Simu ya mkononi:Kifaa hiki kidogo kinaweza kuvuruga maisha yako milele

sm
    • Author, Yusuf Jumah
    • Nafasi, BBC Swahili

Simu ya mkononi au rununu ni kifaa kidogo chenye athari kubwa kwa maisha yetu na kwa wanaokitumia vizuri manufaa yake ni makubwa pia .

Ulimwengu wa teknolojia unamaanisha kwamba matumizi ya simu ya mkononi ni jambo la kawaida na kila mwaka mamilioni ya watu wanaingia katika kundi la wanaoanza kutumia simu za mkononi.

Hilo limerahisisha mawasiliano na huduma kote duniani .

Hata hivyo matumizi ya simu za mkononi yanakuja na madhara yake ambayo mwanzoni watu wengi hawakuwa wakijua yanaweza kuvuruga maisha yao sio tu kiafya bali pia kisaikolojia na hata kuhatarisha maisha yao .

Iwapo hukujua kwamba simu hiyo ya mkononi unayotumia kila siku inaweza kuyavuruga maisha yako -hizi hapa njia nne ambazo unaweza kujipata pabaya endapo hutakuwa muangalifu au makini kuhusu matumizi yako ya simu .

Simu inaweza 'kubadilisha tabia yako kijamii'

Kuna ushahidi wa wazi ambao wanasaikolojia wanasema matumizi ya simu yanaweza kuleta kwa tabia ya mtu hasa kijamii .

Sio jambo la ajabu kujua kwamba kwa sasa kuna watu hasa vijana ambao matumizi ya simu yameathiri sana uwezo wao hata kuweza kutangamana kwa njia ya kawaida.

gl

Chanzo cha picha, Getty Images

Wamezoea kutumia simu na wakati wasipokuwa na simu zao mkononi maisha kwao yanakuwa sio ya kawaida na hata wanaweza kujihisi wagonjwa.Mara ngapi unazungumza na mtu lakini hata hakuangalii ?

Macho yake na umakini wake wote huelekezwa kwa simu yake .

Hilo hutokana na mazoea ambayo Iwapo hayaangaliwi yanaweza kuwa uraibu unaovuruga kabisa jinsi mtu anavyotangamana na wengine kijamii .Je,umewahi kuiweka kando simu yako kwa muda wa saa 24?

Ulihisi ni kama kuna kitu unachokosa maishani mwako? Basi kuna watu wasioweza kuendelea na shughuli zao kamwe bila kuwa na simu zao mikononi .

Visa pia ni vingi vya watoto majumbani kuachwa hoi wakati wazazi wanapojishughulisha na simu zao za mikononi na kukosa kuwapa hata muda wa kuwasikiza au kucheza nao.

Kutumia simu ukiendesha gari au ukifanya kazi inayohitaji umakinifu

Umeskia kuhusu ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva ambao wanaendesha gari wakitumia simu za mkononi .

Takwimu ni nyingi kuhusu idadi ya maafa yanayosababishwa na ajali kama hizo .

Kumekuwa na kampeni kote duniani na hasa kutoka kwa polisi kuhusu hatari ya kuendesha gari ukitumia simu .

gl

Chanzo cha picha, Gety

Visa pia vipo kuhusu watu ambao wanafanya kazi zinazoweza kutajwa kama 'hatari' ambao wanajitia hatarini hata zaidi kwa kutumia simu .

Iwapo utajipata katika hali kama hizo,unashauriwa kuiweka kando simu yako mpaka ufike hatua unayoweza kuitumia.

Ujumbe huo ,simu hiyo au hata video hiyo unaweza kuishughulikia baada ya safari yako au ukiwa salama .

Basi ikiwa ulifikiri simu ya mkononi haiwezi kukutia hatarini kwa njia hii basi ujumbe huu utakupa fursa ya kutafakari matumizi ya simu yako

Umetumiwa pesa kwenye simu ukazitoa na sio zako?

Umeyaskia hayo kuhusu watu kuzitumia simu vibaya kwa kutoa fedha wanazotumiwa kimakosa .

Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakitumia simu kama kinga ya kufanya maovu na uhalifu .Sheria zinabadilika na kuboreshwa na usije ukadanganyika kwamba unaweza kutekeleza uhalifu kutumia simu yako ukifikiri uko salama.

gl

Chanzo cha picha, Getty Images

Nchini Kenya kwa mfano mwanamke mmoja yupo mashakani kwani huenda akafungwa jela kwa kutoa shilingi 271,200 alizotumiwa kimakosa katika akaunti yake ya mpesa kupitia simu .

Elizabeth Karimi inaripotiwa na vyombo vya Habari nchini humo alitumiwa fedha hizo kwa bahati mbaya na mtu aliyekosea nambari ya akaunti . Wakati kampuni husika zilipojaribu kuzirejesha fedha hizo ,Bi.Kirimi alikuwa ameshazitoa fedha hizo kutoka kwa akaunti yake .Baadaye kesi hiyo ilifikishwa polisi na akasakwa ,kukamatwa na kufikishwa kortini .

Hilo linafaa kukupa mwamko kwamba usiwahi kutumia simu yako ya mkononi kutekeleza uhalifu ukifikiria kwamba mkono wa sheria hautokupata .

Hakikisha unanunua simu yako kwa njia halali ama kwa muuzaji mwenye leseni

Iwapo ulifikiri unaweza kuinunua simu ya mkononi kwa yeyote kwa sababu umeipata kwa gharama ya chini ,basi itabidi umeliwazia tena suala hilo . Kuna hatari kubwa sana kununua simu kutoka kwa mtu yeyote.

Kunayo mifano ya watu waliofungwa jela kwa makosa makubwa hata ya mauaji kwa kuuziwa simu ambazo zilipatikana kupitia uhalifu .

Ge

Chanzo cha picha, Getty Images

Amekuuzia mtu simu kwa gharama ya chini kumbe ni simu ya wizi ambayo hata ilisababisha mwenyewe kuuawa .

Wakati polisi inapofanya uchunguzi na kuifuata simu hiyo ,unapatikana nayo wewe bila kujua ilikotoka na visa ni vingi vya watu wanaopambana na kesi mahakamani kuhusu kununua vifaa vya elektroniki kwa njia kama hiyo .Hakikisha simu unayonunua ni halali kutoka kwa muuzaji unayeweza kuthibitisha kwamba alikuuzia simu hiyo .