Nini kitakachofuata baada ya Mali, Niger na Burkina Faso kujiondoa Ecowas?

A woman wearing headscarf and pink earrings waves the flag of Burkina Faso

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wakazi nchini Burkina Faso waliingia barabarani kusherehekea kujiondoa kwa nchi hiyo kutoka kwa Ecowas
    • Author, Chris Ewokor
    • Nafasi, BBC News, Abuja
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Nchi tatu zilizo chini ya utawala wa kijeshi zimeondoka rasmi katika kanda ya Afrika Magharibi Ecowas, baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa mvutano wa kidiplomasia.

Kujiondoa kwa Mali, Burkina Faso na Niger ni pigo kubwa kwa Ecowas, ambayo ina umri wa miaka 50 ikichukuliwa kuwa kundi muhimu zaidi la kikanda barani Afrika.

Mgawanyiko huo ulizuka baada ya nchi hizo tatu zinazoondoka kukataa madai ya Ecowas kurejesha utawala wa kidiplomasia.

Siku ya Jumatano Ecowas ilisema itaweka "milango wazi" kwa Mali, Burkina Faso na Niger, ingawa wameendeleza kambi yao wenyewe, Muungano wa Nchi za Sahel (AES kwa kifupi katika lugha ya Kifaransa).

Ecowas ni nini?

Ecowas - ambayo inawakilisha Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi - ilianzishwa mwaka 1975 katika jitihada za kuboresha ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa katika eneo la Afrika Magharibi.

Kabla ya maamuzi ya Jumatano, kambi hiyo ilikuwa na wanachama 15, yakiwemo mataifa kama Nigeria, Ghana, Ivory Coast na Senegal.

Raia wa nchi zote za Ecowas kwa sasa wana haki ya kuishi na kufanya kazi katika nchi zote wanachama, kadhalika bidhaa kuweza kuzunguka kwa uhuru.

Kwanini Mali, Niger na Burkina Faso zimejiondoa?

Uhusiano kati ya Ecowas na nchi tatu za Sahel umekuwa wa wasiwasi tangu jeshi lilipochukua mamlaka nchini Niger mwaka 2023, Burkina Faso mwaka 2022 na Mali mwaka 2020.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya mapinduzi ya Niger, Ecowas iliweka vikwazo vinavyodhoofisha nchi hiyo, kama vile kufungwa kwa mipaka, kufungwa kwa safari za ndege zote za kibiashara na kufungiwa kwa mali za benki kuu.

Ecowas pia ilitishia kupeleka vikosi vyake nchini Niger ili kurejesha utawala wa kidemokrasia.

Lakini uamuzi huu mgumu uliimarisha tu azimio la mataifa hayo matatu yanayotawaliwa kijeshi.

Mali na Burkina Faso zilikosoa vikwazo vya "kikatili" vya Ecowas na kuapa kuilinda Niger ikiwa umoja huo utaingilia kijeshi.

Baada ya kusimamishwa na Ecowas, mataifa hayo matatu yalijibu kwa kutoa notisi Januari iliyopita kwamba wangejiondoa katika kipindi cha mwaka mmoja, wakitimiza ratiba iliyowekwa na jumuiya hiyo kwa mataifa ambayo yanaamua kujiondoa.

Mazungumzo kati ya Ecowas na mataifa hayo yanayotawaliwa kijeshi yamefanyika tangu wakati huo - lakini yameshindwa kubadili msimamo huo.

Nchi hizo tatu zinaishutumu Ecowas kwa kuwa karibu sana na madola ya Magharibi na badala yake zimeegemea upande wa Urusi.

Je, kujiondoa huko kutaathiri vipi nchi hizo tatu?

Kwa mujibu wa nchi zinazojiondoa, sasa zitapata uhuru mkubwa zaidi na pia uhuru kutoka kwa jeshi ambalo lina ajenda ya kigeni.

Lakini wachambuzi wanasema Niger, Mali na Burkina Faso huenda zikatatizika nje ya jumuiya hiyo - hizi ni nchi maskini na zisizo na bahari ambazo uchumi wake unategemea majirani zao wa Afrika Magharibi.

Wakati Ecowas inafanyia kazi masharti ya uhusiano wake wa siku za usoni na nchi hizo tatu, inasema itaendelea kutambua hati za kusafiria na vitambulisho vyote vyenye nembo ya Ecowas inayotumiwa na raia kutoka Mali, Niger na Burkina Faso.

Nchi hizo pia zitasalia katika mpango wa biashara huria wa umoja huo.

Vile vile, mwenyekiti wa AES, mtawala wa kijeshi wa Mali Assimi Goïta, alisema Januari mwaka jana kwamba haki ya raia wa Ecowas "kuingia, kuzunguka, kuishi, kuanzisha na kuondoka katika eneo" la jumuiya hiyo mpya itadumishwa.

Ilyasu Gadu, mtaalamu wa masuala ya kimataifa na mshauri wa vyombo vya habari anayeishi katika mji mkuu wa Nigeria Abuja, aliiambia BBC: "Viongozi hao watatu wamechukua hatua kusema: 'Ndiyo, tunajiondoa Ecowas lakini tunataka kudumisha uhusiano wetu…tusifunge mipaka yetu' kwa sababu lazima wangetambua kwamba kama wangefanya hivyo, ingekuwa sawa na kujidhoofisha."

Waangalizi wa Afrika Magharibi pia wana wasiwasi kujiondoa huko kutaathiri usalama katika eneo hilo. Sahel - eneo lenye ukame kusini mwa Jangwa la Sahara ambalo linajumuisha nchi tatu zinazojiondoa - linakabiliwa na uasi wa jihadi na sasa linachangia "karibu nusu ya vifo vyote vinavyotokana na ugaidi duniani", afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema mwezi Aprili.

Ecowas ilikuwa ikiziunga mkono Mali, Burkina Faso na Niger katika vita vyao dhidi ya wanajihadi, lakini msaada huu sasa unaweza kufutwa, waangalizi wanahofia.

Ingawa utawala wa kijeshi sasa unapokea silaha na mamluki kutoka Urusi, wanamgambo hao wanaendelea kuwasababishia hasara kubwa raia na vikosi vya jeshi.

Je, uamuzi huu utaathiri vipi Ecowas?

Ecowas itapoteza watu milioni 76 kati ya watu wake milioni 446 na zaidi ya nusu ya eneo lake lote la ardhi.

Pia kuna wasiwasi kwamba kujiondoa kutadhoofisha umoja wa kikanda na ushirikiano katika kupambana na uasi.

Mgawanyiko huo "unazidisha mgogoro wa uhalali wa ECOWAS ambao mara nyingi umeshindwa kukidhi matarajio ya watu katika kuzingatia utawala wa sheria," Ulf Laessing, mkuu wa mpango wa Sahel katika Wakfu wa Konrad Adenauer, aliiambia Associated Press.

"Kwamba nchi tatu masikini zaidi wanachama ziliamua kuondoka kwenye kambi hiyo inaifanya Ecowas machoni pa raia wake kuonekana kama mtu aliyeshindwa katika mzozo huu."

Unaweza pia kusoma

Je, wakazi wa Mali, Niger na Burkina Faso wanajisikiaje?

Siku ya Jumanne, baadhi ya watu katika miji mikuu ya nchi tatu zinazojiondoakatika jumuiya hiyo waliingia barabarani kusherehekea kujiondoa.

Lakini sio kila mtu anaunga mkono maamuzi ya kijeshi.

Omar Hama kutoka Niger alisema anatamani nchi hizo tatu zingebaki Ecowas, wakati huo huo zikiwa za AES.

"Ningependa waondoe tofauti zao kwa sababu tuna nafasi ya pamoja, watu wale wale wenye mambo yanayofanana kihistoria na hali halisi ya kiuchumi," alisema.

Fatouma Harber, mwandishi wa habari na mwanablogu anayeishi Mali, ana wasiwasi kwamba mabadiliko hayo yanaweza hatimaye kusababisha matatizo ya kiutawala na kiuchumi kwake na kwa raia wengine wa nchi hizo tatu.

"Hata hivyo, ikiwa Muungano wa Nchi za Sahel (AES) unaweza kweli kuleta manufaa kwetu, hilo litakuwa jambo zuri," alisema.

Zabeirou Issa, ambaye anaishi katika mji mkuu wa Mali Bamako, ana msimamo thabiti zaidi, akisema: "Ecowas haina mamlaka yoyote, ni watu wa Magharibi wanaoamua viongozi wa Ecowas.

Ndiyo, nina furaha sana kuhusu uamuzi huo."

Huko Ouagadougou, mji mkuu wa Burkina Faso, Cisse Kabore alisema anataka nchi yake kusalia Ecowas kwa sababu sasa eneo hilo "halitakuwa na umoja tena kama hapo awali".

Nini kitatokea baadaye?

Mwezi uliopita, Ecowas ilisema itazipa Niger, Burkina Faso na Mali kipindi cha miezi sita cha msamaha kwa wao kufikiria upya kujiondoa kwao.

Hata hivyo, katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatano, mkuu wa Tume ya Ecowas Omar Alieu Touray alisema: "nchi yoyote inaweza kuamua kurejea katika jumuiya wakati wowote."

Ili kuunganisha kuondoka kwao kutoka Ecowas na kuimarisha muungano wao, nchi hizo tatu zilisema zitaanza kusambaza pasipoti mpya za AES siku ya Jumatano.

Pia wameamua kuunganisha nguvu kuunda kikosi cha wanajeshi 5,000 ili kupambana na ghasia za kijihadi ambazo zimekumba mataifa hayo kwa miaka mingi.