Nchi sita za Kiarabu: Wote walikuwa wanajeshi na walipoingia madarakani hawakutaka kuondoka hadi vita vikawatimua

Kwa mbali unaweza ukafirikia ni kana kwamba safari zao katika uongozi zilipangwa ,lakini kilichowafanyikia baadaye katika maisha yao ya uongozi kinaonekana kama sadfa .
Ukweli ni kwamba marais wa nchi hizi sita za Kiarabu waliingia madarakani kwa njia zinazofanana ,mbinu zao za utawala zilifanana na hata waliondolewa madarakani kupitia njia zinazohusiana kwa vile wengi walifurushwa baada ya maaandamano ya wananchi .
Kwanza viongozi hawa wa zamani wa nchi za Tunisia,Yemen,Algeria,Sudan ,Misri na Libya walianzia katika jeshi ambapo walihudumu kwa muda kisha wakajitosa katika siasa kwa kupindua serikali au kutumia nguvu na baadaye wakaanza udikteta na kukosa kutimiza ahadi walizotoa kwa wananchi wao .
Hatima yao yaonekana kuwa moja kwani wengine waliuawa huku baadhi wakifurushwa madarakani kwa njia ya aibu na kufa ama kuishi maisha ya kimya ulimwengu usijue yaliyowasibu .Hii ni simulizi ya viongozi hao ambao yaliyowakumba ni kama maigizo ya filamu .
Ben Ali -Tunisia
Rais wa zamani wa Tunisia Ben Ali alikuwa mpiganaji wa ukombozi wa taifa lake dhidi ya Ufaransa .Baada ya nchi yake kupata uhuru alipanda ngazi hadi alipokuwa mkuu wa ujasusi .Mnamo mwaka wa 1986 Ben Ali aliteuliwa kuwa waziri mkuu na aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Habib Bourgiba ambaye aliongoza vita vya Tunisia kujitawala.Umaarufu wa Habib ulikuwa umeanza kudidimia wakati huo .

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwezi mmoja baadaye Ben Ali alipanga mapinduzi ya kijeshi na kumuondoa Bourgiba madarakani .Alijitangaza rais mpya wa nchi na chama chake tawala kikadhibiti bunge kwa haraka sana .Utawala wake ulianza kutiliwa doa pale wapinzani ,wakosoaji ,wanahabari na wanaharakati walipoanza kukamatwa na kufungwa jela .
Kufikia mwaka wa 2010 Tunisia ilikuwa ikitajwa kama mojawapo ya nchi kandamizaji zaidi duniani . Vikwazo vya kiuchumi vilifuata na maisha yakawa magumu kwa raia wengi wa Tunisia ambao sasa walianza kumuelekezea Ben Ali hasira zao .
Chuma chake kilikuwa kimeshapashwa moto mwaka wa 2010 wakati mchuuzi mmoja kwa jina Mohammed Bouazizi alipojiteketeza baada ya leseni yake kufutiliwa mbali na idara moja ya serikali .Hapo ndipo maandamano ya nchi nzima yalipozuka na kufikia tarehe 14 Januari mwaka wa 2011 Ben Ali aliacha madaraka na kukimbilia Saudi Arabia pamoja na familia yake ili kukwepa mashtaka mbali mbali hadi kifo chake mwaka wa 2019.Alikuwa ameiongoza Tunisia kwa miaka 23.
Hosni Mubarak-Misri
Hosni Mubarak pia alikuwa mwanajeshi na alikuwa rubani wa ndege za kivita wakati nchi yake ilipokuwa ikipigana na Israel katika vita vya Yom Kipur mwaka wa 1973 .
Ni wakati wa vita hivyo alipojijengea sifa kama shujaa wa nchi yake na miaka miwili baadaye alikuwa katika wadhifa mpya kama makamu wa rais baada ya kuteuliwa na Anwar Sadaat .

Chanzo cha picha, Reuters
Mnamo mwaka wa 1981 Sadaat aliuawa katika hafla moja ya kijeshi na Mubarak akachukua usukani wa nchi kama rais mpya .
Aliwaahidi Wamisri mambo mengi na wengi waliamini kwamba hali ya maisha yao ingeboreka lakini muda mfupi baadaye hali ilianza kuwa mbaya baada ya kuibuka madai kwamba Mubarak na familia yake walikuwa wakiiba kiasi kikuba cha fedha za umma .
Utawala wake ulianza kuwa kama wa kijeshi huku idara za usalama zikichukua udhibiti wa masuala muhimu ya uongozi na sera . Misri ilibadlika na kuwa kama nchi inayoendeshwa kipolisi huku kila mmoja akijawa uwoga .Upinzani haukukubalika na wengi wakaanza kujipata jela au kutoweka .
Mnamo Januari tarehe 25 mwaka wa 2011 maelfu ya watu walikongamana katika eneo maarufu la Tahrir Square ili kumshinikiza rais wao aondoke madarakani .
Siku 18 baadaye baada ya mamia ya waandamanaji kuuawa na polisi Mubarak alilazimishwa na jeshi kuondoka madarakai .Alikamatwa pamoja na wanawe na washirika wake na kushtakiwa kwa ufisadi na mauaji ya waandamanaji.Baadaye chini ya utawala wa jeshi aliachiliwa huru baada ya mashtaka dhidi yake kufutwa na kuaga dunia mwaka wa 2020 baada ya kuitawala Misri kwa miaka 30
Muammar Gaddafi -Libya
Akiwa na umri wa miaka 27 tu , Gaddaf alipindua utawala wa kifalme wa Mfalme Idris wa kwanza mwaka wa 1969. Alianzia katika jeshi pia na alisaidiwa kuingia madarakani na kundi la maafisa wake jeshini waliojiita Free Officers Movement. Jukumu lake la kwanza lilikuwa kutaifisha kampuni za mafuta nchini mwake hatua ambayo haikupokelewa vyema na nchi za magharibi .
Mwanzoni mwa utawala wake Gaddafi alifaulu kuwapa raia wa Libya maisha mazuri na hali ya uchumi haikuwa mbaya .Mnamo mwaka wa 1973 alianzisha marekebisho ya mfumo wa utawala ili kutegemea itikadi zake alizosema ni za kiarabu na kutegemea nguzo za Jamhuri ya umma na ya kiislamu .

Chanzo cha picha, Getty Images
Uhusiano wake na nchi za nje ulikuwa umevurugika na vikwazo vikaanza kuwabana Walibya katika nyanja zote hasa baada ya kuzuiwa kuuza mafuta yao mwaka wa 1982 .
Kisha umoja wa Mataifa pia ukazidisha vikwazo kufuatia shutuma kwamba Libya ilikuwa ikiunga mkono mashambulizi na vitendo vya kigaidi .
Utawala wake ulianza kuchukua sura ya udikteta wakati wananchi walipoanza kunung'unika na kampeni za kuwakandamiza wapinzani zikafuata . Hali iliongezwa kasi maandamano dhidi ya utawala wake yalipoanza mwaka wa 2011.
Maandamano hayo yaligeuka na kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe huku Gaddafi akiapa kamwe hangetoroka nchi yake hadi shambulizi la NATO lilipolenga msafara wake na kisha akashikwa na kundi la wapiganaji waliokuwa wakipambana na wanajeshi wake .
Kufikia wakati huo wengi wa waliokuwa wakimuunga mkono walikuwa wameshamuacha na kujiunga na makundi ya upinzani yaliyojihami na kuendeleeza harakati za kumtimua madarakani . Mojawapo ya makundi hayo ndio yanayolaumiwa kwa kumuua siku hiyo ambayo shambulizi la angani la NATO lililenga msafara wake alipokuwa akitoroka mapigano .Ulikuwa ni mwisho mbaya kwa Gaddafi ambaye alikuwa ameiongoza nchi yake kwa miaka 42 .
Ali Abdalla Saleh -Yemen
Saleh alianzia pia katika kambi ya jeshi wakati akishiriki vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Yemen Kaskazini katika miaka ya 60 na 70 .
Baadaye aliupindua utawala wa kifalme aliposaidiwa na rais wa Misri wakati huo Gamal Abdel Nasser .
Alichukua usukani kama rais wa Yemen Kaskazini na katika mwaka wa 1990 akaanzisha harakati za kuunganishwa kwa Yemen na akawa rais wa Yemen iliyounganishwa sasa.
Hata hivyo vita vilizuka na akapambana na wapinzani wake wa Houthi kwa miaka kadhaa huku akishtumiwa pia kwa wizi wa mabilioni ya pesa za umma .Mnamo mwaka wa 2011 maandamano ya wananchi yalianza huku hali ya uchumi ikiwa mbaya na wengi wakilalamikia ukosefu wa usalama na ufisadi serikalini .

Chanzo cha picha, Reuters
Alisema hatogombea muhula mwingine lakini alikataa kuondoka madarakani na kusababisha raundi nyingine ya vita vya wenyewe kwa wenyewe .
Alishambuliwa na nusura auawe Juni mwaka huo na hata akaachwa na ulemavu .Mnamo mwaka wa 2014 alimuachia naibu wake hatamu za uongozi kumbe ilikuwa na njama ya kwenda kuanza uasi aliposhirikiana na Wahouthi ambao walikuwa ni mahasimu wake wa tangu jadi .
Hali hiyo ilisababisha kuzuka kwa vita na hata yeye na washirika wake wapya walifaulu kuuchukua mji mkuu wa Sanaa . Hata hivyo chake kilifika ukingoni mwaka wa 2017 wakati wahouthi walipogundua kwamba alikuwa akifanya mazungumzo na UAE pamoja na Saudi Arabia ili kurejea uongozini .Hatua hiyo ilichukuliwa kama usaliti na akauawa katika shambulizi la kuviziwa Disemba tarehe 4 .
Aliiongoza Yemen Kaskazini kwa miaka 12 na Yemen kwa miaka 22
Hassan Al Bashir - Sudan
Kiongozi huyo wa muda mrefu wa Sudan alianzia katika jeshi la Misri akishiriki pia vita vya Yom Kipur dhidi ya Israel mwaka wa 1973 . Alipanda ngazi akiwa katika jeshi la Misri hadi aliporejea Sudan kama kanali mwaka wa 1989 na alikuwa ameshajipangia mengi kweli . Aliongoza mapinduzi na kuanzisha matumizi ya sharia na pia utawala wake ulirithi vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya waislamu kaskazini mwa nchi na wakristo kusini mwa nchi hiyo .

Chanzo cha picha, Reuters
Vita vingine katika jimbo la Darfur vilimeletea matatizo ambako alidaiwa kutekeleza mauaji ya maelfu ya watu na uhalifu wa kivita .Alipatikana na hatia hiyo na mahakama ya ICC iliyomtaka ajisalimishe na hata baadaye waranti ikatolewa akamatwe .
Bashiri alikana kutejeleza uhalifu wa aina yoyote licha ya kutangazwa kwa madai hayo mwaka wa 2008 na 2012 . Kufikia mwaka wa 2018 wananchi walikuwa wameanza kupandwa na hamaki dhidi ya utawala wake .Aliposema atawania tena urais maandamano yalizuka na kufikia Aprili 2019 jeshi lilikuwa limeshachukua usukani wa nchi na kuahidi kumfungulia mashtaka mbali mbali .Mnamo februari mwaka wa 2020 jeshi linaloongoza serikali lilisema limekubali kumkabidhi kwa ICC ili ajibu mashtaka kuhusiana na mauaji ya watu yaliyotekelezwa Darfur
Abdelaziz Bouteflika -Algeria
Alikuwa mwanajeshi ambaye alipambana na ukoloni wa Wafaransa na baadaye mwaka wa 1974 alikuwa rais wa bunge la UN .
Baadaye alishtumiwa kwa kuiba mabilioni ya fedha na akatoroka huku akishtakiwa akiwa mafichoni .Alikubali kurejesha sehemu ya fedha hizo na mnamo mwaka wa 1992 jeshi liliipindua serikali na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yakaanza.
Mnamo mwaka wa 1999 aligombea uchaguzi wa urais na kushinda kura kwa kuungwa mkono na jeshi .Aliahidi kuboresha uchumi lakini kilichofuata ni udikteta na ukandamizaji wa wapinzani hatua iliyozua hali ya uwoga nchini mwake .

Chanzo cha picha, Getty Images
Maandamano yalianza mwaka wa 2011 na aliyatuliza kwa kuahidi vijana nafasi za kazi na kuboresha hali ya maisha yao lakini wengi hawakumuamini na miaka miwili baadaye akadaiwa kupondwa na maradhi ya kiharusi .
Wengi hawakumuona hadharani wakashangaa iwapo alikuwa hai na endapo ndiye aliyekuwa akiendesha serikali . Mnamo 2019 alitangaza kwamba atawania tena urais na hapo ndipo mlipuko mwingine wa maandamano ulipomlazimisha kuondoka madarakani Aprili tarehe 2 na amesalia kimya hadi leo














