Houthi: Ni akina nani na harakati zao zilianzaje?

Chanzo cha picha, SCREENSHOT
Tangazo la kundi la Houthi la Yemen la kukamata kile linachosema ni "meli ya Israel" katika Bahari Nyekundu linaendelea kuibua hisia nyingi.
Msemaji wa vikosi vya Houthi, Yahya Saree, alitangaza "meli ya Israel" imepelekwa kwenye pwani ya Yemen, lakini Israel imekanusha kuwa meli hiyo ni yake na wala haina raia wake yeyote.
Oktoba 31, kundi la Houthi lilitangaza kwa mara ya kwanza kuilenga Israel kwa idadi kubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani. Mgogoro wa Israel na Hamas ndio chanzo cha Houth kuilenga Israel.
Houthi ni akina nani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Houthi iliibuka kutoka tumboni mwa mzozo wa serikali ya Yemen, lakini mzizi wa itikadi za madhehebu hayo ni Zayd, moja ya madhehebu ya Kishia.
Mafundisho ya Zayd kihistoria yana sifa ya uasi dhidi ya dhulma. Mizizi yake inarejea kwenye mapinduzi ya Zaid bin Ali bin Al-Hussein bin Ali bin Abi Talib, katika mji wa Kufa, dhidi ya utawala wa Bani Umayya katika karne ya nane AD na kuuawa kwake mikononi mwa gavana wa Khalifa wa Umayyad, Hisham bin Abdul Malik.
Mambo mengi yamechangia kuibuka kwa Houthi, ikiwa ni pamoja na sababu za kiitikadi, kisiasa, kihistoria na kijiografia – yakiwemo madai ya haki za wakazi wa maeneo yenye wa-Zayd wengi.
Mwaka 1990 ndipo lilipoundwa vuguvuvugu la kwanza lililoitwa "Waumini Vijana," likisukumwa na hali halisi ya kutengwa kwa maeneo ya Zayd, yenye takribani asilimia 35 hadi 40 ya idadi ya watu wote wa Yemen.
Harakati hiyo ilizidi umaarufu baada ya kuongezeka wafuasi vijana walioshiriki harakati za kundi hilo – wakiimba kulaani Israel na Marekani wakati wa swala za Ijumaa misikitini.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mamlaka iliwashughulikia vijana hao kwa kuwakamata na kisha kuwaachilia baada ya muda mfupi na kisha walirudi kwenye shughuli zao za awali.
Kiongozi wa kwanza wa vuguvugu hilo, Hussein Badr al-Din al-Houthi, mtoto wa mhubiri mashuhuri, mwanzoni mwa maisha yake ya kisiasa alijihusisha na chama kidogo kinachojulikana kama "Al-Haq."
Chama hiki kilishinda viti viwili katika bunge la Yemen katika uchaguzi wa 1993, na Hussein alishinda mmoja ya viti hivyo katika kipindi cha kati ya 1993 na 1997.
Baada ya Septemba 11, 2001 na matukio yaliyofuata, kama vile uvamizi wa Iraq, Hussein Al-Houthi alifuata njia mpya iliyojumuisha "uamsho wa imani" na "kupinga-ubeberu," iliyoathiriwa na mawazo ya jumla ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Shughuli za "Waumini Vijana," ambazo mwanzoni zilikuwa tu ni kutetea haki za watu wa eneo la Saada, zilipanuka na kujumuisha utoaji wa huduma za kijamii na kielimu na misimamo ya kisiasa ikiwemo upinzani dhidi ya utawala wa aliyekuwa Rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh.
Kubadilika kwa Vuguvugu

Chanzo cha picha, Getty Images
Vuguvugu hilo liligeuka kuwa kundi lenye silaha 2004 katikati ya makabiliano na vikosi vya serikali, mwaka ambao Hussein al-Houthi aliuawa na mdogo wake Abdul Malik akamrithi katika uongozi.
Harakati hiyo ilichukua majina tofauti hadi hatimaye ikatulia kwenye jina la "Houthi."
Japokuwa Wazaidi walitawala Yemen katika kipindi chote cha historia hadi ulipopinduliwa utawala wa Imam wao huko kaskazini mwa Yemen mwaka 1962.
Ngome ya Houthi iliyo mbali na udhibiti wa serikali kuu huko Saada ilibakia kupuuzwa na kutengwa, na kuwalazimu watu wa eneo hilo kujitegemea wenyewe, kujisimamia na kujenga miundombinu kwa rasilimali zao wenyewe.
Mtafiti wa Uingereza wa masuala ya Yemen, Sheila Weir, anaamini sababu nyingine ya kuibuka Houthi huko Yemen, ni kuenea kwa makundi ya Kisalafi na Kiwahabi na ushawishi wao unaoongezeka nchini Yemen na kuwasili kwao hata katika ngome za Houthi.
Ware anasema, “hadi miaka ya 1980, milima ya Saada ilikuwa ni Zayd tu. Katika miaka ya 1990, Usalafi iliibuka katika ngome ya Houthi. Ukiungwa mkono na maafisa wa Yemen, akiwemo Rais Ali Abdullah Saleh, na wafanyabiashara wa Yemen na Saudi."
Makovu ya Vita

Chanzo cha picha, REUTERS
Vuguvugu hilo lilianzisha mzozo wa kivita na serikali ya Saleh, kukawa na vita sita kati ya 2004 na 2010. Katika maeneo ambayo Wahouthi walienea kaskazini – vita viliacha makovu makubwa. Saudi Arabia ilipigana na Wahouthi mwaka 2010 pamoja na vikosi vya serikali ya Yemen.
Idadi halisi ya wahanga wa vita vya mwisho 2009 na 2010 haijulikani kutokana na mifumo ya kutoa taarifa kuzimwa, lakini vilisababisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu.
Wahouthi walishiriki kwa kiasi kikubwa katika maandamano dhidi ya utawala wa Saleh mwaka wa 2011 na walikuwa kundi kuu katika vikao vya mazungumzo ya kitaifa.
Kuanguka kwa utawala wa Saleh mwaka 2012 kulitoa fursa muhimu kwa Wahouthi kuimarisha nafasi na ushawishi wao nchini Yemen, hasa baada ya baadhi ya wafuasi wa adui wao mkuu Saleh kugeuka kuwa wafuasi wao wa kijeshi.
Mwaka wa 2014, Wahouthi waliingia mji mkuu, Sana'a, na kuukalia kwa mabavu baada ya kuvishinda vikosi vya Jenerali Ali Mohsen al-Ahmar na vikosi vya Saleh, na kuchukua udhibiti wa taasisi na idara za serikali.
Mapema 2015, waliizingira Ikulu na kumuweka katika kizuizi cha nyumbani Rais Abd Rabbuh Hadi na maafisa wa serikali yake. Mwezi mmoja baadaye, Hadi alifanikiwa kutoroka kifungo cha nyumbani, alifika kusini mwa Yemen na baadaye kuingia Saudi Arabia.
Wahouthi na adui wao wa zamani - Ali Abdullah Saleh - walishirikiana katika juhudi za kupanua udhibiti wao katika maeneo yote ya Yemen.
Hata hivyo, Saudi Arabia, ambayo mara kwa mara imekuwa ikiishutumu Iran kuwaunga mkono Wahouthi, ilihisi wasiwasi mkubwa kuhusu muungano huu na juhudi zake za kuidhibiti Yemen, hivyo ilianza kampeni ya mashambulizi ya anga.
Mashambulizi hayo yalilenga kuwalazimisha Wahouthi kumrejeshaa Hadi kwenye usukani wa madaraka, lakini kampeni hiyo ilishindwa kufikia lengo hadi sasa.
Kampeni ya kijeshi ya Saudia ilisababisha uharibifu mkubwa kote Yemen, ikitajwa kuwa moja ya nchi masikini zaidi hata kabla ya kuanza kwa mashambulizi ya mabomu, pamoja na mzozo mkubwa wa kibinadamu.
Muungano wa Houthi na Saleh, ambaye aliuawa na Wahouthi alipokuwa akijaribu kutoroka Sanaa, ulivunjika Desemba 2017.
Lakini kwa sasa inaonekana Saudi Arabia imewashawishi wahusika wakuu katika mzozo wa Yemen kukubaliana kusitisha mapigano, ili kuwepo na mazungumzo kuhusu mustakabali wa mchakato wa kisiasa nchini humo.
Maafisa wa Saudia walikutana na Wahouthi, mbele ya wapatanishi kutoka Oman, Aprili 9, 2023 katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa, ambao unadhibitiwa na Houthis. Na mazungumzo yao bado yanaendelea.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla














