Kipi kinachochochea mivutano kati ya Saudi Arabia na UAE?

SDX

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

    • Author, Sumaya Nasr
    • Nafasi, BBC

Habari za hivi punde zinasema; juhudi zinazofanywa na Marekani kukabiliana na mashambulizi yaliyoanzishwa na Wahouthi nchini Yemen dhidi ya meli zinazopita katika Bahari Nyekundu - zinakabiliwa na kikwazo kikubwa kutokana na kutoelewana kati ya washirika wake wa Ghuba, Saudi Arabia na Imarati.

Bloomberg News imewanukuu maafisa wa Yemen na Saudia wakisema Abu Dhabi inaunga mkono hatua za kijeshi dhidi ya Wahouthi, huku Riyadh ikihofia operesheni hizo zinaweza kuhatarisha mapatano tete na Wahouthi nchini Yemen, na kudhoofisha juhudi za Saudia wa kufikia usitishaji wa kudumu wa vita.

Hii sio mara ya kwanza kuwepo tofauti kati ya washirika wawili wa Ghuba ya Kiarabu - licha ya kuwepo kwa ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kimkakati kati ya UAE na Saudi Arabia.

Saudi Arabia na UAE ni nchi mbili kubwa katika Baraza la Ushirikiano la Ghuba kwa ukubwa wa uchumi na idadi ya watu. Huenda ni jambo la kawaida kwa ushindani kuwepo kati yao, kwa kuzingatia uwepo wa kizazi kipya cha watawala katika nchi hizo mbili.

Pia Unaweza Kusoma

Mivutano juu ya mafuta

ASZX
Maelezo ya picha, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Israel zimetia saini Mkataba wa Abraham wa kurejesha uhusiano wakati wa Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Moja ya mzozo maarufu wa kiuchumi uliotokea miongo miwili iliyopita kati ya nchi hizo mbili. Ni pingamizi la Imarati dhidi ya pendekezo la Riyadh la kuwa na makao makuu ya Benki Kuu ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba. Pingamizi hilo lilipelekea kujiondoa katika makubaliano ya umoja wa fedha wa Ghuba. Jambo lililochangia kuvurugika kwa mradi wa kutoa sarafu ya pamoja ya Ghuba.

Julai 2021, Saudi Arabia ilitaka kuongeza muda wa kupunguzwa kwa uzalishaji wa mafuta kwa wanachama wa OPEC Plus, ambao ulipaswa kumalizika Aprili 2022. Lengo lilikuwa ni kufidia hasara iliyosababishwa na kushuka kwa bei ya mafuta wakati wa janga la Covid-19.

Ingawa maafikiano yaliafikiwa mwezi mmoja baadaye, mvutano ulibaki na uvumi ulienea kuhusu nia ya UAE kujiondoa kutoka OPEC Plus, lakini madai hayo yalikanushwa na maafisa wa Imarati.

Mwanadiplomaisa wa zamani wa Marekani, Dkt. Charles Dunn, anaamini, “licha ya pande zote kuufifisha mzozo huo, lakini ulifichua hasira ya UAE kwa kile ilichoona ni hamu ya Saudia kutawala maamuzi ya shirika.”

Ushindani wa Kiuchumi

AS

Chanzo cha picha, GETTY IAMGES

Maelezo ya picha, Yemen iko katika vurugu tangu 2014
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika miaka ya hivi karibuni, Saudia imechukua hatua za kubadilisha vyanzo vyake vya kiuchumi, kupunguza utegemezi wa mafuta, na kupanua nafasi yake ya kikanda na kimataifa katika sekta kama vile miundombinu, usafiri wa anga, utalii na michezo – ndani ya mpango wa dira ya maendeleo ya 2030.

Ilionekana ni jambo lisiloepukika kwamba hilo lingezua ushindani kati yake na Emirates. Kila mmoja kutaka kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika Ghuba na Mashariki ya Kati kwa ujumla.

Kwa mfano, Ufalme ulitangaza mapema mwaka huu uzinduzi wa shirika jipya la ndege, Riyadh Air, linalomilikiwa na Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi.

Shirika hilo litashindana na majirani zake wa Ghuba, hasa Shirika la Ndege la Emirates na Shirika la Ndege la Etihad. Ni shirika linalolenga kuendesha safari za ndege kwenda katika maeneo zaidi ya 100 ifikapo mwaka 2030.

Katika kile ambacho wataalamu waliona ni changamoto nyingine ya kiuchumi kwa jirani yake wa Ghuba, Riyadh iliamua 2021 kufuta ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka maeneo huru ya kiuchumi. Hilo ni pigo kwa uchumi wa UAE, ambayo inategemea sana bidhaa kutoka maeneo hayo.

Ufalme huo ulitangaza kufutwa huko hakujumuishi bidhaa zinazozalishwa na Israel, au zinazotengenezwa na kampuni za wawekezaji kutoka Israel au kampuni zilizojumuishwa katika makubaliano ya Waarabu ya kususia.

Inajulikana Imarati na Bahrain ndio wanachama pekee wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ambao wana mikataba ya ya kiuchumi na kibiashara na Israeli (iliyotokana na Makubaliano ya Abraham).

2021, Saudi Arabia pia iliamua kutoa changamoto kwa UAE kama mahali pa kuwekwa makao makuu ya kampuni za kigeni zinazofanya kazi katika Ghuba. Kampuni hizi zitaanzisha makao yao makuu katika Ufalme huo ifikapo 2024.

Hilo litaleta changamoto kwa UAE kwani kwa sasa falme za Abu Dhabi na Dubai ni wenyeji wa takribani asilimia 76 ya makao makuu ya kikanda ya makampuni makubwa yanayofanya kazi katika Ghuba.

Lakini Saudi Arabia na UAE daima zimeunganisha misimamo yao kuhusu kile wanachokiona kuwa tishio kutoka kwa jirani yao, Iran.

Umoja wa Falme za Kiarabu ulikuwa mshirika mkuu wa Ufalme huo katika muungano wa Waarabu uliouundwa 2015 ili kupambana na vuguvugu la Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran na kuunga mkono serikali ya Rais wa zamani Abd Rabbuh Mansour Hadi.

Lakini 2019, UAE ilitangaza kupunguza kupeleka vikosi vyake huko Yemen. Na 2020 ilisherehekea kurejea kwa wanajeshi wake baada ya kushiriki katika vita hivyo hata kabla ya vita kuisha.

Sudan, UAE na Saudi Arabia

EWD

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Sudan ni eneo muhimu la kimkakati. Inapakana na Bahari Nyekundu na inachukuliwa kuwa kiungo kati ya Mashariki ya Kati, Afrika na eneo la Pembe ya Afrika, pamoja na utajiri wake wa maliasili; dhahabu, fedha, zinki, chuma, shaba, mafuta na gesi asilia, pamoja na kilimo na mifugo.

Sudan ilikuwa moja ya nchi za kwanza kuunga mkono muungano unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen, na kutuma takriban wanajeshi 15,000 kushiriki katika vita hivyo.

Uhusiano kati ya mkuu wa Baraza la Utawala wa Mpito, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na makamu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama "Hemedti," ambaye anaongoza Vikosi vya Msaada wa Haraka vilivyoshiriki katika vita vya Yemen umeharibika.

Wachunguzi wengi wa mambo wanasema Saudi Arabia inamuunga mkono Al-Burhan, wakati UAE inamuunga mkono Hemedti kuendeleza maslahi yao nchini humo.

Msomi Talal Muhammad alifikia kusema "Sudan imekuwa uwanja wa vita vya wakala wa Saudi Arabia na UAE," katika makala aliyoandika katika jarida la Foreign Policy Julai iliyopita.

Ingawa UAE haikuzungumza hadharani juu ya ushirikiano wake na Hemedti. Luteni Jenerali Yasser Al-Atta, aliishutumu hadharani UAE kuunga mkono Vikosi vya Msaada wa Haraka dhidi ya Jeshi la Sudan, na wiki mbili baadaye, aliamuru wanadiplomasia 15 wa UAE waondoke Sudan.

Mchambuzi wa Sudan Kholoud Khair anasema, "nyufa katika uhusiano kati ya Hemedti na Al-Burhan na kutofautiana kwa maslahi yao, yote yanaonyesha kutofautiana kwa maslahi ya Saudi na Imarati.”

Dk. Charles Dunn anasema, "uchumi na siasa ndio vichochezi vikuu vya ushindani kati ya Saudi Arabia na UAE."

Pia Unaweza Kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi