Injili Klabuni: Mtindo mpya wa kuwavuta vijana katika injili

.

Chanzo cha picha, MOJISHOTI INSTAGRAM

    • Author, Phillys Mwatee
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Mamia ya vijana walijitokeza jijini Nairobi kuhudhuria hafla ya Misa ya tatu {'Third Service',} hafla inayochanganya muziki wa injili, dansi, ibada na burudani katika mtindo mpya wa kuwafikia vijana kupitia imani na muziki wa kisasa.

Hafla hiyo inayofanyika baada ya muda na kuandaliwa na DJ maarufu nchini Kenya DJ Moz iliwakutanisha wasanii wa muziki wa injili, ma-DJ, vikundi vya dansi pamoja na makundi ya vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Nairobi kwa lengo moja kuu — kuwahamasisha vijana kupitia muziki wa injili na ushiriki chanya katika jamii.

Kutoka dakika ya kwanza hadi ya mwisho kulikuwa na burudani la hali ya juu huku vijana wengi wakionekana kupendezwa na mtindo huu wa kuabudu.

Sio tu vijana walioburudika na aina hii ya ibada bali hata watu wazima.

Tofauti na hafla za burudani la kawaida katika klabu , hafla hii hairuhusu unywaji wa vileo na vilevile mara kwa mara muziki husitishwa ili vijana kusikiliza mahubiri, maombi na hata ibada za Sakramenti.

Je, mtindo huu wa ibada ulianza vipi?

.

Chanzo cha picha, Kubamba TV/INSTAGRAM

.

Chanzo cha picha, MOJISHOTI INSTAGRAM

.

Chanzo cha picha, MOJISHOTI INSTAGRAM

Kulingana na mwandalizi wa hafla hiyo DJ Moz waliamua kuanzisha ibada hii kwa jina Misa ya tatu {Third Service} wakilenga burudani ili kuwavutia vijana wengi wapenda muziki.

DJ Mos anasema , alianzisha mtindo huu wa ibada baada ya yeye mwenyewe kubadilika na kuanza kumcha mungu akiwa klabuni.

''Mungu alinionyesha wazi kwamba vile nimeokoka nirudi kwa klabu nionyeshe mapenzi yaleyale na vijana ambao hawatakwenda kanisani '', alisema DJ Moz.

Anasema kwamba Ibada ya Misa ya tatu ilianzishwa baada ya Misa ya kwanza na ya pili ambazo hufanyika kanisani siku ya Jumapili.

Anasema lengo la hatua hiyo ilikuwa kuwavutia Vijana ambao hawajakwenda kanisa kupitia mandhari ya burudani wanayopenda sana

.

Chanzo cha picha, INSTAGRAM/Kubamba TV

Maelezo ya picha, Dj Moz katika ibada
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Waliohudhuria wanasema hafla hiyo imekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha waumini wenzao, kuonyesha vipaji vyao na kupata burudani yenye maadili mbali na ushawishi hasi unaowakabili vijana wengi katika jamii ya sasa.

Kwa maonyesho ya muziki wa moja kwa moja, dansi za kusisimua na vipindi vya maingiliano, Misa ya tatu{ Third Service }imeonyesha namna burudani ya injili inavyoendelea kuwa njia muhimu ya kuwafikia vijana.

Hata hivyo, nyuma ya mandhari ya kuvutia, taa za jukwaani na uwepo mkubwa wa vijana, kulikuwa na miezi kadhaa ya maandalizi na uratibu wa kina.

Kuandaa tukio linalowakutanisha mamia ya vijana kutoka sehemu tofauti za jiji la Nairobi sio kazi rahisi. Changamoto za usafiri, usalama na uratibu wa shughuli mbalimbali zilihitaji mipango makini kutoka kwa waandalizi.

Sasa waandalizi wanasema matumaini yao ni kupanua hafla hiyo katika siku zijazo ili kuwafikia vijana wengi zaidi Afrika Mashariki.

Na licha ya changamoto zilizojitokeza, waandalizi wanasisitiza kuwa lengo kuu lilikuwa kuunda mazingira salama, yenye msukumo na matumaini, ambapo vijana wanaweza kuunganishwa kupitia imani, muziki na vipaji vyao.