbili wametayarisha maazimio kuhusu nini kifanyike ili kukomesha uhasama na njia za kuondoka katika mgogoro huo.

Maamuzi yaliyochukuliwa na wakuu hao wa kijeshi walioyapitia tena Jumapili, yanatarajiwa kuchunguzwa na mawaziri wa mambo ya nje katika kikao chao cha Jumatatu, kabla ya pia kuwasilisha mapendekezo yao, ambayo yatapitishwa na wakuu wa nchi kabla ya kutekelezwa.

Majadiliano mjini Harare yataashiria kile kitakachojadiliwa katika tukio kubwa lililopangwa mjini Luanda, Angola.

Unaweza pia kusoma:

Kinshasa na M23 ana kwa ana Luanda

h

Chanzo cha picha, M23

Maelezo ya picha, Bertrand Bisimwa - aliyehukumiwa kifo huko Kinshasa, amealikwa kwenye mazungumzo na mamlaka ya Kinshasa huko Luanda.

Msemaji wa Rais wa DR Congo Félix Tshisekedi, Tina Salama, alinukuliwa na Reuters akithibitisha kwamba Kinshasa itatuma timu ya kuelekeza mazungumzo na M23.

Majina ya wajumbe wa Kinshasa kwa mazungumzo hayo yaliyopangwa kuanza kesho Jumanne, hayajatangazwa.

Vuguvugu la M23 lilithibitisha kwamba mkurugenzi wake wa kisiasa, Bertrand Bisimwa, alialikwa kuwakilisha kundi hilo, ambalo kwa sasa linadhibiti miji mikuu ya majimbo ya Kivu Kaskazini - Goma, na Kivu Kusini - Bukavu, na baadhi ya maeneo ya majimbo haya.

Bissimwa ni miongoni mwa viongozi wa M23, na Wizara ya Sheria ya ya DRC hivi majuzi ilitoa zawadi ya dola milioni 5 kwa habari zitakazowezesha kukamatwa kwake kwa sababu, kama wenzake, alihukumiwa kifo katika kesi iliyoendeshwa Kinshasa bila kuwepo mahakamani.

g

Chanzo cha picha, Rais wa Jamhuri - Angola

Maelezo ya picha, Siku ya Ijumaa, Rais Tshisekedi alimtuma mjumbe wake Mambu Sita Sumbu, ambaye kwa sasa anafuatilia mazungumzo ya Luanda, na ujumbe kwa Rais wa Angola João Lourenço.

Mazungumzo ya mjini Luanda yaliyopangwa kuanza Jumanne, ni mabadiliko makubwa katika suala hili na yanaweza kuleta suluhu

Wachambuzi wanasema kuwa ni hatua kubwa baada ya serikali ya Kinshasa kutangaza kwa muda mrefu kwamba kamwe haitafanya mazungumzo na vuguvugu la M23.

Baadhi ya masuala makuu yanayoweza kujadiliwa kati ya Kinshasa na M23 huko Luanda ni pamoja na;

  • Kusitisha mapigano na jinsi ya kutekeleza hilo
  • Kusoma na kukubaliana na madai ya M23 kwa Kinshasa
  • Kusoma na kukubaliana kuhusu madai ya serikali ya Kinshasa kutoka M23 na Kigali
  • Kukubaliana juu ya matakwa kutoka kwa mamlaka za kikanda katika mikutano kama ule wa Harare
  • Suala la Goma na Bukavu na maeneo yaliyotekwa na M23
  • Mustakabali wa wapiganaji na viongozi wa M23

Wachambuzi mbalimbali wanasema kuwa mazungumzo haya yanaweza kuwa marefu kabla ya kukamilika na kufikiwa kwa makubaliano, na kwamba kufikia muafaka kunaweza kuwa vigumu. Wanathibitisha kwamba kazi muhimu zaidi inafanywa na wapatanishi.

' Rwanda na Ubelgiji kukata uhusiano baina wa kidiplomasia'

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati juhudi zikifanyika barani Afrika kutafuta amani na suluhu la vita hivi, mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) umepangwa kufanyika leo mjini Brussels.

Mkutano huo unaongozwa na Kaja Kallas, Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya wa Mambo ya Nje na Sera ya Usalama - ambaye alikutana na viongozi mbalimbali wa Rwanda wakati wa ziara yake mjini Brussels wiki iliyopita - na ambaye alisema amewataka "kuondoa wanajeshi wa Rwanda kutoka DRC ".

Huku haya yakijiri, serikali ya Rwanda imesitisha uhusiano wake wakidiplomasia na Ubelgiji Jumanne.

Katika ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa X, ''Rwanda imeifahamisha serikali ya Ubelgiji kuhusu uamuzi wake wa kuvunja uhusiano wa kidiplomasia, unaoanza mara moja moja. Uamuzi wa Rwanda umechukuliwa baada ya kuzingatia kwa makini mambo kadhaa, yote yakihusishwa na majaribio ya kusikitisha ya Ubelgiji kuendeleza udanganyifu wake wa ukoloni mamboleo'', Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa imenandika kwenye ukurasa huo wa kijamii.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

Mwisho wa X ujumbe

Kujibu hatua hii ya kigali, Ubelgiji pia imesitisha uhusiano wa kidiplomasia na Rwanda, ikisema imesikituishwa na hatua ya Kigali kukata uhusiano huo, jambo ambalo inasema lingetatuliwa kwa mazungumzo.

Suala la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haliko katika ajenda ya mkutano wa leo wa Umoja wa Ulaya, lakini vyombo mbalimbali vya habari vinaripoti kwamba mkutano huo utaidhinisha vikwazo ambavyo hapo awali vilipangwa kwa watu tisa - wakiwemo Wanyarwanda - na makampuni kwa madai ya kuhusika katika vita mashariki mwa DR Congo.

Redio RFI inaripoti kuwa orodha ya watu hao ilitayarishwa kama sehemu ya vikwazo ambavyo vilitarajiwa kuwekwa na Umoja wa Ulaya mwezi uliopita, lakini vilizuiwa na Luxembourg kwa kutumia kura yake ya turufu ndani ya umoja huo.

h

Chanzo cha picha, Olivier Nduhungirehe/X

Maelezo ya picha, Wiki iliyopita, Kaja Kallas - ambaye ni mwenyekiti wa mkutano wa leo - alikutana na viongozi wa upande wa Rwanda, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Olivier Nduhungirehe

Magazeti mbalimbali ya Ulaya yanathibitisha kwamba vikwazo hivi dhidi ya watu binafsi - ambavyo havijatangazwa bado - vinaweza kuthibitishwa leo, na vikwazo hivyo ikiwa ni pamoja na kupigwa marufuku kuingia Ulaya na kunyang'anywa mali zao, kulingana na magazeti.

Wakati mwezi uliopita Umoja wa Ulaya ulisemekana kuzingatia vikwazo dhidi ya Rwanda, ambavyo ni pamoja na kusimamisha misaada na ushirikiano na Rwanda, pamoja na vikwazo kwa watu binafsi, Luxembourg iliripotiwa kusitisha hatua hiyo, ikisema kuwa umoja huo unapaswa kutoa kipaumbele kwa juhudi za jumuiya za SADC na EAC katika kutatua suala hilo.

Katika siku za hivi karibuni, serikali ya Rwanda haijakanusha waziwazi wala kuthibitisha kuunga mkono vuguvugu la M23, ikieleza tu kwamba imechukua hatua za kulinda mipaka ya nchi hiyo kutokana na wasiwasi ulioibuliwa na vuguvugu la FDLR, ambalo Kinshasa inatuhumiwa kushirikiana nalo, tuhuma ambazo Kinshasa inakanusha.

Mamlaka za Rwanda, zikiendelea na vikwazo vilivyokwisha chukuliwa na vile vinavyopaswa kuchukuliwa, hivi karibuni zimesema kwamba "hatua za upande mmoja" hazitasuluhisha tatizo hilo, bali "zitadhoofisha juhudi za umoja wa Afrika".

Katika hotuba yake Jumapili mjini Kigali, Rais Paul Kagame aliikosoa Ubelgiji kwa kuongoza juhudi za "kutoa wito kwa dunia nzima kuungana kwa ajili ya Rwanda".