Kwa nini Ufaransa ina kambi za kijeshi barani Afrika?

Chanzo cha picha, Getty Images
Huku kukiwa na wimbi la mapinduzi katika makoloni ya zamani ya Ufaransa barani Afrika, Ufaransa inabaini kwamba haiwezi tena kuchukua jukumu lake la kijeshi katika bara hilo kuwa la kawaida.
Kumekuwa na maandamano ya kupinga uwepo wa Ufaransa barani Afrika, ambapo hapo awali ilibadilisha nguvu zake za kijeshi.
Wanajeshi wa Ufaransa hivi karibuni wamefukuzwa kutoka Niger na Mali na wengine wanafikiria kufuta mikataba ya enzi ya uhuru ambayo ilisababisha kuingilia kijeshi moja kwa moja kwa Ufaransa kati ya 1964 na 1995 .
Kwa nini wanajeshi wa Ufaransa wako barani Afrika?
Tangu uhuru, Ufaransa ilitaka "kudumisha na kulinda uthabiti na uimara wa tawala fulani", anasema Dk Bakary Sambe, mkurugenzi wa Taasisi ya Timbuktu.
Serikali ya zamani ya kikoloni iliichukulia Afrika Magharibi na Sahel kama "nafasi ya kupelekwa na ushawishi wa asili," anasema.
Prof Bruno Charbonneau, kutoka Chuo cha Kijeshi cha Kifalme cha Canada cha Saint-Jean na mtaalamu wa usuluhishi wa amani na migogoro katika Afrika Magharibi, anakubali.
"Uwepo wa kijeshi wa Ufaransa barani Afrika pia daima umeruhusu Ufaransa kuwa kiini cha utatuzi wa migogoro na mifumo ya usimamizi katika Afrika inayozungumza Kifaransa, hasa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," anasema.
Kutoa msaada wa kijeshi kwa tawala za kirafiki za Kiafrika kwa namna hii kumemaanisha Ufaransa inaweza kuendeleza na kulinda maslahi yake, na kuanzisha uingiliaji kati wa haraka wa kutumia silaha, anaongeza.
Wizara ya ulinzi ya Ufaransa inasema dhamira yake kuu kupitia operesheni nchini Gabon ni kutoa mafunzo kwa wanajeshi katika eneo hilo na kuongeza uwezo wao wa kupambana na ugaidi, kulinda mipaka ya ardhini na maeneo ya baharini. Hii inahusisha ulinzi wa amani, ujasusi na usafirishaji.
Inasema majukumu haya yanaambatana na programu ya kuimarisha Uwezo wa Kulinda Amani Afrika (Recamp), mpango wa mafunzo ulioanzishwa mwishoni mwa miaka ya 1990 ukihusisha Ufaransa, Uingereza na Marekani.
Nchini Senegal, inafanya kazi ya kusimamia mafunzo kwa wanachama wote 15 wa kanda ya Afrika Magharibi, Ecowas, pamoja na nchi jirani ya Mauritania.
Ni mataifa gani ambayo bado yana ngome za Ufaransa?
Ingawa idadi yao imepunguzwa katika miaka ya hivi karibuni, maelfu kadhaa ya wanajeshi wa Ufaransa bado wametumwa katika nchi zifuatazo:
- Chad: Karibu wanajeshi 1,000, wanaojulikana kama vikosi vya Ufaransa nchini Chad (EFT), wana jukumu la kuhakikisha ulinzi wa maslahi ya Ufaransa na raia.
Pamoja na kutoa msaada wa vifaa na kijasusi kwa jeshi la Chad, pia walikuwa sehemu ya mipango ya kikanda na ya kukabiliana na ugaidi. Wana kambi katika mji mkuu, N'Djamena, Abéché mashariki na kikosi huko Faya kaskazini.
- Djibouti: Kuna kikosi kikubwa zaidi. Kwa sasa wanajeshi 1,500 wapo chini ya mikataba ya mwaka 1977, nchi ilipopata uhuru, na mwaka 2014.
- Gabon: Vikosi vya Ufaransa vimekuwa huko tangu uhuru wake mnamo 1960, na kubadilishwa jina rasmi na kuwa EFG mnamo 2014 kikawa na wanajeshi 350.
Kulingana na wizara ya ulinzi ya Ufaransa, EFG inajumuisha kitengo cha ardhi kilicho katika kambi ya Charles De Gaulle katika mji mkuu, Libreville, na kitengo cha anga katika kituo cha anga cha karibu cha Guy Pidoux.
- Ivory Coast: nyumbani kwa udhibiti wa uendeshaji wa Ufaransa. Kituo cha Uendeshaji (Fob) kilianzishwa hapo mwaka wa 2015 chini ya ushirikiano wa ulinzi kati ya mataifa yaliyo karibu kihistoria.
Kwa miaka 13 iliyopita, wanajeshi wasiopungua 950 waliwekwa kama sehemu ya Operesheni Licorne, kikosi cha kulinda amani cha Ufaransa kilichoanzishwa baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2002.
- Senegal: Kikosi cha karibu wanajeshi 400, kinachojulikana tangu 2011 kama EFS, kinatoa mafunzo ya kijeshi ya kikanda.
Wakiwa katika kambi mbili katika mji mkuu, Dakar, EFS inaweza pia kutumia uwanja wa ndege wa kijeshi wa jiji hilo. Kikosi hicho pia kina kituo cha redio cha masafa ya juu karibu na Dakar huko Rufisque.
Mwezi uliopita, wanajeshi 1,300-1,500 waliokwenda Niger, pamoja na ndege za kivita na ndege zisizo na rubani zilizohusika katika operesheni za kukabiliana na ugaidi, walianza kujiondoa kwenye kambi tatu kwa ombi la viongozi wa mapinduzi ya Julai.
Kwa nini Ufaransa ina 'ngome yake' Afrika?
Afrika inaipa Ufaransa nguvu kwenye ngazi dunia la sivyo isingekuwa na "mamlaka", anasema Prof Tony Chafer, wa Chuo Kikuu cha Portsmouth nchini Uingereza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Katika mazingira yanayozidi kuwa mengi na yenye ushindani wa kimataifa, Ufaransa ina nia ya msingi ya kijiografia katika kudumisha uwepo wake wa kijeshi katika kanda," anasema.
Kuwa barani Afrika kijeshi "kuna jukumu muhimu katika kuhalalisha kiti cha kudumu cha Ufaransa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa-Ufaransa ni 'mhusika muhimu' wakati masuala ya usalama katika Afrika Magharibi na Kati yanajadiliwa katika Umoja wa Mataifa au jumuiya ya kimataifa", anaongeza.
Ufaransa imelinda kwa uangalifu uhusiano wake wa kiuchumi na kidiplomasia na Afrika pia. Hizi zinaendelea hasa katika sarafu za faranga za CFA, ambazo zimeunganishwa kwenye hazina ya Ufaransa, na kupitia kukuza uhusiano wa karibu na wanaotawala.
Prof Chafer anasema ikiwa Ufaransa bado inalichukulia bara la Afrika kuwa "sehemu" yake ni zao la historia ya ukoloni wake na jinsi ilivyojadiliana kuhusu kuondoka kwake: "'Kujifanya kuondoka ili kuingia ndani zaidi', kama wengine walivyosema."
Kwa nini waandamanaji wanataka wanajeshi wa Ufaransa waondoke?
"French armies. Go away," aliimba nyota wa reggae wa Ivory Coast Alpha Blondy mwishoni mwa miaka ya 1990. Wimbo huo uliashiria mwanzo wa enzi mpya.
Hata hivyo kutokana na kuongezeka kwa wanamgambo wa Kiislamu katika Afrika Magharibi, Ufaransa ilikubali ombi la kutuma wanajeshi zaidi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Operesheni ya kwanza ilikuwa Operesheni Serval, operesheni nchini Mali iliyoanzishwa baada ya wanajihadi kuteka kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 2012.
Nafasi yake ilichukuliwa na Operesheni Barkhane, ujumbe wa kikanda zaidi wa kukabiliana na uasi uliomalizika Novemba mwaka 2022.
Dk Sambe anahoji kuwa wote wawili walishindwa huku makundi ya kigaidi katika eneo hilo yakiongezeka wakati huu.
"Nchi zilianza kutilia shaka umuhimu wa uwepo wa kimkakati wa Ufaransa, mawazo na nadharia za njama zilizokuzwa zikisema kwa namna fulani zilivutia au kuzidisha tishio la ugaidi," anasema.
Hii pamoja na wito wa "uhuru" kutoka kwa kizazi kipya inamaanisha watu wengi wanataka kuona wanajeshi wa Ufaransa wakiondoka.
Mapinduzi ya kijeshi ya hivi karibuni nchini Mali, Burkina Faso na Niger , ambapo viongozi wa junta waliamua kuwatimua wanajeshi wa Ufaransa na kupata sifa kwa umma katika mchakato huo, ni ushahidi wa hili.
Je, athari ni zipi?
Wanajeshi wa Ufaransa waliondoka Mali mwaka jana kwa amri ya Bamako, na walinda amani wa Umoja wa Mataifa hivi karibuni wameambiwa kufanya vivyo hivyo.
Wanapoondoka, ndivyo pia kizuizi muhimu, hata kama hali ya usalama imekuwa mbaya zaidi katika muongo uliopita, anasema Prof Chafer.
Tangu kujiondoa, ukiukaji wa haki za binadamu umezidi kuwa mbaya na watu wa Mali sasa wako salama kidogo, anasema.
Jeshi la Mali kwa wakati huo limegeukia kundi la mamluki la Urusi, Wagner, kama mshirika mpya. Pande zote mbili zimeshutumiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu. Prof Chafer anaamini kuwa jukumu kuu la Wagner nchini "si kuboresha usalama wa watu bali kuunga mkono utawala wa kijeshi wa Mali".
Pia inaonekana kuvuruga makubaliano ya amani na muungano wa waasi wa kabila la Tuareg, ambao pia umeanza kuteka eneo la kaskazini huku majeshi ya kigeni yakiondoka.
Je, kuna njia mbadala za usalama?
Wanamgambo wa kujilinda na vikundi vya kijeshi, kama Wagner, sio jibu, anasema Dk Sambe, pia akionesha Mali kama mfano.
Anataka kuona mkusanyiko wa vikosi kutoka Ecowas, Umoja wa Afrika na vikosi vingine vya bara.
"Ni wakati wa kuelekea kwenye Uafrika wa vikosi hivi," anasema.















