Trump aonya Marekani itaingilia kati ikiwa Iran itawaua waandamanaji

Katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii, Trump aliandika: "Tuko tayari kwenda huko."

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha taarifa zetu za moja kwa moja kwa leo. Kwaheri.

  2. Zelensky amteua mkuu wa ujasusi kuongoza ofisi ya rais

    .

    Chanzo cha picha, Telegram/Zelenskiy / Official

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amemteua mkuu wa ujasusi Kyrylo Budanov kuwa mkuu wake mpya wa wafanyakazi, zaidi ya mwezi mmoja baada ya msaidizi wake mkuu wa zamani kujiuzulu kutokana na mzozo wa ufisadi.

    "Kwa wakati huu, Ukraine inahitaji umakini zaidi katika masuala ya usalama," Zelensky alisema katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii, akichapisha picha ya mkutano wake na Budanov huko Kyiv.

    Budanov, mwenye umri wa miaka 39, hadi sasa ameongoza ujasusi wa kijeshi wa Hur, ambao umedai kutekeleza mashambulizi kadhaa yenye ufanisi mkubwa dhidi ya Urusi.

    Mtangulizi wake, Andriy Yermak, alikuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa wakati wote wa uvamizi wa Urusi ulioanzishwa mwaka wa 2022.

    Pia aliongoza timu ya mazungumzo ya Ukraine katika mazungumzo muhimu na Marekani yaliyolenga kukomesha vita.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Mahakama Korea Kusini yaongeza muda wa kuzuiwa kwa rais wa zamani Yoon

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mahakama nchini Korea Kusini imetoa hati mpya ya kumzuilia Rais wa zamani Yoon Suk Yeol kwa miezi mingine sita, Yonhap News TV iliripoti Ijumaa.

    Yoon ameshtakiwa kwa mashtaka zaidi ikiwa ni pamoja na kusaidia taifa la adui kuhusiana na uwekaji wake wa sheria za kijeshi kwa muda mfupi mwaka wa 2024.

    Jaji alitaja wasiwasi wake juu ya kuharibu ushahidi, Yonhap alisema.

    Kizuizi cha Yoon kilipangwa kuisha Januari 18.

    Soma zaidi:

  4. Urusi yaishutumu Ukraine katika shambulio la Mwaka Mpya kwenye eneo ililonyakua

    .

    Chanzo cha picha, Press service of Russian-installed Kherson governor

    Urusi imeishutumu Ukraine kwa kuwaua watu wasiopungua 27 katika shambulio la ndege zisizo na rubani kwenye sherehe ya Mwaka Mpya katika hoteli na mgahawa katika eneo la kusini mwa Kherson linalokaliwa na Urusi.

    Kulingana na gavana wa kikanda aliyeteuliwa na Urusi, Vladimir Saldo, zaidi ya watu 30 walijeruhiwa katika shambulio hilo linalodaiwa, ambalo alisema lilitokea katika kijiji cha Khorly kwenye Bahari Nyeusi.

    Ikitakiwa BBC kutoa maoni, Ukraine ilisema haitajibu moja kwa moja vyanzo vya habari kama vile madai kutoka kwa magavana wa maeneo yaliyokaliwa.

    Lakini ilisema inafuata kanuni za sheria za kimataifa za kibinadamu na inafanya mashambulizi dhidi ya maeneo lengwa kijeshi pekee.

    Soma zaidi:

  5. Trump aonya Marekani itaingilia kati ikiwa Iran itawaua waandamanaji

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump ameonya mamlaka ya Iran dhidi ya kuwaua wanaoandamana kwa njia ya amani, akisema taifa lake "litawaokoa".

    Katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii, aliandika: "Tuko tayari kwenda huko." Hakutoa maelezo zaidi.

    Afisa mwandamizi wa Iran Ali Larijani alijibu maoni ya Trump akionya kwamba kuingilia kati kwa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran itakuwa sawa na kuyumbisha uthabiti wa eneo lote la Mashariki ya Kati.

    Takriban watu sita wameripotiwa kuuawa nchini Iran siku ya Alhamisi baada ya karibu wiki moja ya maandamano makubwa yaliyosababishwa na hali mbaya ya kiuchumi.

    Marekani ilishambulia vituo vya nyuklia vya Iran mwezi Juni, ikijiunga na kampeni ya anga ya Israeli iliyolenga mpango wa nyuklia wa Tehran na uongozi wa kijeshi.

    Iran inaunga mkono makundi nchini Lebanon, Iraq na Yemen.

    Soma zaidi:

  6. Serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi yaanzisha operesheni dhidi ya waasi wanaoungwa mkono na UAE

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi Arabia imeanzisha kile ilichokiita operesheni ya amani ya kuchukua nafasi za kijeshi kutoka kwa waasi wa kusini wanaoungwa mkono na UAE siku ya Ijumaa, ambao nao walisema mashambulizi saba ya anga ya Saudi Arabia yamefanyika tangu tangazo hilo.

    Gavana wa jimbo la Hadramout nchini Yemen anayeungwa mkono na Saudi Arabia alitangaza hatua hiyo ili kuchukua nafasi za kijeshi kutoka kwa Baraza la Mpito la Kusini linaloungwa mkono na UAE, lakini akaongeza kuwa vitendo hivyo sio tangazo la vita.

    Hili linajiri katika hatua ya hivi karibuni huko Yemen ambapo ambapo mzozo umekuwa ukiongezeka kati ya Saudi Arabia na Falme za Kiarabu.

    Serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi Arabia ilisema Ijumaa kuwa imemteua Gavana wa Hadramout Salem Ahmed Saeed al-Khunbashi kuchukua uongozi wa jumla wa vikosi vya "Homeland Shield" katika jimbo la mashariki, na kumpa mamlaka kamili ya kijeshi, usalama na utawala katika kile ilichosema ni hatua ya kurejesha usalama na utulivu.

    Operesheni hiyo inalenga maeneo ya kijeshi pekee na "sio tangazo la vita," ilisema.

    UAE inaunga mkono STC, ambayo iliteka maeneo makubwa ya kusini mwa Yemen mwezi uliopita kutoka kwa serikali inayotambuliwa kimataifa, inayoungwa mkono na Saudi Arabia, ambayo nayo iliona hatua hiyo kama tishio.

    Wiki iliyopita UAE ilisema inaondoa vikosi vyake vilivyobaki kutoka Yemen baada ya Saudi Arabia kuunga mkono wito wa vikosi vyake kuondoka ndani ya saa 24 katika mojawapo ya migogoro mikali zaidi kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu za mafuta ya Ghuba kujitokeza hadharani.

    Soma zaidi:

  7. Ghasia zaongezeka kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama Iran

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Machafuko yanayoongezeka nchini Iran yanaripotiwa kusababisha vifo vya watu wengi zaidi katika siku ya tano ya maandamano dhidi ya kupanda kwa gharama ya maisha.

    Shirika la habari la Fars ambalo si rasmi na pia kundi la haki za binadamu, Hengaw, lilisema watu wawili walifariki wakati wa mapigano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama katika jiji la Lordegan, kusini-magharibi mwa Iran. Watu wengine watatu waliuawa huko Azna na mwingine huko Kouhdasht, Fars iliripoti, wote wakiwa magharibi mwa nchi.

    Siku ya Alhamisi video zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha magari yakiwa yamechomwa moto wakati wa mapigano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.

    Waandamanaji wengi wametaka utawala wa kiongozi mkuu wa nchi hiyo ukomeshwe. Baadhi pia wametaka kurejeshwa kwa utawala wa kifalme.

    Maandamano hayo yalianza mjini Tehran - miongoni mwa wafanyabiashara waliokasirishwa na kushuka kwa thamani ya sarafu ya Iran dhidi ya dola ya Marekani katika soko huria.

    Kufikia Jumanne, wanafunzi wa vyuo vikuu walikuwa wamejiunga na maandamano hayo na yalikuwa yameenea katika miji kadhaa, huku watu wakiimba dhidi ya watawala wa kidini wa nchi hiyo.

    Maandamano hayo yamekuwa mengi zaidi tangu ghasia za mwaka 2022 zilizosababishwa na kifo cha Mahsa Amini, mwanamke kijana ambaye alishtakiwa na polisi wa maadili kwa kutovaa hijab yake ipasavyo.

    Ili kuzuia ongezeko lolote la maandamano, usalama mkali sasa unaripotiwa katika maeneo ya Tehran ambapo maandamano yalianza.

    Rais Masoud Pezeshkian amesema serikali yake itasikiliza "madai halali" ya waandamanaji.

    Lakini mwendesha mashtaka mkuu, Mohammad Movahedi-Azad, pia ameonya kwamba jaribio lolote la kusababisha ukosefu wa utulivu litakabiliwa "vilivyo".

    Pia unaweza kusoma:

  8. Jengo linaloendelea kujengwa laporomoka jiji Nairobi

    .

    Chanzo cha picha, Kenya Red Cross

    Watu wawili wanahofiwa kukwama baada ya jengo la orofa 16 lililokuwa likijengwa kuporomoka katika eneo la South C jijini Nairobi.

    Operesheni ya uokoaji inayohusisha vitengo tofauti ikiwa ni pamoja na wanajeshi, polisi, huduma za dharura za kaunti ya Nairobi na Kenya Power inaendelea katika eneo la tukio.

    Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, tukio hilo lilitokea mapema asubuhi, na kuwaacha wafanyikazi wawili wamekwama katika eneo hilo.

    "Eneo hilo limezingirwa huku Kitengo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Majanga, Kaunti ya Jiji la Nairobi, Huduma ya Kitaifa ya Polisi na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya wakiendelea na shughuli za utafutaji na uokoaji," ilisoma ujumbe wa Kenya Red Cross kwenye mtandao wa X.

  9. Trump asema yuko 'imara' licha ya afya na umri wake kuhojiwa

    Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amedokeaza kwamba anatumia aspirini zaidi kuliko madaktari wanapendekeza, anatumia vipodozi kuziba michubuko kwenye mikono yake, na hafanyi mazoezi ya mara kwa mara kwa sababu anahisi "yanachosha".

    Trump alisema hayo katika mahojiano marefu na Jarida la The Wall Street.

    Aliongeza kuwa alifanyiwa uchunguzi wa CT mnamo Oktoba, baada ya kuwaambia waandishi wa habari kimakosa kwamba alikuwa amefanyiwa uchunguzi wa kina zaidi wa MRI.

    Trump, 79, ndiye rais mwenye umri mkubwa zaidi kuapishwa katika historia ya Marekani, na dalili za umri wake mkubwa zimekuwa zikionekana.

    Kuna wakati aleonekana akisinzia katika mikutano na kutoweza kusikia maswali anayoulizwa.

    Jarida hilo lilisema Trump "alionyesha kukerwa juu ya mjadala wa umma juu ya afya yake", ambayo alielezea kuwa "mkamilifu".

    "Wacha tuzungumze juu ya afya tena kwa mara ya 25," alisema mwanzoni mwa "mahojiano yasio ya kawaida" wakati gazeti hilo likijiandaa kuchapisha habari kuhusu afya ya Trump.

    "Afya yangu ni imara," aliongeza. Trump alisema ametumia dozi kubwa kuliko alivyoshauriwa za aspirini kwa miaka 25 iliyopita, hata kama alisema ilimsababishia michubuko.

  10. Watu 40 wafariki katika moto wa baa Uswizi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takriban watu 40 wamefariki dunia baada ya moto kuzuka kwenye baa katika eneo la mapumziko kusini mwa Uswizi, polisi wamesema.

    Watu wengine 115 wamejeruhiwa, wengi wao "baya".

    Moto huo ulianza mwendo wa wakati wa sherehe za kuukaribisha mwaka mpya katika baa ya Le Constellation huko Crans-Montana.

    Maafisa wanaochunguza tukio hilo hawajathibitisha chanzo cha moto huo, lakini wamekanusha madai kwa huenda ni shambulio.

    Watu kutoka nchi kadhaa za kigeni wameathiriwa.

    Kamanda wa polisi wa kanda Frédéric Gisler amesema kipaumbele kwa sasa ni kutambua wale waliofariki "ili miili yao irejeshwe haraka" kwa familia zao.

  11. BYD ya China inakaribia kuishinda Tesla kama muuzaji mkuu wa magari ya umeme duniani

    ,

    Chanzo cha picha, ge

    BYD ya China inakaribia kuipiku Tesla ya Elon Musk kama muuzaji mkubwa zaidi wa magari ya umeme (EVs), ikiwa ni mara ya kwanza kumpita mpinzani wake wa Marekani kwa mauzo ya kila mwaka.

    Siku ya Alhamisi, BYD ilisema kwamba mauzo ya magari yake yanayotumia betri yalipanda mwaka jana kwa takriban 28% hadi zaidi ya milioni 2.25.

    Tesla, ambayo inatarajiwa kutangaza jumla ya mauzo yake ya 2025 baadaye leo Ijumaa, wiki iliyopita ilichapisha makadirio ya wachambuzi kuashiria kwamba ilikuwa imeuza takriban magari milioni 1.65 kwa mwaka mzima.

    Kampuni hiyo ya Marekani imekabiliwa na mwaka mgumu na mapokezi tofauti kwa matoleo mapya, wasiwasi juu ya shughuli za kisiasa za Elon Musk na kuongezeka kwa ushindani kutoka kwa wapinzani wa China.

    Mnamo Oktoba, Tesla ilianzisha toleo ya bei ya chini ya aina mbili ya magari yake yanayouzwa zaidi nchini Marekani kwa lengo la kuongeza mauzo.

    Ilikuwa imekabiliwa na ukosoaji kwa kile kilichoonekana kuzembea kutoa magari mapya ya bei nafuu zaidi ili kukabiliana na ushindani.

    Musk, ambaye tayari ndiye mtu tajiri zaidi duniani, ana jukumu la kuongeza mauzo ya Tesla na thamani ya soko la hisa katika muongo mmoja ujao ili kupata malipo ya kuvunja rekodi.

    Mkataba huo, ambao uliidhinishwa na wanahisa mnamo Novemba, unaweza kumfanya apate malipo ya takriban $1tn (£740bn).

    Kama sehemu ya makubaliano, Musk pia anatakiwa kuuza roboti milioni moja za humanoid katika miaka kumi ijayo. Tesla imewekeza sana katika bidhaa yake ya "Optimus" na "Robotaxis" ya kujiendesha.

  12. Watu saba wafariki baada ya boti kuzama Gambia

    Mamlaka nchini Gambia inasema takriban watu saba wamefariki baada ya boti kupinduka usiku wa manane siku ya Jumatano.

    Gambia inama baadhi ya waathiriwa ni raia wa kigeni. Nchi hiyo ya Afrika Magharibi inajitahidi kuthibitisha utambulisho wao.

    Tukio hilo limetokea katika Mkoa wa Benki ya Kaskazini. Maafisa wanasema botihiyo ilikuwa imebeba zaidi ya wahamiaji 200.

    Watu 96 wameokolewa na wanapokea matibabu katika vituo viwili vya matibabu. 10 kati yao wako katika hali mbaya na wanapokea huduma ya dharura.

    Mamlaka inasema operesheni ya utafutaji na uokoaji ilianzishwa, ikihusisha jeshi la wanamaji la nchi hiyo.

    Gambia ni mojawapo ya njia zinazotumiwa na wahamiaji wanaojaribu kufika Ulaya, mara nyingi wakiwa katika safari hatari za baharini na nchi kavu.

    Katika miaka ya hivi karibuni, Umoja wa Ulaya umefikia makubaliano na nchi kadhaa za Afrika Kaskazini kwa lengo la kupunguza uhamiaji usio wa kawaida.

  13. Maduro asema Venezuela iko tayari kwa mazungumzo na Marekani

    Meli kubwa ya kubeba ndege za kivita ya Marekani, ni miongoni mwa meli zilizotumwa kwenda Caribbia.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Meli kubwa ya kubeba ndege za kivita ya Marekani, ni miongoni mwa meli zilizotumwa kwenda Caribbia.

    Rais wa Venezuela Nicolas Maduro sasa anasema yuko tayari kwa mazungumzo na Marekani kuhusu ulanguzi wa dawa za kulevya na mafuta, baada ya wiki kadhaa za kampeni ya shinikizo dhidi ya serikali yake.

    Katika mahojiano na Televisheni ya serikali ya Venezuela siku ya Alhamisi, Maduro alisema yuko tayari kwa mazungumzo na Marekani "popote wanapotaka na wakati wowote wanapotaka".

    Pia alikwepa swali kuhusu Rais Donald Trump akisema Marekani ilishambulia kituo cha kizimbani nchini Venezuela, jambo ambalo liliripotiwa kutekelezwa na CIA. BBC imewasiliana na Ikulu ya White House kwa maoni.

    Haya yanajiri huku wanajeshi wa Marekani wakilenga meli wanazoshuku kusafirisha mihadarati kupitia Caribbean na mashariki mwa Pasifiki kwa muda wa miezi mitatu iliyopita.

    Kwa jumla, kumekuwa na zaidi ya mashambulizi 30 dhidi ya meli za Venezuela kama sehemu ya mpango wa "vita dhidi ya madawa ya kulevya" ya utawala wa Trump, na zaidi ya watu 110 wameuawa tangu Marekani kufanya mashambulizi yake ya kwanza kwenye meli katika maji ya kimataifa mnamo 2 Septemba.

    Shambulizi la hivi punde lilitokea Jumatano wakati boti mbili zinazodaiwa kubeba dawa za kulevya zilishambuliwa na watu watano waliokuwa ndani kuuawa, kwa mujibu wa jeshi la Marekani.

    Siku ya Jumatatu, Trump alisema Marekani imeshambulia "eneo la bandari" linalohusishwa na boti zinazodaiwa kuwa za dawa za Venezuela, na kusababisha "mlipuko mkubwa".

    Mlipuko huo ulisababishwa na shambulio la ndege zisizo na rubani zilizofanywa na CIA, kulingana na CNN na New York Times, ambayo ilitaja vyanzo vya karibu na suala hilo.

    Ikiwa hilo litathibitishwa, itakuwa operesheni ya kwanza ya Marekani ndani ya Venezuela.

    Soma pia:

  14. Natumai hujambo

    Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja leo Ijumaa 02.01.2026.